Siasa zetu, Nguvu za Maaskofu na Mahusiano ya jamii zetu

January 2011

Nimekuwa nikisita sana kutoa maoni yangu katika mjadala huu kutokana na kutambua kuwa wengi wetu tumekuwa tukiongozwa na mihemuko na ushabiki zaidi kuliko uhalisia wa mambo katika kuendeleza majadiliano ama malumano yetu. Lakini leo naomba nijitoe muhanga kusema kile ambacho naamini kinapaswa kusemwa kabla ya kujikuta kuwa tumefikia mahala pabaya zaidi kusipokuwa na kurudi nyuma.

Ni kweli kabisa viongozi wa dini, wawe Mashehe, Maulamaa, Maaskofu, Mapadre na Wachungaji wana haki na wajibu wa kukemea maovu yote bila ya kuchagua wakiwa kama wanadamu na pia raia wa nchi yetu.

Ni kweli kabisa kuwa katika historia ya nchi yetu, wakati wote viongozi wa dini wamekuwa wakijihusisha na masuala ya kisiasa kwa njia moja ama nyingine, iwe kushutumu ama kupigia debe kundi fulani ama suala moja na lingine.

Ni kweli kabisa viongozi wa kijamii wana umuhimu mkubwa katika kusaidiana na wale viongozi wa siasa katika kuendeleza jamii kwenye neema zaidi na kuepusha kwenye majanga yawe ya kisiasa, kijamii ama kiuchumi.

Ni kweli kabisa kuwa Maaskofu haswa wale wa kanisa la katoliki wana nguvu kubwa yenye mfumo makini wa ushawishi katika jamii yetu kuanzia katika masuala ya kijamii na hata kisiasa.

Hata hivyo ni muhimu sana kutambua kuwa haki na wajibu huu ni lazima utambue UHALISIA wa mazingira tuliyonayo kama jamii. Ni wajibu wa viongozi kuangalia hali halisi haswa ya mahusiano ya kijamii ili kupima faida na hasara za kutekeleza haki na wajibu wao.

Tanzania yetu ni Tanzania tunayoamini katika UMOJA na AMANI. Hii ni nyenzo muhimu katika kufanikisha dira ya maendeleo ya nchi yetu. Watanzania kama jamii ama taifa tunaamini kuwa tunapendana na kuheshimiana. Lakini hilo halina maana kuwa watanzania wote tunaaminiana, kupendana ama kuheshimiana kama tunavyopenda kuamini na kujigamba mbele ya wengine.

Ni ukweli ambao wengi tunajaribu kuukataa kuwa watanzania hatuaminiani. Na kutokuaminiana huko kupo katika misingi ya kisiasa, kimapato, kiasili, kikabila na hata kidini.

Miaka ya zamani ilikuwa sio kitu cha kawaida kusikia mtu akisema hawezi kumuamini mchaga. Lakini sasa hilo ni neno la kawaida kusemwa tena bila ya kificho wala haya. Miaka ya zamani ilikuwa sio kawaida kusikia Muislam akisema hamuamini Mkristo ama Mkristo kusema kuwa hamuamini Muislam, lakini sasa hilo ni neno la kawaida kusemwa tena bila hata kificho.

Yapo mengi yanayodaiwa kuwa chanzo cha hali hii ya kutokuaminiana tuliyonayo sasa. Wapo wanaoamini ni kutokana na umaskini, wapo wanaoamini ni kutokana na ujinga, wapo wanaoamini ni kutokana na siasa za ushindani usio na kifani, wapo wanaoamini kuwa ni kutokana na historia, wapo wanaoamini ni kutokana na siasa za kidunia hasa siasa za marekani na ulaya katika kupambana na kile kinachotabulika kama ugaidi wa kiislamu na wapo wanaoamini yote kwa pamoja ama sababu nyingine tofauti.

