WAMEBAKA NA KUDUMAZA KADEMOKRASIA KETU

August@2009

Wakati watanzania walio wengi wanaamka na kuonyesha utayari wa kuchukua jukumu la kuleta mabadiliko ya kweli ambayo yataliwezesha taifa letu kusonga mbele katika harakati za kujenga mfumo wa kidemokrasia nchini, ndugu zetu wa CHADEMA wameamua kubaka na kudumaza mfanikio madogo yaliyoweza kupatikana hadi hivi sasa.

Kwa kifupi tukio la kumshinikiza ama kumshawishi kama ambavyo wanapenda watu wajue, kiongozi wao mahiri Zitto Kabwe kuacha kushindana kidemokrasia na Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe katika kugombea nafasi ya mwenyekiti kinatafsirika kwa maneno machache sana. CHADEMA wamebaka na kudumaza harakati za demokrasia nchini.

Kama kuna chama ambacho watanzania hasa vijana walikuwa na matumaini makubwa ya kuwaondoa katika madhila ya ukiritimba wa miaka mingi ulioshiwa na tija wa CCM, basi chama hicho kilikuwa ni CHADEMA.

Natumia neno kilikuwa na matumaini kwa kuwa naamini kuwa kwa hali ilivyo sasa ni vigumu na kama sio kitu kisichowezekana kwa watanzania kuendelea na imani waliyoanza kuijenga kwa chama hicho kuwa kingeliweza kuwakomboa kutoka kwa maovu ya CCM ambayo yanaonekana kukosa dawa.

CHADEMA wamefanya yale ambayo hata mahasimu wao CCM hawakutegemea kuyaona. Wameweza kutupa baharini nafasi ya kipekee ya kuhakikisha ushindi wa kutosha kwa chama hicho katika chaguzi zinazokuja na kuamua kujichimbia kaburi la kisiasa. Yaani wameamua kujiunga na historia ya vyama ambavyo vilikuwa tishio kwa CCM, kuanzia enzi za NCCR Mageuzi hadi CUF ambavyo kwa sasa vimebaki historia tu kama vyama mbadala vya CCM.

Hapa nisingependa kuzungumzia ni nini CHADEMA ingeweza kufaidika ama kuathirika endapo wangelimchagua Zitto Kabwe kama mwenyekiti wao mpya. Ninachojaribu kuchambua ni faida gani CHADEMA kama chama na wapenda demokraisia nchini wangeliweza kupata na hasara gani ambazo uamuzi wa kumshawishi ama kumshinikiza Zitto kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Ukweli ni kuwa kitendo cha mwanachama mwenye ushawishi mkubwa kama alivyo Zitto Kabwe kuthubutu kusimama kushindana na Mwenyekiti aliyeko madarakani kilifungua nafasi kubwa sana kwa CHADEMA. Kitendo hicho kimeweza kuonyesha kwa vitendo kuwa chama chao ni kweli chama cha demokrasia na maendeleo na maneno hayo sio kauli mbiu tu.
Wapo watu wengi, vijana kwa wazee ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakivutiwa na CHADEMA.

Na kama ilivyo utamaduni wa watanzania, wengi wao bado walikuwa wanasubiri uhakikisho kuwa CHADEMA ni mbadala makini wa CCM ili wajiunge katika harakati za kuleta mabadiliko makubwa kisiasa. Wengi wao kuingia kwa Zitto katika kinyang’anyiro hicho ilikuwa ni ishara kuwa CHADEMA inaweza kuaminiwa kwa yale wanayoyasema kwani wanaonyesha kuyatenda.

Ukiangalia kwa undani utaghamua kuwa kule kuingia tu katika kinyang’anyiro hicho kwa Zitto Kabwe kulikuwa ni mtaji mkubwa kwa CHADEMA na zaidi kwa maendeleo ya demokrasia nchini.

Kitendo cha Zitto Kabwe ambaye amekuwa kama kioo cha mafanikio ya wanasiasa vijana wenye uthubutu wa kusimama kupambana na mfumo kandamizi uliokuwa ukiwatisha kuthubutu kujiunga na vyama vya upinzani kuthubutu kuingia katika kinyang’anyiro hicho kulikuwa ni mwaliko wa wazi kwa maelfu ya vijana kujiunga na CHADEMA.

Kama CHADEMA wangeweza kuendelea na kufanya uchaguzi wao na mwishoni mshindwa akamkumbatia mshindi basi ni wazi hilo lingejenga imani kubwa kwa chama hicho miongoni mwa wapenda mabadiliko makini ambao hadi sasa wanashindwa kuamini vyama vyetu vya kisiasa na wanasiasa kwa ujumla.

