Ujumbe mfupi kwa Godless Lema, M.B





Dear Lema


Unapojiandaa na ushahidi wako wa udini dhidi ya CCM kumbuka wapo wanaojiandaa na uhsahidi dhidi ya CHADEMA. Unapojiandaa na ushahidi wako dhidi ya Udini wa Viongozi waislam, kumbuka kuwa wapo wanaojiandaa na ushahidi dhidi ya Viongozi wakristo. Katika kujiandaa huko kuna wenye dhana na wenye uhalisia na kuna wenye vyote hivyo viwili. Dubwana hili la Udini halitaondoka kwa wewe kuwatuhumu wao na wao kukutuhumu wewe. Dubwana hili litaondoka kwa wao kujiangalia na kujitambua makosa yao na wewe kujiangalia na kutambua makosa yako/yenu. Kudhani kuwa CHADEMA itajisafisha na tuhuma za udini wa kikristo kwa kutuhumu CCM kwa udini wa kiislam, ni ama ujinga ama nia halisi sio kuupiga vita udini bali ni kuuendeleza na kuukuza udini huo ukiamini ndio njia ya kulinda na kupigania maslahi ya upande wako.


Kama nilivyowahi kusema hapo kabla anayedhani kuwa Kikwete ni mdini na ndiye mwanzilishi wa vuguvugu hili la udini hana tofauti na wanaodhani ama kuamini kuwa Nyerere alikuwa mdini na ndiye aliyepanda mbegu za udini huu. Kwangu mimi wote hawa ni wajinga. Simuoni Lema kama mdini lakini naamini ni mjinga na pia anasukumwa na dhambi zake katika kujaribu kujikosha kwa kuwashutumu wengine na kujaribu kuwanasabisha na ubaya wake. Hizi ni aina ya suluhu za mambo makubwa zinazoletwa na wale wenye upeo mdogo wa kisiasa, kihistoria na kiuongozi. Ni suluhu za aina ya siasa nyepesinyepesi zenye kulenga zaidi utashi wa siasa za matumbo zaidi ya siasa za maendeleo.


Udini kama ulivyo ukabila ni sehemu ya fikra za kijamii yetu. Tunachotofautiana sisi na mataifa mengine ni kuwa sisi kama Taifa tunaona udini na ukabila kama tatizo kubwa kuliko tatizo lingine lolote na katika historia ya ujenzi wa UTAIFA wetu hilo limewekewa kipaumbele. Ukweli kuwa hili limesaidia kutulinda na maafa mengi kama yaliyowafikia wenzetu wengine waliojaribu kuukubali na kuurasimisha udini na ukabila kama ni kitu cha kawaida. Naamini hadi sasa tuna mjadala huu kwa sababu tumeaminishwa katika utaifa wetu kuwa hili ni tatizo ambalo tunapaswa wakati wote kulikwepa na kulipiga vita.

Mpaka sasa watanzania tume-epushwa na janga la kupata kiongozi mdini ingawa tunapoelekea siasa hizi zitatufikisha mikononi mwa viongozi wenye hulka na kuendeshwa na fikra hizo. Hizi shutuma dhidi ya Mwalimu Nyerere na Rais Kikwete zinaendeshwa kwa hisia zaidi ya uhalisia. Ndio maana naamini kuwa kama kiongozi haupaswi kufanya siasa hizo bali unapaswa kufanya siasa makini, zenye kuonyesha weledi wa tatizo na zitakazoleta suluhu ya muda mrefu na sio ushindi wa muda mfupi wa upande mmoja utakaoleta maafa ya muda mrefu kwa pande zote.

Kinachoendelea sasa ni kukua na kuelekea kuota mizizi kwa fikra hizi na kupata uungwaji mkono wa baadhi ya viongozi wa kisiasa na kijamii ambao wako tayari kuzitumia fikra hizi kama mtaji wa siasa za kulinda maslahi ya kundi na ubinafsi wao au kuwa silaha dhidi ya maslahi ya kundi ama ubinafsi wa wengine. Kinachoendelea sasa ni kustawi kwa mazingira ya kukuwa kwa tatizo na kulegalega kwa uwezo wa kupambana nalo na hili ni zaidi ya mapungufu ya uongozi kama tuliozoea majibu mepesi tungelipenda kuamini, hii sehemu ya evolution ya siasa zetu za ndani na za kimataifa. Kujaribu kutuhumu kuwa mbegu za udini huu zimepandwa na kundi fulani ama mtu fulani ni propaganda za kisiasa, ufinyu wa kifikra na ujinga wa kimtazamo ambao unaweza kumsaidia mtu ama kundi moja kwa muda mfupi lakini kuwa hasara kwa wote kwa muda mrefu.

Kuhusu ya CUF na pia UAMSHO, CHADEMA na CCM, yote hayo yapo katika hali ya hisia na uhalisia. Kuna yanayosemwa na kuaminiwa kutokana na hisia tu na kuna ambayo yanatokana na uhalisia wa matendo ama muonekano wa baadhi ya wanachama ama kama chama. Matendo na muonekano ambao hushawishiwa na kujidanganya na kuamini kuwa kutumia siasa za udini ama ukabila katika harakati zao ama katika mapambano dhidi ya wengine kunawasaidia kuwahakikishia strong and viable political base ama wengine kuamini kuwa ni sehemu ya siasa. Na kama ambavyo nilivyowahi kusema hapo nyuma, baadhi ya hizi hisia zinajengwa kutokana na kuangalia sana nguvu za chama ama kundi fulani katika dini ama kabila fulani bila ya kupima hayo katika muktadha wa sababu halisi zilizopelekea hivyo kama vile historia ya chama ama kundi hilo.

Lakini kwa upande wangu, sikusita kushutumu tatizo hilo ndani ya CUF (UDINI NA UKABILA) enzi zile na sasa katika sura ya UAMSHO, au katika CHADEMA (UDINI NA UKABILA) na CCM (UDINI NA KUCHIPUKA KWA UKABILA PIA) kuanzia katika uchaguzi wa mwaka 2005 na zaidi 2010. Naamini ni muhimu kukemea pande zote kuliko kukekemea upande mwengine pekee kwani kufanya hilo ni ujinga, unafiki, uzandiki na kama nilivyosema, ni siasa nyepesi nyepesi.

Kujidai kupambana na UDINI kwa kushutumu wenzio tu na kukimbilia kuhalalisha yako kwa msingi kuwa eti wewe una-react tu kutokana na udini wa wengine, kama ilivyo upande wa Uislam na makabila madogo yanayoamini kuwa yana haki ya kuendesha udini na ukabila wao kama njia ya kupambana na udini na ukabila wa wengine, ni kuuendeleza na kuukuza Udini na sio njia muafaka ya kutatua tatizo hili.

