My uncle, my hero, my guardian, my role model, my Prof..

My uncle, my hero, my guardian, my role model, my Prof..

The family is at lost,
Tanzania is at lost,
ZANZIBAR is at lost,
Africa is at lost,
Palestine is at lost,
The left is at lost,
U should not leave us now Prof Othman...

Not now when we need ur wisdom,
Not now when we need ur patience,
Not now when we need ur ideals,
Not now when we need ur values,
Not now when we need ur integrity,
Not now when we need u most...

Yes u have given us the most,
Yes u have stand for us during the worst,
Yes u have taught the greatest
Yes u have inspired the best,
Yes u have done ur share,
But u shouldn't leave us the earliest.....

Ur the best,
Ur the greatest,
Ur the LEFT,
Ur the THA PANAFRICANIST,
Ur the teacher, ur the wisdom, ur the hope, ur the role model, ur THA comrade, ur the friend in the struggle...

28th June 2009

TANZANIA BORA HAITAJENGWA KWA STAILI YA BANDIKABANDUA

Ilyas, O.S @ August 2008

Katika miaka ya hivi karibuni nchi yetu imekuwa ikipita katika mitihani migumu inayotishia hatima yake kama taifa na hatima ya watanzania kwa ujumla. Mitihani ambayo kwa hali moja inatusaidia kupevuka kama taifa na kwa hali nyingine inatishia mustakabali wetu kama taifa.

Hali hii imefuata baada ya miaka kadhaa ya mtindo wa bandika bandua katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikumba taifa letu. Mtindo ambao kwa mantiki ya hali ilivyo sasa na dalili zinazonyesha huko tuendako, inatubidi kuachana nao haraka kabla hatujachelewa zaidi.

Changamoto tulizonazo ni lukuki ambazo ni wazi uzito wake utatuelemea. Hizi ni pamoja na tatizo la ufisadi, kuporomoka kwa maadili ya uongozi, kukua kwa hisia na kuongezeka kwa matendo ya kibaguzi miongoni mwetu, kustawi kwa matumizi ya siasa chafu, kupanuka kwa tofauti za kipato na kuongozeka kwa dalili za kuvunjika kwa muungano wetu. Kwa ujumla Tanzania ya sasa ina kila dalili mbaya ambayo hutokea katika jamii na matifa mbalimbali duniani zikiashiria kuvunjika kwa jamii hiyo ama tifa hilo.

Hata hivyo ni bahati mbaya kuwa mabadiliko yanayoendelea yamekuwa ni yale ya mtindo wa bandikabandua ambao unalenga zaidi katika kuendeleza uhalali wa tabaka tawala ambalo limejihodhisha nguvu zote za mabadiliko ya kisasa na kiuchumi badala ya kushughulikia mizizi ya changamoto hizo. Tumegubikwa na ujanjaujanja wa kushughulikia matokeo ya matatizo badala kuwa na uthubutu wa kushughulikia sababu ama mizizi ya matatizo hayo.

Hali ya ufisadi unaokomaa, kuporomoka kwa maadili ya uongozi, kukua kwa hisia na kuongezeka kwa matendo ya kibaguzi miongoni mwetu, kustawi kwa matumizi ya siasa chafu, kupanuka kwa tofauti za kipato na kuongozeka kwa dalili za kuvunjika kwa muungano wetu hayo yote ni matokeo ya matatizo na sio tatizo lenyewe.

Viongozi wetu ni lazima wakubali kuwa wakati umefika kuacha kupendelea hatua za kufunika kombe mwanawazimu apite. Viongozi wetu wanapaswa kukubali kuwa suluhu la matatizo au changamoto tunazokumbana nazo ni kuzungumzia, kukubaliana na kutekeleza makubaliano ya jinsi gani ya kuikoa Tanzania yetu na jinsi gani ya kuijenga kwa pamoja Tanzania iliyo bora kwa wote.

Ni wazi kuwa wakati umefika kwa viongozi wetu kuonyesha njia kwa watanzania kukaa kwa pamoja kujadili na kukubaliana njia mwafaka na ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotukabili. Na viongozi wetu wakishindwa kupata uthubutu wa kuongoza katika hili basi wajue wazi kuwa si kitambo sana watanzania watajitwalia mikononi mwao jukumu hilo.

Yapo mengi ambayo watanzania tunapaswa kuwa tayari kuyaongea na kukubaliana kwa ukweli na uwazi bila ya kuogopa.

Watanzania tunahitaji kupata nafasi ya kuongelea masuala kama aina ya mfumo uchumi tupaswao kufuata, Mfumo wa kisiasa, mfumo wa muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar, Muungano wa Afrika Mashariki, sifa na maadili ya viongozi, utawala na sheria, haki na wajibu wa kijamii na jinsi gani tunaweza kuwa na mfumo wa uwezeshaji wa makundi maalumu ya kijamii bila ya kusababisha kutokuaminiana miongoni mwetu.

Tunapaswa kukaa pamoja na kuongelea kuhusu mfumo wa elimu, mahusiano kati ya vyama vya kisiasa na dola, mfumo wa uchaguzi na uwakilishi, nafasi ya vyama vya kiraia katika jamii yetu na suala zima la mila na tamaduni za kitaifa nayo ni muhimu yaka angaliwa upya kwa pamoja. Vilevile masuala ya uraia na siasa, suala heshima na maelewano ya kijamii na nafasi za viongozi wa kijamii katika uongozi wa nchi yetu.

Ni wazi kuwa hali ilivyo sasa ni ushahidi tosha kuwa wakati umefika sasa wa kuamua ni upi kati ya mfumo wa kibepari ama kijamaa tupaswao kuufuata na kwa faida ipi na njia zipi. Ni wazi kuwa bila ya uoga wowote tunapaswa kuliongelea suala la muungano ambalo kwa miaka sasa limekuwa kama donda liogopwalo kutibiwa ama hata kuguswa. Tunapaswa kulijadili sasa kuliko kuchelewa zaidi hadi kufika mahala chembe ya busara na uongozi thabiti iliyosalia, ikakosekana kabisa na kuacha chuki na dharau kuchukua mkondo kama dalili zinavyo onyesha.

Ni wazi kuwa tunapaswa kujadili suala la maadili katika jamii yetu kwa mapana yake na si hili la muono wa karibu wa siasa na biashara. Suala la maadili ni suala muhimu pia si tu kwa viongozi ambao wanapaswa kuwa kioo cha jamii lakini pia wananchi kwa ujumla. Hivi sasa jamii yetu inageuka jamii ya kichokoraa ambapo kila mtu akishindana na mwenzie kuvunja sheria za nchi na jamii kwa ujumla. Maadili sio suala la watoto na vijana wetu tu kama tulivyozoe. Ni suala la wazee, wazazi, viongozi wakuu na wadogo, matajiri na masikini, wenyeji na wageni, na watawala na watawaliwa.

Mfumo wa kisiasa nao unahitaji kufumwa upya ili kuwezesha demokrasia ya kweli kuweza kukomaa na kusaidia kujenga Tanzania yenye neema. Kamwe hili halitwezekana kama tutaendela na stili ya bandikabandua ambayo inalenga kulinda maslahi na nafsai za kundi fulani tu bila ya kujali mapungufu yanayotokana na staili hiyo ambayo yanamsabibishia mtanzania kuendelea kuishi katika maisha ya unyonge yasiyo na tija ya kimaendeleo.

Uamuzi wa kufanya mjadala huu wa kisiasa unapaswa kufikiwa sasa ili kuweza kutumia nafasi hii tuliyojikuta tunayo bila ya kuchelewa. Ni muhimu kufanikisha mjadala huo mapema ili kupelekea kutungwa kwa katiba mpya kabla ya mwaka 2010 itakayowezesha kuwa na uchaguzi ambao umefanyika chini ya mfumo mpya ulioshirikisha na kukubalika na watanzania wote. Tukawa na katiba ambayo itapata uhalali wa kila mtanzania aliye na haki ya kupiga kura.

Umuhimu wa kufanya hivyo unatokana na kuwa watanzania sasa zaidi ya wakati mwengine wowote wana shauku kubwa ya kuijenga nchi yao kwa uthabiti zaidi kama ari mpya inavyosomeka na wengi

Lakini vilevile ni muhimu kuamua sasa kwani siasa ni fani inayosifika kwa kubadili mwenendo wakati wowote ule. Kama uamuzi huo hautachukuliwa sasa na kutumia mazingira ya kisiasa na kijamii tuliyonayo sasa basi inaweza ikatokea hapo baadae hali ikawa mbaya zaidi na kulazimisha mabadiliko hayo yatokee baada ya kupitia njia mbadala ambayo itakuwa janga kubwa kwa taifa letu.

Tusingoje tufikie hali ya siasa za magomvi na chuki kama zilizowafikisha ndugu zetu wa Burundi, Sudan, Zaire (Kongo DRC), Siera Leone, Liberia walipofikia ndio tufikirie hilo. Na wala tusisubiri hali ya kutatanisha iliyojengwa katika upande mmoja wa muungano wetu yaani visiwa vya Unguja na Pemba ndipo tufikirie kufanya hilo.

Badala ya kuendelea kupoteza muda, fedha, na hata maisha ya watanzania, viongozi wetu wanaotaka kukumbukwa kwa mapendo na sio chuki dhidi yao na vizazi vyao hapo baadae, wanapaswa kuwa na uthubutu wa kushinikiza na kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhus hatima ya nchi yetu sasa bila ya kuechelewa zaidi.

Mjadala bora na wa kujenga, daima hufanyika pale wahusika wanapokuwa katika hali ya mapendo, maelewano na heshima miongoni mwao.

Wapo wanaodhani kuwa kuanzisha mjadala kama huu ni kufungulia matatizo ambayo yanaweza kushindikana kudhibitiwa.

Wapo wanaogopa kufungulia mabadiliko kwa kuwa wanaamini hali iliyopo sasa ni hali ya kupita tu na wataweza kubadili mwelekeo na ukawa unaoridhisha kwa upande wao.
Hawa wote kwa kweli wamesahau kusoma nyakati. Mwenendo uliopo sasa hautabadilika bila ya kuwa tayari kuchukua uamuzi thabiti wa kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu masuala yote muhimu yanayotusibu.

Badala ya leo kuwa na mjadala wa kuwa na KADHI, kesho mjadala wa kuhamia Dodoma, kesho kushokutwa mjadala wa URAIA, mtondogoo mjadala wa Uongozi na Biashara, ni muhimu tukawa makini zaidi na kuanzisha mjadala wa kitaifa wa pamoja ambako haya yote na mengineyo yatajadiliwa kwa mpangilio madhumubuti na utakaopunguza mzigo kwa walipa kodi wa nchi yetu.

Ni mjadala wa kitaifa tu na sio maamuzi ya bandikabandua yanayolenga kulinda mfumo fisadi tulionao ndio yataweza kujenga Tanzania iliyo na neema kwa wote kama kauli mbiu ya chama tawala CCM.

Ni mjadala wa pamoja na sio ule wa wakubwa wachache tu utawezesha kuongeza utashi wa watanzania kulitumikia taifa lao kwa nguvu na uminifu zaidi. Ni utashi binafsi wa watanzania ndio utakaorudisha nidhamu binafsi na uzalendo miongoni mwa watanzania. Na bila ya kurudisha haya tutaendelea longolongo hadi kukuche lakini Tanzania bora kamwe haitawezekana.

Tanzania bora kwa wote itajengwa kwa kushirikisha watanzania wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kamwe haitajengwa kwa mtindo wa mabadiliko ya bandikabandua kama tunaoendeleza sasa.

CCM iende, Tanzania ibaki…



Na Ilyas, O.S @ July 2008

Tangia serikali ya CCM kuamua kwa shingo upande kuanzisha mfumo wa siasa za vyama vingi hapa nchini kumekuwa na taharuki kubwa ndani ya chama hiki katika kuchagua kati ya maslahi ya nchi na maslahi ya chama. Hali hii imejengwa kutokana na sababu mbalimbali ndani na nje ya chama hicho. Moja ya sababu kuu ni kubadilika kwa falsafa na mantiki ya kisiasa ya chama hicho kutoka katika kumuendeleza mtanzania hadi
kulinda na kuendeleza maslahi na nafasi ya tabaka tawala.

