Tulimsaliti na tunaendelea kumsaliti Amina wetu….

I really thank u, from my heart, kuna vitu vingi ulinisaidia, kuna miongozo fulani, courage fulani na mambo mengine mengi, nimeona nikushukuru tu leo, asante na naappriciate as I said before, IT COMES FROM MY INSIDE, DEEPLY IN MY HEART, THANKS ONCE AGAIN, WISH U LUCKY, BE BLA$$ED. Amina chifupa mpakanjia.
Sender: +25577306944
Sent: 10:44:37
04/21/2007

Nimepigwa na butwaa, nimeishiwa na nguvu, sijui nifanyeje….najiuliza, hivi wapi ningelifanya zaidi na kwanini sikufanya mapema?

Hapo juu ni ujumbe alionitumia mtu ambaye karibia mwaka mmoja sasa nilimwita dada na yeye akaniita kaka. Ni Amina binti wa Chifupa. Huyu ni Amina niliye bahatika kumjua kwa kipindi cha karibia mwaka mmoja sasa. Katu sio Amina niliyekuwa nikijidai namjua miaka mitano kabla. Ni ujumbe ambao dada yangu amina alinitumia zaidi ya mara mbili katika usiku wa manane majira ya ughaibuni. Ni ujumbe ambao nilidharau kuujibu kwa siku mbili zaidi hadi Amina alipoamua kunipigia simu kunikumbusha kuhusu ujumbe huo. Sikujua kuwa ni ujumbe wa kwaheri ya milele.

Nakumbuka siku moja nikiwa mahala fulani naelekea nyumbani Tanzania nilimpigia simu rafiki yangu Zitto. Hii ilikuwa ni siku ambayo Rais Kikwete alihutubia Bunge letu kwa mara ya kwanza kama rais wa nne wa jamhuri yetu tukufu. Alitumia muda mwingi kunielezea ni jinsi gani alivyovutiwa na maudhui ya hotuba hiyo kitu ambacho kwa ninavyomjua rafiki yangu Zitto kilinishtua kiasi.

Katikati ya mazungumzo Zitto aliingiza suala la Amina. Akaniambia kuwa kwa muda mfupi aliofanya naye kazi anadhani kuwa Amina sio mtupu kama jamii inavyomtafsiri. Mimi nikamshauri kuwa jaribu kuwa naye karibu kumjua zaidi na kama kuna sehemu za kumsaidia basi asisite kufanya hilo kwa manufaa ya nchi yetu.

Mimi binafsi nilikuja kufunguliwa macho kutambua hazina iliyojificha ndani ya Amina siku alipopanda juu ya madhabahu ya kielemu katika ukumbi wa Nkurumah pale Chuo kikuu cha Dar Es Salaam. Hii ilikuwa ni miezi ya mwanzo ya mwaka 2006.

Mbele yangu nilishuhudia Amina tofauti kabisa na yule ambaye jamii ikiongozwa na wana udaku walivyokuwa wakimtafsiri. Mbele yangu nilimuona kijana mdogo aliyejawa na ushujaa, upendo wa dhati kwa nchi yake na zaidi mwenye kipaji cha hali ya juu cha siasa. Mbele yangu nilimwona kijana ambaye sio tu amejawa na uthubutu wa kujaribu lakini pia aliyekuwa na ndoto ya kufanikisha mambo makubwa katika maisha yake.
Mara baada ya Amina na wakina dada wengine mashujaa waliokuwepo pale kumaliza kutoa ushuhuda wao kuhusu nafasi ya mwanamke katika siasa za nchi yetu, nililazimika kusimama ili nami nitoe ushuhuda wangu.

Nilianza kwa kumuomba radhi dada Amina. Bila ya kusita nilimtaka radhi kutokana na mimi kuwa mmoja wa wale watanzania waliokubali kuamini kashfa, uzandiki, na zaidi unyanyapaa ambao baadhi wanajamii walikuwa wakimfanyia.Baada ya hilo nikamuahidi urafiki naye ili tuweze kubadilishana mawazo na ujuzi ambao niliamini kwa upande wake ungeweza kumwongezea pale alipopungukiwa na mimi kuongeza pale nilopopungukiwa na vilevile kutimiza lengo langu la kusaidia vijana wenzangu haswa kina dada kama Amina kufanikiwa ndoto zao katika ushiriki wa kujenga taifa letu kwa pamoja.

Baada ya muda mfupi wa kujuana na zaidi kufaidika na tabia ya ucheshi na upendo mkubwa aliokuwa nao Amina, nikajikuta naongeza rafiki mwingine wa karibu katika maisha yangu ambaye kwa kweli alifikia kuwa mdogo wangu mpendwa.

Mdogo wangu ambaye leo nasikitika kuwa sikufanya vya kutosha kwake yeye kunishukuru kama alivyofanya katika ujumbe huo hapo juu.

Mdogo wangu ambaye namshukuru mwenyezi mungu kwa kunipa nafasi ya kumtaka radhi kutokana na makosa niliyofanya hapo mwanzoni ya kumtafsiri vibaya.

Mdogo ambaye amenifundisha umuhimu wa kutowatafsiri na kuwahukumu watu ambao tunadhani tunawajua kumbe ukweli ni kuwa hatuwajui.

Mdogo ambaye alinifundisha kumpokea mtu kama alivyo na sio kama tunavyotaka sisi awe.
Mdogo ambaye kwa muda mfupi sana amenifunza mengi kuhusu dunia hii kuzidi hata niliyojifunza katika zaidi ya miaka ishirini niliyokaa darasani.

Muda uliruhusu machache kushauriana. Lakini katika muda huo kiduchu Amina alitokea kuwa mwalimu na mwanafunzi mzuri kwangu na mwenye kuthamini mawazo yangu kama ambavyo alivyokuwa akithamini na kutetea mawazo yake kwa uthabiti mkubwa. Amina hakuwa mtu wa kuburuzwa na wala kutishwa.

Ushahidi unaonyesha kuwa kadiri alivyokuwa akitishwa ndivyo alizidi kuwa na ushujaa wa kusimama na kuongea yale ambayo aliamini kuwa yanapaswa kusemwa bila ya kujali kama wale aliokuwa akiwasemea wanamshukuru ama kumdhihaki.

Siku moja nilikuwa nikipata nasaha za mzee mmoja ambaye alimjua mzazi wangu wakati akiwa hai. Mwishoni mwa mazungumzo aliniasa kitu kimoja. Mzee huyu aliniasa kuwa katika dunia yetu Mawalii huja kwa sura nyingi na mara nyingi huja katika sura ambayo wengi hawakutegemea na hivyo kushindwa kutambua bahati waliyoletewa na mwenyezi mungu hadi pale atakapotoweka. Waseme watakayosema lakini kwangu nathubutu kuamini kuwa Amina alikuwa ni walii aliyeletwa duniani kupima ubinadamu wetu na kutuelimisha mengi.Walii aliyekuja na ujumbe wa kuthubutu kupambana na moudhi yaliyoigubika jamii yetu bila ya woga.

Katika maisha yake tangia akiwa kigori hadi alipokabidhiwa majukumu makubwa ya kutetea maslahi ya vijana wenzake katika chama tawala, Amina amekumbwa na mengi. Kama ni mitihani basi ni wazi Amina alipata mitihani mikubwa sana. Mtihani mmojawapo ulikuwa ni ule wa wanajamii aliokuwa akiwapenda na kujitolea muhanga kuwatetea kujenga mazoea ya kumdharau, kumdhihaki, kumkejeli, kumbeza na zaidi kutomwamini katika katika uthabiti wake wa kutetea maslahi yao.

Wengi walikuwa wakimwona Amina kama mtu aliyekuwa amelewa na mafanikio. Wapo waliodhani kuwa Amina alikuwa akifurahia sana aina maisha aliyokuwa anakumbana nayo kila kukicha.

Masikini hawakujua kuwa ndani ya lile tabasamu murua lilojaa bashasha kulikuwa na mateso makubwa akilini na rohoni. Inasikitisha kuwa hata wale aliokuwa akiwaona kama kimbilio lake ndio kabisa hawakuweza kumpa nafasi ya kupunguza yaliyo rohoni.
Naamini kuwa kamwe sina haki ya kuwasema wanafamilia wake lakini nathubutu kuwasema wanajamii wengine wote. Hawa wakiwemo wanasiasa wenzake haswa wale wenziwe katika chama chake, waandishi wa habari, wanaharakati wa kijamii na hata wenzangu na mimi wasio na chao ambao Amina daima alikuwa akipenda kujinasabisha nao.

Kwa miaka mingi hawa wote nikiwemo na mimi tumekuwa tukimsaliti Amina kila kukicha. Wengi wetu tumekuwa tukimdharau, kumsimanga na hata kutengeneza na kushabikia maneno ya uzandiki ambayo yalikuwa yakitafuna furaha ya Amina kila uchao.

Wakati aliposimama kuwaongelea mamilioni ya watoto wa shule wanaotembea maili kadhaa bila ya viatu na wala uhakika wa kutia kitu tumboni siku nzima wawapo shuleni na hata wanaporudi nyumbani, tulimdhahaki na kumwambia anaongelea upuuzi. Eti amezidi umediocre. Aliposimama kuongelea maswahibu yanayowakuta watoto wa shule haswa katika wilaya za jiji la Dar es Salaam tulimwambia anataka kujijenga ili apate ubunge katika moja ya jimbo la jiji hilo. Waliodai kuwa ni jimbo lao hawakuacha kumtumia maonyo makalimakali.

Hata alipothubutu kusimama kuongelea manyang’au wanaojineemesha kwa kuwabebesha na kuwauzia maelfu wa vijana wenzetu sumu inayowamaliza kila siku, yaani madawa ya kulevya, tukamdhihaki kuwa ni mtoto mdogo hajui afanyalo. Wapo waliofikia kudai kuwa amefanya hivyo kumkomoa mumewe.

Ukweli ni kuwa hakuna aliyetaka kuamini kuwa ndani ya sura ile iliyojaa bashasha kuna uchungu wa dhati juu ya maslahi ya kijana mtanzania wa kawaida anayeathirika na hayo. Kijana wa kawaida ambaye tofauti na waheshimiwa wengine wengi katu Amina hakuacha kujinasabisha nao.

Mara dada yetu alipozimika kila mtu akaibuka kutafuta mchawi. Mara hili mara lile.
Kama kawaida ya wanadamu hakuna mwenye ubavu wa kuthubutu kujiangalia yeye binafsi ni vipi amechangia Dada yetu Amina kutuacha katika mazingira ambayo amefariki. Hakuna anayetka kung’amua ukweli kuwa wote kwa pamoja tulimsaliti Amina wetu. Wakati akituhitaji sisi tulikuwa tukimbeza na kumdharau. Wakati akihitaji mapendo yetu sisi tulimkejeli na kumzodoa.

Yote hayo aliyoyakusanya moyoni miaka nenda miaka rudi yakamalizwa kwa pigo la mwisho. Pigo ambalo lilimpelekea kuamini kuwa hata yule ambaye wazazi wake walitoa idhini ya kuwa mlinzi wa roho yake na mwili wake hapa duniani naye hakuweza kuwa naye pale alipokuwa akihitaji zaidi mapendao na uelewa zaidi. Na zaidi alipotaka kuyatoa yaliyokuwa yakimmaliza rohoni wapo waliothamini maslahi yao zaidi ya roho yake. Wote kwa pamoja tukaendela kumsaliti Amina wetu.

Inasikitisha zaidi kuona kuwa hata katika kifo chake tunaendelea kumsaliti Amina. Badala ya kujiuliza ni vipi tutaendeleza moto aliouwasha kuokoa vijana wenzetu na jamii yetu kwa ujumla, tunaendela kushabikia uzandiki, unafiki na udaku dhidi ya dada yetu Amina. Jamani tusitafute mchawi. Wengine walimalizia tu lakini sote tulimsaliti Amina wetu.

Kwa kweli natamani wote tungelimjua Amina wa kweli. Yule Amina niliyebahatika kumjua karibia mwaka mmoja tu kabla hajatuaga, Amina mwenye ucheshi wa haja. Amina mwenye nidhamu hata kwa wale aliokuwa akijua wanamdhihaki na kumdharau. Amina mwenye upendo wa kweli kwa watu wote, Amina asiyeogopa kusema na kufanya yale yote aliyoamini ni ya haki na yanapaswa kusemwa ama kutendwa. Amina mwenye uthubutu ambao wengi wetu tumeukosa. Amina nyota tuliyoizima hata kabla haijang'ara.

Mwenzenu natamani ningelifanya zaidi na zaidi kuonyesha urafiki wa kweli kwako dada yangu mpendwa Amina. Siamini kuwa eti nami sikuweza kuwa karibu nawe wakati ukihitaji zaidi urafiki wangu hata kwa uchanga wake. Amina dada yangu umetutoka lakini namshukuru mungu uliniaga kwa maneno ya upendo ingawa akati ule sikujua hilo.

Ni Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema tu ndiye ajuaye kuondoka kwako kuna funzo gani kwetu. Watasema yote lakini jua kuwa tupo tuliobahatika kukuamini na kukuthamini kwa dhati hata kama muumba hakutupa muda mrefu wa kufanya mengi. Nasema tumebahatika kwani ni nadra kwa dunia yetu hii kupata bahati ya kuitwa rafiki na walii kama wewe. Cheche ulizowasha kamwe hazitaenda bure. Bendera tutaipeperusha hadi mwisho sio kwa maneno bali kwa vitendo.

Msalimie kaka Chachage. Mwambie akusomee hadithi ya makuwadi wa soko huria. Mwambie ndoto yake ya ukombozi wa mlalahoi wa Tanzania yetu baada ya miaka kadhaa ya unyang’au wa soko huria inaelekea kutotimizika hivi karibuni. Mwambie kuwa yule mswahili mlalahai mwenzio Jakaya anahitaji makarama zaidi kutoka kwake huko alipo ili aweze kutimiza yale matumaini aliyokuwa nayo kwake kabla hajatuaga na kutuacha wapweke pale mlimani.

Namalizia kwa kunukuu ujumbe wa taarifa ya kifo chako kutoka kwa rafiki yetu kipenzi Zitto: AMINA AMETUTOKA….

WAANDISHI WETU NA UKUWADI WA UNYANG'AU

@14th July 2006, Published by Tanzania Daima Newspaper.

Comrade Chachage aliwaita makuwadi wa soko huria, mimi nawaita makuwadi wa unyang’au. Makala hii niliandika miezi mingi iliyopita lakini mengi yalinisababisha kutoiwakilisha kwa wapendwa watanzania. Kutangulia kwa kaka yangu na mwalimu wangu wa fikra changanuzi, kumenipa nguvu za kuwasilisha hoja yangu kwa watanzania, wanyonyaji kwa wanyoge.

Neno manyang’au lina tafsiri mbalimbali katika macho ya watanzania. Kwangu mimi unyang’au ni ile hali ya kufikiri na kutenda mambo ambayo yanaathiri mustakabali mzima wa mwananchi wa kawaida. Manyang’au ni wale wote wanaotenda mambo mbalimbali kwa maslahi ya uchu wao pekee bila ya kujali madhara makubwa ya matendo hayo kwa jamii.

Hawa ni wale walio katika nafasi zote na haswa za juu za kutoa maamuzi serikalini, kwenye vyama vya kisiasa na katika makundi mengine ya kijamii. Hapa nchini mwetu utawakuta katika kila pembe ya maisha yetu. Wapo wenye nguvu kisheria kuwemo katika kundi hilo na wapo walioweza kujipenyeza humo kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile uwezo wa kiuchumi na nafasi zao katika makundi ya kijamii.

Manyang’au wapo wakubwa na wadogo. Wapo wa kutoka nje na wapo wengi tunaotoka nao katika nchi yetu hii hii iliyojaa harufu na ladha ya umasikini wa kutupwa.
Unyang’au ni mfumo rasmi katika jamii yetu ukiwa na baraka za kisheria kama zile za takrima na nyinginezo nyingi.

Makuwadi wa unyang’au ni wengi na wapo katika sekta zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Wapo wanaojiita wafanyabiashara, wapo wanaojiita makada, wapo wanaojiita wasomi, wapo wanaojiita watumishi wa serikali na wengine wengi.
Wapo ambao wanafaidika kweli na unyang’au huo na wapo wale wanaodhani kuwa wanafaidika lakini kumbe wakipatacho ni makombo tu.

Wapo wanaojiona kuwa wanakundi halali katika mfumo wa kinyang’au na wapo waliomo humo kwa kujipendekeza na kuifaragua. Wapo waliomo humo kwa kupenda na wapo waliojikuta humo bila ya wao kujijua. Wakiulizwa wanadai ni kulazimika kutokana na mazingira yaliyopo.

Hawa wote wamekuwa tayari kuuza uwezo na ujuzi wao kifikira na kikazi kutetea, kusadifu na kulinda mfumo unaohalalisha unyang’au katika jamii yetu. Wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa kudhani kuwa wanaenda na wakati ambao unashurutisha kila mmoja wao kuwa na “mahusiano mazuri” na manyang’au wa nchi yetu na wale kutoka nje ya mipaka yetu.