Lakini vilevile naamini kuwa katika game hili la kutumia siasa hizi dhidi ya mwenzako, kati ya CUF na CHADEMA kwa upande mmoja na CCM kwa upande mwengine, ni CUF na CHADEMA ndio wenye urahisi wa kuathirika zaidi ya kufaidika na siasa hizi. Historia, ukomavu na utamaduni wa kisiasa ndani ya CCM unawasaidia sana katika kupunguza madhara ya siasa hizi kuliko hali ilivyo katika vyama vingine. Huo ni ukweli mchungu ambao washindani wa CCM mnapaswa kuutambua. Athari za siasa hizi ni kubwa na zenye uwekano mpana zaidi kuumiza CHADEMA na CUF kuliko CCM. Kwa CCm itawachubua tu, kwa CHADEMA na CUF itawadumaza na kuwaangamiza kisiasa.

Ndugu yangu Edward Kinabo anadai hili suala la ushahidi dhidi ya udini wa Rais Kikwete ni zigo la Lema. Naamini hapa na yeye anajidanganya. Hadi sasa wanasiasa waliowahi kutuhumu Udini wa CCM na Kikwete on the record ni Lema, Mchungaji Msigwa na Selasini. Hawa wote ni viongozi wa CHADEMA na wote hawa wamewahi kusikika wakitamka maneno ya chuki ama kuchochea udini. Lema ameyasema yake katika Uchaguzi, Selasini amesema yake wakati wa sakata la kutaka kumuondoa Zitto katika uongozi wa wabunge wa CHADEMA kule Kunduchi wakati Zitto yuko hospitalini akipambana na tatizo la sumu mwilini, Mchungaji Msigwa ukitoa mengi anayoropoka amethubutu kununua filamu ya kumtukana na Mtume Muhammad na kwenda kuionyesha kwa wapiga kura nyumbani kwake na huu ni ushuhuda wa Mbunge mwezake wa CHADEMA. 

Ukichukulia kuwa Lema amesikika akisema kuwa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe ambaye mimi naamini kuwa yeye si mjinga wala si mdini amemzuia kutoa huo ushahidi wake bungeni kwani sio wakati muafaka pamoja na hayo mengine niliyoyagusia hapo juu, ni wazi kuwa endapo Lema na hawa vinara wengine wa CHADEMA wataendelea na siasa hizi (najua kuwa wapo vinara wa CCM pia wanaozishabikia siasa hizi chini kwa chini), CHADEMA haitaweza kupambana na hisia zitakazojenga mtazamo kuwa zigo hili ni la CHADEMA na sio la Lema pekee.


Ndio maana nasema kuwa UDINI huu hautaondoka kwa kutuhumiana bali kujitambua, kubadilika na kutafuta muafaka na kamwe hautaweza kupigwa vita kwa kuruhusu waliokosa uhalali wa kimsingi ndio kuwa sura ya mapambano dhidi ya udini, hasa udini wa wengine na sio udini wao.


Katika hali iliyofikia sasa, mimi naamini kuwa moja ya njia madhubuti ya kupambana na udini ni sisi wenyewe kuangalia udini wa pande zetu, Kuuepuka, kuukemea na kuupinga wakati tukijaribu kuuelewa undani wa udini wa upande mwengine na kutafuta muafaka wa kukabiliana nao kama kwa kuutambua chembe ya ukweli wa hisia zao ama kuupiga vita kwa ujumla wake. 

Zaidi mimi naamini njia moja kubwa ya kuhakikisha tunadhibiti uhodhi wa siasa nyepesi zinazoshamiri katika kushape mjadala huu wa udini kama inavyoelekea kuwa, na kama njia ya kuondoa mazingira ya siasa hizo kustawi, kuna haja ya kuunda Tume ya Ukweli, Uwazi na Maridhiano ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa jukwaa la kuweka wazi ukweli ili kudhibiti hisia na kutambuana misingi ya madai ya msingi ya pande zote na kukubaliana kwa pamoja jinsi ya kuondokana na janga hili. Na haya tutaweza kuyafanya kwa kukubali kuwa Udini haujaanza na Kikwete wala Nyerere.


Muafaka haupatikani kwa ushindani wa nani mbaya nani mzuri, Muafaka unapatikana kwa kushirikiana wabaya na wazuri. Tujitambue, tubadilike na tuafikiane ndio njia salama.

Mtizamo wangu kuhusiana na sarakasi za CHADEMA na Katiba Mpya!


CHADEMA wapongezwe kukwepa kitanzi cha kisiasa walichojiwekea!



Kitendo cha CHADEMA kushindwa kutimiza ahadi yao ya kujitoa katika mchakato wa katiba mpya kama ilivyotangazwa hapo awali na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe alipotoa hotuba yake bungeni na kuwekewa msisitizo na Katibu Wilbroad Slaa kinatoa mafunzo mengi kisiasa.

Mosi, ni muhimu kuwapongeza wale waliothubutu kuona mbali na kukwepa mtego huo wa kisiasa waliojitegea hapo kabla ambao kama wangeuingia basi ungeliweza kuwamaliza kisiasa. Wahenga wanasema “never use toothless brinksmanship as it will only take you into oblivion”. CHADEMA walifanya makosa kuamua kutishia kujitoa lakini wanapaswa kupongezwa kwa kurudi nyuma kwa style ya aina yake.

Pili ni muhimu kuielewa CHADEMA katika suala zima la Katiba mpya. Kwa mtazamo wangu suala la katiba mpya ndani ya CHADEMA halikuwa na mvuto mkubwa kwa maana ya umuhimu wake katika kuendeleza na kusimika mfumo wa kidemokrasia kama ambavyo wengi tungelitegemea. Kwa CHADEMA Katiba mpya ilikuwa ni propaganda ya kisiasa iliyokuwa ikitumika pale inapotokea haja ya kutafuta mchawi wao kushindwa uchaguzi. Lakini pia kimkakati, katiba mpya ilipaswa kuwa ajenda endelevu ya kisiasa kuelekea katika uchaguzi wa 2015. 

Kitendo cha Rais Kikwete (sio CCM) kuikubali na kuitekeleza hoja hiyo ni kitendo ambacho hawakukitegemea na ukweli kimewaondolea ajenda muhimu kisiasa. Hivyo basi uungaji mkono wao wa hapo awali ulikuwa wa kulazimika lakini sio kwa kupenda hivyo ndio maana kila inapotokea mwanya wa kuchakachua uhalali wa mchakato huo, kina Tundu Lissu hawapotezi muda kuutumia.

Vilevile CHADEMA wanahofia uwezekano wa zoezi hili la katiba mpya kumalizika kwa mafanikio kwani ni wazi kitamkuza sana kisiasa, ndani na nje ya nchi, Rais Kikwete na hivyo yeye kuweza kuwa na ushawishi zaidi katika siasa za uchaguzi mkuu wa 2015. Hivyo kimkakati CHADEMA wanaonelea ni muhimu ama kuchakachua uhalali wa mchakato huo ama hata kuuvuruga kabisa usifanikiwe, hapo watakuwa wameweza kuikomboa ajenda hiyo na kuendelea kuitumia kuelekea 2015 lakini pia kumpunguzia nguvu za kisiasa Rais Kikwete kuelekea 2015.