Ni wazi kuwa CCM ililazimika kukubali mfumo wa vyama vingi sio kwa sababu waliamini ni njia muafaka ya kulinda amani na umoja wa kitaifa. Ni wazi kuwa waiamua kufanya hivyo baada ya kung’amua kuwa bila ya kufanya hivyo wakati wakati ule basi mbeleni wangelazimika kufanya hivyo kwa matakwa na shurutisho za umma. Hali ambayo ni wazi isingewapa nafasi waliyonayo sasa ambapo bado wameweza kuhodhi nguvu za kuzuia mabadiliko ya kweli ambayo hayahakikishi usalama wa nafasi ya tabaka tawala.

Hali hii ya kubadilika kwa mantiki ya kisiasa ya CCM kutoka kujenga na kuendeleza taifa hadi kulinda nafasi ya tabaka tawala naweza kusema ndio mzizi mkuu wa matatizo lukuki tunayokumbana nayo hivi sasa. CCM wamekuwa wakijali zaidi kulinda mfumo wa kisiasa na kiuchumi tulionao ili kuepusha uwezekano wa kutokea mabadiliko ambayo yatadhoofisha nafasi ya kiutawala hata kama uhalali wao utatetereka.

Matatizo hayo ni pamoja na yale mapya ya ufisadi, uongozi mbovu, ubaguzi wa kidini, kikabila, kimapato, kirangi na hata kimaeneo na mengine ya tangia zamani kama lile la la hali na hatma ya muungano wetu. Hivi sasa wapo wanaochukulia haya kama ndio matatizo haswa na kuamua kutumia muda mwingi kufikiria, kuongea na hata kulalama mfululizo kama vile kuna uwezekano wa kuyashinda majanga haya bila ya kuyafikiria kwa mapana yake. Wapo wafanyao kosa hili bila ya kujua lakini wapo ambao wanajua wazi kuwa hali ya kufikiri hivyo ni tatizo kwani kunawezesha kuendelea kwa mfumo tulionao sasa ambao wao ni wafaidika.

Suala la ufisadi ndilo limekuwa agenda kuu ya watanzania hivi sasa kiasi cha kufikia mahala ambapo ndio imekuwa kama taswira ya CCM miongoni mwa watanzania walio wengi, wana CCM na wasio wanaCCM. Bahati mbaya agenda hii ya UFISADI badala ya kutufanya watanzania tufikirie zaidi na zaidi inaelekea kuwa imeanza kutudumaza kifikira. Agenda ya UFISADI imekuwa kama kiongeza mwendo muhimu cha kufisadisha mustakabali wa Tanzania yetu badala ya kulitetea na kulilinda taifa letu.

Wapo wengi wanaoshangaa ni jinsi gani CCM imeshindwa kulishughulikia suala hili katika njia ambayo sio tu ingeweza kuliokoa taifa letu lakini pia kuokoa nafasi ya chama hicho katika utawala wa nchi. Wengi wanaamini kuwa CCM chini ya uongozi wa Jakaya Kikwete kwa kutumia nafasi yake kama mwenyekiti wake lakini zaidi rais wa dola la Tanzania, inaweza kabisa kuchukua hatua madhubuti kuondokana na janga hili.

Hata hivyo ni wazi kuwa wanaoamini hilo wanashindwa kutambua jambo moja muhimu. Kwamba Chama Cha Mapinduzi hakijabadili tu falsafa yake kutoka katika ujamaa na kujitegemea kuelekea kusikojulikana, lakini pia kimebadili hata mantiki ya kisiasa kutoka kujenga na kuendeleza taifa hadi sasa kuwa ni kulinda nafasi ya tabaka tawala. Tabaka linalojumuisha walio wanachama na wasio wanachama wa chama hiki. CCM ya sasa sio ile ya zamani inayoamini hakuna maisha yenye umuhimu kama Tanzania. CCM ya sasa inaamini kuwa maslahi ya tabaka tawala ambalo limehodhiwa na kuneemeshwa na UFISADI yana umuhimu zaidi ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Ni kwa mantiki hii ndio sasa tunaona sio tu tumekuwa na ongwa la uongozi linalosababisha kushindwa kwa kuchukuliwa hatua dhidi ya wale wanaosadikiwa kuwa ni MAFISADI lakini pia sasa kuhatarisha hata muungano wetu ambao wapo walio apa kiapo cha kuulinda kwa hali yoyote ile.

Hivi karibuni kumekuwa na watu wakisema waziwazi na wengine ndani ya vikao vikuu vya CCM kuwa na tuachane na muungano. Wengi wao ni wale ambao agenda ya ufisadi imewakaba kooni hivyo wangelipenda kutumia kila njia kuondoa fokasi ya watanzania kutoka huko. Kwao wao ni bora muungano uende lakini madhambi yao yasahaulike, kwao wa ni bora Tanzania iende na CCM ibaki. Kwao wao Tanzania si chochote si lolote na CCM ndio kila kitu.

Inasikitisha na inatisha kuona kuwa hata wale walioapa mbele ya mungu na watanzania kuwa wataulinda muungano kwa nguvu zote ndio wanafikia kusema maneno kama acha muungano uende. Kwa maana nyingine wanasema acha Tanzania iende kwani ukikubali kuvunjika kwa muungano hakuna Tanzania. Inawezekana kutokana na mfumo wa muungano tulionao wapo wanaodhani kuwa tukirudisha Tanganyika bado tutabaki na Tanzania.

Inasikitisha sana kuwa watanzania tumefikishwa mahala kama hapa ambapo tupo tayari kuvunja nchi yetu ili mradi maslahi ya wachache yaendelee kulindwa. Inatisha mno kuona kuwa wafanyao haya ni wale ambao walibahatika kulelewa kwa misingi madhubuti ya muungano wetu. Yaani wale wa kizazi ambacho Mwalimu Nyerere alijitahidi kwa nguvu zake zote kukijenga katika fikira za utanzania zaidi ya yote. Hawa ndio wamekuwa wa kwanza kuusaliti muungano wetu.

Cha ajabu ni kuwa haohao wanaodiriki kusema wacha muungano uvunjike ndio kwa miaka wamekuwa mstari wa mbele kuwaita wale wanaojaribu kushauri njia muafaka za kushughulikia changamoto za muungano kuwa ni maadui wa muungano.

Katika hali kama hii ni wazi watanzania tunapaswa kujiuliza masuala kadhaa magumu yatakayotapatia majibu muhimu.

Hivi kama hawa wanafanya hivi itakuwaje kizazi chetu cha vijana wa sasa ambacho kimenyimwa malezi ya kitanzania na kukuzwa katika fikira za ubinafsi na ufisadi kitafanyaje ?

Jee, kukubali usaliti huu unaoendelea sasa wa kuthamini maslahi ya CCM zaidi ya TANZANIA yetu ndio kutatuwezesha kutatua matatizo na changamoto tulizonazo sasa?

Hivi ni kipi muhimu kati ya CCM na maslahi ya tabaka tawala ama Tanzania na maslahi ya watanzania ?

Wakati umefika wa watanzania kuamka na kuwaeleza wazi na kwa nguvu zote ndugu zetu hawa kuwa ni bora CCM iende lakini Tanzania ibaki. Uoga wao wa kuthubutu kuchukua maamuzi magumu ambayo yaweza kuhatarisha usalama wa maslahi yao lakini ukalinda na kundeleza ujenzi wa taifa letu hauna uhalali wa kuifikisha Tanzania yetu tulipoifikisha.

Wakati umefika kwa viongozi wetu ambao wangependa tuendelee kuwatofautisha wao na mafisadi mashuhuri tunaowanyoshea vidole sasa, kuthubutu kusimama kidete na kusema, ni bora CCM iende lakini Tanzania ibaki.

Tulimsaliti na tunaendelea kumsaliti Amina wetu….

I really thank u, from my heart, kuna vitu vingi ulinisaidia, kuna miongozo fulani, courage fulani na mambo mengine mengi, nimeona nikushukuru tu leo, asante na naappriciate as I said before, IT COMES FROM MY INSIDE, DEEPLY IN MY HEART, THANKS ONCE AGAIN, WISH U LUCKY, BE BLA$$ED. Amina chifupa mpakanjia.
Sender: +25577306944
Sent: 10:44:37
04/21/2007

Nimepigwa na butwaa, nimeishiwa na nguvu, sijui nifanyeje….najiuliza, hivi wapi ningelifanya zaidi na kwanini sikufanya mapema?

Hapo juu ni ujumbe alionitumia mtu ambaye karibia mwaka mmoja sasa nilimwita dada na yeye akaniita kaka. Ni Amina binti wa Chifupa. Huyu ni Amina niliye bahatika kumjua kwa kipindi cha karibia mwaka mmoja sasa. Katu sio Amina niliyekuwa nikijidai namjua miaka mitano kabla. Ni ujumbe ambao dada yangu amina alinitumia zaidi ya mara mbili katika usiku wa manane majira ya ughaibuni. Ni ujumbe ambao nilidharau kuujibu kwa siku mbili zaidi hadi Amina alipoamua kunipigia simu kunikumbusha kuhusu ujumbe huo. Sikujua kuwa ni ujumbe wa kwaheri ya milele.

Nakumbuka siku moja nikiwa mahala fulani naelekea nyumbani Tanzania nilimpigia simu rafiki yangu Zitto. Hii ilikuwa ni siku ambayo Rais Kikwete alihutubia Bunge letu kwa mara ya kwanza kama rais wa nne wa jamhuri yetu tukufu. Alitumia muda mwingi kunielezea ni jinsi gani alivyovutiwa na maudhui ya hotuba hiyo kitu ambacho kwa ninavyomjua rafiki yangu Zitto kilinishtua kiasi.

Katikati ya mazungumzo Zitto aliingiza suala la Amina. Akaniambia kuwa kwa muda mfupi aliofanya naye kazi anadhani kuwa Amina sio mtupu kama jamii inavyomtafsiri. Mimi nikamshauri kuwa jaribu kuwa naye karibu kumjua zaidi na kama kuna sehemu za kumsaidia basi asisite kufanya hilo kwa manufaa ya nchi yetu.

Mimi binafsi nilikuja kufunguliwa macho kutambua hazina iliyojificha ndani ya Amina siku alipopanda juu ya madhabahu ya kielemu katika ukumbi wa Nkurumah pale Chuo kikuu cha Dar Es Salaam. Hii ilikuwa ni miezi ya mwanzo ya mwaka 2006.

Mbele yangu nilishuhudia Amina tofauti kabisa na yule ambaye jamii ikiongozwa na wana udaku walivyokuwa wakimtafsiri. Mbele yangu nilimuona kijana mdogo aliyejawa na ushujaa, upendo wa dhati kwa nchi yake na zaidi mwenye kipaji cha hali ya juu cha siasa. Mbele yangu nilimwona kijana ambaye sio tu amejawa na uthubutu wa kujaribu lakini pia aliyekuwa na ndoto ya kufanikisha mambo makubwa katika maisha yake.
Mara baada ya Amina na wakina dada wengine mashujaa waliokuwepo pale kumaliza kutoa ushuhuda wao kuhusu nafasi ya mwanamke katika siasa za nchi yetu, nililazimika kusimama ili nami nitoe ushuhuda wangu.

Nilianza kwa kumuomba radhi dada Amina. Bila ya kusita nilimtaka radhi kutokana na mimi kuwa mmoja wa wale watanzania waliokubali kuamini kashfa, uzandiki, na zaidi unyanyapaa ambao baadhi wanajamii walikuwa wakimfanyia.Baada ya hilo nikamuahidi urafiki naye ili tuweze kubadilishana mawazo na ujuzi ambao niliamini kwa upande wake ungeweza kumwongezea pale alipopungukiwa na mimi kuongeza pale nilopopungukiwa na vilevile kutimiza lengo langu la kusaidia vijana wenzangu haswa kina dada kama Amina kufanikiwa ndoto zao katika ushiriki wa kujenga taifa letu kwa pamoja.

Baada ya muda mfupi wa kujuana na zaidi kufaidika na tabia ya ucheshi na upendo mkubwa aliokuwa nao Amina, nikajikuta naongeza rafiki mwingine wa karibu katika maisha yangu ambaye kwa kweli alifikia kuwa mdogo wangu mpendwa.