Kwao wao, ili kuwa na kile wakionacho ni mafanikio kimaisha, ni lazima wajitumikishe kwa manyng’au wa nchi hii ambao wengi wao wana nguvu za ushawishi katika dola la nchi yetu.

Moja ya sifa ya pamoja ya ndugu zangu hao walio amua kukuwadia unyang’au ni kutoacha kulalamika kuhusu masahibu ya unyang’au katika jamii lakini kwa upande mwingine wanageuka kuwa ndio wasadifu na walinzi mahiri wa mfumo sababishi.Hapo mbeleni tutawachambua wote kwa makundi yao, katika makala hii ningependa kuongelea makuwadi waliomo katika sekta ya uandishi wa habari.

Fani ya uandishi ya habari ni moja ya nguzo muhimu za kiutawala ambazo jamii yoyote inayothamini umuhimu wa mfumo wa demokrasia inapaswa kuipa kipaumbela na umuhimu wa hali ya juu. Bahati mbaya katika Tanzania yetu fani hii imegeuka kuwa adui mkubwa wa demokrasia ya kweli na hata kutishia hatima ya mchakato mzima wa kuanzisha na kuboresha misingi ya kidemokrasia katika jamii yetu.

Kwa miaka mingi sasa, wachunguzi wa mambo ya siasa na jamii wamekuwa wakijadili nafasi ya fani ya uandishi wa habari katika nchi yetu. Wengi wamekuwa wakihoji uwezo wa wahusika wa fani hii. Wengi wamekuwa wakijaribu kuchambua uwezo wa kitaaluma wa wengi wa waandishi wetu ambao wameonekana kana kwamba huwa wakifanya kazi hiyo bila ya kuwa na sifa za kitaalamu zinazohitajika katika fani hiyo.

Kwa kweli ukiangalia historia ya nchi yetu na zaidi sera za serikali yetu kuhusiana na suala zima la elimu na sio katika fani ya uandishi wa habari tu, utang’amua kuwa mfumo mbovu wakutojali elimu bora ni moja ya sababu kuu ya tatizo hilo. Hata hivyo ukosefu wa nia thabiti, utashi wa kutetea haki zao na hata uzalendo wa kweli, ndugu zangu waandishi wa habari ambao mimi huwaita wahandisi wa habari, wamegeuka kuwa makuwadi wa unyang’au unaoendelea kuligubika taifa letu.

Ndugu zangu hawa ama kwa kupenda au kulazimika kimazingira wamegeuka kuwa watetezi na waficha maovu ya manyang’au wa nje na wa ndani.

Ndugu zangu hawa wameamua kuwa wasadifu wa manyang’au wa nchi yetu na mfumo wao. Kazi yao kubwa imekuwa ni kuhalalisha na kuusimika mfumo wa kinyang’au uliojengeka katika nchi yetu katika fikira za watanzania.

Waandishi wetu wamekuwa tayari kuwapaka rangi za kuvutia baadhi ya manyang’au wa nchi hii, wakubwa wao kwa wadogo, na kuwavika sura ya utakatifu mbele ya watanzania walio wengi.

Wakati vyama vya upinzani vikiwa vimenyang’anywa nguvu za kutekeleza ipasavyo jukumu kukosoa na kuwaeleza wananchi ubaya ama uwongo wakubwa wa mfumo wetu wa kinyang’au, ndugu zangu waandishi wameamua kuwaacha watanzania katika msitu wa giza.

Wanahabari wetu wanapaswa kujua kuwa ushabiki wa ajabu wanao uonyesha kwa watawala wetu ambao miongoni mwao wamelewa utamaduni wa kuwadhulumu watanzania haki zao za msingi, unalipeleka taifa letu katika mustakabali wa kutisha.

Ni wazi kuwa kama ndugu zetu wanahabari hawatazinduka na kuanza kutekeleza kwa dhati wajibu wao kwa wananchi, kuna hatari ya wajanjawajanja miongoni mwetu kutulazimisha kurudi rasmi katika enzi za siasa za chama kimoja.

Wakati wa uchaguzi na mchakato mzima ndani ya vyama kuelekea katika uchaguzi huo, tulishuhudia jinsi kujitokeza wazi kwa hali hii ya ukuwadi miongoni mwa ndugu zangu.
Mwanzoni wengi wetu tulidhani kuwa hilo lilikuwa ni zoezi muda mfupi la wachache kujipenyeza katika timu ya ushindi na wengine kutimiza wajibu wao kutoka kwa wafadhili wao waliogeuka kuwa waajiri mbadala wao.

Lakini kwa hali inavyoendelea hivi sasa, inaelekea uozo uliopo ambao tayari umeshatanda katika nyanja zote za fani hii ya uandishi. Hii ni kuanzia wamililiki, waajiri, wahariri, waandishi wa kawaida na hata wasomaji umesababisha donda ndugu ambalo linaweza likashindwa kutibika.

Wapo waliofikia hata kubeza na kudhihaki juhudi za wachache waliokubali kuchukua jukumu la kuendeleza mapambano ya kutukomboa katika mfumo butu wa utawala wa chama kimoja. Tabia hii ya kuwakuwadia manyang’au kwa kutumia wino ni kuwageuza watanzania kuwa kama bendera inayofuata upepo ambayo haina uwezo wa kuhoji maamuzi yanayobariki unyang’au katika jamii yetu.

Kukuwadia unyang’au wa aina yoyote na mahala popote ni kujidanganya nafsi zetu. Sumu ya unyang’au kamwe haiachi kumdhuru kila mtu katika jamii husika na hata ile ya mbali. Hata kama madhara yake hayataonekana kwa mhusika binafsi wakati wa uhai wake, ni lazima itamsibu huko aendako kupitia kwa vizazi vyake.

Hivyo, ni wajibu wa ndugu zangu waandishi wa habari kuwa wa mwanzo kujinasua katika laana ya unyang’au kwa kuacha kuwakuwadia makuwadi wetu, wa ndani na nje na kuwaonya wengine wa aina yao katika sekta zengine.

MWANZO WA SAFARI YA MWISHO YA CCM

@2005..Published by by a local Tanzania Newspaper

Ni ukweli usiopingika kuwa matokeo ya uchaguzi wa mgombea wa nafasi ya urais katika Chama Cha Mapinduzi yameweza kuliepusha kundi hili kisiasa katika hatari ya kugawanyika kwa kasi kama ilivyokuwa ikionekana awali.

Naongelea dhana ya kugawanyika kwa kasi tu, kwa kuwa nina uhakika kuwa mwenendo mzima wa siasa za uchaguzi huo na mambo kadhaa yaliyojitokeza katika siku za mwisho za shughuli hizo ndani ya chama hicho, zimeleta mgawanyiko mkubwa na wa hatari zaidi utakaodumu daima.

Hata kama kwa njia za ajabu mno ndugu hawa wameweza kumchagua mtu ambaye kwa maoni yao wana uhakika wa kuendelea kutawala watazania kwa miongo kadhaa ijayo.
Ni wazi kuwa CCM ya sasa si ile tena iliyokuwa ikiwavutia watu kwa utulivu wake, uongozi wa kufuata maadili ya utanzania, falsafa zake zenye kujali utu, kupinga ubaguzi na mengineyo mengi mazuri yaliyokuwa yakitofautisha chama hiki na makundi mengine ya kisiasa.

Chama cha mapinduzi kama ilivyo kwa vyama vingine vikubwa tawala barani afrika, kimepitia mabadiliko mbalimbali hadi kufikia sasa.Mabadiliko hayo yameanzia kutoka kuwa chama cha ukombozi, kikaja kuwa chama cha kujenga utaifa na baadaye kuwa chama cha kuimarisha uchumi na kuboresha maisha ya watanzania kabla ya sasa kugeuka kuwa chama cha kuhakikisha kuendelea kubaki madarakani kwa tabaka tawala.

Mbadiliko huu umekuja kutokana na nguvu mbalimbali za kimfumo na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani ambayo yamepelekea washika dau wa chama hiki ambao mwanzo walijitahidi kukabiliana vilivyo, kuamua kufuata mkondo wa mabadiliko ili kuweza kuendelea kuongoza taifa hili.

Mfano mkubwa wa mabadiliko haya nje ya mipaka yetu ni chama cha Labour cha Uingereza kinachoongozwa na mwanasiasa “kijana” machachari Tony Blair. Chama ambacho wiki iliyopita kilipata pigo kubwa la kisiasa kwa kupoteza viti vingi katika baraza la wanaojiita wawakilishi wa makabwela.

Kama ilivyokuwa CCM, chama hiki kilianzishwa kama kundi la kutetea wafanyakazi na makabwela wa Taifa hilo la kibwanyenye. Na mama ilivyo kwa vyama vingi vya aina hii duniani, chama cha Labour kama kilivyokuwa CCM hapo awali, kilikuwa ni chama kinachoendeshwa na misingi na falsafa madhubuti za kutetea wanyonge.

Falsafa na misingi ambayo walijiwekea ili kila anayetaka kuchaguliwa kukiongoza chama hicho na hivyo kugombea nafasi ya kuongoza serikali ya Uingereza alipaswa kuonyesha wazi kuwa ni mfuasi makini na mwaminifu wa misingi hiyo kwa kauli thabiti na vitendo.
Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani yalikipelekea chama hicho kukosa mvuto wa kuaminiwa na wapiga kura wengi na hivyo kuwekwa kando katika kuingoza Uingereza kwa miaka kadhaa.

Hali hiyo iliwapelekea kundi dogo la wanasiasa vijana machachari wa chama hicho akiwemo bwana.. Mandelson ambaye aliwahi kuishi Musoma, Tanzania kwa miaka kadhaa akitafiti siasa ya ujama na kujitegemea na utaalamu wa kiuongozi wa baba wa Taifa, kuja na mbinu mpya walioita LABOUR MPYA.

Tofauti na Labour ya kihistoria, New Labour kama ilivyo CCM hivi sasa, ililenga matumizi ya siasa za kubabaisha zilizo tofauti na misingi na falsafa asilia ya chama hicho ili kuweza kuwalaghai wapiga kura waliokitupa, kukichagua na kukirudisha madarakani.

Kwao wao ni kuwa mara baada ya kurudi madarakani wangeweza kuzirejesha siasa makini za kihistoria za chama hicho na hivyo kuendeleza misingi na falsafa zake asilia kwa mtindo unaoendana na wakati uliopo.

Kama hapo baadae ilivyokuwa kwa upande wa wahafidhina wa chama cha Republican cha Marekani walipomchagua George W Bush kuwauzia fikira zao za kulinda nafasi ya ubabe wa marekani duniani, Mandelson na wenzake waliamua kumchagua mwanasiasa machachari aliyekuwa akikubalika wakati huo yaani Tony Blair kuongoza mpango huo.
Matokeo yake ni hali inayonekana hivi sasa huko Uingereza. Sio tu chama hicho kimegeuka kuwa cha kinyang’au zaidi kuliko chama cha mahafidhina wa kijadi cha Conservative, hivi sasa kinaelekea kaburini kwa mwendo wa kasi mno. Kitu pekee kinachowezesha wao kuwa madarakani hadi hivi leo sio uhalali wa kidhati kutoka kwa wananchi isipokuwa propaganda za kuwapumbaza wapiga kura. Propaganda zinazolenga kuwaweka mateka Waingereza walio wengi kwa kutumia dhana ya kuwa hakuna mwengine mwenye mvuto kama yeye anayeweza kuwalinda waingereza kwa madhila makubwa zidi kutoka kwa chama cha wahafidhina.

Ukiangalia mlolongo mzima wa historia ya chama cha Labour ni wazi kuwa kuna mambo yanayoshabihiana na hali inayojikita ndani ya chama cha mapinduzi.

Hapo zamani hata baada ya kuruhusu siasa za vyama vingi chama cha mapinduzi kilikuwa ni chama kilichokuwa kinapata wafuasi wengi kutokana na hali ya kuwa wengi wa wananchi hawa walikuwa wakijinasabisha na misingi na falsafa za chama hicho.

Hata kama wengi walikuwa wakikatishwa tamaa na matendo ya viongozi walio wengi wa chama hicho ambayo ni tofauti na sura yake asili, kuwepo kwa umakini wa kimaamuzi haswa yale makubwa kama vile mtiririko mzima wa kubadilishana madaraka kuliwapa faraja wanachi wengi waliokuwa wanaendelea kukata tamaa.

Hili na lile la kuwepo kwa baadhi ya viongozi wachache ambao tofauti na walio wengi, kauli zao na matendo yao yenye kuonyesha kuendelea kwao kuamini misingi na falsafa asilia za chama hicho, kuliwapa moyo wa matumaini watanzania walio wengi, wanachama na wasio wanachama.

Hali hii iliweza kuwazuia wanachama waaminifu wa chama hicho vijana kwa wazee, wenye sifa za umakini wa hali ya juu kutokisusa ama kutohama chama hicho kwa muda mrefu sasa. Wengi hawa walikuwa bado wakiamini kuwa ipo siku chama hiki kitapata uongozi imara na makini utakaowezesha kurudisha chama na nchi yetu katika mstari ulionyooka na kuachana na siasa za sera za kukurupuka kwa minajili ya kuwalaghai wapiga kura tu. Ndio maana hata hivi karibuni tulipokuwa tukishuhudia siasa chafu za kupindukia mipaka ya utanzania na ubinadamu kwa ujumla, bado walikuwepo waliukuwa wakiamini kuwa mwishoni busara za uongozi wa chama hicho zingesimama na kurekebisha mambo.

Hata hivyo hilo halikutuokea na waliukuwa wakiaminiwa kwa kazi hiyo ama walinyamaza kimya, walinyamazishwa au waliamua kukubali yaishe na kubariki siasa chafu zenye kukiuka misingi madhubuti ya chama hicho kutawala maamuzi ya vikao vyake vikuu.
Yote yanaweza kufumbiwa macho lakini kitendo cha Mwenyekiti wa chama hicho kuamua kuzuia taarifa ya siri ya sekretarieti ya maadili ya chama hicho iliyokuwa ikielezea vigezo vya kimaadili vya wagombea wote kuzungumziwa na wanakamati kuu ni kosa kubwa la kihistoria.

Maelezo kuwa wote wametoa rushwa hivyo wote sawa, kwa kweli ni upuuzi wa hali ya juu ambao kamwe hakuna aliyefikiri kuna siku mwenyekiti wa chama hicho anaweza akaufanya (sasa tunajua ni kwa nini).Hata kama historia na tafiti mbalimbali zinaonyesha wazi kuwa chama hiki kimekuwa kikumbatia rushwa na kiongozi wake kuishia kutoa vitisho vya mdomo tu, lakini inapofika mkuu huyo anahalalisha uchafu huo ambao ni tofauti na nguzo kuu asili za chama hicho ati kwa kuepusha kubomoka kwa chama, ni wazi safari ya mwisho imewadia.

Lingine ni lile la kuruhusu wanakamati kuu ambao wengine ni viongozi waandamizi bila ya aibu kutumia siasa ya ubaguzi ndani ya vikao vikuu kama hivyo. Pale wahuni kadhaa walipokuwa wakitumia siasa haramu na chafu kama hizo kwenye vyombo mbalimbali vya habari, halali na haramu, baadhi ya watanzania makini ambao ndio walikuwa ngome ya mwisho wa chama hiki waliweza kuelewa na kuvumilia.

Lakini pale anapokuja mtu mkubwa kama Waziri mwandamizi akasimama akipinga kuchaguliwa kwa fulani kwa kuwa amezaliwa akiwa na mchanganyo wa kabila au rangi fulani, na wakubwa hao wakapigia makofi, kunyamaza au mwenyekiti akahalalisha jambo hilo kama ni demokrasia, kwa kweli hiyo ni ishara mbaya mno.

Vilevile ni dalili mbaya pale wakuu wa chama hicho na haswa wazee wa busara waliokuwa katika makuzi ya siasa asilia za chama hicho na wengine kushiriki katika ujenzi wake wanapokuwa tayari kuweka kando maslahi ya watanzania kwa ujumla na kujali ushindi wa chama tu kama dira yao kuu ya kufanya maamuzi.

Ushindi ambao kwao wao ni muhimu tu kutokana na uhakikisho wa kuwa wao na vizazi vyao vitaendelea kuwa madarakani daima milele hata kama ishara zinaonyesha kupotea kabisa kwa utaifa wetu ambao ndio umekuwa nguzo yetu muhimu kama nchi na jamii staarabu.
Kwa ujumla ingawa wengi wanaamini kuwa chama cha mapinduzi kimeweza kuvuka mtihani mkubwa kwa ushindi, ni wazi kuwa ushindi huo unaendana na kujisimika rasmi kwa siasa mpya zisizojali misingi na falsafa asilia za chama hicho ambazo kwa kweli ndizo zimekuwa nguzo kuu za kuendelea kwa uimara wake wakati wote huu.