Kwa nini tishio la CHADEMA kujitoa katika mchakato lilikuwa ni kitanzi cha wao wenyewe kujinyonga kisiasa?

Endapo CHADEMA wangejitoa leo na huko mbeleni, Tume ikaja na Rasimu ya Katiba Mpya ambayo itakuwa na mabadiliko makubwa yatakayokubalika na watanzania walio wengi wenye kuangalia mustakabali wa taifa zaidi ya ushabiki wa kisiasa, hilo lingekuwa kosa kubwa sana kwao kisiasa kwani wangeonekana wamekurupuka kuchukua msimamo wa kujitoa na pia ingelikuwa rahisi kwa wapinzani wao kisiasa kutumia hilo kudhihirisha kuwa CHADEMA ni chama pinga tu na hakina weledi wa kisiasa.

Vilevile mtego mwengine waliokuwa wamejiwekewa na ulikuwa ukiwasuburi kama hatua ya pili baada ya kujitoa ni jinsi gani wange-deal na uasu wa Prof Baregu ambaye amesema wazi kuwa akiambiwa kati ya kuchagua chama na Taifa basi atachagua chama. CHADEMA ambao wanatuhumu kuwa CCM inaingilia mchakato wamekuwa wakimlaumu Prof Baregu kwa kutuwapa ya ndani ya Tume ya Katiba kitu ambacho kwa wenye busara na maadili walipaswa kumpongeza Prof Baregu kwa kutii miiko ya kazi yake. Hapo ndipo wangelazimika kufanya makosa makubwa zaidi. Ukichukulia vita ya muda mrefu wanayompiga Naibu Katibu mkuu wao Zitto ambaye anaonekana kama sura ya siasa za kisomi na kimuono ndani ya CHADEMA na anayeonekena kushabihiana kifikra na Prof Baregu, CHADEMA wangefanya kosa kubwa sana kumuongeza na Prof Baregu katika listi yao ya wanaoawachimba kama maadui wa ndani. Ni dhahiri hili lingekuwa kosa jingine la kuwathibitishia wenye akili zao kuwa kile kirusi cha kupiga vita USOMI kimejikita pia CHADEMA. NA hapo wangeweza kupuputisha baadhi ya wasomi na watu wa tabaka la kati ambao wamekuwa waki-sympathies nao wakidhani kuwa kuna uwezekano wa CHADEMA kuwa mbadala makini wa CCM.

Kuhusu hoja ya kuwa CCM wanaingilia mchakato wa katiba, ukweli huu ni uthibitisho wa muendelezo wa siasa za hisia usio zisizojali kuchanganua ukweli ambazo wamekuwa wakizitegemea kufikia maamuzi yao mengi. Ni wazi kuwa vyama vyote vya siasa na hata makundi mengine ya kimaslahi vyote vimekuwa na mikakati ya kuhakikisha kuwa maon, mitizamo na maslahi yao yanakuwa na ushawishi katika mchakato huo. Cha ajabu ni kuwa CHADEMA hawakukemea wala kuhoji kitendo cha makundi ya kidini kuingilia mchakato huo kwa kuwaamuru wafuasi wao kwenda katika mikutano ya uchaguzi wa mabaraza ya katiba na kuchagua wawakilishi kwa vigezo vya Udini. Haya yamefanyika na makundi ya dini zetu zote mbili, Waislam na Wakristo na yamefanyika misikitini na makanisani. Kwanini CHADEMA hawajalichukulia kosa hilo kwa uzito unaostahili?

Kitendo cha viongozi wa CCM kujadiliana wao kwa wao bila ya kuwasiliana ama kushurutisha Tume ya Katiba hakuvunji sheria ya mchakato wa katiba kama Tundu Lissu alivyotaka kuaminisha umma. Walichofanya viongozi wa CCM ni kujipanga kisiasa kama ambavyo wenzao wengine wakiwemo CHADEMA wanavyofanya. Ni CHADEMA ambao wamefikia hata kukaa kama kamati kuu ya chama, kujadili kuhusu jinsi gani ya kuendeleza harakati zao ikiwemo jinsi gani ya kushutisha tume kufuata matakwa yao yatakayowezesha maslahi yao kisiasa, kumlaumu mwenzao kwa kukosa kuwapa ushirikiano na hata kufikia kupiga kura za kama chama kujitoa katika mchakato mzima na kumuondoa mwakilishi wao Prof Baregu katika tume ya katiba. CHADEMA wanapaswa kuchukulia matokeo ya kushindwa kupenyeza watu wao kwa wingi katika mabaraza ya katiba ni somo la wao kujijenga zaidi kimikakati na kuwa watanzania bado hawajawa mashabiki sana wa siasa za mipasho na kupiga kelele sana kama ambavyo makada wao wengi wamekuwa wakijipambanua hata huko mitaani kulipofanyika chaguzi za awali za mabaraza ya katiba.

Hivi kesho ikaja kujulikana kuwa hata Mwenyekiti wa CCM hakuwa tayari kutoa maoni yake mbele ya tume kwa kuepuka kuishinikiza ama labda maoni rasmi ya CCM yaliyowakilishwa katika tume hayana sehemu yoyote ambayo hawako tayari kutafuta muafaka wa pamoja, CHADEMA walionyesha wazi misimamo yao na kufikia hata kuweka vitisho endapo misimamo yao haitafuatwa, ni nani ataonekana hayuko makini?

Suala la kutumia ujanja wa kuikashifu, kuishusha na kuiadhiri Tume ya Katiba kwa kigezo cha posho wanazopangiwa na wizara sitaliingilia kwa undani wake, lakini mtizamo wangu ni kuwa siamini kama kuna Mbunge mwenye audacity ya kushutumu posho za wengine isipokuwa ndugu yangu Zitto Kabwe na wengine wachache ambao hadi leo wameendelea na msimamo wa kususia posho walizojiwekea wabunge wenzie. Tundu Lissu anapohoji walimu kulipwa shilingi 325,000 kwa mwezi anasahau kulinganisha na yeye anavyolipwa shilingi 330,000 za posho kwa siku. Mbunge anayelipwa milioni 11.2 kwa mwezi kwa kazi aliyogombania kutumikia anahoji malipo ya mil 7 kwa mwezi kwa kazi ya kuombwa kutumikia. Anasahau ama anajisahaulisha kuwa kila siku anakusanya posho ya kikao 200,000 na posho ya kujikimu 130,000 ambapo Jumla 330,000. Hapo bado mshahara na posho ya ubunge jumla tshs 11.2m kwa mwezi. Kwa ujumla kila siku Tundu Lissu anapokea wastani wa 370,000 awepo au asiwepo bungeni. ie mshahara na posho ya ubunge na 330,000 kwa siku katika siku 130 kama posho anapokuwepo bungeni na katika vikao vya kama. Sasa kwa kweli inahitaji ujasiri wa ajabu kwa mtu kama huyu kusimama na kuhoji posho za wenzie tena tofauti na yeye aliyegombea kutumikia, wenzake ambao wameombwa kutumikia Taifa na kuacha shughuli zao zingine.