Mdogo wangu ambaye leo nasikitika kuwa sikufanya vya kutosha kwake yeye kunishukuru kama alivyofanya katika ujumbe huo hapo juu.

Mdogo wangu ambaye namshukuru mwenyezi mungu kwa kunipa nafasi ya kumtaka radhi kutokana na makosa niliyofanya hapo mwanzoni ya kumtafsiri vibaya.

Mdogo ambaye amenifundisha umuhimu wa kutowatafsiri na kuwahukumu watu ambao tunadhani tunawajua kumbe ukweli ni kuwa hatuwajui.

Mdogo ambaye alinifundisha kumpokea mtu kama alivyo na sio kama tunavyotaka sisi awe.
Mdogo ambaye kwa muda mfupi sana amenifunza mengi kuhusu dunia hii kuzidi hata niliyojifunza katika zaidi ya miaka ishirini niliyokaa darasani.

Muda uliruhusu machache kushauriana. Lakini katika muda huo kiduchu Amina alitokea kuwa mwalimu na mwanafunzi mzuri kwangu na mwenye kuthamini mawazo yangu kama ambavyo alivyokuwa akithamini na kutetea mawazo yake kwa uthabiti mkubwa. Amina hakuwa mtu wa kuburuzwa na wala kutishwa.

Ushahidi unaonyesha kuwa kadiri alivyokuwa akitishwa ndivyo alizidi kuwa na ushujaa wa kusimama na kuongea yale ambayo aliamini kuwa yanapaswa kusemwa bila ya kujali kama wale aliokuwa akiwasemea wanamshukuru ama kumdhihaki.

Siku moja nilikuwa nikipata nasaha za mzee mmoja ambaye alimjua mzazi wangu wakati akiwa hai. Mwishoni mwa mazungumzo aliniasa kitu kimoja. Mzee huyu aliniasa kuwa katika dunia yetu Mawalii huja kwa sura nyingi na mara nyingi huja katika sura ambayo wengi hawakutegemea na hivyo kushindwa kutambua bahati waliyoletewa na mwenyezi mungu hadi pale atakapotoweka. Waseme watakayosema lakini kwangu nathubutu kuamini kuwa Amina alikuwa ni walii aliyeletwa duniani kupima ubinadamu wetu na kutuelimisha mengi.Walii aliyekuja na ujumbe wa kuthubutu kupambana na moudhi yaliyoigubika jamii yetu bila ya woga.

Katika maisha yake tangia akiwa kigori hadi alipokabidhiwa majukumu makubwa ya kutetea maslahi ya vijana wenzake katika chama tawala, Amina amekumbwa na mengi. Kama ni mitihani basi ni wazi Amina alipata mitihani mikubwa sana. Mtihani mmojawapo ulikuwa ni ule wa wanajamii aliokuwa akiwapenda na kujitolea muhanga kuwatetea kujenga mazoea ya kumdharau, kumdhihaki, kumkejeli, kumbeza na zaidi kutomwamini katika katika uthabiti wake wa kutetea maslahi yao.

Wengi walikuwa wakimwona Amina kama mtu aliyekuwa amelewa na mafanikio. Wapo waliodhani kuwa Amina alikuwa akifurahia sana aina maisha aliyokuwa anakumbana nayo kila kukicha.

Masikini hawakujua kuwa ndani ya lile tabasamu murua lilojaa bashasha kulikuwa na mateso makubwa akilini na rohoni. Inasikitisha kuwa hata wale aliokuwa akiwaona kama kimbilio lake ndio kabisa hawakuweza kumpa nafasi ya kupunguza yaliyo rohoni.
Naamini kuwa kamwe sina haki ya kuwasema wanafamilia wake lakini nathubutu kuwasema wanajamii wengine wote. Hawa wakiwemo wanasiasa wenzake haswa wale wenziwe katika chama chake, waandishi wa habari, wanaharakati wa kijamii na hata wenzangu na mimi wasio na chao ambao Amina daima alikuwa akipenda kujinasabisha nao.

Kwa miaka mingi hawa wote nikiwemo na mimi tumekuwa tukimsaliti Amina kila kukicha. Wengi wetu tumekuwa tukimdharau, kumsimanga na hata kutengeneza na kushabikia maneno ya uzandiki ambayo yalikuwa yakitafuna furaha ya Amina kila uchao.

Wakati aliposimama kuwaongelea mamilioni ya watoto wa shule wanaotembea maili kadhaa bila ya viatu na wala uhakika wa kutia kitu tumboni siku nzima wawapo shuleni na hata wanaporudi nyumbani, tulimdhahaki na kumwambia anaongelea upuuzi. Eti amezidi umediocre. Aliposimama kuongelea maswahibu yanayowakuta watoto wa shule haswa katika wilaya za jiji la Dar es Salaam tulimwambia anataka kujijenga ili apate ubunge katika moja ya jimbo la jiji hilo. Waliodai kuwa ni jimbo lao hawakuacha kumtumia maonyo makalimakali.

Hata alipothubutu kusimama kuongelea manyang’au wanaojineemesha kwa kuwabebesha na kuwauzia maelfu wa vijana wenzetu sumu inayowamaliza kila siku, yaani madawa ya kulevya, tukamdhihaki kuwa ni mtoto mdogo hajui afanyalo. Wapo waliofikia kudai kuwa amefanya hivyo kumkomoa mumewe.

Ukweli ni kuwa hakuna aliyetaka kuamini kuwa ndani ya sura ile iliyojaa bashasha kuna uchungu wa dhati juu ya maslahi ya kijana mtanzania wa kawaida anayeathirika na hayo. Kijana wa kawaida ambaye tofauti na waheshimiwa wengine wengi katu Amina hakuacha kujinasabisha nao.

Mara dada yetu alipozimika kila mtu akaibuka kutafuta mchawi. Mara hili mara lile.
Kama kawaida ya wanadamu hakuna mwenye ubavu wa kuthubutu kujiangalia yeye binafsi ni vipi amechangia Dada yetu Amina kutuacha katika mazingira ambayo amefariki. Hakuna anayetka kung’amua ukweli kuwa wote kwa pamoja tulimsaliti Amina wetu. Wakati akituhitaji sisi tulikuwa tukimbeza na kumdharau. Wakati akihitaji mapendo yetu sisi tulimkejeli na kumzodoa.

Yote hayo aliyoyakusanya moyoni miaka nenda miaka rudi yakamalizwa kwa pigo la mwisho. Pigo ambalo lilimpelekea kuamini kuwa hata yule ambaye wazazi wake walitoa idhini ya kuwa mlinzi wa roho yake na mwili wake hapa duniani naye hakuweza kuwa naye pale alipokuwa akihitaji zaidi mapendao na uelewa zaidi. Na zaidi alipotaka kuyatoa yaliyokuwa yakimmaliza rohoni wapo waliothamini maslahi yao zaidi ya roho yake. Wote kwa pamoja tukaendela kumsaliti Amina wetu.

Inasikitisha zaidi kuona kuwa hata katika kifo chake tunaendelea kumsaliti Amina. Badala ya kujiuliza ni vipi tutaendeleza moto aliouwasha kuokoa vijana wenzetu na jamii yetu kwa ujumla, tunaendela kushabikia uzandiki, unafiki na udaku dhidi ya dada yetu Amina. Jamani tusitafute mchawi. Wengine walimalizia tu lakini sote tulimsaliti Amina wetu.

Kwa kweli natamani wote tungelimjua Amina wa kweli. Yule Amina niliyebahatika kumjua karibia mwaka mmoja tu kabla hajatuaga, Amina mwenye ucheshi wa haja. Amina mwenye nidhamu hata kwa wale aliokuwa akijua wanamdhihaki na kumdharau. Amina mwenye upendo wa kweli kwa watu wote, Amina asiyeogopa kusema na kufanya yale yote aliyoamini ni ya haki na yanapaswa kusemwa ama kutendwa. Amina mwenye uthubutu ambao wengi wetu tumeukosa. Amina nyota tuliyoizima hata kabla haijang'ara.

Mwenzenu natamani ningelifanya zaidi na zaidi kuonyesha urafiki wa kweli kwako dada yangu mpendwa Amina. Siamini kuwa eti nami sikuweza kuwa karibu nawe wakati ukihitaji zaidi urafiki wangu hata kwa uchanga wake. Amina dada yangu umetutoka lakini namshukuru mungu uliniaga kwa maneno ya upendo ingawa akati ule sikujua hilo.

Ni Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema tu ndiye ajuaye kuondoka kwako kuna funzo gani kwetu. Watasema yote lakini jua kuwa tupo tuliobahatika kukuamini na kukuthamini kwa dhati hata kama muumba hakutupa muda mrefu wa kufanya mengi. Nasema tumebahatika kwani ni nadra kwa dunia yetu hii kupata bahati ya kuitwa rafiki na walii kama wewe. Cheche ulizowasha kamwe hazitaenda bure. Bendera tutaipeperusha hadi mwisho sio kwa maneno bali kwa vitendo.

Msalimie kaka Chachage. Mwambie akusomee hadithi ya makuwadi wa soko huria. Mwambie ndoto yake ya ukombozi wa mlalahoi wa Tanzania yetu baada ya miaka kadhaa ya unyang’au wa soko huria inaelekea kutotimizika hivi karibuni. Mwambie kuwa yule mswahili mlalahai mwenzio Jakaya anahitaji makarama zaidi kutoka kwake huko alipo ili aweze kutimiza yale matumaini aliyokuwa nayo kwake kabla hajatuaga na kutuacha wapweke pale mlimani.

Namalizia kwa kunukuu ujumbe wa taarifa ya kifo chako kutoka kwa rafiki yetu kipenzi Zitto: AMINA AMETUTOKA….

WAANDISHI WETU NA UKUWADI WA UNYANG'AU

@14th July 2006, Published by Tanzania Daima Newspaper.

Comrade Chachage aliwaita makuwadi wa soko huria, mimi nawaita makuwadi wa unyang’au. Makala hii niliandika miezi mingi iliyopita lakini mengi yalinisababisha kutoiwakilisha kwa wapendwa watanzania. Kutangulia kwa kaka yangu na mwalimu wangu wa fikra changanuzi, kumenipa nguvu za kuwasilisha hoja yangu kwa watanzania, wanyonyaji kwa wanyoge.

Neno manyang’au lina tafsiri mbalimbali katika macho ya watanzania. Kwangu mimi unyang’au ni ile hali ya kufikiri na kutenda mambo ambayo yanaathiri mustakabali mzima wa mwananchi wa kawaida. Manyang’au ni wale wote wanaotenda mambo mbalimbali kwa maslahi ya uchu wao pekee bila ya kujali madhara makubwa ya matendo hayo kwa jamii.

Hawa ni wale walio katika nafasi zote na haswa za juu za kutoa maamuzi serikalini, kwenye vyama vya kisiasa na katika makundi mengine ya kijamii. Hapa nchini mwetu utawakuta katika kila pembe ya maisha yetu. Wapo wenye nguvu kisheria kuwemo katika kundi hilo na wapo walioweza kujipenyeza humo kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile uwezo wa kiuchumi na nafasi zao katika makundi ya kijamii.

Manyang’au wapo wakubwa na wadogo. Wapo wa kutoka nje na wapo wengi tunaotoka nao katika nchi yetu hii hii iliyojaa harufu na ladha ya umasikini wa kutupwa.
Unyang’au ni mfumo rasmi katika jamii yetu ukiwa na baraka za kisheria kama zile za takrima na nyinginezo nyingi.

Makuwadi wa unyang’au ni wengi na wapo katika sekta zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Wapo wanaojiita wafanyabiashara, wapo wanaojiita makada, wapo wanaojiita wasomi, wapo wanaojiita watumishi wa serikali na wengine wengi.
Wapo ambao wanafaidika kweli na unyang’au huo na wapo wale wanaodhani kuwa wanafaidika lakini kumbe wakipatacho ni makombo tu.

Wapo wanaojiona kuwa wanakundi halali katika mfumo wa kinyang’au na wapo waliomo humo kwa kujipendekeza na kuifaragua. Wapo waliomo humo kwa kupenda na wapo waliojikuta humo bila ya wao kujijua. Wakiulizwa wanadai ni kulazimika kutokana na mazingira yaliyopo.