Zote zaweza kuwa ni sababu lakini cha muhimu ni kuwa uhalisia unaonyesha kuwa watanzania hatuaminiani. Na mbaya zaidi ni kuwa kutokuaminiana katika misingi ya kikabila na kidini kumekuwa kunakuwa ama kukuzwa zaidi kuliko kushughulikiwa kwa nia ya kupunguzwa kama sio kuondolewa kabisa.

Katika moja ya hotuba zake, Mwalimu Nyerere aliwahi kusisitiza kuwa ingawa nchi yetu inajengwa katika misingi ya kutokuwa na ukabila, udini ama ubaguzi wa aina yeyote ile, si kweli kuwa watanzania sio wabaguzi. Aliendelea kudai kuwa utakuta wengie tunajigamba kuwa tunachukia udini ama ukabila lakini tukiminya kidogo tunatoka mapovu ya udini na ukabila. Na ndio maana UTANZANIA wetu ukajengwa kwa misingi ya kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote ile kwa sababu uo na ni hatari kwa taifa.

Mtizamo huu unasisitiza ule mtizamo ambao yawezekana hakuandikwa katika sheria zetu lakini ulikuwepo miongoni mwa fikira za utanzania wetu kuwa si BUSARA kuchanganya dini na siasa. Hii ni busara ambayo inatambua haki na wajibu wa viongozi wa dini zetu kushiriki katika kupiga vita maovu ya aina zote lakini pia inatambua umuhimu wa kuepuka athari za kufanya hivyo kutokana na hali halisi ya jamii yetu.

Wote tunakumbuka ni jinsi gani viongozi wa kisiasa na kidini walivyokuwa mstari wa mbele kusisitiza BUSARA hii katika miaka ya tisini ambako kulikuwa na vuguvugu kubwa la viongozi wa dini ya kiislamu kutoa matamko ya kisiasa. Wengine ambao leo hii tunajaribu kuhalalisha hilo ndio tuliokuwa mstari wa mbele kulaani vitendo vya mashehe hao wakati ule.

Wapo ambao wanatumia matamshi ama uungwaji mkono wa wazi wa Askofu Kilaini katika ugombea wa Rais Kikwete mwaka 2005. Lakini wanaacha kusema ni jinsi gani viongozi wenzake wengineo ambao walilaani kitendo chake hicho na kumpelekea kupunguziwa madaraka yake kama ilivyo sasa.

Moja ambalo wengi wanashindwa kung'amua ni kutambua mchango mkubwa wa kujenga maelewano na kupunguza kutoakuaminiana kulikowahi kufanywa na kiongozi huyo miaka ile. Wengi tunashindwa kufikiria tamko lake lile katika upana wake na ni jinsi gani tamko kama lile kutoka kwa kiongozi mkubwa wa kanisa la Katoliki kumpigia debe mgomba urais Muislam linavyoweza kujenga na sio kubomoa kama endapo lingekuwa ni tofauti na lile.

Wengi hawajui ama wameshasahau nini kilichowapata baadhi ya mashehe ambao wamekuwa mstari wa mbele kusifia uongozi wa Mwalimu Nyerere ambaye kwa baadhi ya waislamu yeye anawakilisha chanzo kikuu cha madhila yote ambayo wanaamini wanayapata kutokana tu kuwa wao waislamu. Lakini wengine tunatambua umuhimu wa mitazamo chanya ya baadhi ya viongozi wa kiislam kwa Baba wa Tafa sio tu kwa kuendeleza misingi aliyotuachia lakini hata kupunguza hali ya kutokuaminiana miongoni mwa wanajamii wa dini zetu mbili kubwa.

Wakati wengi wa waislamu wakitambua mapungufu mengi yaliyopo katika serikali ya Rais Kikwete na chama chake ni ukweli usiofichika kuwa kuna mtazamo unaolingana miongoni mwa waislamu walio wengi kuhusiana na matamshi ama makaripio yasiyoisha kutoka kwa viongozi wa dini ya kikristo ambayo wanaamini yanamlenga zaidi Rais Kikwete kuliko utashi wa kupiga vita ufisadi, ombwe la uongozi ama haki na demokrasia. Mtizamo huo ni ule wa kutokuamini nia ya dhati ya makaripio hayo.