Kwa kweli hadi kufikia sasa tumeona mengi na wenye upeo wa kujifunza naamini watakuwa wamefaidika sana kujifunza jinsi ya kutofanya makosa ya kisiasa kirahisirahisi kama wenzetu hawa, lakini zaidi kwa wanachama na wapenzi wa CHADEMA tambueni kuwa kwa maslahi ya nchi yetu, CHADEMA hakipaswi kurudia historia ya vyama vilivyokuja na kupita na hivyo kurudisha nyuma harakati za kujenga mfumo makini wa demokrasia ya vyama vingi nchini. Jitambueni, Jifunzeni na Jirekebisheni kwani mnaweza kama mlivyofanya leo kwa kuacha kutekeleza kitisho chenu cha kujitoa mlichokiweka wiki mbili zilizopita...



Ya CUF cum UAMSHO na propaganda zao dhidi ya Muungano

Ni wazi kuwa baadhi ya vinara wa CUF na wadau wao UAMSHO hawautaki na wanauchukia Muungano na wameamua kufanya ajenda yao kuuvunja. Katika miezi ya karibuni vinara wa kundi hili wamakumbatia mfumo wa wanachokiita Muungano wa Mkataba ambao ni wazi wamevutiwa nao kutokana na urahisi wake wa kuuvunja Muungano. Na ukweli hii ni kama strategy ya kuwaficha ukweli wafuasi wao ambao bado wanaamini katika umuhimu wa Muungano. Wamekosa uthubutu wa kusema tuvunje Muungano lakini wanatumia neno Muungano wa Mkataba kama ngozi ya kondoo juu ya chui ambaye ni kuvunja Muungano.

Wahafidhina hawa wa harakati za kurudisha Zanzibar ya kabla ya Mapinduzi, wanajua wazi kuwa madai wanayoyatoa hayawezi kukubalika kwa upande wa Bara. Hivyo madai yao ya Muungano wa Mkataba na mengineyo ni ujanja wa kuwalazimu Watanganyika ndio waamue kuvunja Muungano huo na kuwafanyia kazi wao na maslahi yao ya kihafidhina. Wanjua wazi jibu la mwisho litakuwa na tuvunje Muungano ili tukutane katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kama itahitajika tukiwa kama nchi tofauti zenye maslahi tofauti yakiwemo yanayoendana na yanayopingana.

Moja ya njia wanazotumia wahafidhina hawa kuwalaghai Wazanzibari ni kuendeleza ile ndoto ya Zanzibar ya kabla ya Mapinduzi ambayo ilikuwa ikivuma kutokana na kuwa kitovu cha biashara katika Afrika Mashariki na kuaminisha watu kuwa Muungano ndio umeiondolea Zanzibar nafasi hiyo. Wanasahau kuwa geopolitics ambazo ni muhimu kwa uchumi wa eneo fulani katika enzi hizo ni tofauti kabisa na sasa. Wanasahau kuwa moja ya vitu vilivyofanikisha kujenga na kuendeleza msingi wa hali hiyo ilikuwa ni biashara ya utumwa na magendo ya bidhaa mbalimbali za thamani ya juu kutoka maeneo mengine ya Afrika Mashariki, zaidi ilikuwa kutoka Tanganyika.

Biashara ya utumwa iliendelea hata wakati wa ufalme wa Waarabu wa Omani ambao serikali iliyopinduliwa na mnayotaka kuirudisha kwa mlango wa nyuma ilikuwa ni wadau wa Sultan huyo. Lakini zaidi ninacho ongela hapa ni msingi wa uchumi uliojengwa na faida kubwa ya biashara hiyo na mabaki ya kimfumo ya biashara hiyo hata baada ya kusimamishwa kwake.

Hata baada ya biashara ya utumwa kuvunjwa Waarabu na wengineo waliendelea kutumia watumwa kuneemesha shughuli zao za kiuchumi ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na Zanzibar ile wanayoiota na hata baadae mfumo wa mabwana na watwana uliendelea hata baada ya uhuru wa 1963 na kukatishwa ghafla na Mapinduzi ya 1964. Hivyo huwezi kuepusha uhusiano wa bishara ya Utumwa na hali ya kiuchumi na biashara kabla ya Mapinduzi na hata mafanikio mengi ya wakati wa Karume yaliendelea kutumia matunda ya uchumi uliojengwa na mtaji uliokusanywa katia biashara ya Utumwa.

Pia wanasahau kuwa mafanikio yale ya wakati ule yalikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mfumo wa ukoloni na ubwana na utwana uliokuwepo enzi zile ambao ulitoa nafasi maalum ya Zanzibar na sehemu fulani ya Wazanzibari kiuchumi.

Haya yote na hata hili la sasa ambapo Zanzibar bado ina nafasi ya kunufaika na soko la karibia watu milioni Arobaini na Tano la Tanganyika, kamwe hayawezi kuwepo hasa baada ya kuvunja Muungano wetu. Tukivunja Muungano Zanzibar itakuwa just another sovereign country ambayo itaangaliwa kama mshindani wa kiuchumi zaidi kuliko mshirika wa Muungano. Tukivunja Muungano hata special status ambayo Zanzibar imekuwa ikipata ndani ya Muungano wa Tanzania na katika Shirikisho la Afrika Mashariki haitakuwepo.

Hivyo kwa wale wanaoamini katika kufufua ndoto ya Zanzibar ya kabla ya Mapinduzi na baadaye Muungano wanapaswa kuipima ndoto yao hiyo kwa mizania ya uhalisia wa mazingira ya sasa na sio mazingira ya wakati ule. Zanzibar njema inawezekana katika mfumo wa siasa za kuaminiana na kushirikiana ndani ya Muungano na sio katika siasa za kushindana kwa visa, chuki na utengano nje ya Muungano.