Hawa wote wamekuwa tayari kuuza uwezo na ujuzi wao kifikira na kikazi kutetea, kusadifu na kulinda mfumo unaohalalisha unyang’au katika jamii yetu. Wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa kudhani kuwa wanaenda na wakati ambao unashurutisha kila mmoja wao kuwa na “mahusiano mazuri” na manyang’au wa nchi yetu na wale kutoka nje ya mipaka yetu.

Kwao wao, ili kuwa na kile wakionacho ni mafanikio kimaisha, ni lazima wajitumikishe kwa manyng’au wa nchi hii ambao wengi wao wana nguvu za ushawishi katika dola la nchi yetu.

Moja ya sifa ya pamoja ya ndugu zangu hao walio amua kukuwadia unyang’au ni kutoacha kulalamika kuhusu masahibu ya unyang’au katika jamii lakini kwa upande mwingine wanageuka kuwa ndio wasadifu na walinzi mahiri wa mfumo sababishi.Hapo mbeleni tutawachambua wote kwa makundi yao, katika makala hii ningependa kuongelea makuwadi waliomo katika sekta ya uandishi wa habari.

Fani ya uandishi ya habari ni moja ya nguzo muhimu za kiutawala ambazo jamii yoyote inayothamini umuhimu wa mfumo wa demokrasia inapaswa kuipa kipaumbela na umuhimu wa hali ya juu. Bahati mbaya katika Tanzania yetu fani hii imegeuka kuwa adui mkubwa wa demokrasia ya kweli na hata kutishia hatima ya mchakato mzima wa kuanzisha na kuboresha misingi ya kidemokrasia katika jamii yetu.

Kwa miaka mingi sasa, wachunguzi wa mambo ya siasa na jamii wamekuwa wakijadili nafasi ya fani ya uandishi wa habari katika nchi yetu. Wengi wamekuwa wakihoji uwezo wa wahusika wa fani hii. Wengi wamekuwa wakijaribu kuchambua uwezo wa kitaaluma wa wengi wa waandishi wetu ambao wameonekana kana kwamba huwa wakifanya kazi hiyo bila ya kuwa na sifa za kitaalamu zinazohitajika katika fani hiyo.

Kwa kweli ukiangalia historia ya nchi yetu na zaidi sera za serikali yetu kuhusiana na suala zima la elimu na sio katika fani ya uandishi wa habari tu, utang’amua kuwa mfumo mbovu wakutojali elimu bora ni moja ya sababu kuu ya tatizo hilo. Hata hivyo ukosefu wa nia thabiti, utashi wa kutetea haki zao na hata uzalendo wa kweli, ndugu zangu waandishi wa habari ambao mimi huwaita wahandisi wa habari, wamegeuka kuwa makuwadi wa unyang’au unaoendelea kuligubika taifa letu.

Ndugu zangu hawa ama kwa kupenda au kulazimika kimazingira wamegeuka kuwa watetezi na waficha maovu ya manyang’au wa nje na wa ndani.

Ndugu zangu hawa wameamua kuwa wasadifu wa manyang’au wa nchi yetu na mfumo wao. Kazi yao kubwa imekuwa ni kuhalalisha na kuusimika mfumo wa kinyang’au uliojengeka katika nchi yetu katika fikira za watanzania.

Waandishi wetu wamekuwa tayari kuwapaka rangi za kuvutia baadhi ya manyang’au wa nchi hii, wakubwa wao kwa wadogo, na kuwavika sura ya utakatifu mbele ya watanzania walio wengi.

Wakati vyama vya upinzani vikiwa vimenyang’anywa nguvu za kutekeleza ipasavyo jukumu kukosoa na kuwaeleza wananchi ubaya ama uwongo wakubwa wa mfumo wetu wa kinyang’au, ndugu zangu waandishi wameamua kuwaacha watanzania katika msitu wa giza.

Wanahabari wetu wanapaswa kujua kuwa ushabiki wa ajabu wanao uonyesha kwa watawala wetu ambao miongoni mwao wamelewa utamaduni wa kuwadhulumu watanzania haki zao za msingi, unalipeleka taifa letu katika mustakabali wa kutisha.

Ni wazi kuwa kama ndugu zetu wanahabari hawatazinduka na kuanza kutekeleza kwa dhati wajibu wao kwa wananchi, kuna hatari ya wajanjawajanja miongoni mwetu kutulazimisha kurudi rasmi katika enzi za siasa za chama kimoja.

Wakati wa uchaguzi na mchakato mzima ndani ya vyama kuelekea katika uchaguzi huo, tulishuhudia jinsi kujitokeza wazi kwa hali hii ya ukuwadi miongoni mwa ndugu zangu.
Mwanzoni wengi wetu tulidhani kuwa hilo lilikuwa ni zoezi muda mfupi la wachache kujipenyeza katika timu ya ushindi na wengine kutimiza wajibu wao kutoka kwa wafadhili wao waliogeuka kuwa waajiri mbadala wao.

Lakini kwa hali inavyoendelea hivi sasa, inaelekea uozo uliopo ambao tayari umeshatanda katika nyanja zote za fani hii ya uandishi. Hii ni kuanzia wamililiki, waajiri, wahariri, waandishi wa kawaida na hata wasomaji umesababisha donda ndugu ambalo linaweza likashindwa kutibika.

Wapo waliofikia hata kubeza na kudhihaki juhudi za wachache waliokubali kuchukua jukumu la kuendeleza mapambano ya kutukomboa katika mfumo butu wa utawala wa chama kimoja. Tabia hii ya kuwakuwadia manyang’au kwa kutumia wino ni kuwageuza watanzania kuwa kama bendera inayofuata upepo ambayo haina uwezo wa kuhoji maamuzi yanayobariki unyang’au katika jamii yetu.

Kukuwadia unyang’au wa aina yoyote na mahala popote ni kujidanganya nafsi zetu. Sumu ya unyang’au kamwe haiachi kumdhuru kila mtu katika jamii husika na hata ile ya mbali. Hata kama madhara yake hayataonekana kwa mhusika binafsi wakati wa uhai wake, ni lazima itamsibu huko aendako kupitia kwa vizazi vyake.

Hivyo, ni wajibu wa ndugu zangu waandishi wa habari kuwa wa mwanzo kujinasua katika laana ya unyang’au kwa kuacha kuwakuwadia makuwadi wetu, wa ndani na nje na kuwaonya wengine wa aina yao katika sekta zengine.

MWANZO WA SAFARI YA MWISHO YA CCM

@2005..Published by by a local Tanzania Newspaper

Ni ukweli usiopingika kuwa matokeo ya uchaguzi wa mgombea wa nafasi ya urais katika Chama Cha Mapinduzi yameweza kuliepusha kundi hili kisiasa katika hatari ya kugawanyika kwa kasi kama ilivyokuwa ikionekana awali.

Naongelea dhana ya kugawanyika kwa kasi tu, kwa kuwa nina uhakika kuwa mwenendo mzima wa siasa za uchaguzi huo na mambo kadhaa yaliyojitokeza katika siku za mwisho za shughuli hizo ndani ya chama hicho, zimeleta mgawanyiko mkubwa na wa hatari zaidi utakaodumu daima.

Hata kama kwa njia za ajabu mno ndugu hawa wameweza kumchagua mtu ambaye kwa maoni yao wana uhakika wa kuendelea kutawala watazania kwa miongo kadhaa ijayo.
Ni wazi kuwa CCM ya sasa si ile tena iliyokuwa ikiwavutia watu kwa utulivu wake, uongozi wa kufuata maadili ya utanzania, falsafa zake zenye kujali utu, kupinga ubaguzi na mengineyo mengi mazuri yaliyokuwa yakitofautisha chama hiki na makundi mengine ya kisiasa.

Chama cha mapinduzi kama ilivyo kwa vyama vingine vikubwa tawala barani afrika, kimepitia mabadiliko mbalimbali hadi kufikia sasa.Mabadiliko hayo yameanzia kutoka kuwa chama cha ukombozi, kikaja kuwa chama cha kujenga utaifa na baadaye kuwa chama cha kuimarisha uchumi na kuboresha maisha ya watanzania kabla ya sasa kugeuka kuwa chama cha kuhakikisha kuendelea kubaki madarakani kwa tabaka tawala.

Mbadiliko huu umekuja kutokana na nguvu mbalimbali za kimfumo na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani ambayo yamepelekea washika dau wa chama hiki ambao mwanzo walijitahidi kukabiliana vilivyo, kuamua kufuata mkondo wa mabadiliko ili kuweza kuendelea kuongoza taifa hili.

Mfano mkubwa wa mabadiliko haya nje ya mipaka yetu ni chama cha Labour cha Uingereza kinachoongozwa na mwanasiasa “kijana” machachari Tony Blair. Chama ambacho wiki iliyopita kilipata pigo kubwa la kisiasa kwa kupoteza viti vingi katika baraza la wanaojiita wawakilishi wa makabwela.

Kama ilivyokuwa CCM, chama hiki kilianzishwa kama kundi la kutetea wafanyakazi na makabwela wa Taifa hilo la kibwanyenye. Na mama ilivyo kwa vyama vingi vya aina hii duniani, chama cha Labour kama kilivyokuwa CCM hapo awali, kilikuwa ni chama kinachoendeshwa na misingi na falsafa madhubuti za kutetea wanyonge.

Falsafa na misingi ambayo walijiwekea ili kila anayetaka kuchaguliwa kukiongoza chama hicho na hivyo kugombea nafasi ya kuongoza serikali ya Uingereza alipaswa kuonyesha wazi kuwa ni mfuasi makini na mwaminifu wa misingi hiyo kwa kauli thabiti na vitendo.
Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani yalikipelekea chama hicho kukosa mvuto wa kuaminiwa na wapiga kura wengi na hivyo kuwekwa kando katika kuingoza Uingereza kwa miaka kadhaa.

Hali hiyo iliwapelekea kundi dogo la wanasiasa vijana machachari wa chama hicho akiwemo bwana.. Mandelson ambaye aliwahi kuishi Musoma, Tanzania kwa miaka kadhaa akitafiti siasa ya ujama na kujitegemea na utaalamu wa kiuongozi wa baba wa Taifa, kuja na mbinu mpya walioita LABOUR MPYA.

Tofauti na Labour ya kihistoria, New Labour kama ilivyo CCM hivi sasa, ililenga matumizi ya siasa za kubabaisha zilizo tofauti na misingi na falsafa asilia ya chama hicho ili kuweza kuwalaghai wapiga kura waliokitupa, kukichagua na kukirudisha madarakani.

Kwao wao ni kuwa mara baada ya kurudi madarakani wangeweza kuzirejesha siasa makini za kihistoria za chama hicho na hivyo kuendeleza misingi na falsafa zake asilia kwa mtindo unaoendana na wakati uliopo.

Kama hapo baadae ilivyokuwa kwa upande wa wahafidhina wa chama cha Republican cha Marekani walipomchagua George W Bush kuwauzia fikira zao za kulinda nafasi ya ubabe wa marekani duniani, Mandelson na wenzake waliamua kumchagua mwanasiasa machachari aliyekuwa akikubalika wakati huo yaani Tony Blair kuongoza mpango huo.
Matokeo yake ni hali inayonekana hivi sasa huko Uingereza. Sio tu chama hicho kimegeuka kuwa cha kinyang’au zaidi kuliko chama cha mahafidhina wa kijadi cha Conservative, hivi sasa kinaelekea kaburini kwa mwendo wa kasi mno. Kitu pekee kinachowezesha wao kuwa madarakani hadi hivi leo sio uhalali wa kidhati kutoka kwa wananchi isipokuwa propaganda za kuwapumbaza wapiga kura. Propaganda zinazolenga kuwaweka mateka Waingereza walio wengi kwa kutumia dhana ya kuwa hakuna mwengine mwenye mvuto kama yeye anayeweza kuwalinda waingereza kwa madhila makubwa zidi kutoka kwa chama cha wahafidhina.

Ukiangalia mlolongo mzima wa historia ya chama cha Labour ni wazi kuwa kuna mambo yanayoshabihiana na hali inayojikita ndani ya chama cha mapinduzi.