Kwa watanzania ambao tungependa kuona kunakuwa na mfumo ambao unawezesha nchi yetu kuwa na demokrasia ya kweli yenye kujenga umakini wa kisiasa katika kuchagua viongozi wetu na kufanya maamuzi makubwa na madogo ya kikatiba, kisheria, kisera, kifalsafa na kiutawala. Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na chama ambacho kitaweza kwanza kuondoa ukiritimba wa CCM katika vyombo vya maamuzi na baadae kutupa chaguo mbadala pale itakapowezekana kubadilisha chama tawala.

CHADEMA ilishaanza kujenga muono huo miongoni mwa watanzania walio wengi. Zitto Kabwe ni mmoja wa watu ndani ya CHADEMA ambao wameweza kujenga hisia miongoni mwa jamii kuwa kama wangendelea vizuri ni muonekano wa kidemokrasia na maendeleo, basi wangeweza kujenga imani miongoni watanzania hao. Yaani CHADEMA walikuwa ndio wanaelekea katika kufanikiwa kujenga imani kuwa lipo chaguo mbadala la CCM katika nchi yetu.

Ukweli ni kwamba baada ya kuyafanya waliyoyafanya, ni wazi kama ilivyo vigumu kwa viongozi wa CCM kuzungumzia vita dhidi ya ufasadi mbele ya watanzania, kwa CHADEMA itakuwa ni vigumu kwa viongozi wao kusimama kuongelea umuhimu wa demokrasia na kupiga vita ukandamizaji nchini na kuaminika ama hata kueleweka.

Ni wazi CHADEMA wamejifunga uhalali hata wa kuongelea UFISADI ambayo imekuwa ajenda yao muhimu katika miaka ya kariuni. Kwani hapa wameonyesha ufisadi wa hali ya juu dhidi ya misingi ya kidemkrasia ambayo ina nafasi kubwa katika kufikia maamuzi ya kisiasa miongoni wa wapenda mabadiliko katika nchi yetu.

Kitendo walichokifanya, tena kwa kumkandamiza Zitto Kabwe ambaye ni alama ya uthubutu na umakini miongoni mwa vijana ambao ndio mtaji mkuu katika chaguzi zinazokuja, CHADEMA wamewaondolea hata nafasi waliyokuwa nao baadhi ya vijana wao katika kushinda kwenye chaguzi zijazo.

Ni wazi kutokana na hali iliyotokea kuanzia sasa itakuwa vigumu sana kwa vijana wa CHADEMA ambao walikuwa nyota zinazotegemewa kubadili sura ya siasa katika uchaguzi ujao kuweza kuwashinda vijana wenzao wa CCM. Hii inatokana na ukweli kuwa hata wao o wamejijengea taswira ya ama kuunga mkono, kubariki ama kunyamazia nguvu za wazee ndani ya chama chao zikifisadisha misingi ya kidemorasia ambayo wao walipaswa vijana hao walipaswa kusimama kidete kuitetea na kuipigania. Ni wazi kuwa kuanzia sasa itakuwa vigumu kwa vijana wa CCM kusimama mbele ya vijana wenzao katika chaguzi zijazo na kuwashawishi kuwa wao ndio chaguo la mabadiliko ya kweli.

Zaidi, sababu ya kumshikiza Zitto kuacha kushindana na Mwenyekiti wao aliyekuwepo madarakani ili kuepusha mpasuko ndani ya chama ni sababu inayoleta maswali zaidi ya majibu.

Kwa chama ambacho kinasema kinapigania demokrasia na maendeleo nchi kuamini kuwa kuwaacha viongozi wawili kushinda katika uchaguzi ni tishio la umoja wa chama ni sawa na kukubaliana na fikiria mgando zilizomo miongoni mwa wahafidhina ndani ya CCM kuwa kuruhusu ushindani wa haki na huru kati ya vyama vya siasa nchini ni kuhatarisha amani na maelewano ya nchi yetu.

Pia, kusema kuwa Mbowe akipata mshindani mkali kutaleta mtafaruku ndani ya chama kunatoa sura ya ama wazee kumuogopa Mbowe ama kukiri kuwa CHADEMA hawawezi kufanya siasa za kiungwana na zisizo na chuki ambazo zingeleta mgawanyiko. Ni wazi fikira kama hizo sio tu zitazuia wengi wengine kujiunga na chama hicho lakini pia si ajabu tukasikia kuendelea kwa mlolongo wa wanachama na viongozi wa chama hicho kuondoka na kwenda kujiunga na jinamizi walilolizoea yaani CCM.