Siasa hizi mpya ambazo zinalenga wingi wa kura tu na sio mipango madhubuti ya muda mrefu yenye kulenga kustawisha jamii kwa mapana na marefu daima haziwezi kuifanya CCM kuendelea kuwa chama cheney mvuto asili ambo hata kama mambo hayaenda sawa wananchi wataendelea kukiamini na kikihamini.

Siasa hizi zinazofuata mbinu za soko huria ambazo zinalenga kumnadi mtu kama bidhaa nyingine sokoni zinafanya chama hicho kutegemea uhalali wa umaarufu wa mwanasiasa huyo tu na sio mapenzi na imani juu ya chama hicho.

Bahati mbaya umaarufu huu unajengwa na matarajio hewa ndani ya mioyo ya wananchi, ambayo ama kwa mapungufu ya kiutendaji ya mwanasiasa huyo au ya kimfumo ni vigumu kuyafanikisha.

Hivyo basi kukifanya chama hicho kuwa mateka wa mwanasiasa huyo na wajanja wachache waliomzunguka wanye uwezo wa kucheza na akili za wapiga kura kwa muda Fulani tu.
Hawa huwezesha hilo kwa kutumia mbinu mbalimbali za kihadaa ambazo daima huishia ama kuvuruga jamii au kuchokwa na wapiga kura.

Wapo wanaofikiri kuwa kupatikana kwa mgombea na baadaye kiongozi mwenye mvuto kama aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa ni silaha muhimu ya kuhakikisha uimara wa chama hiki.

Mimi nasema ndio lakini ni kwa muda mfupi tu na hiyo hiyo ndiyo silaha ya kujiangamiza kwa muda mrefu.

Ni dhahirikuwa ushindi uliopatikana Dodoma hivi karibuni ni mwanzo wa safari isiyo rasmi ya mwisho ya chama cha mapinduzi.

NINI FALSAFA YA MAPINDUZI YA CHIMWAGA 2005?

@2005..Published by Mtanzania Jumapili soon after CCM nomination process.

Baada ya miaka mingi ya Chama Cha Mapinduzi kudorora na kukosa chachandu zinazoendana na jina lake hatimaye katika hali ya kustajabisha kabisa Mapinduzi mengine ya ndani yametokea.

Ni ukweli usiofichika kuwa moja ya mbinu iliyotumika katika kuhakikisha kuwa mheshimiwa Jakaya Kikwete anashinda mchakamchaka wa kuchaguliwa kugombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi, ni kauli mbiu inayosema ARI MPYA, KASI MPYA NA NGUVU MPYA.


Lakini kubwa zaidi ni kuwa kauli mbiu hii ilikuwa na bado inaendelea kuashiria kufanyika kwa mapinduzi makubwa ndani ya CCM. Mapinduzi ambayo kwa kiasi fulani yamefanikiwa ingawa mengi bado yatakiwa kufanyika.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na kukua kwa mtindo wa vijana wengi wa kizazi kipya kuvaa fulana zenye picha za viongozi mbalimbali duniani ambao wamekuwa wakihusishwa na mapambano mbalimbali ya kimapinduzi.

Miongoni mwao, picha ya Hayati Ernesto Che Guevara ndio imekuwa maarufu zaidi kama ilivyo katika jamii zengine za vijana katika nchi mbalimbali duniani.

Kwa wale wasiomjua Che Guavara, huyu ni mwanamapinduzi mwenye asili ya Argentina kule Amerika ya kusini.

Mwanamapinduzi huyo amefanya mengi katika kupigania kuundwa kwa jamii isiyo na matabaka na inayoheshimu thamani ya utu wa kila mtu.

Katika jitihada zake hizo ambazo zilikuwa zikiongozwa na dira ya falsafa ya mapinduzi ya kijamaa, Che Guevara alijitolea muhanga maisha yake kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano ya ukombozi kuondoa tawala mbalimbali za kibepari uchwara katika pande zote za dunia.

Ni yeye ndiye akiwa begabega kwa bega na kiongozi wa CUBA, Mwanamapinduzi Fidel Castro katika mapinduzi ya CUBA. Mnamo maka 1959, Che aliongoza majeshi ya walalahoi wa nchi hiyo kuuteka mji wa Havana na kusimika utawala wa kimapinduzi wa kijamaa unaotawala hadi hivi sasa.

Ni Che ndiye aliyeamua kuacha maisha ya anasa ya kuwa waziri muhimu katika seriakali ya CUBA na kuja afrika kusaidiana na wanamapinduzi kadhaa kama Mzee Ben Bella wa FNL ya Algeria. Baadaye alijipenyeza hadi Kigoma, Tanzania alikokwenda kusaidiana na Marehemu Mzee Kabila wa DRC.

Wakati huo Mzee Kabila alikuwa akiongoza kikundi cha wanamapinduzi wanaofuata falsafa za kijamaa waliokuwa wakijaribu kurudisha madarakani masalia ya utawala wa mwanamapinduzi mwengine, Hayati Patrice Lumbumba.

Baada ya hapo, Che alienda nchi zengine zilizokuwa zikikabiliwa na unyang’au wa tawala za kibepari ambazo zilikuwa zikiongozwa na viongozi vibaraka wa Marekani, akiwa na mkoba wake uliojaa fikira za kimapinduzi.

Maisha ya mwanamapinduzi huyu yaliishia mikononi mwa mawakala wa shirika la ujasusi la marekani CIA waliokuwa wakisaidia kuulinda utawala wa kinyang’au wa René Barrientos huko Bolivia, amerika ya kusini.

Inasemekana kuwa picha ya sura ya Che Guevara ndio picha maarufu zaidi ya binadamu yeyote kuchapwa katika vitu mbalimbali duniani.

Mimi ni moja wa vijana ambaye nimetokea kuvutiwa sana na kuvaa fulana zenye picha za wanamapinduzi hawa akiwe,o Che Guevara na kwa kweli huwa najisikia vizuri sana ninapokuwa katika vazi hilo.Lakini hilo ni tofauti na mimi ambaye nilianza kuvaa fulana zenye picha za wanamapinduzi hawa mara baada ya kusoma na kuwafahamu katika vitabu mbalimbali.

Wengi wa vijana wenzangu nchini wamekuwa wakivaa mavazi ya aina hii bila hata kujua mtu huyo wanayemshabikia ni nani na ni nini alichokuwa anakiamini na kukisimamia katika maisha yake.

Wengi hawajui kabisa ni falsafa gani ambayo Che Guevara alikuwa akiamini na jinsi gani alivyokuwa akichukia kwa ukweli kabisa madhila yaliyokuwa yakimsulubu mwanadamu yeyote yule katika pande zote za dunia.

Hali kama hii imekuwa ikionekana katika kinyang’anyiro cha na nafasi ya kugombea urais ndani na nje ya CCM.

Katika CCM kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa na mabadiliko ya sura katika ngazi za uongozi wa chama hicho kuanzia kata hadi Taifa. Kuna wakati mabadiliko haya yalikuwa na baraka zote za viongozi wa chama hicho haswa wale wazee kama “Komredi” Kingunge Ngombale Mwiru, Mzee Rashid Kawawa, Mzee John Malecela na wengineo.

Kwao wao waliamini kwa dhati kuwa damu mpya inahitajika ili kuhakikisha kuwa chama kinaendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya jamii ya watanzania ambayo vijana ndio wawakilishi wakuu.

Bahati mbaya wazee hawa hawakuweka wazi vijana wa aina gani wanaotaka wao waaminiwe na kukabidhiwa dhamana ya kuwaongoza wenzao. Kosa ambalo sasa limewafanya wao kujikuta na mtihani mgumu wa kuamua ni nani haswa anapaswa kuaminiwa kupewa nafsi ya kuwa rais wan chi yetu kwa miaka mitano au kumi ijayo.Mtihani ambao ulihitimishwa kule Dodoma wiki iliyopita ambapo kwa kweli waliweza kuushinda kwa busara za hali ya juu.

Kwa kweli mimi kama kijana ningelipenda kuona mapinduzi haya yakitokea ndani ya chama hiki ili kukipa nguvu mpya na uhalali wa kutosha kutawala kwa ufanisi zaidi.

Lakini tatizo linakuja pale ambapo ninapoona kuwa dhana ya mapinduzi ndani ya chama ambayo hawa “vijana” wenzangu wanajaribu kuionesha inakuwa imekosa kiungo kikubwa muhimu.

Kiungo ambacho ni lazima kuwepo ili mapinduzi yeyote yale ya kisiasa au kijamii yawe yana manufaa kwa mwanachi wa kawaida aliyezingukwa na madhila yasiyo na kifani.

Kiungo hiki ni kuwepo kwa falsafa itakayoongoza mapinduzi hayo wakati wa kufanyika na baada ya kufanikiwa kubadili mfumo wa uongozi uliopo katika chama cha mapinduzi.

Siasa za kimapinduzi za mwalimu Nyerere ziliongozwa na fikira za mzee wetu huyu ambaye kwake aliheshimu kila mtu bila ya kujali kipato chake, kabila lake, rangi yake, elimu yake ama utashi wake kisiasa.

Fikira hizi zikiongozwa na kanuni binafsi za mwenendo wa kimaisha wa kiongozi huyu wetu mpendwa zenye kuendeshwa na maadili bora ya kiuongozi ndizo zilizopelekea kutangazwa kwa Azimio la Arusha.

Ni Azimio la Arusha ndilo lilionyesha wazi nafasi ya falsafa ya ujamaa na kujitegemea ambayo ndiyo iliyongoza mapinduzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ndani na nje ya chama cha TANU na baadaye CCM.

Bahati mbaya tofauti na mapinduzi ya wakati huo, mapinduzi tunayoshuhudia sasa kwa kweli yamekosa kabisa kuweka wazi falsafa ambayo inaonyesha kuwa ni mapinduzi yanayolenga masilahi za mtanzania wa kawaida na sio vinginevyo.

Hivi karibuni niliweza kupata habari nyeti ambazo zilikuwa zikionyesha wazi ni wajumbe gani ndani ya halmashauri kuu ya CCM ambao wanatambulika kama wafuasi wa mapinduzi haya.

Kwa kweli ukiangalia hao wafuasi tuu ni dhahiri kuwa wengi wao si tu wamekosa utashi wa dhati wa kimapinduzi lakini zaidi hata upeo wao wa siasa za kimapinduzi ni mdogo mno.

Wengi wao katika maisha yao ya kawaida wameonyesha kuwa makuwadi wakubwa wa siasa za kibepari uchwara zenye kujali maslahi binafsi.

Wengi wao kwao ukombozi wa mtanzania wa kawaida utatokea pale tuu wao na washirika wao wachache watakapoweza kupata madaraka zaidi.

Wao ni walokole wa dhana mpya ya utajirisho inayojikita katika nchi yetu.
Dhana ambayo inaelezea kuwa dawa ya umasikini katika nchi yetu ni kuwaacha wao wachache wenye nafasi katika uwanja wa siasa na maharamia wenzao waruka kodi watajirike zaidi bila kujali maslahi ya walio wengi.

Kwa kweli dhana hii ndio inayoendesha fikira za ndugu zangu hawa waliojivika kilemba cha uwanamapinduzi. Uwanamapinduzi unaodai kulenga ukombozi wa mimi na wewe na yule.
Si bure kwao wao kuyachukulia mapinduzi yao ni ya kirika na kamwe si kifikira.

Kama ni fikira za umimi na usisi zenye kusadifiwa na falsafa ya ubinafsi ambayo sidhani kama ni falsasfa muafaka ya kuwasaidia watanzania walio wengi ambao kwao wao tatizo si sura bali mfumo mzima wa kisiasa uliowazunguka.

Tatizo la wanamapinduzi hawa wa karne mpya ni kuwa wengi wao na zaiid wale walio karibu zaidi na chaguo lao wamekosa utashi wa kujiendeleza kifikra kwa kukosa ustarabu wa kujisomea.

Wengi wao hawana tofauti na vijana wenzangu niliowaelezea hapo juu ambao wanavaa fulana na nembo zinazonyesha wanamapinduzi mbalimbali bila hata kujua nini watu hao walikuwa wakisimamia

Hawa ni wanamapinduzi wa CNN, BBC na MNET ambao kwao wao shule pekee ya kimapinduzi ni ile wanayoiona katika vyanzo hivi vya habari vikionyesha kinachoitwa “mapinduzi” mbalimbali yanayotokea katika nchi za Ulaya ya mashariki na kati.

Hawajui kwamba mapinduzi haya hayana tofauti na mapinduzi kibwanyenye yaliyotokea Uingereza, Ufaransa, Marekani katika karne kadhaa zilizopita ambayo badala ya kumkomboa mwananchi wa kawaida kutoka katika unyang’au wa kikabaila, yalisimika makabaila wapya katika sura ya ubinafsi wa kibepari.

Mbaya zaidi ni kuwa tofauti na mapinduzi hayo ya kibwanyenye ambayo yalikuwa na mwongozo wa kifalsafa uliojengwa na ujuzi wa kisayansi, mapinduzi haya ya “vijana wa CCM” yamekosa ufanisi wa kisayansi na kielimu ambo ungeweza kujenga falsafa bora na makini.

Wengi wa wahubiri wa mapinduzi haya hawana elimu wala uzoefu ya kutosha ya siasa za kidunia ambazo zingeliwawezesha kuwa na dira imara ya kulinda mapinduzi hayo mara baada ya wao kuweza kutwaa madaraka ya dola.

Na wale walioweza kubahatika kujua umuhimu wa hilo kutokana na elimu kubwa waliyonayo wengi wao wamechoka kifikira na wameamua kusalimisha silaha zao na kujitwika majoho ya ubinafsi wakisema kubali yaishe.

Wao (wasomi wachache walio katika kundi hili) wamechoka na dharuba za kimaisha wanazozipata kuotokana na misimamo yao iliyokuwa ikilenga jamii bora zaidi.

Wameamua kujiunga na timu ya ushindi na kusema kubali yaishe, bora hichi kidogo kuliko kuendelea kukosa kabisa.

Kwa kifupi wote kwa pamoja wanaamini kuwa ili kurekebisha mambo kwa haraka zaidi ni bora kuja na dhana ya mapinduzi ya kirika yenye kulenga mbadiliko wa kisura katika nyanja za utawala bila ya kujali nafasi ya fikira mbadala katika mapinduzi hayo.

Fikira ambazo zinaonyesha umakini wa kiongozi wa mapinduzi hayo ambaye daima ndiye anayetakiwa kuhodhi mawazo dira ya mapinduzi hayo na yeye mwenyewe kuweza kuyauza kwa walengwa ili kupata uhalali wao.

Inapotokea kuwa kiongozi wa mapinduzi hayo anakosa au anashindwa kuweka wazi fikira za kiuanamapinduzi zenye kujengwa na kulindwa na fasafa makini ya ukombozi wa kweli, basi hizo ni dalili mbaya za matokea ya mapinduzi haya.

Na inapotokea kuwa kiongozi wa mapinduzi hayo anakuwa amezungukwa na manyang’au wenye uchu tu wa madaraka na utajirisho wao binafsi. Waliojaa kashfa za kuwadhulumu wananchi wa kawaida basi hiyo ni dalili ya hatari kubwa zaidi.

Hata kama kiongozi huyo amekuwa akilelewa kifikira tangia ujana wake, mazingira kama yaliyomzunguka kiongozi wa mapinduzi haya yanaonyesha uwezekano tofauti kidogo.

Uwezekano ambao historia za nchi kadhaa zilizowahi kufikwa na hali hiyo zinaonyehsa jinsi gani mapinduzi kama haya yameweza kupelekea kueseka, kuabika, kunyanyasika na kuuawa kwa mamilioni ya hao waliokuwa wakidhani wanapiganiwa.

Lakini yote haya yanatokea na makosa waliyofanya wazee hawa wa CCM ambao kuanzia miaka ya mwanzo ya tisini wamekuwa wakiruhusu kila mtu kuingia katika ngazi za uongozi za chama hicho. Bila ya kujali utashi wake wa kuwahudumia wananchi na sio kujihudumia yeye binafsi.

Mbaya zaidi inakuja pale ambapo chama hiki kilipoondoa umuhimu wa elimu ya maadili na ya kifalsafa ambayo hapo mwanzo kila anayejiunga na chama hicho na haswa vijana alipaswa kipitia.

Makosa haya yote na lile la chama chenyewe kukosa mwelekeo wa kifalsafa zaidi ya falsafa ya ubinafsi ndivyo vimepelekea chama hiki kujikuta njia panda katika kuamua kama jee mapinduzi ya aina hiyo ni ya muafaka au la.

Mungu ibariki Tanzania
Mungu ibariki afrika
Mapambano daima.

MPAMBANO KATI YA SIASA ZA UMAARUFU, UHAFIDHINA NA UMAKINI NDANI YA CCM: NINI HATMA YA MTANZANIA.