Hapo zamani hata baada ya kuruhusu siasa za vyama vingi chama cha mapinduzi kilikuwa ni chama kilichokuwa kinapata wafuasi wengi kutokana na hali ya kuwa wengi wa wananchi hawa walikuwa wakijinasabisha na misingi na falsafa za chama hicho.

Hata kama wengi walikuwa wakikatishwa tamaa na matendo ya viongozi walio wengi wa chama hicho ambayo ni tofauti na sura yake asili, kuwepo kwa umakini wa kimaamuzi haswa yale makubwa kama vile mtiririko mzima wa kubadilishana madaraka kuliwapa faraja wanachi wengi waliokuwa wanaendelea kukata tamaa.

Hili na lile la kuwepo kwa baadhi ya viongozi wachache ambao tofauti na walio wengi, kauli zao na matendo yao yenye kuonyesha kuendelea kwao kuamini misingi na falsafa asilia za chama hicho, kuliwapa moyo wa matumaini watanzania walio wengi, wanachama na wasio wanachama.

Hali hii iliweza kuwazuia wanachama waaminifu wa chama hicho vijana kwa wazee, wenye sifa za umakini wa hali ya juu kutokisusa ama kutohama chama hicho kwa muda mrefu sasa. Wengi hawa walikuwa bado wakiamini kuwa ipo siku chama hiki kitapata uongozi imara na makini utakaowezesha kurudisha chama na nchi yetu katika mstari ulionyooka na kuachana na siasa za sera za kukurupuka kwa minajili ya kuwalaghai wapiga kura tu. Ndio maana hata hivi karibuni tulipokuwa tukishuhudia siasa chafu za kupindukia mipaka ya utanzania na ubinadamu kwa ujumla, bado walikuwepo waliukuwa wakiamini kuwa mwishoni busara za uongozi wa chama hicho zingesimama na kurekebisha mambo.

Hata hivyo hilo halikutuokea na waliukuwa wakiaminiwa kwa kazi hiyo ama walinyamaza kimya, walinyamazishwa au waliamua kukubali yaishe na kubariki siasa chafu zenye kukiuka misingi madhubuti ya chama hicho kutawala maamuzi ya vikao vyake vikuu.
Yote yanaweza kufumbiwa macho lakini kitendo cha Mwenyekiti wa chama hicho kuamua kuzuia taarifa ya siri ya sekretarieti ya maadili ya chama hicho iliyokuwa ikielezea vigezo vya kimaadili vya wagombea wote kuzungumziwa na wanakamati kuu ni kosa kubwa la kihistoria.

Maelezo kuwa wote wametoa rushwa hivyo wote sawa, kwa kweli ni upuuzi wa hali ya juu ambao kamwe hakuna aliyefikiri kuna siku mwenyekiti wa chama hicho anaweza akaufanya (sasa tunajua ni kwa nini).Hata kama historia na tafiti mbalimbali zinaonyesha wazi kuwa chama hiki kimekuwa kikumbatia rushwa na kiongozi wake kuishia kutoa vitisho vya mdomo tu, lakini inapofika mkuu huyo anahalalisha uchafu huo ambao ni tofauti na nguzo kuu asili za chama hicho ati kwa kuepusha kubomoka kwa chama, ni wazi safari ya mwisho imewadia.

Lingine ni lile la kuruhusu wanakamati kuu ambao wengine ni viongozi waandamizi bila ya aibu kutumia siasa ya ubaguzi ndani ya vikao vikuu kama hivyo. Pale wahuni kadhaa walipokuwa wakitumia siasa haramu na chafu kama hizo kwenye vyombo mbalimbali vya habari, halali na haramu, baadhi ya watanzania makini ambao ndio walikuwa ngome ya mwisho wa chama hiki waliweza kuelewa na kuvumilia.

Lakini pale anapokuja mtu mkubwa kama Waziri mwandamizi akasimama akipinga kuchaguliwa kwa fulani kwa kuwa amezaliwa akiwa na mchanganyo wa kabila au rangi fulani, na wakubwa hao wakapigia makofi, kunyamaza au mwenyekiti akahalalisha jambo hilo kama ni demokrasia, kwa kweli hiyo ni ishara mbaya mno.

Vilevile ni dalili mbaya pale wakuu wa chama hicho na haswa wazee wa busara waliokuwa katika makuzi ya siasa asilia za chama hicho na wengine kushiriki katika ujenzi wake wanapokuwa tayari kuweka kando maslahi ya watanzania kwa ujumla na kujali ushindi wa chama tu kama dira yao kuu ya kufanya maamuzi.

Ushindi ambao kwao wao ni muhimu tu kutokana na uhakikisho wa kuwa wao na vizazi vyao vitaendelea kuwa madarakani daima milele hata kama ishara zinaonyesha kupotea kabisa kwa utaifa wetu ambao ndio umekuwa nguzo yetu muhimu kama nchi na jamii staarabu.
Kwa ujumla ingawa wengi wanaamini kuwa chama cha mapinduzi kimeweza kuvuka mtihani mkubwa kwa ushindi, ni wazi kuwa ushindi huo unaendana na kujisimika rasmi kwa siasa mpya zisizojali misingi na falsafa asilia za chama hicho ambazo kwa kweli ndizo zimekuwa nguzo kuu za kuendelea kwa uimara wake wakati wote huu.

Siasa hizi mpya ambazo zinalenga wingi wa kura tu na sio mipango madhubuti ya muda mrefu yenye kulenga kustawisha jamii kwa mapana na marefu daima haziwezi kuifanya CCM kuendelea kuwa chama cheney mvuto asili ambo hata kama mambo hayaenda sawa wananchi wataendelea kukiamini na kikihamini.

Siasa hizi zinazofuata mbinu za soko huria ambazo zinalenga kumnadi mtu kama bidhaa nyingine sokoni zinafanya chama hicho kutegemea uhalali wa umaarufu wa mwanasiasa huyo tu na sio mapenzi na imani juu ya chama hicho.

Bahati mbaya umaarufu huu unajengwa na matarajio hewa ndani ya mioyo ya wananchi, ambayo ama kwa mapungufu ya kiutendaji ya mwanasiasa huyo au ya kimfumo ni vigumu kuyafanikisha.

Hivyo basi kukifanya chama hicho kuwa mateka wa mwanasiasa huyo na wajanja wachache waliomzunguka wanye uwezo wa kucheza na akili za wapiga kura kwa muda Fulani tu.
Hawa huwezesha hilo kwa kutumia mbinu mbalimbali za kihadaa ambazo daima huishia ama kuvuruga jamii au kuchokwa na wapiga kura.

Wapo wanaofikiri kuwa kupatikana kwa mgombea na baadaye kiongozi mwenye mvuto kama aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa ni silaha muhimu ya kuhakikisha uimara wa chama hiki.

Mimi nasema ndio lakini ni kwa muda mfupi tu na hiyo hiyo ndiyo silaha ya kujiangamiza kwa muda mrefu.

Ni dhahirikuwa ushindi uliopatikana Dodoma hivi karibuni ni mwanzo wa safari isiyo rasmi ya mwisho ya chama cha mapinduzi.

NINI FALSAFA YA MAPINDUZI YA CHIMWAGA 2005?

@2005..Published by Mtanzania Jumapili soon after CCM nomination process.

Baada ya miaka mingi ya Chama Cha Mapinduzi kudorora na kukosa chachandu zinazoendana na jina lake hatimaye katika hali ya kustajabisha kabisa Mapinduzi mengine ya ndani yametokea.

Ni ukweli usiofichika kuwa moja ya mbinu iliyotumika katika kuhakikisha kuwa mheshimiwa Jakaya Kikwete anashinda mchakamchaka wa kuchaguliwa kugombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi, ni kauli mbiu inayosema ARI MPYA, KASI MPYA NA NGUVU MPYA.


Lakini kubwa zaidi ni kuwa kauli mbiu hii ilikuwa na bado inaendelea kuashiria kufanyika kwa mapinduzi makubwa ndani ya CCM. Mapinduzi ambayo kwa kiasi fulani yamefanikiwa ingawa mengi bado yatakiwa kufanyika.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na kukua kwa mtindo wa vijana wengi wa kizazi kipya kuvaa fulana zenye picha za viongozi mbalimbali duniani ambao wamekuwa wakihusishwa na mapambano mbalimbali ya kimapinduzi.

Miongoni mwao, picha ya Hayati Ernesto Che Guevara ndio imekuwa maarufu zaidi kama ilivyo katika jamii zengine za vijana katika nchi mbalimbali duniani.

Kwa wale wasiomjua Che Guavara, huyu ni mwanamapinduzi mwenye asili ya Argentina kule Amerika ya kusini.

Mwanamapinduzi huyo amefanya mengi katika kupigania kuundwa kwa jamii isiyo na matabaka na inayoheshimu thamani ya utu wa kila mtu.

Katika jitihada zake hizo ambazo zilikuwa zikiongozwa na dira ya falsafa ya mapinduzi ya kijamaa, Che Guevara alijitolea muhanga maisha yake kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano ya ukombozi kuondoa tawala mbalimbali za kibepari uchwara katika pande zote za dunia.

Ni yeye ndiye akiwa begabega kwa bega na kiongozi wa CUBA, Mwanamapinduzi Fidel Castro katika mapinduzi ya CUBA. Mnamo maka 1959, Che aliongoza majeshi ya walalahoi wa nchi hiyo kuuteka mji wa Havana na kusimika utawala wa kimapinduzi wa kijamaa unaotawala hadi hivi sasa.

Ni Che ndiye aliyeamua kuacha maisha ya anasa ya kuwa waziri muhimu katika seriakali ya CUBA na kuja afrika kusaidiana na wanamapinduzi kadhaa kama Mzee Ben Bella wa FNL ya Algeria. Baadaye alijipenyeza hadi Kigoma, Tanzania alikokwenda kusaidiana na Marehemu Mzee Kabila wa DRC.

Wakati huo Mzee Kabila alikuwa akiongoza kikundi cha wanamapinduzi wanaofuata falsafa za kijamaa waliokuwa wakijaribu kurudisha madarakani masalia ya utawala wa mwanamapinduzi mwengine, Hayati Patrice Lumbumba.

Baada ya hapo, Che alienda nchi zengine zilizokuwa zikikabiliwa na unyang’au wa tawala za kibepari ambazo zilikuwa zikiongozwa na viongozi vibaraka wa Marekani, akiwa na mkoba wake uliojaa fikira za kimapinduzi.

Maisha ya mwanamapinduzi huyu yaliishia mikononi mwa mawakala wa shirika la ujasusi la marekani CIA waliokuwa wakisaidia kuulinda utawala wa kinyang’au wa René Barrientos huko Bolivia, amerika ya kusini.

Inasemekana kuwa picha ya sura ya Che Guevara ndio picha maarufu zaidi ya binadamu yeyote kuchapwa katika vitu mbalimbali duniani.

Mimi ni moja wa vijana ambaye nimetokea kuvutiwa sana na kuvaa fulana zenye picha za wanamapinduzi hawa akiwe,o Che Guevara na kwa kweli huwa najisikia vizuri sana ninapokuwa katika vazi hilo.Lakini hilo ni tofauti na mimi ambaye nilianza kuvaa fulana zenye picha za wanamapinduzi hawa mara baada ya kusoma na kuwafahamu katika vitabu mbalimbali.

Wengi wa vijana wenzangu nchini wamekuwa wakivaa mavazi ya aina hii bila hata kujua mtu huyo wanayemshabikia ni nani na ni nini alichokuwa anakiamini na kukisimamia katika maisha yake.

Wengi hawajui kabisa ni falsafa gani ambayo Che Guevara alikuwa akiamini na jinsi gani alivyokuwa akichukia kwa ukweli kabisa madhila yaliyokuwa yakimsulubu mwanadamu yeyote yule katika pande zote za dunia.

Hali kama hii imekuwa ikionekana katika kinyang’anyiro cha na nafasi ya kugombea urais ndani na nje ya CCM.

Katika CCM kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa na mabadiliko ya sura katika ngazi za uongozi wa chama hicho kuanzia kata hadi Taifa. Kuna wakati mabadiliko haya yalikuwa na baraka zote za viongozi wa chama hicho haswa wale wazee kama “Komredi” Kingunge Ngombale Mwiru, Mzee Rashid Kawawa, Mzee John Malecela na wengineo.