Kuhusiana na suala la Zanzibar ni nchi ama sio nchi ambalo nalo limekuwa likitumika kama propaganda dhidi ya Muungano ukweli ni kuwa kisiasa Zanzibar ni nchi lakini kisheria Zanzibar si nchi na suala lolote lonalohusiana na Muungano ni lazima lifuate taratibu za Muungano. Kwa kutumia suala la OIC, maadui wa Muungano wamewadanganya na kuwaaminisha Wazanzibari kuwa Zanzibar inazuiwa kufanya chochite wakitakacho hadi wapate ridhaa ya Tanganyia. Ukweli ni kuwa hakuna suala ambalo Zanzibar wanalokataliwa kilifanya kama sio suala la Muungano na kwa masuala ya Muungano kuna vyombo vya Muungano kulishughulikia. Yawezekana wahafidhina wanaopinga Muungano wanaamini kuwa masuala ya taratibu sio sehemu ya utamaduni wa Kizanzibari lakini kama nchi lazima utaratibu ufuatwe hasa inapohusiana na mahusiano na mataifa ya nje kama lile suala la OIC ambalo naamini ni Katika mfumo ulikokuwepo ambapo masuala ya mahusiano ya kimatifa ni suala la Muungano ni Tanzania na sio Zanizbar yenye kupaswa kujiunga na shirikisho hilo linalouunganisha Waislamu na wasio Waislam katika mashirikiano ya kimaendeleo.

Lakini huu ni unafiki wa hawa wahafidhina wanaota kurudisha Zanzibar ya kabla ya Mapinduzi kung'ang'ana na Zanzibar ni nchi wakati wao ndio walioshangilia (hata mimi pia) maamuzi ya kikatiba kupitia mahakama ya rufaa katika kesi ya watu wao wa CUF waliokuwa na kesi ya uhaini lakini baadae wakaona hukumu hiyo chungu pale ilipopingana na matakwa yao wapinga Muungano. Kwa muda sasa wamekuwa wakitumia ujanja wa kulaani uhalisia huo wa kuwa Zanzibar sio nchi na hata ilipotelewa ufafanuzi katika hotuba ya Rais bungeni kuwa Zanzibar ni nchi ndani ya Tanzania na na nje ya nchi katika yale masuala yasiyo ya Muungano tu, kama mbinu ya kujenga hisia kuwa ajenda zao nyingi ikiwemo ya kuvunja Muungano ni ajenda ya Kitaifa ya Wazanzibari uuku wakijua kuwa hilo sio kweli.

Kuhusu mfumo wa kiuchumi, ni kweli Zanzibar inapaswa kuwa na nafasi maalum - special status ambayo itaiwezesha kushirikiana kiuchumi na Tanganyika na sio kushindana kama ilivyo sasa. Sioni sababu nzito ya kulazimisha bidhaa zinazoingizwa kupitia Zanzibar kutozwa kodi sawa na zile zinazoingizwa kupitia Tanganyika. Kama tumeweza kuwa na special status katika mfumo wa soko la Afrika Mashariki ambako pia Zanzibar inaendelea kufaidika nao, sioni sababu ya kushindwa kufanya hivyo ndani ya Muungano wetu.

Suala la kushindanisha uchumi wa Bara na Visiwani nakubaliana nalo kuwa linahitajika kuangaliwa upya. Inawezekana kabisa kuipa Zanzibar status maalum ya kiuchumi ambayo italindwa hata katika masuala ya Muungano au Jumuiya ya Afrika Mashariki na hiyo ndio imekuwa principle inayotumika katika negotiations zote kama Tanzania inavyosisitiza. Na kwa faida ya Zanzibar ni kuwa ili uchumi wa Zanzibar kuwa na nguvu unahitaji soko kubwa na utakuwa ni uhayawani kudhani nje ya muungano Zanzibar itapata kuwa na special status ya kiuchumi bali hilo lawezekana tu ndani ya Muungano. Hili linawezekana tu tukiwa ndani ya Muungano na si vinginevyo. Muungano huu ukivunjika Zanzibar haitakuwa na leverage za kudai special status hasa katika masuala ya kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kuhusu hii propaganda inayoaminiwa na Wazanzibari wengi eti kodi ya ya Zanzibar inakusanywa na kupelekwa Tanganyika huu ni uzandiki mwengine usio na chembe ya ukweli. Ni propaganda ambayo inaelekea kuaminiwa hata na wale ambao wamekuwa wakisambaza huku wakijua haina ukweli wowote. Ndio matokeo ya siasa za fitna hizo. Hakuna senti ya kodi inayokusanywa Zanzibar inayoenda Bara. Pesa zote zinazokusanywa na TRA Zanzibar zinabaki kwa kutumiwa huko ktk masuala ya Muungano.

Zaidi ni kuwa Kuna kiasi kingine kikubwa kinachokusanywa Tanganyika na kuletwa huko kuongezea na hapo bado haujaingiza mabilioni mengine yanayoletwa huko kinyume cha vigezo vya Muungano. Ukweli uwazi kuwa kodi inayokusanywa Zanzibar yote hubaki na kutumika katika shuguuli za Muungano za upande wa Zanzibar na kamwe haijawahi kufikia asilimia 11 ya makusanyo. Sanasana fedha zingine ambazo hukusanywa Tanganyika huongezewa kufikia ile asilimia 4.5 ya Bajeti inayopaswa kuwa ya Zanzibar.

Kuhusu dhana ya kuwa kwa sababu Bunge la Tanzania lina wabunge zaidi ya 200 kutoka upande wa Tanganyika wakati wengine 50 wanatoka Zanzibar hivyo maslahi ua Zanzibar hayawezi kulindwa katika bunge hilo ukweli ni kuwa katika Bunge hakuna suala linalohusu Muungano linalopita bila ya kuwa na baraka za three third majority ya Wabunge kutoka Zanzibar. Sasa kama unadhani nguvu za kibunge ni kuwa na Zanzibar kuwa na wabunge 300 pia inaonyesha jinsi gani mlivyokosa busara. Labda kama na ninyi mliokimbia Zanzibar na kujilipua huko ughaibuni nanyi mnatka uwakilishi bungeni. Hilo linaweza kuzungumzwa.

Kuhusu Zanzibar kuwa na Baraza lao la Mitihani kama ilivyokuwa hapo kabla na sio kutumia mitihani na mfumo wa NECTA sidhani kama hilo tatizo kubwa sana. Kama mnataka kuendeleza uyaghe katika elimu ili kujifurahisha kuwa vijana wenu wamefaulu mnaweza kuwa na baraza lenu la mitihani. Lakini muwe tayari tu kwa vijana wenu ama watosheke na nafasi za vyuo vya elimu ya juu huko Zanzibar na vyenye sifa za kutambulika kimataifa ama muwe tayari kufanya mitihani maalum ya kuweza kuingia katika vyuo vya bara na kwengineko.