@2005..Published by RAI
NA ILYAS, O. S

Ilikuwa miaka, ikaja miezi na sasa imebakia wiki moja tu watanzania wachache watukufu katika ulingo wa maamuzi ya nchi wakutane kule Dodoma katika madhabahu makuu ya siasa nchini kuamua ni nani anapewa nafasi ya kugombea ubwana mkubwa wa nchi yetu kwa tiketi ya kile kinachoitwa chama cha mapinduzi.

Mimi kama mtanzania mwanachama wa chama kinachoitwa TANZANIA kinachofuata imani ya MWAMKO WA UAFRIKA naamini ni wajibu wangu kuchambua na kuelezea yale ninayoyaona yakiendelea na yatakayoendelea wakati na baada ya uchaguzi huu bila ya woga na hata kama nafasi yangu kubadilisha mawazo ya ndugu zangu wa CCM ni finyu mno.

Chama cha mapinduzi kama yalivyo makundi mengine yenye nia ya kuwa na uwezo wa kisiasa na kikatiba kushikilia mihimili ya nchi inayotoa na kuelekeza maamuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika dola lolote, daima huwa katika mivutano ya hapa na pale inayoletwa na tofouti mbalimbali miongoni mwa wanakundi hilo.

Mivutano hiyo inaweza kuwa ya kifikira, kiutashi, kimuono ama kimaslahi. Mivutano hiyo inaweza kuwa ya siri ndani ya wanakundi pekee, inaweza kuwa inatokana na mawazo ya wanakundi pekee au kama ilivyo sasa kwa CCM ikawa ya wanakundi wakishirikiana, kuhusisha au kuendana na mawazo ya wasio wanakundi kutoka ndani au nje ya mipaka ya nchi yetu.

Kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa yakiendelea ndani ya kundi hili linaloitwa Chama cha Mapinduzi. Mabadiliko ambayo yanalenga kulifanya kundi hili kuendana na fikra za baadhi ya wanakundi hilo.

Wanakundi ambao wanadhani kuwa fikra zao ni bora zaidi kwa maslahi ya nchi na wananchi wake, chama na wanachama wake na vilevile maslahi binafsi ya baadhi ya wanakundi hili ambao nao wamejenga vikundi uchwala vyenye lengo la kufanikisha fikira zao, utashi wao, muono ama maslahi yao binafsi.

Ili hilo lifanikiwe wanakundi hawa wamekuwa wakitumia mbinu mbali mbali halali na haramu kufanikisha mapambano au mikakati yao dhidi ya fikira na muono tofauti wa wanakundi wenzao.

Baadhi ya mbinu ni kama kuanzisha vikundi uchwara ndani kundi kuu yaani CCM, kushirikiana na wanambinu mbalimbali kama vile wasomi, waandishi wa habari, viongozi wa kijamii, vyombo vya dola na hata wafadhili kutoka ughaibuni kueneza, kuzipamba na kuzilinda fikra zao kwa wananchi ili waweze kupata uhalali rasmi kutoka kwao.
Lakini ili hili lifanikiwe ni lazima waweze kushika hatamu za madaraka ya dola kwa kumweka yule wamuonaye ni chaguo bora kuwaongoza katika kufanikisha utekelezaji wa fikra na maslahi yao.

Hapa ndipo tunapokuja katika umuhimu wa suala zima la mbio za kugombea nafasi ya urais wa Tanzania kupitia kundi kuu la CCM na baadaye uongozi mkuu (uenyekiti) wa kundi hilo kama taratibu walizojiwekea ndugu hawa.

Kwa upeo wa uchambuzi wangu wagombea wote wa CCM wanawakilisha makundi makuu matatu. La kwanza ni lile linawakilisha fikira za siasa za umaarufu, la pili ni lile linalowakilisha wanakundi wenye kuamini siasa za kihafidhina na la tatu ni lile linaloamini umuhimu wa siasa za umakini.

Ingawa kuna wagombea zaidi ya kumi lakini ukweli ni kuwa wote hawa ni wawakilishi wa moja ya makundi haya ambayo yana wagombea halisi na wagombea vivuli.

Kwa wale waliosoma makala yangu iliyopita niliyoiita KIKWETE CHAGUO MAARUFU, SALIM CHAGUO MAKINI ni wazi wameshajua viongozi wa makundi mawili. Kundi la tatu ni lile linaloongozwa na mgombea mwingine machachari ndugu MALECELA.

Wengi mnaweza kudhani kuwa chimbuko la makundi haya ni miaka miwili au mitatu ya hivi karibuni.

La hasha, chimbuko hasa la siasa hizi za kimakundi ni miaka ya mwanzo ya themanini ambapo hata kama mimi binafsi nilikuwa mdogo sana kwa umri, lakini utundu wangu wa kuhoji uliweza kuniangaza na kung’amua mwanzo wa mwisho wa CCM imara na hata Tanzania ya amani tuliyokuwa tunajivunia popote pale duniani.

Chimbuko hili mimi naliita chimbuko la falsafa ya UNYANG’AU iliyozaliwa rasmi kule katika visiwa vilivyokuwa vikijulikana duniani kote kama vya marashi ya karafuu na sasa vinaelekea kupata umaarufu wa kufananishwa na marashi ya damu.

Hivi ni visiwa vya Zanzibar ambako ndipo ule mkutano maarufu wa wateule wa mtetezi wa kweli wa siasa za upendo, heshima, maadili na umoja kwa jina la siasa za Ujamaa, waliamua kukaa chini na kuondokana na kile walichokiona ni ushamba wa kifikira wa hayati mzee wetu, Mwalimu Nyerere.

Hili sio lingine bali ni azimio la Zanzibar la mwaka 1986 ambalo pamoja na mambo mengine liliondoa nguzo muhimu za uimara wa jamii yetu zilizokuwa zikisisitiza maadili ya kiuongozi na siasa nadhifu zenye kulinda na kupigania maisha mema kwa wote bila ya kujali hali ya kimaisha, nafasi ya kisiasa au kidola, tofauti za kidini na kabila au asili ya mtanzania.

Falsafa hii ya unyang’au ndio iliyozaa makundi makuu mawili yaani kundi la siasa za kihafidhina na kundi la siasa za umaarufu. Matokeo ya kuchipua, kujikita na sasa uwezekano wa kushika hatamu kwa siasa hizi ndizo zilizopelekea kuzindukana na kutahayari kwa kundi la siasa za umakini.

Ni wazi kuwa miongoni mwa wana makundi haya ndani ya CCM kwa njia moja au nyingine wameshiriki katika ile hafla ya kuzaliwa rasmi kwa falsafa ya unyang’au kule Zanzibar. Ama walikuwa miongoni mwa waliosimamia kupitishwa kwake au walikuwa katika nafasi ya utazamaji tu wakidhani kuwa wao ni vichuguu wasingeweza kupambana na mibuyu ya wakati huo.

Lakini vilevile inawezekana walidhani kuwa zoezi hilo lilikuwa ni la busara ambalo kwa mahesabu yao lingewawezesha kuondokana na umasikini mali uliokuwa ukiwakumba wakati huo ambao kwa mtazamo wao ni falsafa za siasa za ujamaa ndizo zilikuwa chanzo kikuu.

Miaka kadhaa ya majaribio ya falsafa hii ya unyang’au ilipeleka baadhi ya wanakundi kuu kuanza kujiuliza kama falsafa hii ni bora na zaidi ina mnufaisha nani. Hapa ndipo lilipoibuka kundi la siasa za uhafidhina ambalo lilinza kujijenga na kujipanua katika miuondo mbinu yote ya kiutawala ili kuhakikisha kuwa falsafa hii ambayo iliweza kuwaonyesha nuru yao kimaslahi inabaki kutawala taifa letu.

Kundi hili lilitumia mbinu mbali mbali hata ikafikia wakati likawa tayari hata kuvunja muungano wa nchi yetu ilimradi kuondokana na kanguvu cha ajabu cha baba wetu wa taifa aliyeweza kung’amua hatari ya kusimikwa kwa falsafa hii ya unyang’au kwa kusingizia Utanganyika na Uzanzibari. Baba wa taifa alijaribu kupinga safari hiyo ya wahafidhina waliokuwa wakijaribu kushikisha hatamu kwa falsafa yao ya unyang’au wakati huo.

Upinzani ambao aliweza kuendeleza hadi katika uchaguzi wa mwaka 1995 lakini bila ya kujua akapigwa chenga ya mwili na wajanja wajanja wachache walioweza kumlaghai kuwa wao wana dawa ya tatizo lilikuwa likimuumiza kichwa chake.

Matokeo yake hadi mzee wetu huyu alipoelekea dunia nyingine ambako hivi sasa nina uhakika amekuwa BIZE akipokea ripoti mbalimbali za hali mambo hapa kwetu kwa wajumbe waliomfuata hivi karibuni, Unyang’au umeendelea kishamiri na hivi sasa unajaribu kushika hatamu kwa sura mbii tofauti.

Kushamiri kwa unyang’au na uwezo wake wa kuamsha chuki za kimfumo miongoni mwa watanzania wengi kumepelekea kuibuka kwa kundi la siasa za Umaarufu katikati mwa miaka ya tisini kama fikra mbadala za uny’angau uliokuwa ukiendeshwa na kulindwa na wanakundi la kihafidhina.

Ama kwa uchungu wa nchi yetu na watu wake (fikira ambayo najaribu kuendelea kuiamini ingawa mengi yananielekeza tofauti) au kwa POLITICAL OPPORTUNISM, kundi la siasa za Umaarufu limeweza kuibuka ndani ya kundi kuu na kujaribu kuonyesha kuwa lenyewe linaweza kumalizia kazi aliyoianza baba wa taifa ya kuondoa unyang’au na manyanga’au wote kutoka katika mihimili ya kisiasa na kidola nchini mwetu.

Kundi hili lilibahatika kupata baraka za wananchi wengi waliochoshwa na madhila ya unyang’au huu ambao umeleta umasikini na aibu za kimaisha zisiso na kifani miongoni mwa watanzania walio wengi.

Ni ukweli usiofichika kuwa kundi hili ambalo lilikuja usoni mwa watanzania wakati wa uchaguzi wa mwaka 1995 na kuzuiliwa kitaalamu na mwalimu Nyerere ambaye aliamini kuwa halijawa tayari kukabidhiwa majukumu makubwa ya kuongoza nchi yetu, lilikuwa limesheheni vijana wachache ambao ni wazi walikuwa na uchungu mkubwa kwa nchi yetu.
Kwa bahati mbaya manyang’au wachache waliona hatari ya kundi hilo mbeleni hivyo kwa mwendo wa taratibu wakaanza kujipenyeza ndani ya kundi hili na hatimaye kushika miundo mbinu yote ya kisiasa.

Manyang’au hawa ambao walijuwa wazi kuwa kamwe hawataweza kufanikisha ndoto yao ya kushika hatamu za kiutawala za nchi hii na hivyo kurutubisha neema zao bila ya kujipenyeza katika kundi hili.

Wao walijuwa wazi kuwa kutokana na laana ya wazi ya baba wa Taifa aliyolipa kundi la siasa za kihafidhina, laana ambayo alikuwa akiendelea kuisisitiza hata katika matamshi yake ya mwisho kabla ya kukatwa kauli, kamwe wateule wao wasingekuwa na nafasi ya kushika hatamu ya taifa letu na kundi kuu yaani CCM hapo baadae.

Hawa waliamua kuelekeza nguvu zao kwa mteule wa kundi la siasa za umaarufu wakijua kuwa kama watafanikiwa kushika hatamu za madaraka nchini na ndani ya CCM wataweza kuendeleza unyang’au wao kwa mgongo wa mteule wa kundi la siasa za umaarufu aliyetokea kuwa maarufu na hivyo kwa mawazo yao ni rahisi kushinda jaribio la ugombea wa urais wakati huu.

Kwa bahati mbaya ama kwa kudhani kuwa ni uamuzi sahihi, mteule wa kundi hili linaloamini siasa za umaarufu zenye mlengo wa kile kinachoitwa utawala mpya na mawazo mapya, amewaachia manyang’au hawa nafasi kubwa katika mkakati wake za kuchukua madaraka ya nchi yetu.

Ndio maana imefika wakati watanzania kwa namba inayokuwa kila kukicha kuanza kuhoji kama kweli hata yeye binafsi ni suluhisho la madhila yanayowakumba na kama kweli anaweza kuundoa falsafa ya unyang’au wakati amekuwa akiwategemea manyang’au na kuachia mbinu za kinyanga’au kutawala mkakati wake kile wanachidai wa kujenga historia mpya hapa nchini.

Pamoja na mambo mengine, kutokana na hali hii ndipo likazuka kundi lingine ambalo ni dogo mno kwa hesabu lakini kubwa kwa kimkakati ambalo linadhani kuwa ni siasa za kanadhifu na kimaadili pekee ndizo zinaweza kutimiza ndoto za mwisho za baba wa Taifa za kuondokana na falsafa hii ya kinyang’au katika kundi kuu, yaani CCM na hivyo Tanzania kwa ujumla.

Kundi hli ambalo linajumuisha watu mashuhuri ambao baadhi yao walikuwa na nafasi katika tawala mbili za mwanzo za taifa letu pamoja na wanasiasa wapya wenye kukerwa na mambo na msuguano wa makundi mengine mawili limejikita chini ya mgombea wamuonaye makini zaidi yaani Dr Salim.

Kwao wao wanadhani uzoefu, ustaarabu, umakini na uaminifu wa kimaadili alio nao mgombea huyu ambaye kwa mara kadhaa marehemu baba wa taifa alipendelea awe mrithi wake wa uongozi wa siasa zake za Kinadhifu, kiupendo na kimaadili, ndio kweli unaweza kutuepusha na madhila ya unyang’au.

Madhila ambayo kama wao hawatafanikiwa yanaweza kuongezeka zaidi endapo waumini wa falsafa hiyo ya unyang’au ndani ya kundi lao la CCM wataweza kushika hatamu ama wao binafsi au kwa kutumia mgongo wa kiongozi mwingine.

Kundi hili linaamini siasa makini ndizo kama ndio silaha muhimu ya mwisho ya kunusuru ya kundi lao kuu (CCM) na Taifa letu na vilevile hatma ya watanzania kwa ujumla. Linaamini kuwa siasa za umakini zenye kuendeshwa na uaminifu wa uongozi wa kimaadili na wenye kung’amua hasara za siasa za kihafidhina na umaarufu sio tu unaweza kuondoa madhila ya unyang’au unao ota mizizi katika jamii yetu lakini vilevile kuepusha janga linalotujia mbeleni kutokana na msuguano wa hayo makundi mengine mawili.

Katika mtazamo wangu ninaamini kuwa angalao kundi hili ndilo linaloweza kutuokoa watanzania na kitimtimu kilichoko mbeleni cha wanamakundi mawili ya umaarufu na uhafidhina ambayo kwa kweli pamoja na mapungufu mengine yameonyesha chuki na uadui mkubwa ambao ni dhahiri ndio utakawo kuwa dira ya ama wateule wao wakuu au wateule wao vivuli watakaposhinda mpambano huu haramu.

Sio tu kwamba itawabidi kusafisafisha wale wanaodhani wanatofautiana na kifikira na kiutashi kuhusiana na vipi nchi yetu iendeshwe lakini vilevile ni dhahiri watalazimika kuwandoa au kuwanyamazisha wale wote waliokuwa wakiwaona ni maadui zao na pengine wakawa kikwazo kwao kufanikisha yale yaliyopelekea wao kuamua kupigania nafasi hiyo ya juu ya kimaamuzi ndani ya chama na jamii kwa ujumla endapo watashika hatamu zote zikiwemo za dola.

Mimi kama nilivyodokeza hapo juu sina mahusiano ya ki-uwanachama na kundi hilo kuu linalojiita la chama cha mapinduzi hivyo kwa kile tunachosema ni kawaida isingenipasa kuingilia mpambano wa ndugu zangu hawa wa CCM.

Lakini nikiwa kama mtanzania na muafrika ninayeamini amani na upendo kama nguzo kuu za uanadamu na mwenye uchungu na nchi yangu hii ninamuomba mungu asikie vilio vya wengi vya kuwaamsha baadhi ya wapiga kura ndani ya CCM.

Ndugu zetu ambao wamegubikwa na ushabiki na tama ya maslahi binafsi waweze kuzinduka na kuona umuhimu wa umakini katika kufikia uamuzi wao wa mwisho ili kuliepesha taifa letu na janga lunalotujia.

Janga la muendelezo wa falsafa ya unyang’au, ama kwa sura ya sasa ama sura, ambayo kwa muda wa sasa ndio imekuwa rutuba bora ya machafuko na ukosefu wa amani kwa taifa letu na hata majirani zetu.

Hatma ya watanzania ipo mikononi mwa ndugu hawa wachache ambao mpaka sasa wameweza kufanikiwa kutwaa utukufu wa kidunia wa kuwawezesha kutuamulia watanzania milioni 36 ni nani atakeyekuwa ameshika uhai wetu wa kifikira na kibailojia kwa miaka mitano ama kumi ijayo.