Kwao wao waliamini kwa dhati kuwa damu mpya inahitajika ili kuhakikisha kuwa chama kinaendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya jamii ya watanzania ambayo vijana ndio wawakilishi wakuu.

Bahati mbaya wazee hawa hawakuweka wazi vijana wa aina gani wanaotaka wao waaminiwe na kukabidhiwa dhamana ya kuwaongoza wenzao. Kosa ambalo sasa limewafanya wao kujikuta na mtihani mgumu wa kuamua ni nani haswa anapaswa kuaminiwa kupewa nafsi ya kuwa rais wan chi yetu kwa miaka mitano au kumi ijayo.Mtihani ambao ulihitimishwa kule Dodoma wiki iliyopita ambapo kwa kweli waliweza kuushinda kwa busara za hali ya juu.

Kwa kweli mimi kama kijana ningelipenda kuona mapinduzi haya yakitokea ndani ya chama hiki ili kukipa nguvu mpya na uhalali wa kutosha kutawala kwa ufanisi zaidi.

Lakini tatizo linakuja pale ambapo ninapoona kuwa dhana ya mapinduzi ndani ya chama ambayo hawa “vijana” wenzangu wanajaribu kuionesha inakuwa imekosa kiungo kikubwa muhimu.

Kiungo ambacho ni lazima kuwepo ili mapinduzi yeyote yale ya kisiasa au kijamii yawe yana manufaa kwa mwanachi wa kawaida aliyezingukwa na madhila yasiyo na kifani.

Kiungo hiki ni kuwepo kwa falsafa itakayoongoza mapinduzi hayo wakati wa kufanyika na baada ya kufanikiwa kubadili mfumo wa uongozi uliopo katika chama cha mapinduzi.

Siasa za kimapinduzi za mwalimu Nyerere ziliongozwa na fikira za mzee wetu huyu ambaye kwake aliheshimu kila mtu bila ya kujali kipato chake, kabila lake, rangi yake, elimu yake ama utashi wake kisiasa.

Fikira hizi zikiongozwa na kanuni binafsi za mwenendo wa kimaisha wa kiongozi huyu wetu mpendwa zenye kuendeshwa na maadili bora ya kiuongozi ndizo zilizopelekea kutangazwa kwa Azimio la Arusha.

Ni Azimio la Arusha ndilo lilionyesha wazi nafasi ya falsafa ya ujamaa na kujitegemea ambayo ndiyo iliyongoza mapinduzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ndani na nje ya chama cha TANU na baadaye CCM.

Bahati mbaya tofauti na mapinduzi ya wakati huo, mapinduzi tunayoshuhudia sasa kwa kweli yamekosa kabisa kuweka wazi falsafa ambayo inaonyesha kuwa ni mapinduzi yanayolenga masilahi za mtanzania wa kawaida na sio vinginevyo.

Hivi karibuni niliweza kupata habari nyeti ambazo zilikuwa zikionyesha wazi ni wajumbe gani ndani ya halmashauri kuu ya CCM ambao wanatambulika kama wafuasi wa mapinduzi haya.

Kwa kweli ukiangalia hao wafuasi tuu ni dhahiri kuwa wengi wao si tu wamekosa utashi wa dhati wa kimapinduzi lakini zaidi hata upeo wao wa siasa za kimapinduzi ni mdogo mno.

Wengi wao katika maisha yao ya kawaida wameonyesha kuwa makuwadi wakubwa wa siasa za kibepari uchwara zenye kujali maslahi binafsi.

Wengi wao kwao ukombozi wa mtanzania wa kawaida utatokea pale tuu wao na washirika wao wachache watakapoweza kupata madaraka zaidi.

Wao ni walokole wa dhana mpya ya utajirisho inayojikita katika nchi yetu.
Dhana ambayo inaelezea kuwa dawa ya umasikini katika nchi yetu ni kuwaacha wao wachache wenye nafasi katika uwanja wa siasa na maharamia wenzao waruka kodi watajirike zaidi bila kujali maslahi ya walio wengi.

Kwa kweli dhana hii ndio inayoendesha fikira za ndugu zangu hawa waliojivika kilemba cha uwanamapinduzi. Uwanamapinduzi unaodai kulenga ukombozi wa mimi na wewe na yule.
Si bure kwao wao kuyachukulia mapinduzi yao ni ya kirika na kamwe si kifikira.

Kama ni fikira za umimi na usisi zenye kusadifiwa na falsafa ya ubinafsi ambayo sidhani kama ni falsasfa muafaka ya kuwasaidia watanzania walio wengi ambao kwao wao tatizo si sura bali mfumo mzima wa kisiasa uliowazunguka.

Tatizo la wanamapinduzi hawa wa karne mpya ni kuwa wengi wao na zaiid wale walio karibu zaidi na chaguo lao wamekosa utashi wa kujiendeleza kifikra kwa kukosa ustarabu wa kujisomea.

Wengi wao hawana tofauti na vijana wenzangu niliowaelezea hapo juu ambao wanavaa fulana na nembo zinazonyesha wanamapinduzi mbalimbali bila hata kujua nini watu hao walikuwa wakisimamia

Hawa ni wanamapinduzi wa CNN, BBC na MNET ambao kwao wao shule pekee ya kimapinduzi ni ile wanayoiona katika vyanzo hivi vya habari vikionyesha kinachoitwa “mapinduzi” mbalimbali yanayotokea katika nchi za Ulaya ya mashariki na kati.

Hawajui kwamba mapinduzi haya hayana tofauti na mapinduzi kibwanyenye yaliyotokea Uingereza, Ufaransa, Marekani katika karne kadhaa zilizopita ambayo badala ya kumkomboa mwananchi wa kawaida kutoka katika unyang’au wa kikabaila, yalisimika makabaila wapya katika sura ya ubinafsi wa kibepari.

Mbaya zaidi ni kuwa tofauti na mapinduzi hayo ya kibwanyenye ambayo yalikuwa na mwongozo wa kifalsafa uliojengwa na ujuzi wa kisayansi, mapinduzi haya ya “vijana wa CCM” yamekosa ufanisi wa kisayansi na kielimu ambo ungeweza kujenga falsafa bora na makini.

Wengi wa wahubiri wa mapinduzi haya hawana elimu wala uzoefu ya kutosha ya siasa za kidunia ambazo zingeliwawezesha kuwa na dira imara ya kulinda mapinduzi hayo mara baada ya wao kuweza kutwaa madaraka ya dola.

Na wale walioweza kubahatika kujua umuhimu wa hilo kutokana na elimu kubwa waliyonayo wengi wao wamechoka kifikira na wameamua kusalimisha silaha zao na kujitwika majoho ya ubinafsi wakisema kubali yaishe.

Wao (wasomi wachache walio katika kundi hili) wamechoka na dharuba za kimaisha wanazozipata kuotokana na misimamo yao iliyokuwa ikilenga jamii bora zaidi.

Wameamua kujiunga na timu ya ushindi na kusema kubali yaishe, bora hichi kidogo kuliko kuendelea kukosa kabisa.

Kwa kifupi wote kwa pamoja wanaamini kuwa ili kurekebisha mambo kwa haraka zaidi ni bora kuja na dhana ya mapinduzi ya kirika yenye kulenga mbadiliko wa kisura katika nyanja za utawala bila ya kujali nafasi ya fikira mbadala katika mapinduzi hayo.

Fikira ambazo zinaonyesha umakini wa kiongozi wa mapinduzi hayo ambaye daima ndiye anayetakiwa kuhodhi mawazo dira ya mapinduzi hayo na yeye mwenyewe kuweza kuyauza kwa walengwa ili kupata uhalali wao.

Inapotokea kuwa kiongozi wa mapinduzi hayo anakosa au anashindwa kuweka wazi fikira za kiuanamapinduzi zenye kujengwa na kulindwa na fasafa makini ya ukombozi wa kweli, basi hizo ni dalili mbaya za matokea ya mapinduzi haya.

Na inapotokea kuwa kiongozi wa mapinduzi hayo anakuwa amezungukwa na manyang’au wenye uchu tu wa madaraka na utajirisho wao binafsi. Waliojaa kashfa za kuwadhulumu wananchi wa kawaida basi hiyo ni dalili ya hatari kubwa zaidi.

Hata kama kiongozi huyo amekuwa akilelewa kifikira tangia ujana wake, mazingira kama yaliyomzunguka kiongozi wa mapinduzi haya yanaonyesha uwezekano tofauti kidogo.

Uwezekano ambao historia za nchi kadhaa zilizowahi kufikwa na hali hiyo zinaonyehsa jinsi gani mapinduzi kama haya yameweza kupelekea kueseka, kuabika, kunyanyasika na kuuawa kwa mamilioni ya hao waliokuwa wakidhani wanapiganiwa.

Lakini yote haya yanatokea na makosa waliyofanya wazee hawa wa CCM ambao kuanzia miaka ya mwanzo ya tisini wamekuwa wakiruhusu kila mtu kuingia katika ngazi za uongozi za chama hicho. Bila ya kujali utashi wake wa kuwahudumia wananchi na sio kujihudumia yeye binafsi.

Mbaya zaidi inakuja pale ambapo chama hiki kilipoondoa umuhimu wa elimu ya maadili na ya kifalsafa ambayo hapo mwanzo kila anayejiunga na chama hicho na haswa vijana alipaswa kipitia.

Makosa haya yote na lile la chama chenyewe kukosa mwelekeo wa kifalsafa zaidi ya falsafa ya ubinafsi ndivyo vimepelekea chama hiki kujikuta njia panda katika kuamua kama jee mapinduzi ya aina hiyo ni ya muafaka au la.

Mungu ibariki Tanzania
Mungu ibariki afrika
Mapambano daima.

MPAMBANO KATI YA SIASA ZA UMAARUFU, UHAFIDHINA NA UMAKINI NDANI YA CCM: NINI HATMA YA MTANZANIA.

@2005..Published by RAI
NA ILYAS, O. S

Ilikuwa miaka, ikaja miezi na sasa imebakia wiki moja tu watanzania wachache watukufu katika ulingo wa maamuzi ya nchi wakutane kule Dodoma katika madhabahu makuu ya siasa nchini kuamua ni nani anapewa nafasi ya kugombea ubwana mkubwa wa nchi yetu kwa tiketi ya kile kinachoitwa chama cha mapinduzi.

Mimi kama mtanzania mwanachama wa chama kinachoitwa TANZANIA kinachofuata imani ya MWAMKO WA UAFRIKA naamini ni wajibu wangu kuchambua na kuelezea yale ninayoyaona yakiendelea na yatakayoendelea wakati na baada ya uchaguzi huu bila ya woga na hata kama nafasi yangu kubadilisha mawazo ya ndugu zangu wa CCM ni finyu mno.

Chama cha mapinduzi kama yalivyo makundi mengine yenye nia ya kuwa na uwezo wa kisiasa na kikatiba kushikilia mihimili ya nchi inayotoa na kuelekeza maamuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika dola lolote, daima huwa katika mivutano ya hapa na pale inayoletwa na tofouti mbalimbali miongoni mwa wanakundi hilo.

Mivutano hiyo inaweza kuwa ya kifikira, kiutashi, kimuono ama kimaslahi. Mivutano hiyo inaweza kuwa ya siri ndani ya wanakundi pekee, inaweza kuwa inatokana na mawazo ya wanakundi pekee au kama ilivyo sasa kwa CCM ikawa ya wanakundi wakishirikiana, kuhusisha au kuendana na mawazo ya wasio wanakundi kutoka ndani au nje ya mipaka ya nchi yetu.

Kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa yakiendelea ndani ya kundi hili linaloitwa Chama cha Mapinduzi. Mabadiliko ambayo yanalenga kulifanya kundi hili kuendana na fikra za baadhi ya wanakundi hilo.

Wanakundi ambao wanadhani kuwa fikra zao ni bora zaidi kwa maslahi ya nchi na wananchi wake, chama na wanachama wake na vilevile maslahi binafsi ya baadhi ya wanakundi hili ambao nao wamejenga vikundi uchwala vyenye lengo la kufanikisha fikira zao, utashi wao, muono ama maslahi yao binafsi.

