MPAMBANO KATI YA SIASA ZA UMAARUFU, UHAFIDHINA NA UMAKINI NDANI YA CCM: NINI HATMA YA MTANZANIA.

@2005..Published by RAI
NA ILYAS, O. S

Ilikuwa miaka, ikaja miezi na sasa imebakia wiki moja tu watanzania wachache watukufu katika ulingo wa maamuzi ya nchi wakutane kule Dodoma katika madhabahu makuu ya siasa nchini kuamua ni nani anapewa nafasi ya kugombea ubwana mkubwa wa nchi yetu kwa tiketi ya kile kinachoitwa chama cha mapinduzi.

Mimi kama mtanzania mwanachama wa chama kinachoitwa TANZANIA kinachofuata imani ya MWAMKO WA UAFRIKA naamini ni wajibu wangu kuchambua na kuelezea yale ninayoyaona yakiendelea na yatakayoendelea wakati na baada ya uchaguzi huu bila ya woga na hata kama nafasi yangu kubadilisha mawazo ya ndugu zangu wa CCM ni finyu mno.

Chama cha mapinduzi kama yalivyo makundi mengine yenye nia ya kuwa na uwezo wa kisiasa na kikatiba kushikilia mihimili ya nchi inayotoa na kuelekeza maamuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika dola lolote, daima huwa katika mivutano ya hapa na pale inayoletwa na tofouti mbalimbali miongoni mwa wanakundi hilo.

Mivutano hiyo inaweza kuwa ya kifikira, kiutashi, kimuono ama kimaslahi. Mivutano hiyo inaweza kuwa ya siri ndani ya wanakundi pekee, inaweza kuwa inatokana na mawazo ya wanakundi pekee au kama ilivyo sasa kwa CCM ikawa ya wanakundi wakishirikiana, kuhusisha au kuendana na mawazo ya wasio wanakundi kutoka ndani au nje ya mipaka ya nchi yetu.

Kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa yakiendelea ndani ya kundi hili linaloitwa Chama cha Mapinduzi. Mabadiliko ambayo yanalenga kulifanya kundi hili kuendana na fikra za baadhi ya wanakundi hilo.

Wanakundi ambao wanadhani kuwa fikra zao ni bora zaidi kwa maslahi ya nchi na wananchi wake, chama na wanachama wake na vilevile maslahi binafsi ya baadhi ya wanakundi hili ambao nao wamejenga vikundi uchwala vyenye lengo la kufanikisha fikira zao, utashi wao, muono ama maslahi yao binafsi.

Ili hilo lifanikiwe wanakundi hawa wamekuwa wakitumia mbinu mbali mbali halali na haramu kufanikisha mapambano au mikakati yao dhidi ya fikira na muono tofauti wa wanakundi wenzao.

Baadhi ya mbinu ni kama kuanzisha vikundi uchwara ndani kundi kuu yaani CCM, kushirikiana na wanambinu mbalimbali kama vile wasomi, waandishi wa habari, viongozi wa kijamii, vyombo vya dola na hata wafadhili kutoka ughaibuni kueneza, kuzipamba na kuzilinda fikra zao kwa wananchi ili waweze kupata uhalali rasmi kutoka kwao.
Lakini ili hili lifanikiwe ni lazima waweze kushika hatamu za madaraka ya dola kwa kumweka yule wamuonaye ni chaguo bora kuwaongoza katika kufanikisha utekelezaji wa fikra na maslahi yao.

Hapa ndipo tunapokuja katika umuhimu wa suala zima la mbio za kugombea nafasi ya urais wa Tanzania kupitia kundi kuu la CCM na baadaye uongozi mkuu (uenyekiti) wa kundi hilo kama taratibu walizojiwekea ndugu hawa.

Kwa upeo wa uchambuzi wangu wagombea wote wa CCM wanawakilisha makundi makuu matatu. La kwanza ni lile linawakilisha fikira za siasa za umaarufu, la pili ni lile linalowakilisha wanakundi wenye kuamini siasa za kihafidhina na la tatu ni lile linaloamini umuhimu wa siasa za umakini.