Huu ujinga wa kulaumu NECTA kufeli kwa vijana wa Zanzibar ambao wenyewe mnajua walivyokosa nidhamu na tamaduni za elimu unazidi kuwadanganya vijana wa Zanzibar ambao sasa imekuwa fashion kujigamba kuwa hawajasoma na wala hawana kazi. Hata yule kijana aliyekuwa wa mwisho kabisa darasani naye sasa anaamini alifelishwa. Wanatumia sumu kupata mradi wao sasa, lakini sumu hiyohiyo ndio inaaendelea kuathiri msingi mkuu wa maendeleo ya jamii yenu, ELIMU ya vijana wenu. Kama tatizo ni NECTA mbona vijana wa Pemba na wale wenye kuishi katika mazingira ya kielimu wanafaulu?

Kuhusu umeme wa Tanesco ukweli ni kwamba Zanzibar inauziwa kwa bei tofauti na wengine. Serikali ya Muungano ina-subsidize kwa kiasi kikubwa. Lakini pia kiasi kikubwa cha deni hakilipwi na huishia kwa hazina ya Muungano kubeba mzigo wa madeni hayo. Lakini ni kweli suala hilo sio kubwa kwani uwezekano wa wafadhili kuwawekea mitambo ya gesi upo lakini suala ni kuwa na uchumi wa kuweza kuendesha mitambo hiyo na sio kuwa tegemezi jumla jumla.

Na kuhusu dai la kuwa Wazanzibari wanapaswa kuwa na paspoti yao wengine hata wakadai kurudishiwa paoti yao ambayo ukweli Zanzibar huru haijawahi kuwa nayo labda wakimaanisha ile ya Sultan wa Omani ni kweli tukifikia kuwa na paspoti tofauti Wazanzibar wataweza kwenda Tanganyika kama wageni wengine kutoka Kenya endapo mtaweza kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini pia thamani ya passpoti inategemea na hali za kisiasa na uchumi wa nchi hiyo. Ukiangalia mbele kuna kila dalili ya Zanzibar kuwa black spot katika enzi hizi za ugaidi wa "waislamu wenye siasa kali" ambao wamejificha katika kivuli cha CUF na sasa wameanza kujitokeza kaika sura ya UAMSHO. Sasa kama Wazanzibari wako tayari kuondokana na kivuli cha Utanzania na kuingia katika kivuli cha Zanzibar ya UAMSHO na majinamizi mengine, then wanapaswa kuangalia machaguo yao kwa uangalifu zaidi.

Wadau wengi wa Ushirika wa kuvunja Muungano ndani ya CUF wanaamini ama hupenda kuwaaminisha Wazanzibari kuwa baada ya kuvunja Muungano tutaendelea kuwa na mahusiano ya kindugu kati ya Tanganyika na Zanzibar. Hili wakimaanisha kuwa Wazanzibari waliopo Tanganyika hawataathirika na biashara na maingiliano mengine ya kijamii yataendelea kuwa kama kawaida. Huu ni uongo na kama wapo wanaoamini hilo basi ni wajinga.

Ukweli ni kuwa tukivunja Muungano haki za Mzanzibari aliyepo Tanganyika zitabadilika na hatakuwa na nafasi kama aliyo nayo sasa. Atakauwa mgeni kama alivyo Mkenya ama Mganda na usitegemee kuwa Wazanzibari wataendelea kupata upendeleo ktk suala la Ardhi. Lakini pia hata wale tutakaoamua kuwa Watanganyika ni wazi tutabaguliwa zaidi na madhila ya siasa za chuki mnazoendesha ninyi huko hivi sasa zinatatuangukia. Kumbuka huku Tanganyika kuna zaidi ya Wazanzibari 300,000 wahamiaji na zaidi ya 1,000,000 ambao ni vizazi vyao ama wenye nasaba za Kizanzibari. Wengi wao ni Wapemba. Hawa wakilazimika robo tu kurudi Zanzibar sijui hizo social and economic pressures mtazihandle vipi na zaidi wakizaliana nao Zanzibar itakuwa kama Rwanda kwa kukosa ardhi ya kutosha na hivyo itaongezea chachu ya siasa za chuki miongoni mwenu na kamwe Zanzibar haitaweza kustabilize na kujiendeleza Kiuchumi.

Kuvunjika kwa Muungano lazima kutakuwa na remifications zake na hakuna mwenye kuweza kujua ama kucontrol dynamics za baada ya Muungano. CUF wengi huangalia Muungano katika mizania ya imani kuwa bila ya Muungano ni rahisi wao kuchukua utawala wa Zanzibar na ili kufikia lengo hilo kila kitu ni halali na kuwa wanauwezo wa kucontrol dynamics za baada ya hapo. Hii ni falacy ambayo haina uhalisia wowote. Dynamics za baada ya muungano hasa katika suala mahusiano ya Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe na Wazanzibari na Watanganyika zitategemea zaidi na mchakato wa kuvunja Muungano kama unavyendelea sasa. Kama Muungano utavunjika kwa makubaliano ya pamoja ama kwa vitimbwi na chuki ambazo CUF na Wadau wao UAMSHO wanavyozipalilia hivi sasa ndio itakavyo shape dynamics za mahusiano yetu baada ya Muungano kuvunjika. Zaidi huu upatu wa CUF na UAMSHO unapelekea kufanya geopolitical calculations kati ya Tanganyika na Zanzibar nje ya Muungano kutokuwa za kidugu wala za kuaminiana.


Wapo wanaoijidanganya kuwa wanaweza kuchezea Muungano na baadae wataweza kutumia baadhi ya vyombo vya Muungano kuwasaidia kuwaepusha na majinamizi ya kuamalizana wao kwa wao. Wanajidanganya kuwa hata wakivunja Muungano bado mtaweza kutumia majeshi ya Muungano kuwa buffer kati yao msimalizane. Ujumbe ni kuwa katika harakati hizi zao za sasa ni muhimu wakajiandaa Vizuri na mpambano wa mahafidhina wa ASP MASALIA na MAZIMWI YA HIZBU peke yao kwani hakuna uhakika kuwa Watanganyika hasa baada ya kutukanwa, kulaaniwa na hata kuuawa hovyo kama hali inavyoendelea hivi sasa watakuwa tayari kujitolea muhanga huo kwa watu ambao walipokuwa pamoja hawakuonyesha kuwathamini!


Mahusiano ya Tanganyika na Zanzibar mara baada ya kuvunjika kwa Muungano pia yaategemea na Mtu ama Chama kitakachokuwa madarakani wakati huo na mara baada ya kuvunjika kwa Muungano huo. Kuna scenario moja ambayo wengi hawaiangalii. Hii ni scenario ya chama cha CUF kikitwaa madaraka Zanzibar na CHADEMA kutwaa madaraka upande wa Tanganyika. Sioni mahasimu hawa kisiasa na kijamii wanavyoweza kuwa na ustaarabu wa kuheshimiana na kudumisha historia ya udugu wetu. Wote hawa nawajua na prejudices za udini na nyinginezo miongoni mwa fikra zao kisiasa ni kubwa mno ambazo kuna uwezekano mkubwa ndizo zitakuwa zinaongoza misimamo yao kuhusiana na mahusiano ya watu wa pande zao. Kama Zanzibar ni CUF na Tanganyika ni CHADEMA, dyanamics za mahusiano yetu baada ya kuvunja Muungano zitakuwa tofauti sana. Hii ni scenario ambayo fanatics united against the Union upande wa Zanzibar wameshindwa kuiona hadi sasa ama wameamua kuidharau kutokana na kugubikwa zaidi na chuki zao na urari wao wa kurudisha enzi za kabla ya mapinduzi. Na scenario kama hii ndio inaniambia kuwa hii propaganda ya kuwaaminisha Wazanzibari kuwa mambo yatakuwa shwari tu baada ya kuvunja Muungano ni falacy ambayo ina hatari kubwa kwa maslahi ya Wazanzibari zaidi ya Watanganyika!