Ndio maana baada ya kuona hili nimekuwa nikijiuliza sana ukweli wa sababu za viongozi na wanachama kadhaa wa CHADEMA ama kuhama, kusimamishwa ama kufukuzwa uanachama katika miaka ya karibuni. Nimekuwa nikijiuliza kama ni kweli hawa walikuwa vidudu mtu vinavyohatarisha ustawi wa chama ama kuna tatizo la kiuongozi ndani ya chama hiki. Kutokana na maamuzi yaliyofanyika hivi karibuni nachelea kuamini kuwa wapo walio ondoka CHADEMA baada ya kushindwa kuvumilia kuvunjika moyo katika nia yao ya kujenga mabadiliko ya ndani ili kuweza kushawishi mabadiliko ya nje.

Na katika hili, ni wazi muathirika si Zitto, si Mbowe na wala sio CHADEMA tu bali ni mustakali mzima wa mapambano ya kujenga demokrasia nchini.

Kitendo cha kuonyesha taswira ya kuwa kuna uwezekano wa kiongozi wa CHADEMA kuwa tayari kutumia mbinu zozote zile, halali na haramu, makini na hovyohovyo, salama na hatari ili kulinda nafasi yake kileleni, kinaonyesha kuwa ile ndoto ya vyama vya upinzani kuungana ili kukishinda chama dola cha CCM zinaendelea kubaki hivyo, yaani ni ndoto tu.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi kuwa kitendo hiki kinahalalisha propaganda ya CCM na dola kuwa viongozi wa vyama vya upinzani wamegubikwa na ubinafsi na hawana nia ya kuwakomboa watanzania kama wasemavyo.

Na hapa napenda kuwashauri wana CHADEMA kuacha kutumia ujanja wa CCM kama sababu ya yaliyotokea na yanayoendelea kuwakumba. Kufanya hivyo ni sawa na kuwaunga mkono watwala wetu wa sasa ambao daima hawachoki kuwalaumu wazungu ama wakoloni kwa umasikini na madhila waliyowezesha katika nchi yetu kutokana na makosa yao wenyewe. Ilichofanya CHADEMA ni kujianika mbele ya mashamulizi ya CCM na maadui wengi. Na itakuwa ajabu sana kama madui hao wataacha nafasi hii kuwashambulia na hata kuwamaliza kabisa wakati huu nyeti wa kuelekea katika chaguzi za kitaifa.

Zaidi, kitendo walichokifanya CHADEMA kinawapa nafasi na nguvu zaidi maadui wa demokrasia kuendelea kudhihaki harakati za demokrasia nchini. Wapo ambao wamekuwa wakipita mitaani kusema kuwa wanaopiga kelele kutaka demokrasia hawana nia ya kweli ya kuleta demokrasia ya kweli bali ni mbinu tu ya kuweza kujipatia madaraka na baadae kufanya yaleyale ambayo wanayalalamikia wakati wasipokuwa madarakani.

Hatua ya kumshikinikiza Zitto Kabwe kutotumia haki yake ya kidemokrasia ya kuomba ridhaa ya kuongoza chama chake kwa wanachama wenzake kinahalalisha mitazamo ya maadui wa demokrsia kama hao.

Ni wazi, uamuzi wa wazee wa CHADEMA kumshinikiza Zitto Kabwe kujitoa katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama chake kwa kuhofia uwepo wa siasa chafu zitakazoweza kugawanya chama chao ulichofanikiwa ni kuhalalisha matumizi ya siasa chafu na hovyohovyo na hivyo kudumaza kabisa ndoto na juhudi za watanzania wanaopenda kuona mfumo wa demokrasia makini unatawala nchini mwetu.

Baada ya kufuatilia kwa karibu mwenendo wa siasa zetu wakati wa uchaguzi uliopita (2005) na baadae kupata taarifa za ufisadi mkubwa uliokuwa na na bado unaendelea katika nchi yetu mara baada utawala Mwalimu Nyerere, nilikuja katika hitimisho kuwa CCM na wadau wake wamelibaka taifa letu, na sasa nachelea kuhitimisha kuwa CHADEMA wamebaka kademkorasia ketu ambako katika miaka ya hivi karibuni tulianza kujenga imani na matarajio nako.