Ili hilo lifanikiwe wanakundi hawa wamekuwa wakitumia mbinu mbali mbali halali na haramu kufanikisha mapambano au mikakati yao dhidi ya fikira na muono tofauti wa wanakundi wenzao.

Baadhi ya mbinu ni kama kuanzisha vikundi uchwara ndani kundi kuu yaani CCM, kushirikiana na wanambinu mbalimbali kama vile wasomi, waandishi wa habari, viongozi wa kijamii, vyombo vya dola na hata wafadhili kutoka ughaibuni kueneza, kuzipamba na kuzilinda fikra zao kwa wananchi ili waweze kupata uhalali rasmi kutoka kwao.
Lakini ili hili lifanikiwe ni lazima waweze kushika hatamu za madaraka ya dola kwa kumweka yule wamuonaye ni chaguo bora kuwaongoza katika kufanikisha utekelezaji wa fikra na maslahi yao.

Hapa ndipo tunapokuja katika umuhimu wa suala zima la mbio za kugombea nafasi ya urais wa Tanzania kupitia kundi kuu la CCM na baadaye uongozi mkuu (uenyekiti) wa kundi hilo kama taratibu walizojiwekea ndugu hawa.

Kwa upeo wa uchambuzi wangu wagombea wote wa CCM wanawakilisha makundi makuu matatu. La kwanza ni lile linawakilisha fikira za siasa za umaarufu, la pili ni lile linalowakilisha wanakundi wenye kuamini siasa za kihafidhina na la tatu ni lile linaloamini umuhimu wa siasa za umakini.

Ingawa kuna wagombea zaidi ya kumi lakini ukweli ni kuwa wote hawa ni wawakilishi wa moja ya makundi haya ambayo yana wagombea halisi na wagombea vivuli.

Kwa wale waliosoma makala yangu iliyopita niliyoiita KIKWETE CHAGUO MAARUFU, SALIM CHAGUO MAKINI ni wazi wameshajua viongozi wa makundi mawili. Kundi la tatu ni lile linaloongozwa na mgombea mwingine machachari ndugu MALECELA.

Wengi mnaweza kudhani kuwa chimbuko la makundi haya ni miaka miwili au mitatu ya hivi karibuni.

La hasha, chimbuko hasa la siasa hizi za kimakundi ni miaka ya mwanzo ya themanini ambapo hata kama mimi binafsi nilikuwa mdogo sana kwa umri, lakini utundu wangu wa kuhoji uliweza kuniangaza na kung’amua mwanzo wa mwisho wa CCM imara na hata Tanzania ya amani tuliyokuwa tunajivunia popote pale duniani.

Chimbuko hili mimi naliita chimbuko la falsafa ya UNYANG’AU iliyozaliwa rasmi kule katika visiwa vilivyokuwa vikijulikana duniani kote kama vya marashi ya karafuu na sasa vinaelekea kupata umaarufu wa kufananishwa na marashi ya damu.

Hivi ni visiwa vya Zanzibar ambako ndipo ule mkutano maarufu wa wateule wa mtetezi wa kweli wa siasa za upendo, heshima, maadili na umoja kwa jina la siasa za Ujamaa, waliamua kukaa chini na kuondokana na kile walichokiona ni ushamba wa kifikira wa hayati mzee wetu, Mwalimu Nyerere.

Hili sio lingine bali ni azimio la Zanzibar la mwaka 1986 ambalo pamoja na mambo mengine liliondoa nguzo muhimu za uimara wa jamii yetu zilizokuwa zikisisitiza maadili ya kiuongozi na siasa nadhifu zenye kulinda na kupigania maisha mema kwa wote bila ya kujali hali ya kimaisha, nafasi ya kisiasa au kidola, tofauti za kidini na kabila au asili ya mtanzania.

Falsafa hii ya unyang’au ndio iliyozaa makundi makuu mawili yaani kundi la siasa za kihafidhina na kundi la siasa za umaarufu. Matokeo ya kuchipua, kujikita na sasa uwezekano wa kushika hatamu kwa siasa hizi ndizo zilizopelekea kuzindukana na kutahayari kwa kundi la siasa za umakini.

Ni wazi kuwa miongoni mwa wana makundi haya ndani ya CCM kwa njia moja au nyingine wameshiriki katika ile hafla ya kuzaliwa rasmi kwa falsafa ya unyang’au kule Zanzibar. Ama walikuwa miongoni mwa waliosimamia kupitishwa kwake au walikuwa katika nafasi ya utazamaji tu wakidhani kuwa wao ni vichuguu wasingeweza kupambana na mibuyu ya wakati huo.

Lakini vilevile inawezekana walidhani kuwa zoezi hilo lilikuwa ni la busara ambalo kwa mahesabu yao lingewawezesha kuondokana na umasikini mali uliokuwa ukiwakumba wakati huo ambao kwa mtazamo wao ni falsafa za siasa za ujamaa ndizo zilikuwa chanzo kikuu.

Miaka kadhaa ya majaribio ya falsafa hii ya unyang’au ilipeleka baadhi ya wanakundi kuu kuanza kujiuliza kama falsafa hii ni bora na zaidi ina mnufaisha nani. Hapa ndipo lilipoibuka kundi la siasa za uhafidhina ambalo lilinza kujijenga na kujipanua katika miuondo mbinu yote ya kiutawala ili kuhakikisha kuwa falsafa hii ambayo iliweza kuwaonyesha nuru yao kimaslahi inabaki kutawala taifa letu.

Kundi hili lilitumia mbinu mbali mbali hata ikafikia wakati likawa tayari hata kuvunja muungano wa nchi yetu ilimradi kuondokana na kanguvu cha ajabu cha baba wetu wa taifa aliyeweza kung’amua hatari ya kusimikwa kwa falsafa hii ya unyang’au kwa kusingizia Utanganyika na Uzanzibari. Baba wa taifa alijaribu kupinga safari hiyo ya wahafidhina waliokuwa wakijaribu kushikisha hatamu kwa falsafa yao ya unyang’au wakati huo.

Upinzani ambao aliweza kuendeleza hadi katika uchaguzi wa mwaka 1995 lakini bila ya kujua akapigwa chenga ya mwili na wajanja wajanja wachache walioweza kumlaghai kuwa wao wana dawa ya tatizo lilikuwa likimuumiza kichwa chake.

Matokeo yake hadi mzee wetu huyu alipoelekea dunia nyingine ambako hivi sasa nina uhakika amekuwa BIZE akipokea ripoti mbalimbali za hali mambo hapa kwetu kwa wajumbe waliomfuata hivi karibuni, Unyang’au umeendelea kishamiri na hivi sasa unajaribu kushika hatamu kwa sura mbii tofauti.

Kushamiri kwa unyang’au na uwezo wake wa kuamsha chuki za kimfumo miongoni mwa watanzania wengi kumepelekea kuibuka kwa kundi la siasa za Umaarufu katikati mwa miaka ya tisini kama fikra mbadala za uny’angau uliokuwa ukiendeshwa na kulindwa na wanakundi la kihafidhina.

Ama kwa uchungu wa nchi yetu na watu wake (fikira ambayo najaribu kuendelea kuiamini ingawa mengi yananielekeza tofauti) au kwa POLITICAL OPPORTUNISM, kundi la siasa za Umaarufu limeweza kuibuka ndani ya kundi kuu na kujaribu kuonyesha kuwa lenyewe linaweza kumalizia kazi aliyoianza baba wa taifa ya kuondoa unyang’au na manyanga’au wote kutoka katika mihimili ya kisiasa na kidola nchini mwetu.

Kundi hili lilibahatika kupata baraka za wananchi wengi waliochoshwa na madhila ya unyang’au huu ambao umeleta umasikini na aibu za kimaisha zisiso na kifani miongoni mwa watanzania walio wengi.

Ni ukweli usiofichika kuwa kundi hili ambalo lilikuja usoni mwa watanzania wakati wa uchaguzi wa mwaka 1995 na kuzuiliwa kitaalamu na mwalimu Nyerere ambaye aliamini kuwa halijawa tayari kukabidhiwa majukumu makubwa ya kuongoza nchi yetu, lilikuwa limesheheni vijana wachache ambao ni wazi walikuwa na uchungu mkubwa kwa nchi yetu.
Kwa bahati mbaya manyang’au wachache waliona hatari ya kundi hilo mbeleni hivyo kwa mwendo wa taratibu wakaanza kujipenyeza ndani ya kundi hili na hatimaye kushika miundo mbinu yote ya kisiasa.

Manyang’au hawa ambao walijuwa wazi kuwa kamwe hawataweza kufanikisha ndoto yao ya kushika hatamu za kiutawala za nchi hii na hivyo kurutubisha neema zao bila ya kujipenyeza katika kundi hili.

Wao walijuwa wazi kuwa kutokana na laana ya wazi ya baba wa Taifa aliyolipa kundi la siasa za kihafidhina, laana ambayo alikuwa akiendelea kuisisitiza hata katika matamshi yake ya mwisho kabla ya kukatwa kauli, kamwe wateule wao wasingekuwa na nafasi ya kushika hatamu ya taifa letu na kundi kuu yaani CCM hapo baadae.

Hawa waliamua kuelekeza nguvu zao kwa mteule wa kundi la siasa za umaarufu wakijua kuwa kama watafanikiwa kushika hatamu za madaraka nchini na ndani ya CCM wataweza kuendeleza unyang’au wao kwa mgongo wa mteule wa kundi la siasa za umaarufu aliyetokea kuwa maarufu na hivyo kwa mawazo yao ni rahisi kushinda jaribio la ugombea wa urais wakati huu.

Kwa bahati mbaya ama kwa kudhani kuwa ni uamuzi sahihi, mteule wa kundi hili linaloamini siasa za umaarufu zenye mlengo wa kile kinachoitwa utawala mpya na mawazo mapya, amewaachia manyang’au hawa nafasi kubwa katika mkakati wake za kuchukua madaraka ya nchi yetu.

Ndio maana imefika wakati watanzania kwa namba inayokuwa kila kukicha kuanza kuhoji kama kweli hata yeye binafsi ni suluhisho la madhila yanayowakumba na kama kweli anaweza kuundoa falsafa ya unyang’au wakati amekuwa akiwategemea manyang’au na kuachia mbinu za kinyanga’au kutawala mkakati wake kile wanachidai wa kujenga historia mpya hapa nchini.

Pamoja na mambo mengine, kutokana na hali hii ndipo likazuka kundi lingine ambalo ni dogo mno kwa hesabu lakini kubwa kwa kimkakati ambalo linadhani kuwa ni siasa za kanadhifu na kimaadili pekee ndizo zinaweza kutimiza ndoto za mwisho za baba wa Taifa za kuondokana na falsafa hii ya kinyang’au katika kundi kuu, yaani CCM na hivyo Tanzania kwa ujumla.

Kundi hli ambalo linajumuisha watu mashuhuri ambao baadhi yao walikuwa na nafasi katika tawala mbili za mwanzo za taifa letu pamoja na wanasiasa wapya wenye kukerwa na mambo na msuguano wa makundi mengine mawili limejikita chini ya mgombea wamuonaye makini zaidi yaani Dr Salim.

Kwao wao wanadhani uzoefu, ustaarabu, umakini na uaminifu wa kimaadili alio nao mgombea huyu ambaye kwa mara kadhaa marehemu baba wa taifa alipendelea awe mrithi wake wa uongozi wa siasa zake za Kinadhifu, kiupendo na kimaadili, ndio kweli unaweza kutuepusha na madhila ya unyang’au.

Madhila ambayo kama wao hawatafanikiwa yanaweza kuongezeka zaidi endapo waumini wa falsafa hiyo ya unyang’au ndani ya kundi lao la CCM wataweza kushika hatamu ama wao binafsi au kwa kutumia mgongo wa kiongozi mwingine.

Kundi hili linaamini siasa makini ndizo kama ndio silaha muhimu ya mwisho ya kunusuru ya kundi lao kuu (CCM) na Taifa letu na vilevile hatma ya watanzania kwa ujumla. Linaamini kuwa siasa za umakini zenye kuendeshwa na uaminifu wa uongozi wa kimaadili na wenye kung’amua hasara za siasa za kihafidhina na umaarufu sio tu unaweza kuondoa madhila ya unyang’au unao ota mizizi katika jamii yetu lakini vilevile kuepusha janga linalotujia mbeleni kutokana na msuguano wa hayo makundi mengine mawili.

