Maoni yangu kuhusu mjadala wa mchakato wa katiba mpya

******Maoni yangu kuhusu mjadala wa mchakato wa katiba mpya


Nakubaliana na suala la kuwa na muswada wa Kiswahili ingawa sidhani kama hilo liwe jambo la kuathiri mchakato huu muhimu kama ambavyo baadhi ya watu wanavyojaribu kuchochea na wengine kushabikia.

Pia nakubaliana na suala la muda wa mchakato na ukomo wa hatua moja hadi nyingine kuwekwa bayana.

Vilevile nakubaliana na maoni kuhusu suala la kutajwa kwa wazi constitution making bodies na nguvu zake na Kupunguza nguvu za maamuzi mikononi mwa Rais.

Pia suala la hadidu za rejea kuwekwa na bunge lakini naunga mkono suala la uteuzi kubaki mikononi mwa Rais huku bunge likaachiwa jukumu la kuwapitisha na pia kuchagua uongozi wake ingawa nafasi ya Katibu kubaki kuwa jukumu la serikali iwe Rais ama waziri mhisika.

Suala la sheria dhidi ya watakaozuia shughuli za kamati ni muhimu kuwepo ukichukulia dalili mbaya zinazoanza kujionyesha na utamaduni wa kutoheshimu wala kuvumilia mawazo mbadala unaojijenga katika jamii. Si CCM itakayoamua lakini ni mahakama zetu.

Napinga kabisa maoni ya kuwa mijadala ya maoni kufanyika majomboni chini ya uongozi wa wabunge. Wabunge wetu wengi hawana ujuzi wa kuongoza mijadala ya maoni tofauti, wengi hawana heshima katika jamii zao, wamejawa na chuki za kiitikadi na pia hawana nidhamu ya ukweli.

Maoni yangu ni kuwa mijadala ianze katika ngazi za kata ambako itasimamiwa na watendaji wa kata wakisimamiwa na wawakilishi wa kamati, asasi za kiraia na vyama vya siasa(mmoja mmoja). Hapa watakusanya maoni yote kama yalivyo na kusimamia uchaguzi wa wawakilishi wao (idadi iwe watano- mwanaume, mwanamke, kijana, mwanamama, kiongozi wa kijamii) watakaokwenda katika mjadala wa wilaya ambao nao utachakusanya maoni kama yalivyo na kuchagua wawakilishi wa mkutano wa mjadala wa kitaifa.

Maoni yatakayotoka katika ngazi ya wilaya yatakuwa streamlined katika masuala na wingi wake halafu yapelekwe katika mjadala wa kitaifa ambako watashiriki wawakilishi wawili AMA watatu kutoka katika kila wilaya ambao watachukua asilimia 50 hadi 60 ya mkutano.

Pia kutakuwa na wawakilishi wa makundi maalumu, asasi za kiraia, viongozi ama makundi ya kijamii, wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, wataalamu na pia wawakilishi wa vyama vya siasa (mmoja kutoka kila chama chenye usajili na uwiano wa kura za uchaguzi uliopita (popular votes) kwa vile vilivyopo bungeni)

Maoni hayo ndiyo yatumike kutengeneza rasimu ya katiba mpya itakayopelekwa na kujadiliwa katika national constitutional assembly or convention kabla ya kupelekwa bungeni kama mswada halafu kupelekwa katika kura ya maoni.

Nawakilisha