Mtizamo wangu kuhusu matukio ya hivi karibuni na mitazamo kuhusu kesi ya Balozi Mahalu

Wednesday 18th May 2011

Naweza kusema kuwa siasa za ujanjanja na hovyohovyo zimefanikiwa kuifikisha nchi kwenye state of paralysis, from state capacity to political thinking even among the self anointed critical citizens....

Nimejaribu kuisoma sijui ni ripoti ama makala iliyotumwa katika jukwaa la Jamiiforums.com hivi leo, kuona ni wapi ama ni vipi Mkapa amemkaanga Kikwete zaidi ya kujikaanga mwenyewe sioni.

Nikiangalaia kwa karibu nakubaliana na Mbopo kuwa huu ni muendelezo wa siasa za ujanjaujanja ambazo sasa zinaelekea kujikita katika mahakama zetu na kugeuza kuwa kama yale majukwaa rasmi na yasiyo rasmi kisiasa ambayo inaelekea kwa baadhi ya wanasiasa kama Mabere Marando, hayajatosheleza kufisadisha siasa za nchi yetu kwa manufaa ya muda mfupi na yale binafsi.

Watanzania wote tumegeuzwa kuwa mashabiki wa ama upande wa Kikwete ama upande wa “Wengine” bila ya kujali jukumu letu la kuweka mbele umakini zaidi ya ushabiki katika kufuatilia, kuchambua na kuzungumzia maswala muhimu ya kuikomboa nchi yetu kama ambavyo tunapenda kujinadi.

Siamini kama ushahidi huu wa kuwa serikali ilikuwa na taarifa na kwamba eti taratibu zote zilifuatwa zingeliweza kuwa ushahidi wa maonevu dhidi ya mshitakiwa katika macho ya washabiki wa upande mwengine ambao unadai kuwa huu ni uonevu na ulipaji kisasi.

Wote hapa tunajua kuwa utawala wa Mheshimiwa Mkapa ulikuwaje, inashangaza kuona kuwa kuna watu wanadhani kuwa Waziri wa wakati ule alikuwa na uwezo wa kukataa kile ambacho bosi wake Rais anataka ama amekubali kifanyike.

Lakini pia inashangaza kuona kuwa usemi wa kuwa ununuzi huo ulifuata taratibu na ulikuwa na baraka zote za serikali unaweza kusafisha uwezekano wa wizi ama rushwa wakati wote tunajua kuwa hata EPA ilikuwa na baraka na utaratibu uliofuatwa.

Halafu huu mchezo wa kukimbilia kuwa kesi kama hizi ni uthibitisho dhana, madai ama shutuma kuwa Rais ana hulka ya kisasi ni ujinga na upumbavu. Haiwezekani watu tupige kelele Rais achukuwe hatua dhidi ya ufisadi na mafisadi halafu anapochukuwa hatua dhidi ya wale ambao hawamo katika listi zetu za kuwachukia ama kuwahukumu kuwa ndio mafisadi basi Rais ndio ageuzwe mkosaji.

Kwa mtazamo wangu, fikira kama hizi ndio zinazowavunja nguvu na kuwafanya baadhi ya viongozi wetu kuamua ama kujiunga na ufisadi ama kuunyamazia huku wakilinda na kuboresha maslahi yao kwani wanakuja amini kuwa hao wanaopaswa kuwapigania ni mabingwa wa kutoa shukurani za punda kwa kuwapiga mateke pale wanapojitahidi kuwatetea na kuwalinda.

Zaidi naamini umefika wakati na ni muhimu kwa Uongozi wa Mahakama zetu kuchukua hatua kuzuia madhubutu kuhakikisha kuwa mahakama zake hazirasimishwi kuwa majukwaa ya siasa za ujanjaujanja na hovyohovyo kama ambavyo imekuwa ikijionyesha katika miaka ya hivi karibuni. Kama kweli hii habari imetolewa na upande wa utetezi unaongozwa na Wakili Marando ambaye hivi karibuni amekuwa wazi akitumia habari ama sehemu yake katika shughuli za mahakama kufanyia siasa, ni lazima hatua kali zichukuliwe kabla hali hii haijaota mizizi. Inatosha kuona jinsi mahakama zetu zimegeuzwa kuwa kisima cha rushwa na uonevu mwengine, kuruhusu siasa za majukwaani kuota mizizi katika mahakama zetu ni kucheza na hatima ya nchi yetu.