Katika mtazamo wangu ninaamini kuwa angalao kundi hili ndilo linaloweza kutuokoa watanzania na kitimtimu kilichoko mbeleni cha wanamakundi mawili ya umaarufu na uhafidhina ambayo kwa kweli pamoja na mapungufu mengine yameonyesha chuki na uadui mkubwa ambao ni dhahiri ndio utakawo kuwa dira ya ama wateule wao wakuu au wateule wao vivuli watakaposhinda mpambano huu haramu.

Sio tu kwamba itawabidi kusafisafisha wale wanaodhani wanatofautiana na kifikira na kiutashi kuhusiana na vipi nchi yetu iendeshwe lakini vilevile ni dhahiri watalazimika kuwandoa au kuwanyamazisha wale wote waliokuwa wakiwaona ni maadui zao na pengine wakawa kikwazo kwao kufanikisha yale yaliyopelekea wao kuamua kupigania nafasi hiyo ya juu ya kimaamuzi ndani ya chama na jamii kwa ujumla endapo watashika hatamu zote zikiwemo za dola.

Mimi kama nilivyodokeza hapo juu sina mahusiano ya ki-uwanachama na kundi hilo kuu linalojiita la chama cha mapinduzi hivyo kwa kile tunachosema ni kawaida isingenipasa kuingilia mpambano wa ndugu zangu hawa wa CCM.

Lakini nikiwa kama mtanzania na muafrika ninayeamini amani na upendo kama nguzo kuu za uanadamu na mwenye uchungu na nchi yangu hii ninamuomba mungu asikie vilio vya wengi vya kuwaamsha baadhi ya wapiga kura ndani ya CCM.

Ndugu zetu ambao wamegubikwa na ushabiki na tama ya maslahi binafsi waweze kuzinduka na kuona umuhimu wa umakini katika kufikia uamuzi wao wa mwisho ili kuliepesha taifa letu na janga lunalotujia.

Janga la muendelezo wa falsafa ya unyang’au, ama kwa sura ya sasa ama sura, ambayo kwa muda wa sasa ndio imekuwa rutuba bora ya machafuko na ukosefu wa amani kwa taifa letu na hata majirani zetu.

Hatma ya watanzania ipo mikononi mwa ndugu hawa wachache ambao mpaka sasa wameweza kufanikiwa kutwaa utukufu wa kidunia wa kuwawezesha kutuamulia watanzania milioni 36 ni nani atakeyekuwa ameshika uhai wetu wa kifikira na kibailojia kwa miaka mitano ama kumi ijayo.

BARUA WAZI KWA WAPIGA KURA WA CCM..

@2005..published by RAI

Ndugu watanzania wenzangu,
Kwanza hongereni kwa kuweza kuwa miongoni mwa watanzania wachache ambao mungu amewajalia kuwa na nafasi ya juu kabisa nchini mwetu ya kuamua ni nani anakuwa kiongozi wa nchi yetu kwa miaka mitano au kumi ijayo.

Vilevile nawapongezeni kwa kuwa wavumilivu wa madhila ya usumbufu wa hali ya juu kutoka kwa wale wanaowakilisha maslahi ya wakubwa wenzenu wanaotaka kuingia ikulu kwa makeke ya karne.

Ndugu zangu mimi si mwanachama wa chama chenu kitukufu lakini kama mtanzania ninayejua wajibu wangu najua umuhimu mlio nao wakati huu katika kuamua maslahi yangu, ya ndugu zangu na watanzania wenzangu wote kwa ujumla.

Ninajua kuwa chaguo lenu ndilo litakalofanikisha au kuvuruga ndoto zangu nyingi kuhusiana na nchi yangu na bara langu nilipendalo la Afrika.

Ninajua kuwa ufunguo wa chembe ya uhuru ninayo jivunia hivi sasa na nikaweza kukaa hapa nilipo na kuandika barua hii kwenu mnao ninyi na ni ninyi ndio mtakaoamua kama nitaendelea kuwa nao hata baada ya usiku wa tarehe nne mwezi ujao.

Ninajua kuwa ni ninyi wenye kushika mstakabali wa maisha yangu ya upendo na uvumilivu kwa watanzania wenzangu ambao daima nimekuwa nikiwapenda bila ya kujali dini zao, makabila yao, rangi zao ama hali zao za kimaisha.

Ninajua kuwa kura zenu mtakazopiga wiki ijayo ndizo zitakazoamua kama na mimi nitabahatika kuoana na nimpendaye na kuzaa naye watoto wazuri watakaojivunia na Tanzania nitakayowachia.

Ninajua kuwa wengi wenu tayari mmeshamua ni nani mngependa awe rais wa nchi yetu ama kutokana na mvuto wake, ukaribu wake nanyi, umaarufu wake, ucheshi wake, unyenyekevu wake na hata uchapakazi wake mnaodhani kuwa ni muhimu kwa uongozi wa nchi yetu kuondokana na hali tuliyonayo sasa.

Ninajua kuwa wengi wenu mnadhani kuwa ni lazima kulipa fadhila kwa wale waliofanikisha ninyi kupata nafasi hii hata kama kwa masharti ya kudhalilisha kama kulazimika kumpigia kura mgombea wa yule aliyekusaidia kufanikisha mambo na wewe ukapata nafasi uliyona nayo.

Ninajua kuwa wengi wenu mna deni la kulipa kutokana na misaada mbalimbali kama vile kumlipia mwanao ada ya shule, kulipia matibabu yako au ya mpendwa wako wakati akiumwa, au kukupa nafasi ya kwenda kusoma elimu ya juu ama pale mlimani ama kwengineko duniani. Haya yote mliyopata kutoka ama kwa wafadhili mbalimbali waliokaribu na mgombea Fulani ama hata mgombea mwenyewe.

Najua kuwa wengine tayari mmeshaahidiwa nafasi kubwa kubwa za uongozi katika nchi yetu ili mradi mhakikishe kura yako inaandikwa jina la mgombea Fulani.

Najua wengine mna amini kabisa kuwa kutokana na ukweli kuwa wagombea wengine wote ni ‘wachafu’ na wengine sio watanzania basi huna la kufanya ispokuwa kumpigia kura mgombea ambaye mnadhani kuwa ni msafi na hana hata tone la uchafu isipokuwa harufu ya neema tu.

Ndugu watanzania wenzangu naomba uchukue muda huu hata vidakika vichache kwanza kufikiria kama hayo unayoamini kuhusu mgombea huyo ni kweli na hakuna uwezekano kuwa kuna upande mwingine wa mgombea huyo ambaye wewe hujapata nafasi ya kuujua kwa sababu wenye majukumu ya kukujulisha wamelazimika kutokujulisha.

Halafu ndugu mtanzania mwenzangu naomba ufikirie kama kweli vigezo unavyotumia kuamua mtu wa kumpigia kura yako tukufu ni vigezo tosha vya kumpa mtu jukumu zito la kuwa rais wako mwenye nguvu za juu za kimaamuzi katika kila kona ya maisha yako kwa mika mitano ama kumi ijayo?

Hivi vigezo hivyo vimeweza kukusaidia kutambua mtu ambaye kweli na sio anayejidai, ambaye atahakikisha chama chako kinaendelea kuwa na umoja na nidhamu ya kweli iliyowezesha kushinda mitihani mbalimbali ambayo kimekumbana nayo kwa miaka yote hii tangu kianzishwe na wazee wetu waliotutangulia?

Hivi vigezo hivyo vilijitosheleza kukuongoza wewee kufikia uamuzi wako kwa umakini wenye kuhitajika kuamua mtu bora wa kumkabidhi hazina yetu, utamaduni wetu, uvumilivu wetu, upendo wetu, unoja wetu na zaidi maisha yetu na wote tuwapendao na watupendao.
Hivi uamuzi wako umetilia maanani kama huyo utakayemchagua atakuwa ndiye anayetakiwa kukuongoza wewe na familia yako katika mapambano dhidi ya gonjwa la ukimwi kwa yeye mwenyewe kuwa mfano bora wa kubadili tabia.

Hivi huyo mgombea umpendaye au unayelazimika kumchagua ndio kweli yeye atayeweza kuiongoza Tanzania katika dunia hii ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa umakini wa hali ya juu wenye kutambua nini haswa kinatakiwa kifanyike ili nchi yetu iheshimike duniani na hivyo kusikilizwa matakwa yake.

Hivi huyo mgombea anaweza kumlinda mdogo wako, dada yako, kaka yako, mpendwa wako, mwanao au rafiki yako mpendwa na masahiba ya utandawazi yaliyojaa ulaghai na utapeli wa kila aina.

Ndugu yangu umejaribu kufikiri ikiwa ni mgombea wako anayeweza kutuokoa katika janga la kuvunjika kwa amani ya nchi yetu kutokana na tamaa ya madaraka ya baadhi ya wagombea ambao wameamua kutumia mbinu za chuki na visasi ili kufanikisha matamanio yao ya kidunia.

Hivi ni kweli mgombea unayetka kumpigia kura yako anaweza kusema hapana kwa wababe wa dunia pale wanapotka kufanya nchi yetu ni tambara lao bovu la kufutia vinyesi vyao vya kibeberu vinavyopita vikidondoka kila kukicha.

Hivi kweli ndugu yangu hudhani kuwa hata kama una deni la kulipa fadhila za mgombea uliyeambiwa umpigie kutokana na mamilioni uliyopewa, maslahi ya ndugu zako pale nyumbani na watanzania kwa ujumla yana umuhimu zaidi kuliko ya hao.

Hivi kweli ndugu yangu unadhani kuwa mgombea uliyeambiwa umpigie kura ulipokuwa unapewa msaada ule wa kifedha ndiye atakeyeweza kukupunguzia kero la rushwa linalowasibu kila siku wewe na familia yako.

Hivi ni kweli kuwa mgombea huyo uliyevutiwa naye anaweza kujenga nyufa za nguzo za dola letu zinazobomolewa na wapambe wake kila kukicha ili nao wapate kuingia ikulu bila ya appointment kuanzia mwezi wa kumi na moja mwaka huu.

Hivi umefikiria jinsi kura yako inavyoweza kuwaingiza ikulu mabaradhuli, wezi, wauza nchi, waruka kodi, mafuska na walaghai ambao wanakuja kwako na sura ya ucheshi lakini ndani imejaa ushetani wa hali ya juu kabisa.

Ndugu yangu kwa kweli sipendi kukuchosha maana najua hapo ulipo una majukumu makubwa mbele yako, lakini naomba ufikirie kidogo kama kura yako haiendi kwa mtu ambaye ameonyesha dhahiri kuwa hakubaliani kabisa na nyendo na maadili ya utanzania ambayo mwalimu wetu baba wa Taifa alituwekea kama vipimo vya mapenzi yetu ya kweli kwa nchi yetu.

Mwisho ndugu yangu mpendwa naomba ufikiri hivi ni kweli kura yako haiwezi ikatoa chaguo bora zaidi litakalotuwezesha kuokoa taifa letu kutoka katika janga la kuangamia, litakalotuwezesha watanzania kwa mara nyingine kutembea vichwa juu kwa kujiamini, litakalotuwezesha kutuepusha kuwa na baraza la mawaziri lilojaa matapeli na walaghai watakaokuwa wakitudanganya kila kukicha, chaguo litakalotuletea viongozi waadilifu kwa mungu na kwetu sisi bila ya kujali hali zetu za kimaisha, chaguo litakalolinda thamani ya kila mtanzania, chaguo litakalotusaidia kuinua hali ya elimu ya nchi yetu kwa kujua thamani yake na zaidi chaguo litakalo simama kidete kuchukua maamuzi kwa utulivu na umakini wa hali ya juu ilojawa na busara za kiuongozi bila ya kuhatarisha maisha yetu na wala kurubuniwa na wapambe uchwara.

Ndugu yangu mwana CCM, ni wewe ndiye utakeyeamua ni Tanzania ya aina gani tutakayokua nayo wiki mbili zijazo.