BARUA WAZI KWA WAPIGA KURA WA CCM..

@2005..published by RAI

Ndugu watanzania wenzangu,
Kwanza hongereni kwa kuweza kuwa miongoni mwa watanzania wachache ambao mungu amewajalia kuwa na nafasi ya juu kabisa nchini mwetu ya kuamua ni nani anakuwa kiongozi wa nchi yetu kwa miaka mitano au kumi ijayo.

Vilevile nawapongezeni kwa kuwa wavumilivu wa madhila ya usumbufu wa hali ya juu kutoka kwa wale wanaowakilisha maslahi ya wakubwa wenzenu wanaotaka kuingia ikulu kwa makeke ya karne.

Ndugu zangu mimi si mwanachama wa chama chenu kitukufu lakini kama mtanzania ninayejua wajibu wangu najua umuhimu mlio nao wakati huu katika kuamua maslahi yangu, ya ndugu zangu na watanzania wenzangu wote kwa ujumla.

Ninajua kuwa chaguo lenu ndilo litakalofanikisha au kuvuruga ndoto zangu nyingi kuhusiana na nchi yangu na bara langu nilipendalo la Afrika.

Ninajua kuwa ufunguo wa chembe ya uhuru ninayo jivunia hivi sasa na nikaweza kukaa hapa nilipo na kuandika barua hii kwenu mnao ninyi na ni ninyi ndio mtakaoamua kama nitaendelea kuwa nao hata baada ya usiku wa tarehe nne mwezi ujao.

Ninajua kuwa ni ninyi wenye kushika mstakabali wa maisha yangu ya upendo na uvumilivu kwa watanzania wenzangu ambao daima nimekuwa nikiwapenda bila ya kujali dini zao, makabila yao, rangi zao ama hali zao za kimaisha.

Ninajua kuwa kura zenu mtakazopiga wiki ijayo ndizo zitakazoamua kama na mimi nitabahatika kuoana na nimpendaye na kuzaa naye watoto wazuri watakaojivunia na Tanzania nitakayowachia.

Ninajua kuwa wengi wenu tayari mmeshamua ni nani mngependa awe rais wa nchi yetu ama kutokana na mvuto wake, ukaribu wake nanyi, umaarufu wake, ucheshi wake, unyenyekevu wake na hata uchapakazi wake mnaodhani kuwa ni muhimu kwa uongozi wa nchi yetu kuondokana na hali tuliyonayo sasa.

Ninajua kuwa wengi wenu mnadhani kuwa ni lazima kulipa fadhila kwa wale waliofanikisha ninyi kupata nafasi hii hata kama kwa masharti ya kudhalilisha kama kulazimika kumpigia kura mgombea wa yule aliyekusaidia kufanikisha mambo na wewe ukapata nafasi uliyona nayo.

Ninajua kuwa wengi wenu mna deni la kulipa kutokana na misaada mbalimbali kama vile kumlipia mwanao ada ya shule, kulipia matibabu yako au ya mpendwa wako wakati akiumwa, au kukupa nafasi ya kwenda kusoma elimu ya juu ama pale mlimani ama kwengineko duniani. Haya yote mliyopata kutoka ama kwa wafadhili mbalimbali waliokaribu na mgombea Fulani ama hata mgombea mwenyewe.

Najua kuwa wengine tayari mmeshaahidiwa nafasi kubwa kubwa za uongozi katika nchi yetu ili mradi mhakikishe kura yako inaandikwa jina la mgombea Fulani.

Najua wengine mna amini kabisa kuwa kutokana na ukweli kuwa wagombea wengine wote ni ‘wachafu’ na wengine sio watanzania basi huna la kufanya ispokuwa kumpigia kura mgombea ambaye mnadhani kuwa ni msafi na hana hata tone la uchafu isipokuwa harufu ya neema tu.

Ndugu watanzania wenzangu naomba uchukue muda huu hata vidakika vichache kwanza kufikiria kama hayo unayoamini kuhusu mgombea huyo ni kweli na hakuna uwezekano kuwa kuna upande mwingine wa mgombea huyo ambaye wewe hujapata nafasi ya kuujua kwa sababu wenye majukumu ya kukujulisha wamelazimika kutokujulisha.

Halafu ndugu mtanzania mwenzangu naomba ufikirie kama kweli vigezo unavyotumia kuamua mtu wa kumpigia kura yako tukufu ni vigezo tosha vya kumpa mtu jukumu zito la kuwa rais wako mwenye nguvu za juu za kimaamuzi katika kila kona ya maisha yako kwa mika mitano ama kumi ijayo?

Hivi vigezo hivyo vimeweza kukusaidia kutambua mtu ambaye kweli na sio anayejidai, ambaye atahakikisha chama chako kinaendelea kuwa na umoja na nidhamu ya kweli iliyowezesha kushinda mitihani mbalimbali ambayo kimekumbana nayo kwa miaka yote hii tangu kianzishwe na wazee wetu waliotutangulia?

Hivi vigezo hivyo vilijitosheleza kukuongoza wewee kufikia uamuzi wako kwa umakini wenye kuhitajika kuamua mtu bora wa kumkabidhi hazina yetu, utamaduni wetu, uvumilivu wetu, upendo wetu, unoja wetu na zaidi maisha yetu na wote tuwapendao na watupendao.
Hivi uamuzi wako umetilia maanani kama huyo utakayemchagua atakuwa ndiye anayetakiwa kukuongoza wewe na familia yako katika mapambano dhidi ya gonjwa la ukimwi kwa yeye mwenyewe kuwa mfano bora wa kubadili tabia.

Hivi huyo mgombea umpendaye au unayelazimika kumchagua ndio kweli yeye atayeweza kuiongoza Tanzania katika dunia hii ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa umakini wa hali ya juu wenye kutambua nini haswa kinatakiwa kifanyike ili nchi yetu iheshimike duniani na hivyo kusikilizwa matakwa yake.

Hivi huyo mgombea anaweza kumlinda mdogo wako, dada yako, kaka yako, mpendwa wako, mwanao au rafiki yako mpendwa na masahiba ya utandawazi yaliyojaa ulaghai na utapeli wa kila aina.

Ndugu yangu umejaribu kufikiri ikiwa ni mgombea wako anayeweza kutuokoa katika janga la kuvunjika kwa amani ya nchi yetu kutokana na tamaa ya madaraka ya baadhi ya wagombea ambao wameamua kutumia mbinu za chuki na visasi ili kufanikisha matamanio yao ya kidunia.

Hivi ni kweli mgombea unayetka kumpigia kura yako anaweza kusema hapana kwa wababe wa dunia pale wanapotka kufanya nchi yetu ni tambara lao bovu la kufutia vinyesi vyao vya kibeberu vinavyopita vikidondoka kila kukicha.

Hivi kweli ndugu yangu hudhani kuwa hata kama una deni la kulipa fadhila za mgombea uliyeambiwa umpigie kutokana na mamilioni uliyopewa, maslahi ya ndugu zako pale nyumbani na watanzania kwa ujumla yana umuhimu zaidi kuliko ya hao.

Hivi kweli ndugu yangu unadhani kuwa mgombea uliyeambiwa umpigie kura ulipokuwa unapewa msaada ule wa kifedha ndiye atakeyeweza kukupunguzia kero la rushwa linalowasibu kila siku wewe na familia yako.

Hivi ni kweli kuwa mgombea huyo uliyevutiwa naye anaweza kujenga nyufa za nguzo za dola letu zinazobomolewa na wapambe wake kila kukicha ili nao wapate kuingia ikulu bila ya appointment kuanzia mwezi wa kumi na moja mwaka huu.

Hivi umefikiria jinsi kura yako inavyoweza kuwaingiza ikulu mabaradhuli, wezi, wauza nchi, waruka kodi, mafuska na walaghai ambao wanakuja kwako na sura ya ucheshi lakini ndani imejaa ushetani wa hali ya juu kabisa.

Ndugu yangu kwa kweli sipendi kukuchosha maana najua hapo ulipo una majukumu makubwa mbele yako, lakini naomba ufikirie kidogo kama kura yako haiendi kwa mtu ambaye ameonyesha dhahiri kuwa hakubaliani kabisa na nyendo na maadili ya utanzania ambayo mwalimu wetu baba wa Taifa alituwekea kama vipimo vya mapenzi yetu ya kweli kwa nchi yetu.

Mwisho ndugu yangu mpendwa naomba ufikiri hivi ni kweli kura yako haiwezi ikatoa chaguo bora zaidi litakalotuwezesha kuokoa taifa letu kutoka katika janga la kuangamia, litakalotuwezesha watanzania kwa mara nyingine kutembea vichwa juu kwa kujiamini, litakalotuwezesha kutuepusha kuwa na baraza la mawaziri lilojaa matapeli na walaghai watakaokuwa wakitudanganya kila kukicha, chaguo litakalotuletea viongozi waadilifu kwa mungu na kwetu sisi bila ya kujali hali zetu za kimaisha, chaguo litakalolinda thamani ya kila mtanzania, chaguo litakalotusaidia kuinua hali ya elimu ya nchi yetu kwa kujua thamani yake na zaidi chaguo litakalo simama kidete kuchukua maamuzi kwa utulivu na umakini wa hali ya juu ilojawa na busara za kiuongozi bila ya kuhatarisha maisha yetu na wala kurubuniwa na wapambe uchwara.

Ndugu yangu mwana CCM, ni wewe ndiye utakeyeamua ni Tanzania ya aina gani tutakayokua nayo wiki mbili zijazo.

DHANA YA ARI MPYA NA SIASA ZA MATUMBO

@2005...kuelekea uchaguzi mkuu. Published by Mtanzania Jumapili..


Baada ya mbio za ugombea nafasi ya Urais katika Chama Cha Mapinduzi kutulia na anayedhaniwa kuwa mkombozi kupatikana sasa mapambano yamehamia katika nafasi za ubunge na udiwani.

Katika siku za hivi karibuni sura nyingi mpya zimeibuka zikijitangaza kuwa na nia ya kuomba ama kupigania uwakilishi wa watanzania katika nafasi mbalimbali za uwakilishi zilizobadilishwa jina na wajanjawajanja wa sasa na kuitwa nafasi za uongozi na uheshimiwa.

Tofauti na miaka iliyopita ambapo tulizoe sura Fulani fulani tu, mwaka huu mambo ni nguvu mpya tu.

Ni dhahiri kuwa hivi sasa zaidi ya wakati mwengine wowote vijana wanawake kwa waume wamekuwa tayari zaidi kuwania nafasi za uongozi (uwakilishi) katika jamii zao kitu ambacho kwa upande mmoja ni kizuri na muhimu kwa taifa letu kwa ujumla.

Ni wazi kuwa ushindi wa mgombea wa CCM aliyetumia jukwaa la ujana katika kujihakikishia nafasi hiyo umekuwa na athari kubwa katika mfumo mzima wa siasa ndani na nje ya CCM.

Kwa kiasi Fulani ushindi huo umekuwa ni chachu kwa wanasiasa wachanga ambao hapo awali kamwe hawakuthubutu kusimama na kuhoji uhalali wa wazee wao pekee kuendelea kushika nafasi za kiutawala milele amina.

Ushindi huu dhidi ya wale walioitwa wazee umeweza kuwatia moyo vijana kwa malaki kuwa hata wao wanaweza kupata uheshimiwa kama wataamua kama alivyoamua “kijana” mwenzao.
Ushindi huo umeweza kuwaamsha vijana wote kwa pamoja, makini na wajanjawajanja, ambao kwa miaka kadhaa walikuwa katika ndoto ya kuweza ama kuwa wawakilishi makini au kuukwa uheshimiwa kama walivyo wengine.

Kwa ujumla vijana wa kitanzania wameonyesha nia ya dhati ya kuacha kutumiwa kama ngazi za madaraka na wale wanaowaita wazee waliochoka na sasa wameamua kuingia uwanjani wao wenyewe.

Leo ningependa kuchambua suala zima la ari mpya na nguvu mpya katika taswira inayojengeka ya maelfu ya vijana kuonyesha nia na kuanza kampeni kubwa ili kuaminiwa na kupewa nafasi ya uwakilishi katika utawala ujao.

Kati ya vijana waliojitokeza wapo vijana wa makundi mawili ama matatu.
Wapo vijana wazee ambao ni zaidi ya miaka 35-40. Hawa wanatumia dhana ujana kama propaganda ya kukubalika katika jamii iliyogubikwa na ndoto ya “ujana ukombozi”. Hawa wengi wao ni vijana wa zamani kiumri lakini wanaweza kuwa vijana wa sasa kimatendo.

Wao wamekuwa wakitumia nafasi walizonazo kisiasa, kiserikali ama kibinafsi kujikusanyia nguvu za kifedha (kiuchumi) ili wakati ukifika waweze kujichomeka ndani ya mioyo ya watanzania na ili ama wawatumikie watanzania au waweze kujiongozea walichonacho.

Wengi wao ni wanajiita wasomi kwa kuwa wana digrii kadhaa hata kama zengine ni za kudesa na hazina uhusiano wowote na uongozi, mimi siwezi kuwaita wasomi.

Kwa mahesabu yao ni kuwa kijana mwenzao akishapewa madaraka basi ni wazi atataka kushirikiana nao kutekeleza kauli mbiu ya “ARI MPYA, NGUVU MPYA NA KIZAZI KIPYA”
Hivyo basi wao wanadhani ama wanadai wanamtayarishia mazingira kijana mwenzao ili atakapokuwa anatengeneza jeshi lake la makomando wa kichina aweze kuwaona na kuwasimika utukufu.

Kundi la pili ni lile la vijana wenzangu wenye miaka kati ya 25-40 ambao kwa kweli wengi wao ni vijana kweli kiumri, kifikira na kimatendo.

Wengi wao hawana elimu ya kutosha ya kujiita wasomi lakini wapo walio na digrii moja nao lakini wana ujasiri wa kujitanabahisha na kina Prof Shivji, Baregu na wengineo.

Katika kundi hili wapo wengi ambao hadi hivi karibuni uongozi kwao ulikuwa ni kupoteza muda na kuhatarisha maslahi yao binafsi. Hii iwe maofisini wanapofanya kazi, mashuleni wanaposoma na vilevile katika biashara zao binafsi haramu na halali.

Katika kundi hili ambalo ni kubwa si haba, kuna wengine ambao uwezo wao wa kifedha ambao hata kama umetokana na kuibia serikali, kulisha watanzania vyakula vyenye sumu, kuuza siri za nchi, kutetea majambazi na wezi wa mali za umma, kusainisha nchi mikataba ya kihuni na machafu mengineyo, umewapa jeuri kuwa hakuna cha kuwazuia na wao kuwa waheshimiwa.

Kwao wao kujiingiza kwenye siasa ilikuwa ni mwiko eti watahatarisha maslahi yao. Wengi wa hawa katika siku za nyuma kamwe hawajawahi kujitokeza kipigania hai ya yeyote yule hata kama ni motto ananyanyaswa katika daladala. Kwao wao ilikuwa ni bora wao wamekaa kwenye viti ya wengine shauri yao.

Wengi wa hawa siku hizi ndio wamekuwa wakombozi kila sehemu mradi kuna wapiga kura wanawaona.

Kundi la tatu ambalo ni dogo mno lakini ndilo muhimu kwa taifa letu ni la wale vijana wa kati ya umri wa miaka 20-35 ambao katika maisha yao yote ya nyuma wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania maisha mema kwa watanzania wote.

Katika kundi hili wapo wenye elimu ya kutosha na elimu ndogo kama tukipima kwa vigezo vya madarasa.

Lakini zaidi wana elimu ya matitizo ya kijamii na kisiasa yaliyomzunguka mtanzania na kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa mstari wa mbele kuyaongelea kila pale inapowapasa kufaya hilo.

Kwa vitendo wameweza kuonyesha umma jinsi gani walivyoweza kujitoa mhanga katika nyakati mbalimbali kwa ajili ya kutaka kuona watanzania wenzao wakiacha kuteseka na kuonewa kwa kunyimwa haki zao mbalimbali.

Tatizo ni kuwa kundi hili halina fedha za kufanya kile tunachokiita kampeni hivyo kuna hatari kubwa ya kushindwa ama kununuliwa na wenye fedha hivyo kushindwa kutekeleza kile wanachofikiria kukifanikisha.

Watashindwa kwa kuwa tayari na kuna wajanja wajanja ambao kwa ufanisi wa hali ya juu wameweza kubadilisha kabisa maana nzima ya uongozi na kiongazi.

Hawa wamefanikiwa kutumia mwanya wa demokrasia kufanya mchakato mzima wa kuchagua wawakilishi wetu kutoka kuwa wa kutafuta yule mwenye sifa za kuongoza wenzie kwa umakini hadi kuwa kama vile kazi ya kuchagua bidhaa katika mfumo huu tunaouita wa soko huria.