Ingawa kuna wagombea zaidi ya kumi lakini ukweli ni kuwa wote hawa ni wawakilishi wa moja ya makundi haya ambayo yana wagombea halisi na wagombea vivuli.

Kwa wale waliosoma makala yangu iliyopita niliyoiita KIKWETE CHAGUO MAARUFU, SALIM CHAGUO MAKINI ni wazi wameshajua viongozi wa makundi mawili. Kundi la tatu ni lile linaloongozwa na mgombea mwingine machachari ndugu MALECELA.

Wengi mnaweza kudhani kuwa chimbuko la makundi haya ni miaka miwili au mitatu ya hivi karibuni.

La hasha, chimbuko hasa la siasa hizi za kimakundi ni miaka ya mwanzo ya themanini ambapo hata kama mimi binafsi nilikuwa mdogo sana kwa umri, lakini utundu wangu wa kuhoji uliweza kuniangaza na kung’amua mwanzo wa mwisho wa CCM imara na hata Tanzania ya amani tuliyokuwa tunajivunia popote pale duniani.

Chimbuko hili mimi naliita chimbuko la falsafa ya UNYANG’AU iliyozaliwa rasmi kule katika visiwa vilivyokuwa vikijulikana duniani kote kama vya marashi ya karafuu na sasa vinaelekea kupata umaarufu wa kufananishwa na marashi ya damu.

Hivi ni visiwa vya Zanzibar ambako ndipo ule mkutano maarufu wa wateule wa mtetezi wa kweli wa siasa za upendo, heshima, maadili na umoja kwa jina la siasa za Ujamaa, waliamua kukaa chini na kuondokana na kile walichokiona ni ushamba wa kifikira wa hayati mzee wetu, Mwalimu Nyerere.

Hili sio lingine bali ni azimio la Zanzibar la mwaka 1986 ambalo pamoja na mambo mengine liliondoa nguzo muhimu za uimara wa jamii yetu zilizokuwa zikisisitiza maadili ya kiuongozi na siasa nadhifu zenye kulinda na kupigania maisha mema kwa wote bila ya kujali hali ya kimaisha, nafasi ya kisiasa au kidola, tofauti za kidini na kabila au asili ya mtanzania.

Falsafa hii ya unyang’au ndio iliyozaa makundi makuu mawili yaani kundi la siasa za kihafidhina na kundi la siasa za umaarufu. Matokeo ya kuchipua, kujikita na sasa uwezekano wa kushika hatamu kwa siasa hizi ndizo zilizopelekea kuzindukana na kutahayari kwa kundi la siasa za umakini.

Ni wazi kuwa miongoni mwa wana makundi haya ndani ya CCM kwa njia moja au nyingine wameshiriki katika ile hafla ya kuzaliwa rasmi kwa falsafa ya unyang’au kule Zanzibar. Ama walikuwa miongoni mwa waliosimamia kupitishwa kwake au walikuwa katika nafasi ya utazamaji tu wakidhani kuwa wao ni vichuguu wasingeweza kupambana na mibuyu ya wakati huo.

Lakini vilevile inawezekana walidhani kuwa zoezi hilo lilikuwa ni la busara ambalo kwa mahesabu yao lingewawezesha kuondokana na umasikini mali uliokuwa ukiwakumba wakati huo ambao kwa mtazamo wao ni falsafa za siasa za ujamaa ndizo zilikuwa chanzo kikuu.

Miaka kadhaa ya majaribio ya falsafa hii ya unyang’au ilipeleka baadhi ya wanakundi kuu kuanza kujiuliza kama falsafa hii ni bora na zaidi ina mnufaisha nani. Hapa ndipo lilipoibuka kundi la siasa za uhafidhina ambalo lilinza kujijenga na kujipanua katika miuondo mbinu yote ya kiutawala ili kuhakikisha kuwa falsafa hii ambayo iliweza kuwaonyesha nuru yao kimaslahi inabaki kutawala taifa letu.