Ninachosema kuwa ndoto ile ya Zanzibar ile ya kabla ya Mapinduzi ni falacy kwani haiangalii mazingira ya wakati ule na inadharau kwa makusudi mazingira ya sasa! Na kusisitiza kuwa Zanzibar bado ina nafasi ya uhakika zaidi ndani ya Muungao na sio nje ya Muungano! Anyway, najua ni vigumu kurationalize na fanatics kwani kwao rationality ni jambo adimu sana lakini naamini wapo wenye upeo mkubwa wa kupima mambo ambao wataweza kuchambua masuala haya kwa utulivu zaidi kuliko hizi hisia za Ki-UAMSHO!

UFISADI KUSHIKA HATAMU?


UFISADI KUSHIKA HATAMU?
Ilyas, O.S

Ni muda mrefu sasa nimekuwa na mtazamo kuwa baada ya kuondokana na mfumo wa chama kushika hatamu, kuna mchakato umekuwa ukiandelezwa na wajanja kadhaa katika nchi yetu wenye nia ya kujenga mfumo mpya ambao ninaita MFUMO FISADI.

Matokeo na mchakato wa uchaguzi wa ndani unaolekea kkufika tamati katika Chama cha Mapinduzi una kila dalili za kufikia hatua ya juu ya mchakato huu wa ujenzi wa MFUMO FISADI kwa kufanikisha kusimika rasmi uhodhi wa chama hicho mikononi mwa vinara na makuwadi ama mawakala wa mfumo huo na hivyo kuwezesha kuhatamisha mfumo huo katika uongozi wa taifa letu.

MFUMO FISADI ni mfumo wenye nia ya kurasimisha na kuhalalisha mambo ambayo ni kunyume kabisa na misingi ya utaifa wetu kama ambavyo ilijengwa na kuachwa na Baba wa taifa letu Mwalimu Nyerere na wafuasi wake adhimu kuanzia alipokuwa TANU na baadaye CCM.

Ni mfumo ambao umekuwa ukijengwa ama kujengeka katika sura mbalimbali kama vile kujenga mfumo wa soko huria, kuendana na uhalisia na usasa wa kukubali kuwa hatuna ujanja isipokuwa kukumbatia misingi ya kibepari, umuhimu wa kujenga tabaka la kati, siasa za ushindani na kadhalika.

Wengi wetu kama si wote kwa namna moja ama nyingine tumeshiriki katika harakati hizi za kujenga MFUMO FISADI.  Ushiriki wetu upo katika ama katika kupanga ama kutekeleza mikakati yake kwa kujua ama kutokujua, kuhalalisha mambo yake kwa kutetea ama kuhalalisha chembechembe za ufisadi, kuwawezesha kiuchumi na kisiasa wale vinara na mawakala wa ujenzi wa MFUMO FISADI na vinginevyo.

Naomba niweke wazi kabla sijaingia ndani katika kuchambua na kuelezea mtazamo wangu kuhusu hili la ujenzi wa MFUMO FISADI na hatari tunayokumbana nayo sasa ambapo yawezekana tukawa katika hatua za mwisho katika kuusimika mfumo huu katika hatamu za nchi yetu.

MFUMO FISADI hauna chama wala wanachama. MFUMO FISADI hauna dini hii ama ile. MFUMO FISADI hauna kabila hili ama lile. MFUMO FISADI hauna rika hili ama lile. MFUMO FISADI hauna sekta moja ama nyingine. MFUMO FISADI hauna tabaka hili wala lile. MFUMO FISADI unaratibiwa, kujengwa na kulindwa na vyama vyote, sekta zote, dini zote, makabila yote, marika yote,matabaka yote na makundi mengine.

Kwa leo nitaongelea mfumo huu haramu katika muktadha wa kinachoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho hivi karibuni tumekuwa tukisikia na kuona mengi yakitokea na kusemwa katika mchakato wa chaguzi za ndani za chama hicho. Chama ambacho hadi sasa ndio chama tawala.

Moja ya kitu ambacho kimegeuka kama ndio kioo cha kupima mafanikio ama athari za uchaguzi huu kimekuwa ni jinsi gani nguvu ya pesa imeweza kuonyesha makucha yake katika uchaguzi huu.

Wengi tumekuwa tukiuangalia, kuupima na kuchanganua uchaguzi huu kama ni kioo cha kupima nani atakuwa mgombea na wengine hata kuamini kuwa ndiye atakayekuwa Rais ajaye.

Wengi tumekuwa tukiuangalia uchaguzi huu kama ishara ya ama kukirudisha chama katika mstari ama kukiacha kiteketee kwa kukitunuku rasmi kwa wale wanaonekana ama kujipambanua kama vinara na makuwadi wakuu wa ujenzi wa MFUMO FISADI.

Kwa kiasi fulani kuna ukweli wake, kwani kuna wengi ama wamegombea, wamechagua ama wamechaguliwa kutokana na kushawishiwa, kuwezeshwa ama kuahidiwa neema na ama wapambe au vigogo wenye kuamini kuwa wakishashinda ndani ya CCM basi Urais wa 2015 ni wao na kwamba ulaji utakaokuja nao utakuwa wao wa kugawana.

Hali hii inasikitisha na kutisha sana kwa mustakabali wa taifa letu. Inatia uchungu na kukatisha tamaa kwa mzalendo yeyote yule awe mwanachama wa chama hiki na hata yule ambaye sio mwanachama wake lakini anatambua umuhimu wa chama hiki kwa taifa letu haswa wakati huu wa miparaganyiko lukuki.

Harakati za kujenga MFUMO FISADI zimelenga katika kuwaangusha na kuwakatisha tamaa wale wote waliokiunga mkono chama cha CCM kutokana na Misingi yake imara ya kuweka mbele UTU wetu na kukiaacha chama mikononi mwa wale walioweka mbele IMANI YA NGUVU ZA FEDHA.