Mfumo ambao hivi sasa ndio unatopatia viongozi wa kila aina kwa kuwa unaruhusu yeyote yule kuweza kushinda kuwa kiongozi mradi ana uwezo wa kujiuza na kuulaghai umma kwa nguvu kuwa yeye ndio anameremeta hata kama kwa kutumia mkorogo tunaouita takrima.

Bahati mbaya zaidi wapiga kura wa sasa tumeondokana na umakini wa kuhoji ubora wa bidhaa kama hizo na kukubali kuvutiwa na mwonekano wake tu eti kuwa Fulani anakubalika.

Kwa kweli wanaotoka katika kundi hili ni wachache mno lakini wapo wakijaribu nafasi yao hata wakijua kuwa wanacheza katika uwanja huu wa kisiasa uliojaa visiki na mbigili.

Wao ndio pekee wanaoweza kuwambia watanzania ni kipi wamekifanya kwa faida ya jamii wakati wakiwa bado wachanga kiumri na kisiasa hata kama hawakuwa na uwezo wa kutosha.

Hawa ndio wanaweza kuwaambia wananchi ni maslahi mangapi binafsi wameyapoteza kwa kujaribu kusimamia ukweli pale inapobidi.

Mfano wa hawa ni kijana mwenzangu mmoja mwenye umri wa miaka ushirini na nne ambaye siku alipojitokeza kutangaza kugombea ubunge jimbo fulani jijini Dar es Salaam, vyombo vya habari vilimkejeli kuwa ni motto na kumchora akiwa na nyonyo mdomoni akidai haki yake ya kupigiwa kura.

Pamoja na umri wake mdogo kwa kipimo cha uwana siasa wa Tanzania, kijana huyu niliyotokea kumjuwa wakati bado akiwa mwanafunzi wa kidato cha tano lakini tayari mpambanaji shupavu wa haki za binadamu na vijana kwa ujumla ndio mfano wa wale haswa wanaoweza kutekeleza kwa dhati ari mpya hii tunayoahidiwa endapo ni ari ya kumkomboa mtanzania kama wengi tunavyodhania.

Nasema hivyo kwa kuwa tofauti na hao wengine wanaotaka kutumia dhana ya Ujana ama ari mpya , nguvu mpya na kizazi kipya, kwa bahati mbaya au nzuri ndio waliojazana katika uwanja wa CCM, vijana wa namna hii ni nadra sana katika jamii yetu iliyogubikwa na siasa za ndio mzee kwa miaka mingi sasa.

Ni nadra kuwaona kwa sababu nyingi tu lakini moja ya wazi ni ile hali ya kutopenda kuingia katika mpambano wa kisiasa kama unaoendelea hivi sasa kwa kuwa umejaa uchafu ambao wengi wao wasingependa kujitambulisha ama kujihusisha nao.

Bahati mbaya ni kuwa kwa kufanya hivyo ndipo wanaacha mwanya kwa “vijana” wa aina ya kundi la kwanza na la pili ambao ni wachache mno ndio wenye uchungu wa kweli na taifa letu ukiachilia mbala na swala zima la sifa za kiuongozi waliaonazo, kuweza kutawala ulingo wa kisiasa nchini.

Ingawa nakubali kuwa wapo wachache walio tofauti, wengi wa vijana wenzangu hawa wa kundi la kwanza na la pili kwa kweli ukiwauliza ni kwa nini wanataka kupewa nafasi kwa kweli hawana jipya zaidi ya yaleyale tuliyoyazoea na hadithi nyingine za kizazi kipya

Kwa kweli hawana ajenda mpya kabisa zaidi ya kuukwaa uheshimiwa ili waweze kuyafanya kwa ufanisi zaidi yale mambo hovyo waliyokuwa wakiyafanya wakati huu wasipokuwa na nguvu za kisiasa.

Kwao wao nguvu za kisiasa ni muhimu sasa ili kujihakikishia nafasi yao katika mfumo wa kinyanga’u uliojaa rushwa, ufuska, uonevu, ufujaji wa mali za umma na uozo wa kila aina tunaojitahidi kuusimika katika jamii yetu.

Yupo msomi mmoja ambaye alikuwa akijaribu kuangalia aina ya siasa katika upande wetu huu wa dunia. Yeye aliita aina za siasa za dunia ya tatu kama nchi yetu ilivyo ni siasa za matumbo.

Siasa ambazo kwanza zinajali matumbo ya wachache walio na nguvu na suala la kusaidia jamii linakuja pale tu kura zao zinapohitajika ili kuendeleza nafasi ya utawala kwa wale waliomo na kutoa mwanya ya kuingia kwa wale wajanjwajanja wengine waliochoka kula mabaki.

Kwa kweli kwa kutumia dhana hii ndipo ikanijia washawasha ya kujaribu kufuatilia mchakamchaka huu wa vijana wenzangu katika kugombea nafasi za uwakilishi ambao wao kwao ni nafasi za uheshimiwa.

Hapo ndipo nilipochukua juhudi zaidi za kujua nani na nani anayetaka uheshimiwa hapo mwezi Oktoba na kwa nini yeye na nini sifa zake.

Kitu kimoja ambacho uchambuzi wangu unaniambia ni kuwa kuna hatari ya kuwa badala ya kutengeneza safu ya wachezaji wa kweli wenye kuweza kuweza kutimiza ndoto ya taifa jipya kama tunaloambiwa na kuishia kubadili sura za manyag’au tu.

Na ubaya ni kuwa manyang’au wa damu mpya huwa daima wanakuwa hatari zaidi kwa jamii kutokana na ukweli kuwa wametumia muda wa mwingi kusoma siasa chafu ambazo daima ndizo watakazotumia kufanikisha malengo yao binafsi na kuwanyamazisha wale watakaukuwa na kuburi cha kuhoji machafu yao hapo mbeleni.

Tofauti na tuliowazoea, hawa manyang’au watarajiwa ni wazi kima chao cha kuridhika ni kigumu kufikika na hivyo ari na nguvu watakazotumia kushibisha matumbo yao na ya wapambe wao zitakuwa ni za kutisha mno kuliko tunazoziona hivi sasa.
Si ajabu kuona kuwa aina hii ya vijana kwa wingi wapo katika chama tawala. Jibu ni rahisi mno.

Kwao wao kugombea kwa chama tawala kunawahakikishia usalama wao wa kutuanikwa machafu yao, kunawahakikishia ushindi kama wataweza kuteuliwa, kunawapa nafasi kubwa zaidi ya kukumbukwa na Rais ajaye ambaye kwa mahesabu yao ni lazima atoke huko na vilevile hata wakishindwa bado maslahi yao yatendelea kulindwa kwa kuwa wameonyesha kuwa wenzi wa watawala.

Kwa kifupi hawana jeuri ya kujaribu kubadili mfumo kwani siku nyingi wameshakubali yaishe, dhana yao ni kuwa huu ni wakati wa kucheza na timu ya ushindi ili kufanikisha mambo.

Kwa kweli ukiangalia mwenendo huu kwa ujumla ni wazi hatima ya Tanzania yetu ipo katika hatihati kwani kwa jinsi hali inavyokwenda ni dhahiri vijana wa kundi la kwanza na la pili ndio watakaoibuka washindi.

Hii ni kwa kuwa wazee wetu walishabadili mfumo wa siasa ndani na nje ya chama cha mapinduzi kuweza kufanya iwe rahisi kwa aina hiyo ya wanasiasa kupenya katika nafasi za uongozi katika jamii yetu.

Ni watanzania wenye ujasiri wa hali ya juu tu ndio wanaoweza kuwazuia hawa jamaa wanapita wakitufitinisha na kila aliye na umri mkubwa ili wao waoenekane ndio watakatifu.

Kama vijana wachache wenye uchungu wa kweli na taifa lao wataamua kusimama kidete na kuwapinga hawa walaghai wanaotumia madhila yetu kwa faida ya matamanio yao binafsi ni wazi makali yake yanaweza kupunguzwa kabla hawajafika mbali.

Ni wazi tukiamua hilo litafanikiwa kwani hawa tuko nao mitaani, viwanjani, mashuleni, majumbani na hata kwenye taasisi mbalimbali za umma na binafsi walipojaza historia ya machafu ya kila aina.

Kusimama na kuwaelezea machafu yao kwa wapiga kura ni wajibu wetu sote kwani ushindi wao ni balaa kwetu na salama yetu inategemea ujasiri wetu.

Tukiwaacha hawa malaghai wa kizazi chetu ni wazi tutakuwa tunajipotezea nafasi hii tuliyoipata baada ya muda mrefu wa kulalama kuwa vijana tunanyimwa haki yetu ya kujiongoza na kuongoza taifa letu.

KIKWETE CHAGUA MAARUFU, SALIM CHAGUO MAKINI

Published by Mtanzania Jumapili@ 2005

Hata kama kuna wengi watakaokasirika, ni ukweli ulio wazi kuwa uteuzi wa mgombea wa Urais wa Tanzania kupitia chama cha CCM utakaofanyika tarahe Mosi mwezi Mei 2005 kule DODOMA, ndio utakao amua kuwa harakati za kumtafuta rais wa Tanzania kwa miaka mitano au kumi ijayo zimekwisha au ndio kwanza zinaanza.

Nasema hivi kwa kuwa ni wazi kati ya wagombea wote waliojitokeza kuna wagombea wawili au watatu ambao wakipitishwa, sio tu watatoa nafasi kwa vyama mbalimbali vya upinzani ambavyo bado havijaweza kujiuza vyema kwa watanzania kujitutumua kisiasa na kutoa upinzani mkali kwa baba wa dola, yaani CCM.

Lakini vilevile kuna wagombea wengine wawili ambao kwa kweli CCM ikimpitisha mmoja wapo na mwingine kutopiga kelele za mizengwe, basi ushindi wa kishindo unakuwa tayari umeshajikita kwa ndugu zetu wa hawa, yaani CCM.

Wawili hao si wengine bali ni Mtanzania mmoja maarufu hapa nchini na pande zote za dunia, Dr Salim Ahmed Salim na mwengine maarufu sana hapa nchini na maeneo mbalimbali katika maziwa makuu ya afrika, Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.

Ni ukweli usio fichika kuwa Ndugu Kikwete ni chaguo maarufu kabisa kupita wote waliojitokeza kuwania nafasi hii kupitia CCM, akifuatiwa kwa mbali ingawa hali inaonekana kubadilika kwa kasi mno, na Dr Salim Ahmed Salim.

Sababu za umaarufu huu ambao kwa kweli ni muhimu kwa taifa linalozidi kupoteza mwelekeo kila kukicha, ni nyingi na mimi nitajitahidi kuzitoa kwa kadri ya niwezavyo bila ya unafiki.

Ndugu Kikwete ambaye ni mwanasisa mkongwe ndani ya CCM tangia ujana wake, chini ya usimamizi wa Mwalimu Nyerere ambaye yeye anasahibiana naye kwa undugu wa kiapo, kwa wanaokumbuka mchango wa Sheikh Bharamiya wa kule Bagamoyo ambaye anasahibiana naye, kikwete ameweza kujitokeza kama mwnasiasa kijana tangia pale alipogombea na kushindwa nafasi hiyo mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 45.

Hivi sasa ndugu huyu anakaribia miaka 55, lakini kutokana na kujitambulisha zaidi na vijana ambao ndio wengi wanaonekana kumzunguka, na hulka yake ya uhalisia “simplicity”, ndugu huyu ameweza kujitengenezea mhimili wa kisiasa katika jukwaa la vijana ambao ama kwa bahati au kwa makusudi wameweza kupenyeza ngome za CCM kwa wingi kuanzia mwaka 1998 na kuendelea.

Wako wanaohoji kuwa yeye si kijana lakini ningependa kuwakumbusha kuwa ujana unaozungumziwa hapa si umri bali ni fikra, ambazo vijana walio wengi ambao ndio wamiliki halali wa taifa hili wanaamini kuwa Ndugu Kikwete pekee ndiye anayewakilisha ndoto zao za kuondokana na ufedhuli wa kimaisha unaotugubika.

Kingine ambacho Ndugu Kikwete ameweza kukiwakilisha kwa jamii, ni dhana ya uasi wa ndani UASI WA NDANI ya mfumo wa kuhafidhina wenye kuendeshwa na falsafa ya rushwa iliyokithiri ndani ya Chama kinachojiita cha Mapinduzi.

Ukiondoa karibia wote wanagombea nafasi hiyo ndani ya CCM, Ndugu Kikwete ndiye pekee mwenye kuonyesha kuwa ni kweli mwakilishi wa wakulima na wafanyakazi wa tabaka la kati na la chini kutokana na haiba yake ya uhalisia. Ndugu huyu ambaye ama kwa uthabiti wa kimaadili au mahesabu ya kisiasa, pamoja na mambo mengine ameweza kukataa “kuzawadiwa” nyumba zilizojengwa kwa jasho na damu za watanzania, kitu ambacho kinawapa matumaini vijana na wazee wengi kuwa ataweza kupambana na rushwa na hata kusafisha uozo huo ndani ya CCM na tabaka tawala kwa ujumla.

Sifa nyingine aliyonayo Ndugu Kikwete ni suala la mvuto. Hili kwa kweli ni silaha kubwa ambayo hata wenzanke wakimdhihaki vipi, kamwe hawataweza kumuangusha. Suala la sura ya mvuto ni muhimu sana kwa jamii iliyokata tama kama Tanzania.

Sio kwamba inampaa wapenzi wengi kisiasa hasa wale wa jinsia tofauti naye ambao ndio wenye kura nyingi zisizotetereka kirahisi ndani na nje ya CCM, sura na haiba ya mvuto ni silaha muhimu kwa kuongoza katika mwenendo wa siasa za kimaarufu “popular politics” ambazo wengi tunadhani zinahitajika ili kusafisha uozo wa kisiasa tulionao.

Uozo ambao umejengwa na kulindwa na baadhi ya wagombea pinzani wa ndugu huyu ambao watanzania wengi hasa vijana wangependa kuona wanatoka katika medani za kisiasa.

Sifa za Dr Salim duniani nadhani wote twazijua, sio tu kutokana na majukumu mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ambayo aliwahi na bado amekabidhiwa na wanadunia, lakini pia haiba yake ya unadhifu wa kisiasa ya mfano wa Mwalimu wake kipenzi, hayati Mwalimu Nyerere ambayo kwa sasa imekuwa ni fimbo muhimu katika jaribio lake la kuomba dhamana ya kuwaongoza watanzania moja kwa moja kama Rais wa nchi yetu.

Mengi yamesemwa kuhusu Dr Salim lakini mimi ningependa kwa kutumia kautaalamu kangu kadogo cha uchambuzi wa siasa wanachonipatia wasomi wetu pale mlimani kwa miaka kadhaa hivi sasa, kuongezea yale machache ambayo nadhani hayasemwi au hayajasemwa bado na vyopmbo vyetu vya habari.

Kutokana na upeo wa juu alionao ndugu huyu kuhusiana na mambo ya siasa za kidunia, Wengi na hata kutoka vyama pinzani na CCM wanaona Dr Salim anaweza kuwa ndio tunu ya nchi yetu kutupeleka kwenye Demokrasia ya kweli na si kwa maneno tu bali kwa vitendo.

Kwa wengi wanovutiwa naye, hilo kwake hakuna mjadala kwani ingawa wengi hubadilika na nguvu za madaraka, kwake yeye kama aliyewahi kuwa kiongozi wa mapambano dhidi ya unyonge, ukoloni na ubaguzi wa aina yeyote popote pale duniani pamoja na kuwa mpiga mbiu mkuu wa utawala wa demokrasia ya kweli barani Afrika, kufanya tofauti utakuwa ni unafiki ambao hata mtu asiye na haiba ya aibu hataweza kufanya hilo.

Lengine ni kuwa uhusiano wake wa karibu na Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Nyerere ambye ndiye amekuwa dira yake kisisasa. Uhusiano huo na mwalimu pamoja na wale watukufu wengine wa zamani (Disgruntled old guards) ambao walilitumikia taifa kwa adabu na heshima ya juu kwa wananchi.

Hawa ni kama wazee wetu akina Judge Warioba, Mzee Ibrahim Kaduma na wengineo wachache lakini washupavu ambao hadi sasa wanajaribu kuwa nguzo na dira ya dhana ya utawala wa kamaadili ambao kwa kweli umemong’onyoka mno kama sio kuisha kabisa. Hawa wameweza kumpa Dr Salim imani ya kuwa ataweza kurudisha utawala wa nidhamu ya kimaadili nchini.

Katika safari yake kuelekea uchaguzi, Dr Salim ameweza kuonyesha kuwa mbali na kusimamia ujenzi wa uchumi imara lakini anaweza kurudisha dhana ya maadili ambayo si tu tunaihitaji kwa kulinda haka kaamani ketu kwa kulinda utu wa kila mtanzania bila ya kujali nafasi yake kiuchumi, bali pia kutupunguzi janga la ukimwi ambalo kwetu sisi ni adui kama ilivyo ugaidi wa kidini kwa Taifa la Marekani hivi sasa.