Ni ukweli ambao wengi tunapaswa kuutambua kuwa mtizamo kama huo hapo mwanzo ulikuwa miongoni mwa wale ambao wengi tungependa kuwatambua kama SIASA KALI/ EXTREMISTS ambao wapo katika pande zote za dini zetu, hivi sasa ni mtazamo wa wengi ama MAINSTREAM feelings. Huo ni ukweli ambao wanaoshabikia hali iliyojijenga katika miaka karibia minne iliyopita wanapaswa kutambua na kupima kama ni busara viongozi wa dini wawe waislamu ama wakristo wanapaswa kuendelea kuachwa ama hata kushabikiwa pale wanapotoa matamshi yenye kuonekana kama yana malengo ya kisiasa.

Yawezekana kabisa hali hii ya viongozi wa kidini kuwa mstari wa mbele kutoa matamko ya kisiasa yakawa yanaendana kabisa na matakwa na nia njema kabisa miongoni mwa watanzania kuona kuwa taifa letu linaepushwa na wingi zito za madhila ya ufisadi linalotanda, lakini pia kama raia makini ni muhimu kupima kama msaada huo unazidi umuhimu wa BUSARA ya viongozi wa kidini kutofanya hivyo.

Kuna watu wa mtazamo kuwa chanzo cha hali ya kutokuaminiana kati ya watanzania ama makundi ya kidini nchini ni viongozi wetu wa dini. Mtazamo wangu ni kuwa katika suala la kutokuaminiana viongozi wa dini wana dhambi ya kuchochea na kutofanya juhudi za kutosha kuondoa hali hiyo.

Mzizi wa hali hii ni jamii zetu kuanzia ngazi za familia. Wengi wetu tunakuzwa katika hali ya kuaminishwa kuwa dini zetu ni nzuri na za kweli sio kwa mafanikio yake bali kwa kulinganisha na "ubaya" wa dini zingine. Hali hii hutoka katika familia hadi katika mfumo mzima wa kijamii ukiwemo mfumo wa elimu yetu. Na hata tunapokuwa wakubwa hali hii tunakutana nayo mitaani na vijiweni. Inapofika katika ngazi ya makazini na nafasi za kiuchumi na kisiasa ndio hali inakuwa mbaya zaidi. Tatizo linakuwa zaidi pale viongozi wetu wa kidini wanapoamua kuchagua makundi ya kisiasa kama nyenzo za kulinda, kutetea ama kuhakisha maslahi yao binafsi na pia makundi yao.

Sasa unapokuta tunakuwa mfumo hovyo wa kisiasa unao hodhiwa na wanasiasa wajanjawajanja na wenye tamaa isiyo na kifani, ndipo mchanyato huo unapokuwa mkubwa na kupelekea hali hii ya kutukuaminiana kugeuka kuwa hali ya kuchukiana kama ambavyo inajijenga sasa.

Naamini kuwa wanasiasa na wanaharakati kama watakuwa tayari kuwajibika zaidi na kwa umakini zaidi wanaweza kabisa kufanikisha kile ambacho viongozi wa kidini wanachojaribu kukifanikisha ama kuzuia. Ni wazi kuwa kukaa pembeni kwa viongozi wa kidini kutotumia haki yao ama kutotekeleza wajibu wao wa kukemea maovu kwa style ya makaripio ya wazi ama matamshi ya majukwaani, kutaweza kujenga zaidi kuliko kubomoa kama mbavyo hali inavyoelekea hivi sasa.

Wanasiasa, wanaharakati na raia makini wana wajibu wa kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kuhakikisha kuwa viongozi wetu wa kidini wanatilia maanani uhalisia wa mazingira ya kisiasa na kijamii tuliyonayo kama taifa ambayo ukweli yanataka yanataka subira zaidi, busara zaidi na uvumilivu wa hali ya juu kuliko hali ilivyo sasa.