Wakati mwengine huwa najenga fikra kuwa yawezekana nguvu za harakati hizi za vinara na makuwadi wa ujenzi wa MFUMO FISADI ndani ya CCM zinatokana na nia ya dhati ya kukiondoa madarakani chama hiki. Kwao wao na wakubwa zao wanakiona chama hiki chenye misingi na historia adhimu ya utu, usawa na ukombozi wa ndani na nje ya mipaka yetu ni kama kizingiti dhidi ya nia yao ya kuhatamisha mfumo fisadi kwa jina la Ubepari.

Yawezekana, na inajionyesha wazi kuwa vinara na mawakala wa MFUMO FISADI huu ambao wengi tayari wana mahusiano maalum na vyama mbadala katika kinyang’anyiro cha utawala wa nchi, nia yao hasa sio kuhodhi madaraka ya chama hiki bali kukivunjilia mbali na baadaye kutumia vyama vyenye misingi ya kibepari ambavyo sasa vimevaa ngozi za hisia za kijamaa katika mpango kabambe wa kusimika rasmi MFUMO FISADI katika hatamu za utawala wa taifa letu.

Na hapa ndipo ninaona kuna tatizo kuu ya jinsi baadhi ya wanaojitambulisha kama wapambanaji dhidi ya ujenzi wa MFUMO FISADI wanakosea katika mapambano yao. Wengi wa wapambanji hawa, wa ndani na nje ya CCM, wamekuwa wakijikita zaidi katika mkakati wa kupanga safu za uongozi wa chama dhidi ya washindani wao ndani ya chama kama maandalizi ya mpambano mkuu ujao wa kumpata mgombea wa Urais kupitia chama chao.

Kwa kuweka mbele ushindani huu unaotegemea sana wa nguvu za fedha na sio imani ya wanachama kwa chama na viongozi wao kundi hili la wana CCM limeweza kujenga mazingira ambayo maadui ama washindani wao katika sakata la uhodhi wa chama wamepata urahisi wa kipropaganda na kimkakati.
Matokeo yake hata hao wenye kujipambanua kama CCM-Misingi ambao wakati fulani walijulikana kama MTANDAO MATUMAINI wanalazimika katika kuamini katika nguvu za fedha ili kupambana na washindani wao wa kundi la MTANDAO MASLAHI ambao kwao wao nguvu za fedha ndio msingi mkuu wa mafanikio yoyote.

Na hapa ndipo tunapokuja katika tatizo lingine katika hizi juhudi za kupambana na harakati za MFUMO FISADI ambazo kama mambo hayajabadilika sasa na sio baadaye basi ni wazi zitafanikiwa katika kushika hatamu za taifa letu.

Kitendo cha wana CCM wengine na hasa wale ninaowaita CCM ASILIA, yaani wana CCM wenye kuamini katika misingi ya chama na utaifa wetu, kuwaachia “WANAMTANDAO” kupambana wenyewe kwa wenyewe ni kosa kubwa linaloendelea ambalo nalo limewezesha ujenzi wa MFUMO FISADI na uwezekano wa mfumo huo kushika hatamu.

Mapambano ya dhati ya kukikomboa chama hiki ambacho kwa mtazamo wangu ni kuwa hadi sasa kimekosa mbadala makini wa kukibadili na kutegemea ukombozi wa kweli hayatafanikiwa kwa kuwaacha wanamtandao wenyewe kwa wenyewe kuhodhi uwanda wa mapambano.

Zaidi kuna uwezekano mkubwa wa hao tunaoamini kuwa wanapambana dhidi ya wingu la vinara na mawakala wa MFUMO FISADI kutoka katika kundi la MTANDAO MATUMAINI wakaishia kukubali kushindwa na kujiunga na timu ya ushindi ya wenzao. Tukumbuke kuwa hawa kwa pamoja walishirikiana katika kuendesha mapinduzi ya ndani ya chama hapo kabla na hivyo kuweka msingi wa ujenzi wa mfumo fisadi. Wakati wao wameamua kujitenga na jitihada za kujenga mfumo fisadi. Wenzao wa MTANDAO MASLAHI kwa nguvu zote wameamua kuubeba hadi watakapofanikiwa kuuhatamisha katika siasa na uongozi wa nchi yetu.

Mapambano ya dhati na yanayoweza kuirudisha CCM katika mstari na kukilinda dhidi ya nia mbaya za vinara na wapambe wa MFUMO FISADI ni yale yatakayojikita katika ajenda za DIRA, MISINGI na ITIKADI ya chama na sio vinginevyo.

Na hapa ndipo wana CCM, Wazee kwa Vijana wenye kuamini katika umuhimu wa dira, misingi na itikadi za chama hicho na taifa letu wanakuwa na umuhimu wake kwani ni wao tu na sio wengineo ndio watakaoweza kubadili mwenendo wa mpambano huu na hatima ya chama chao na taifa letu.

Ndani ya kiwingu cha habari mbaya za ushindi wa nguvu za fedha katika chaguzi hizi, pia kuna habari njema kiasi. Tofauti na chaguzi zilizopita, katika chaguzi hizi wapo baadhi ya wagombea waliofanikiwa kushinda hivi sasa ambao hapo nyuma walishindwa katika kila chaguzi walizokuwa wakishiriki kutokana na “ushamba” wao wa kutokuamini katika nguvu za fedha na kujikita katika kampeni za misingi na tamaduni za chama.

Ushindi wa hawa ambao wanaweza kuwa kidogo lakini wenye umuhimu unaonyesha matumaini na uwezekano wa nguvu za MISINGI ndani ya chama hiki na kutoa ujumbe kuwa hii kansa ya nguvu za fedha haijakikumba chama kizima. Hivyo endapo wengi zaidi wa aina hiyo wakiamua kusimama na kupambana, bado kuna uwezekano wa mpambano wa kuzuia uhodhi na hatimaye uwezekano wa Ufisadi kushika hatamu kufanikiwa kwa manufaa ya chama chao na taifa letu.

Ni mapambano yaliyojikita katika nguvu za misingi tu na sio nguvu za fedha ndio yatakayotuepusha na tishio la UFISADI KUSHIKA HATAMU na madhara yake mengineo. Tishio ambalo kuna uwezekano mkubwa wa kurasimishwa rasmi hivi karibuni tunapoelekea katika tamati ya chaguzi za ndani za CCM. Na kama ikishindikana kuzuia tishio hilo sasa basi wote kwa pamoja tujiandae na hasira za wapiga kura ambao wanaonyesha kila dalili za kukumbatia fikra ya “bora mbadala na liwalo na liwe” kama fimbo yao kwa wasaliti wa imani yao waliyoitunuku kwa miaka mingi ndani ya CCM.

Mwandishi ni Mkurugenzi wa kampuni ya ushauri wa masuala ya siasa, uongozi na maendeleo inayoitwa TANZANIANJEMA ADVISORY. Anapatikana omar.ilyas@tanzanianjema.com, www.omarilyas.com, twitter; @omarilyas