Kingine ambacho haka kaupeo kangu ka kuchambua masuala ya siasa kameweza kunionyesha ni kwa msomi kama Dr Salim ambaye sio tu wa darasani bali hata katika kufikia maamuzi yake, ni dhahiri atweza kusimamia kuona kuwa thamani ya usomi makini na wasomi wetu itarudishwa.

Katika duru ya wasomi, ingawa si wote, wengi hata wale wanaompinga kwa sababu zingine wanaamini kuwa Dr Salim ataweza kutumia vyema nafasi ya kutuongoza kunusuru hali ya mbambo katika madhabahu zetu za kisomi na elimu, ambazo sio tu hali inatisha bali pia ni hatari kubwa kwa taifa letu hasa katika dunia hii ya ushindani usiokuwa na huruma wala haiba.

Bila ya kuwa ni kiongozi anayethamini hali na mawazo wa wasomi, kutambua umuhimu wa ELIMU BORA na sio BORA ELIMU, anayejiongoza kisiasa na kuwaongoza wananchi wake kwa lugha na mtindo wa kisomi, ni wazi hata tukiletewa malaika, safari ya tunapoelekea kusikojulikana itakuwa ya mwendo kasi na wa hatari mno.

Lingine ambalo kwa kweli si ajabu kuona watanzania wengi wa kizazi chetu hawakioni ni kuwa watanzania kama washika dau wakuu wa dunia ya tatu, au kwa kifupi masikini wa dunia, hivi sasa tunakabiliwa na zoezi kubwa la kupambana kuweza kupata mfumo wa siasa za kimataifa ambo utatambua na kutetea zaidi maisha yetu kiuchumi na kijamii kwa miaka mingi ijayo.

Hili ni suala la marekebisho mbalimbali katika mfumo wa umoja wa mataifa (UN) ambao kutokana na mchango wa Dr Salim na viongozi wenzake wengi wapatao kumi na tano pamoja na wasomi wetu kama Prof Mwesiga Baregu na Prof Haroub Othman, kuanzia mwezi September 2005 kule New York, Marekani na kwengine pote duniani, majadiliano makali yataendelea kujaribu kubadili mfumo wa kimataifa.

Mfumo ambao kwa miaka mingi umekuwa ukiwapendelea mno mataifa makubwa na tajiri dunia na kukandamiza ndoto zetu za kupata ahuani ya kweli ya kimaisha. Kwa kweli kama hatutakuwa na kiongozi shupavu, makini, msomi, mwenye kuheshimika katika medani za kimataifa na mjuzi wa hali ya juu wa masuala haya, Tanzania ambayo ina jukumu la kuongoza sauti ya wanyonge kupitia nafasi yetu katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama mwanachama wa muda kwa miaka miwili kuanzia mwezi January mwaka huu, ni dhahiri mpambano huu tunaweza tukaupoteza hivyo tukawa tumejisaliti na kuwasaliti mabilioni ya wanadunia masikini na wanyonge wanaotegemea sauti yetu huko.

Nasisitiza hili kwa sababu najua wazi kuwa bila ya kubadili mfumo wa siasa wa kimataifa, hata kama utaletewa malaika wa juu kabisa, kamwe mbio zetu zitaishia ukingoni na kuendelea na siasa za longolongo, kama wanavyosema vijana wa mjini.

Ukiangalia hizo baadhi ya sifa za wagombea hawa wawili wa CCM hapo juu na nyingine nyingi zilisosemwa na zinazosemwa na watanzania mbalimbali, kama za kweli au za uongo, ni wazi kuwa mmoja kati yao ndiye turufu ya ushindi wa kirahisi kwa CCM.

Kama siasa zingekuwa ni kufuata kigezo cha umaarufu tu na sio vinginevyo basi ni wazi kuwa wagombea wengine wangeshajitoa muda mrefu na kuupunguzia umma wa watanzania adha ya kufukiri sana kuhusu hatma ya maisha yao na nchi yao kwa ujumla. Lakini ukweli sio hivyo.



SEHEMU YA PILI: CCM inavuna ilichopanda..........

Wiki iliyopita nilijaribu kuwaelezea wagombea wawili na kwa nini wameweza kuonekna kwa upeo wa wengi kuwazidi wenzao wengine katika nafasi ya umaarufu sio tu ndani ya CCM bali kwa watanzania kwa ujumla. Leo napenda kuendelea uchambuzi wangu kwa kuongelea siasa za uchaguzi kwa ujumla kama zinavyoendelea.

Tofauti na wenzetu katika demokrasia zilizoendelea kule ughaibuni yaani sehemu kubwa ya Ulaya na Amerika kaskazini, Watanzania na Tanzania kama nchi na dola lake wana vigezo tofauti kidogo katika kumchagua kiongozi wa aina yoyote ile katika medani ya kisiasa. Kama ingekuwa ni suala la uzoefu na mvuto tu ndio turufu pekee basi kama nilivyosema wakati ule, mbio za uchaguzi zingekuwa zimekwisha. Lakini kwa jinsi ninayoona mimi, siasa za uchaguzi za CCM na Tanzania kwa ujumla kwa wakati huu zimejitwika katika maeneo kadhaa yafuatayo.

Moja kubwa ni nafasi ya matakwa binafsi ya mtanzania mmoja mmoja bila ya kujali maslahi ya taifa kwa ujumla, ukiachilia bara la afrika na dunia yetu. Hili limejitokeza sana katika mijadala mbalimbali inayoendelea katika kila pande ya nchi yetu. Suala la mimi nitafaidka na nini kutoka kwa nani ndilo haswa limejikita kati ya wapiga kura wa CCM katika vikao vikuu vya chama ambavyo ndivyo vitateua mwakilishi wao katika kugombea nafasi ya Urais hapo Oktoba.

Suala hili ambalo kwa kiasi kikubwa limechangia kuweko kwa uchambuzi unaolenga zaidi majina ya wagombea na sio vigezo vya wagombea bora ndilo pia limekuwa dira ya uchaguzi miongoni mwa watanzania wa ngazi na kada zote nchini, kuanzia wafanyabiashara wa aina zote, kubwa na ndogo, halali na haramu, wasomi, wafanyakazi na wasio na kazi, wakulima na wafugaji, na zaidi waandishi wa habari wetu.

Wengi wetu tumegubikwa na kuangalia upatikanaji wa kirahisi wa mahitaji yetu binafsi ya muda mchache na kusahau au kutotilia umuhimu mahitaji ya muda mrefu ya taifa letu tukufu. Hili limetufanya tuongelee siasa kwa msingi wa majina zaidi ya uwezo na vipaji vya wenye majina hayo kwani kwetu bora ni yule tunayemuona tunashabihiana naye kama ni kidini, kikabila, kirika, kifikira, kijamii, kiuchumi na hata kirangi!!!.

Hata hivyo itakuwa ni dhambi kubwa kwa kuwalaumu watanzania kwa kosa hili, yaani kutumia maslahi binafsi kama ndio dira pekee ambayo watanzania tulio wengi tunaitumia kuamua nani anafaa na nani hafai. Dira hii potofu ya uchaguzi iliyotanda katika fikra za watanzania walio wengi, sio tu inatawala katika suala zima la kuchagua rais kwa sasa lakini pia hata katika masuala mengine yoyote ya kimaisha iwe rafiki, thamani za nyumba, kazi, aina ya elimu, na memnngineyo mengi kma sio yote.

Dira hii ambayo imepandwa na kupaliliwa na dhana ya kihafidhina inayoendeshwa na falsafa ya unyang’au yenye kupitia njia ya BORA ELIMU, ambayo ndiyo iliyozaa taifa lenye upungufu wa umakini, tupende tusipende ina nafasi kubwa ya kuiamulia CCM nani anakuwa mgombea wao na si nani mgombea bora kutoka kwao.

Tafiti mbali mbali zimefanywa na wasomi wetu na zimeonyesha wazi kuwa watanzania kwa kiasi kikubwa wamepunguza umakini wao katika kuchagua kinachowafaa na hivyo kujiweka VULNERABLE na siasa za kiujanja ujanja ambazo zina mvuto wa faida au mapato ya kirahisi rahisi na sio yenye umakini wa kutufaidisha kwa muda mrefu.

Hili linatokana na sera ya BORA ELIMU inayoendeshwa na wakubwa hawa kwa muda mrefu sasa ambayo inalenga kupata watanzania wa aina ya ndiyo mzee na sio wakorofi wenye chachu ya kuhoji. Sera ambayo umuhimu wake mkubwa umetokana na kuporomoka kwa uwezo wa kiutawala wenye kuamini maadili ya uongozi na umakini wa kiuongozi kitu ambacho kimefuatana kwa pamoja na mfumuko wa madhila ya kimaisha ambao umepelekea kumomonyoka kwa uhalali wa kisiasa wa tabaka tawala la nchi yetu.

Ninasema kuwa CCM inavuna ilichopanda kutokana na hali inayojionyesha hivi sasa ya kuwa njia panda iliyojikuta imewekwa na kampeni za baadhi ya wagombea wake. Hali ambayo imewaweka katika hatari ya kupata bora mgombea atakeyewahakikishia ushindi wa kishindo na sio mgombea bora ambaye sio tu atahakikisha kujenga nyufa zinazojitokeza ndani ya muhimili ya chama na dola bali pia atarudisha sifa ya chama hiki kinachoelekea kaburini kwa mwendo wa mwanga wa taa. Mtu ambaye kutokna na haiba, upeo na mtazao wa kimaadili atweza kukirudishia chama hiki sifa iliyopotea ya kuwa ni chama imara, chenye nidhamu na kinachiaminika kama kimbilio la wengi na wananchi.

Ukifuatilia kwa ndani sana mwenendo wa siasa ndani ya chama hicho hasa matamshi ya viongozi wa juu wa chama hicho, ni dhahiri kuwa kama jadi yake tangia enzi za Baba wa Taifa, hayati mwalimu Nyerere, tayari watukufu wachache wamekwishaamua nani anakuwa mrithi wa rais Benjamin Mkapa.

Hata kama manung’uniko ni mengi miongoni mwao lakini ni wazi hali ya kampeni zinazoendelea zimewapelekea kuamua kuchukua uamuzi mzito mno miongoni mwao wa kuhakikisha chama kinatoa mgombea makini ambaye sio tu kwa uzoefu wake na haiba ya yake ya umakini ataweza kupambana na uasi wa watanzania kama watakosea kuchagua, lakini pia uasi ndani ya chama ambao ndio tishio kubwa zaidi kuliko mengine.

Lakini kwa jinsi hali ilivyo, ingawa kuna mabadiliko ya upepo wa kisiasa unaotokea kwa kasi kubwa ambayo haikutegemewa na walio wengi, kazi ya kuwabadilisha mawazo watanzania walio wengi na hasa wapiga kura wa CCM inakua ngumu mno kama si ya hatari sana.

Ni wazi wengi wao wameshaweka msimamo wao, na utmaduni wa mtanzania kwa kweli ni wa kutokuwa tayari kufanya mabadiliko makubwa ya kimaamuzi kwa urahisi (conservatism) hivyo majaribio haya ambayo ukiyatazama kwa undani ni yenye nia njema kabisa ya kuwahakikishia wana CCM na na hasa watanzania kwa ujumla, kuwa chaguo litakaloletwa na CCM ambao wao (watukufu wachache) tayari wamelikubali ndilo bora zaidi na makini kwa CCM na watanzania kwa ujumla, limekumbwa na ugumu wa kipekee kabisa.

Ugumu huu unatokana na kuwa chaguo hilo sio lile ambalo wengi wamekwisha amua kuwa ndio la manufaa yao na hivyo kudhani kuwa ndio la manufaa ya taifa. Vilevile dhana ya uwezekano wa uasi wa kiasiasa wa wananchi na wana CCM walio wengi kwa ujumla wakiwemo nuru ya tamaa ya mabadiliko kwa walio wengi, yaani baadhi ya wagombea vigogo, inawafanya watukufu hawa ndani ya medani za juu za CCM kuwa na mtihani mzito mno.

Kwa ujumla ugumu huu chanzo chake kikuu kinatokea katika aina ya usomi wa watanzania walio wengi ambao umewapelekea kuamini mengi bila ya uchambuzi wa kina na wa makini hivyo kiurahisi kabisa kuamua nani atakayewatatulia madhila yao kwa wale waliogubikwa nayo na kuwaongezea zaidi wale walifaonikiwa kwa kiasi, ambao wangependa kufika juu zaidi na kuwapiku wale waliojisimika huko kwa muda mrefu mno.

Kama watukufu hawa wangeona kuna umuhimu wa kuendeleza ELIMU BORA yenye kugubikwa na dhana na fikira za uzalendo wa kweli wenye kuneemeshwa na chachu ya kuhoji, basi kazi ya kuwashawishi wana CCM na watanzania walio wengi kuwa chagua wanalowapa ndilo bora zaidi kwao na kwa Tanzania kwa ujumla sio tu kwa wakati huu bali hata kwa wakati ujao, isingekuwa ngumu na ya hatari kama inavyonekana hivi sasa.

Kazi nyengine ambayo ndiyo kubwa zaidi inayowagubika wakuu hawa wa CCM ni kupambana na upinzani mkali utakaotoka kwa wapambe wa mgombea maarufu ambaye inaonyesha tayari wameshamuona kuwa ni hatari kwa maslahi ya nchi kama waonavyo wao ingawa wanakubali kuwa ndio mgombea maarufu kuliko wote.

Wapambe hawa ambao wengi wana upeo wa hali ya juu wa propaganda za kisiasa wakisaidiwa na nafasi ya kukubalika kwao ingawa sio wote katika jukwaa la vijana walio wengi ambao ndio nguzo ya umaarufu wa CCM, ni dhahiri hawatakuwa tayari kuona kuwa wanapokonywa nafasi ya wao pia kupenya na kuchukua nafasi za juu kisiasa nchini kutoka kwa wanasiasa wakongwe au wazee kwa lugha maarufu hivi sasa.

Hata kama mgombea wao waliyeweza kumhakikishia umaarufu wake kwa wananchi walio wengi mno kwa utaalamu wa hali ya juu wa kipropaganda halali na haramu, atakubali yaishe ile naye ajihakikishie kuendelea kwa nafasi na umuhimu wake kisiasa kwa gharama nafuu, ni wazi wapambe hawa wanajua wazi kuwa ndoto zao nyingi hazitafanikiwa na pengine hata wakapoteza umuhimu wa kisiasa na kijamii wanaotmba nao hivi sasa.

Hofu hii inaonekana wazi hivi sasa kiasi ya kuwa wale wachache ambao wanasukumwa na uzalendo wao kwa nchi zaidi ya mafanikio yao binafsi wameshaanza kuona umuhimu wa kujenga daraja kati yao na mgombea makini ambaye kwa njia moja au nyingine ndiye kimbilio lao.

Lakini hili nalo linaweza kuwa tatizo kwa watukufu wa CCM wanaojaribu kuhalalisha uamuzi wao wa kumrithisha mgombea wanayemuona ni makini na bora zaidi kwa chamaa kwanza na jamii kwa ujumla.

Ni tatizo kutokana na kuwa endapo daraja hili litajengeka vema na mgombea maarufu ambaye hadi sasa ana uhakika mkubwa wa kushinda kinyang’anyiro hicho endapo hakutakuwa na kile wengi wanakiita mizengwe na wasomi wanaita ukweli wa kisiasa, na akakubali yaishe mapema. Ni wazi kuwa kundi lengine la wagombea ndani ya CCM halitakubali kushindwa kirahisi.

Kundi hilo linawahusisha wagombea wengine wawili au watatu ambao kwa hali ilivyo linaweza kuondoa uwezekano wa kumaliza uchaguzi mwezi Mei na kufanya uendelee hadi Oktoba na pengine zaidi ya hapo kutokana na uwezekano mkubwa wa kuamsha upinzani wa hali ya juu kutoka kwa watanzania walio wengi ambao wamejengewa dhana ya kuwa hao ni maadui wa amani na maendeleo yao.

Kundi hili linaweza kuleta madhara makubwa kwa CCM na watanzania wote kwa ujumla, kutokana na ukweli ulio wazi kuwa muungano au makubaliano yoyote kati ya MGOMBEA MAARUFU na MGOMBEA MAKINI unaweza au yanaweza kuwahakikishia wengi wao mwisho wao kisiasa, kitu ambacho kwa siasa za dunia yetu ya tatu kama ilnavyojionyesha kwa majirani zetu, maana yake inaweza hata ikawa mwiso wao kimaisha.

Kundi hili litajaribu kutumia kila aina ya mbinu, halali na haramu kujaribu kuzuia hali hiyo, kitu ambacho kitaendeleza mpasuko ndani ya CCM na mbaya zaidi kwenye vyombo muhimu na nyeti vya dola ambavyo ndivyo kwa miaka mingi sasa vimekuwa mihimili muhimu kwa tabaka tawala na taifa kwa ujumla.

Wapo wanaofikiri kuwa mpasuko ndani ya CCM utakuwa neema kwa watanzania kwani utawezesha wananchi walio wengi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta chama mbadala na kushindwa kukiona nje CCM, kuamini kuwa upinzania unaweza kuwa nusura yao.

Dhana hii ina ukweli wake lakini kwa bahati mbaya kwa jinsi mambo yanavyokwenda, kuvunjika kwa CCM kwa staili inayojionyesha ni wazi kutafuatana na kuvunjika kwa dola hivyo kusababisha hasara kubwa kwa Taifa kwa ujumla.

Hii inatoka ukweli kuwa tofauti na katika nchi za wenzetu kama Kenya na kwengineko, hapa kwetu CCM si chama tawala tu bali ni chama dola. Pale inapotokea kinavunjika kwa siasa za chuki na visasi kama tunazoziona sasa ni dhahiri viongozi wa juu wa CCM hawataweza kuhakikisha usalama wa dola ambalo kwa bahati mbaya limeachana na wajibu wake wa kuwa msimamizi wa siasa ndani ya chama tawala na kuwa sehemu ya ushindani wa kisiasa ndani ya mpambano huu.

Suala hili la hatari ya kuvunjika kwa dola ndilo haswa limepelekea sio tuu viongozi wa kisiasa makini wa nchi yetu pamoja na viongozi wa kidini na kielimu kujawa na woga wa hali juu na kujikukuta wako njia panda katika kutimiza wajibu wao wa kulinda tabaka tawala na hivyo jamii kwa ujumla.

Hii inatokana na ukweli kuwa ni wazi hata kama mambo yakawa shwari hata baada ya CCM kuchagua yeyote yule wanayempenda na wanaona anawafaa, kuna hatari kubwa kuwa mara baada ya mmoja wa hawa wanaochuana kwa nguvu zote atakapokabidhiwa dhamana ya ulinzi na usalama wa taifa wa nchi yetu, itambidi kuchukua hatua za kusafisha chama na dola na kuondokana na vile vinasaba vilivyokuwa vikimpinga waziwazi alipokuwa anawania kuteuliwa na chama au hata wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.

Hilo halitakuja tu kwa ajili ya chaguo maarufu kujihakikishia usalama wake bali pia litambidi kufanya hivyo kwa ajili kujaribu kukidhi hamu kubwa ya wafuasi wake waliompigia debe na kumshindisha kwa kishindo. Hamu ambayo imejengwa katika dhana ya usafi wa kisiasa na uthabiti wa ki hulka ambao wengi weu tunadhani ni silaha muhimu katika kuondoa unyang’au huu unaotukumba hat kama kuna hatari gani itayoukumba hapo mbeleni. Wanasayansi wa kisiasa kuchambua dhana hii kama mwisho unahalalalisha njia (ends justifies the means).

Na endapo atapita mtu anayetoka kwenye upande ule mwingine, yaani wale ambao CCM inaona watakuwa mzigo mzito ku-ubeba lakini kutokana na nguvu mbalimbali zikiwemo za dola na udhaifu wa baadhi ya viongozi wa vyama kadhaa pinzani wa CCM, wanaweza kushinda mwezi Oktoba, ni wazi itabidi wajikoshe kwa watanzania ili kujihalalishia nafasi zao.

Hapa pia kuna hatari ya kuwaona kina Mutharika wengine ambao ingawa wao wenyewe ni wachafu wa kutupwa lakini wangependa kuwabebesha wengine lawama ili wao waonekane ni malaika. Hili lazima litaleta vurugu zaidi miongoni mwa tabaka tawala na kuathiri uthabiti wa mhimili wa amani yetu yaani dola.

Kwa hali hiyo hapo juu na sababu nyingine kadhaa wa kadhaa, ni wazi CCM kwa sasa inavuna ilichopanda kwa kujikuta njia panda baada ya kushindwa kwa viongozi wa juu ambao daima ndio wamekuwa watoa uamuzi wa kweli wa nani anamrithi nani, kusimama wazi na kuwaonyesha wana CCM na watanzania kwa ujumla chaguo wanaloliona wao kuwa makini na bora zaidi dhidi ya chaguo maarufu zaidi, na wangependa wananchi kupitia watukufu wachache kule DODOMA kuridhia chagua hilo kwa kile waonavyo wao nap engine kuna ukweli, ni kwa manufaa ya taifa.

Hii ilikuwa ni makala maalumu wakati tunaelekea kule Chimwaga mwaka 2005..

KIKWETE CHAGUA MAARUFU, SALIM CHAGUO MAKINI. (Sehemu ya kwanza)

Published by Mtanzania Jumapili@ 2005

Hata kama kuna wengi watakaokasirika, ni ukweli ulio wazi kuwa uteuzi wa mgombea wa Urais wa Tanzania kupitia chama cha CCM utakaofanyika tarahe Mosi mwezi Mei 2005 kule DODOMA, ndio utakao amua kuwa harakati za kumtafuta rais wa Tanzania kwa miaka mitano au kumi ijayo zimekwisha au ndio kwanza zinaanza.

Nasema hivi kwa kuwa ni wazi kati ya wagombea wote waliojitokeza kuna wagombea wawili au watatu ambao wakipitishwa, sio tu watatoa nafasi kwa vyama mbalimbali vya upinzani ambavyo bado havijaweza kujiuza vyema kwa watanzania kujitutumua kisiasa na kutoa upinzani mkali kwa baba wa dola, yaani CCM.

Lakini vilevile kuna wagombea wengine wawili ambao kwa kweli CCM ikimpitisha mmoja wapo na mwingine kutopiga kelele za mizengwe, basi ushindi wa kishindo unakuwa tayari umeshajikita kwa ndugu zetu wa hawa, yaani CCM.

Wawili hao si wengine bali ni Mtanzania mmoja maarufu hapa nchini na pande zote za dunia, Dr Salim Ahmed Salim na mwengine maarufu sana hapa nchini na maeneo mbalimbali katika maziwa makuu ya afrika, Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.

Ni ukweli usio fichika kuwa Ndugu Kikwete ni chaguo maarufu kabisa kupita wote waliojitokeza kuwania nafasi hii kupitia CCM, akifuatiwa kwa mbali ingawa hali inaonekana kubadilika kwa kasi mno, na Dr Salim Ahmed Salim.

Sababu za umaarufu huu ambao kwa kweli ni muhimu kwa taifa linalozidi kupoteza mwelekeo kila kukicha, ni nyingi na mimi nitajitahidi kuzitoa kwa kadri ya niwezavyo bila ya unafiki.

Ndugu Kikwete ambaye ni mwanasisa mkongwe ndani ya CCM tangia ujana wake, chini ya usimamizi wa Mwalimu Nyerere ambaye yeye anasahibiana naye kwa undugu wa kiapo, kwa wanaokumbuka mchango wa Sheikh Bharamiya wa kule Bagamoyo ambaye anasahibiana naye, kikwete ameweza kujitokeza kama mwnasiasa kijana tangia pale alipogombea na kushindwa nafasi hiyo mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 45.

Hivi sasa ndugu huyu anakaribia miaka 55, lakini kutokana na kujitambulisha zaidi na vijana ambao ndio wengi wanaonekana kumzunguka, na hulka yake ya uhalisia “simplicity”, ndugu huyu ameweza kujitengenezea mhimili wa kisiasa katika jukwaa la vijana ambao ama kwa bahati au kwa makusudi wameweza kupenyeza ngome za CCM kwa wingi kuanzia mwaka 1998 na kuendelea.

Wako wanaohoji kuwa yeye si kijana lakini ningependa kuwakumbusha kuwa ujana unaozungumziwa hapa si umri bali ni fikra, ambazo vijana walio wengi ambao ndio wamiliki halali wa taifa hili wanaamini kuwa Ndugu Kikwete pekee ndiye anayewakilisha ndoto zao za kuondokana na ufedhuli wa kimaisha unaotugubika.

Kingine ambacho Ndugu Kikwete ameweza kukiwakilisha kwa jamii, ni dhana ya uasi wa ndani UASI WA NDANI ya mfumo wa kuhafidhina wenye kuendeshwa na falsafa ya rushwa iliyokithiri ndani ya Chama kinachojiita cha Mapinduzi.

Ukiondoa karibia wote wanagombea nafasi hiyo ndani ya CCM, Ndugu Kikwete ndiye pekee mwenye kuonyesha kuwa ni kweli mwakilishi wa wakulima na wafanyakazi wa tabaka la kati na la chini kutokana na haiba yake ya uhalisia. Ndugu huyu ambaye ama kwa uthabiti wa kimaadili au mahesabu ya kisiasa, pamoja na mambo mengine ameweza kukataa “kuzawadiwa” nyumba zilizojengwa kwa jasho na damu za watanzania, kitu ambacho kinawapa matumaini vijana na wazee wengi kuwa ataweza kupambana na rushwa na hata kusafisha uozo huo ndani ya CCM na tabaka tawala kwa ujumla.

Sifa nyingine aliyonayo Ndugu Kikwete ni suala la mvuto. Hili kwa kweli ni silaha kubwa ambayo hata wenzanke wakimdhihaki vipi, kamwe hawataweza kumuangusha. Suala la sura ya mvuto ni muhimu sana kwa jamii iliyokata tama kama Tanzania.

Sio kwamba inampaa wapenzi wengi kisiasa hasa wale wa jinsia tofauti naye ambao ndio wenye kura nyingi zisizotetereka kirahisi ndani na nje ya CCM, sura na haiba ya mvuto ni silaha muhimu kwa kuongoza katika mwenendo wa siasa za kimaarufu “popular politics” ambazo wengi tunadhani zinahitajika ili kusafisha uozo wa kisiasa tulionao.

Uozo ambao umejengwa na kulindwa na baadhi ya wagombea pinzani wa ndugu huyu ambao watanzania wengi hasa vijana wangependa kuona wanatoka katika medani za kisiasa.

Sifa za Dr Salim duniani nadhani wote twazijua, sio tu kutokana na majukumu mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ambayo aliwahi na bado amekabidhiwa na wanadunia, lakini pia haiba yake ya unadhifu wa kisiasa ya mfano wa Mwalimu wake kipenzi, hayati Mwalimu Nyerere ambayo kwa sasa imekuwa ni fimbo muhimu katika jaribio lake la kuomba dhamana ya kuwaongoza watanzania moja kwa moja kama Rais wa nchi yetu.

Mengi yamesemwa kuhusu Dr Salim lakini mimi ningependa kwa kutumia kautaalamu kangu kadogo cha uchambuzi wa siasa wanachonipatia wasomi wetu pale mlimani kwa miaka kadhaa hivi sasa, kuongezea yale machache ambayo nadhani hayasemwi au hayajasemwa bado na vyopmbo vyetu vya habari.

Kutokana na upeo wa juu alionao ndugu huyu kuhusiana na mambo ya siasa za kidunia, Wengi na hata kutoka vyama pinzani na CCM wanaona Dr Salim anaweza kuwa ndio tunu ya nchi yetu kutupeleka kwenye Demokrasia ya kweli na si kwa maneno tu bali kwa vitendo.

Kwa wengi wanovutiwa naye, hilo kwake hakuna mjadala kwani ingawa wengi hubadilika na nguvu za madaraka, kwake yeye kama aliyewahi kuwa kiongozi wa mapambano dhidi ya unyonge, ukoloni na ubaguzi wa aina yeyote popote pale duniani pamoja na kuwa mpiga mbiu mkuu wa utawala wa demokrasia ya kweli barani Afrika, kufanya tofauti utakuwa ni unafiki ambao hata mtu asiye na haiba ya aibu hataweza kufanya hilo.

Lengine ni kuwa uhusiano wake wa karibu na Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Nyerere ambye ndiye amekuwa dira yake kisisasa. Uhusiano huo na mwalimu pamoja na wale watukufu wengine wa zamani (Disgruntled old guards) ambao walilitumikia taifa kwa adabu na heshima ya juu kwa wananchi.

Hawa ni kama wazee wetu akina Judge Warioba, Mzee Ibrahim Kaduma na wengineo wachache lakini washupavu ambao hadi sasa wanajaribu kuwa nguzo na dira ya dhana ya utawala wa kamaadili ambao kwa kweli umemong’onyoka mno kama sio kuisha kabisa. Hawa wameweza kumpa Dr Salim imani ya kuwa ataweza kurudisha utawala wa nidhamu ya kimaadili nchini.

Katika safari yake kuelekea uchaguzi, Dr Salim ameweza kuonyesha kuwa mbali na kusimamia ujenzi wa uchumi imara lakini anaweza kurudisha dhana ya maadili ambayo si tu tunaihitaji kwa kulinda haka kaamani ketu kwa kulinda utu wa kila mtanzania bila ya kujali nafasi yake kiuchumi, bali pia kutupunguzi janga la ukimwi ambalo kwetu sisi ni adui kama ilivyo ugaidi wa kidini kwa Taifa la Marekani hivi sasa.

Kingine ambacho haka kaupeo kangu ka kuchambua masuala ya siasa kameweza kunionyesha ni kwa msomi kama Dr Salim ambaye sio tu wa darasani bali hata katika kufikia maamuzi yake, ni dhahiri atweza kusimamia kuona kuwa thamani ya usomi makini na wasomi wetu itarudishwa.

Katika duru ya wasomi, ingawa si wote, wengi hata wale wanaompinga kwa sababu zingine wanaamini kuwa Dr Salim ataweza kutumia vyema nafasi ya kutuongoza kunusuru hali ya mbambo katika madhabahu zetu za kisomi na elimu, ambazo sio tu hali inatisha bali pia ni hatari kubwa kwa taifa letu hasa katika dunia hii ya ushindani usiokuwa na huruma wala haiba.

Bila ya kuwa ni kiongozi anayethamini hali na mawazo wa wasomi, kutambua umuhimu wa ELIMU BORA na sio BORA ELIMU, anayejiongoza kisiasa na kuwaongoza wananchi wake kwa lugha na mtindo wa kisomi, ni wazi hata tukiletewa malaika, safari ya tunapoelekea kusikojulikana itakuwa ya mwendo kasi na wa hatari mno.

Lingine ambalo kwa kweli si ajabu kuona watanzania wengi wa kizazi chetu hawakioni ni kuwa watanzania kama washika dau wakuu wa dunia ya tatu, au kwa kifupi masikini wa dunia, hivi sasa tunakabiliwa na zoezi kubwa la kupambana kuweza kupata mfumo wa siasa za kimataifa ambo utatambua na kutetea zaidi maisha yetu kiuchumi na kijamii kwa miaka mingi ijayo.

Hili ni suala la marekebisho mbalimbali katika mfumo wa umoja wa mataifa (UN) ambao kutokana na mchango wa Dr Salim na viongozi wenzake wengi wapatao kumi na tano pamoja na wasomi wetu kama Prof Mwesiga Baregu na Prof Haroub Othman, kuanzia mwezi September 2005 kule New York, Marekani na kwengine pote duniani, majadiliano makali yataendelea kujaribu kubadili mfumo wa kimataifa.

Mfumo ambao kwa miaka mingi umekuwa ukiwapendelea mno mataifa makubwa na tajiri dunia na kukandamiza ndoto zetu za kupata ahuani ya kweli ya kimaisha. Kwa kweli kama hatutakuwa na kiongozi shupavu, makini, msomi, mwenye kuheshimika katika medani za kimataifa na mjuzi wa hali ya juu wa masuala haya, Tanzania ambayo ina jukumu la kuongoza sauti ya wanyonge kupitia nafasi yetu katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama mwanachama wa muda kwa miaka miwili kuanzia mwezi January mwaka huu, ni dhahiri mpambano huu tunaweza tukaupoteza hivyo tukawa tumejisaliti na kuwasaliti mabilioni ya wanadunia masikini na wanyonge wanaotegemea sauti yetu huko.

Nasisitiza hili kwa sababu najua wazi kuwa bila ya kubadili mfumo wa siasa wa kimataifa, hata kama utaletewa malaika wa juu kabisa, kamwe mbio zetu zitaishia ukingoni na kuendelea na siasa za longolongo, kama wanavyosema vijana wa mjini.

Ukiangalia hizo baadhi ya sifa za wagombea hawa wawili wa CCM hapo juu na nyingine nyingi zilisosemwa na zinazosemwa na watanzania mbalimbali, kama za kweli au za uongo, ni wazi kuwa mmoja kati yao ndiye turufu ya ushindi wa kirahisi kwa CCM.

Kama siasa zingekuwa ni kufuata kigezo cha umaarufu tu na sio vinginevyo basi ni wazi kuwa wagombea wengine wangeshajitoa muda mrefu na kuupunguzia umma wa watanzania adha ya kufukiri sana kuhusu hatma ya maisha yao na nchi yao kwa ujumla. Lakini ukweli sio hivyo.

Na: Omar S Ilyas
University of Dar Es Salaam.