Kundi hili lilitumia mbinu mbali mbali hata ikafikia wakati likawa tayari hata kuvunja muungano wa nchi yetu ilimradi kuondokana na kanguvu cha ajabu cha baba wetu wa taifa aliyeweza kung’amua hatari ya kusimikwa kwa falsafa hii ya unyang’au kwa kusingizia Utanganyika na Uzanzibari. Baba wa taifa alijaribu kupinga safari hiyo ya wahafidhina waliokuwa wakijaribu kushikisha hatamu kwa falsafa yao ya unyang’au wakati huo.

Upinzani ambao aliweza kuendeleza hadi katika uchaguzi wa mwaka 1995 lakini bila ya kujua akapigwa chenga ya mwili na wajanja wajanja wachache walioweza kumlaghai kuwa wao wana dawa ya tatizo lilikuwa likimuumiza kichwa chake.

Matokeo yake hadi mzee wetu huyu alipoelekea dunia nyingine ambako hivi sasa nina uhakika amekuwa BIZE akipokea ripoti mbalimbali za hali mambo hapa kwetu kwa wajumbe waliomfuata hivi karibuni, Unyang’au umeendelea kishamiri na hivi sasa unajaribu kushika hatamu kwa sura mbii tofauti.

Kushamiri kwa unyang’au na uwezo wake wa kuamsha chuki za kimfumo miongoni mwa watanzania wengi kumepelekea kuibuka kwa kundi la siasa za Umaarufu katikati mwa miaka ya tisini kama fikra mbadala za uny’angau uliokuwa ukiendeshwa na kulindwa na wanakundi la kihafidhina.

Ama kwa uchungu wa nchi yetu na watu wake (fikira ambayo najaribu kuendelea kuiamini ingawa mengi yananielekeza tofauti) au kwa POLITICAL OPPORTUNISM, kundi la siasa za Umaarufu limeweza kuibuka ndani ya kundi kuu na kujaribu kuonyesha kuwa lenyewe linaweza kumalizia kazi aliyoianza baba wa taifa ya kuondoa unyang’au na manyanga’au wote kutoka katika mihimili ya kisiasa na kidola nchini mwetu.

Kundi hili lilibahatika kupata baraka za wananchi wengi waliochoshwa na madhila ya unyang’au huu ambao umeleta umasikini na aibu za kimaisha zisiso na kifani miongoni mwa watanzania walio wengi.

Ni ukweli usiofichika kuwa kundi hili ambalo lilikuja usoni mwa watanzania wakati wa uchaguzi wa mwaka 1995 na kuzuiliwa kitaalamu na mwalimu Nyerere ambaye aliamini kuwa halijawa tayari kukabidhiwa majukumu makubwa ya kuongoza nchi yetu, lilikuwa limesheheni vijana wachache ambao ni wazi walikuwa na uchungu mkubwa kwa nchi yetu.
Kwa bahati mbaya manyang’au wachache waliona hatari ya kundi hilo mbeleni hivyo kwa mwendo wa taratibu wakaanza kujipenyeza ndani ya kundi hili na hatimaye kushika miundo mbinu yote ya kisiasa.

Manyang’au hawa ambao walijuwa wazi kuwa kamwe hawataweza kufanikisha ndoto yao ya kushika hatamu za kiutawala za nchi hii na hivyo kurutubisha neema zao bila ya kujipenyeza katika kundi hili.

Wao walijuwa wazi kuwa kutokana na laana ya wazi ya baba wa Taifa aliyolipa kundi la siasa za kihafidhina, laana ambayo alikuwa akiendelea kuisisitiza hata katika matamshi yake ya mwisho kabla ya kukatwa kauli, kamwe wateule wao wasingekuwa na nafasi ya kushika hatamu ya taifa letu na kundi kuu yaani CCM hapo baadae.

Hawa waliamua kuelekeza nguvu zao kwa mteule wa kundi la siasa za umaarufu wakijua kuwa kama watafanikiwa kushika hatamu za madaraka nchini na ndani ya CCM wataweza kuendeleza unyang’au wao kwa mgongo wa mteule wa kundi la siasa za umaarufu aliyetokea kuwa maarufu na hivyo kwa mawazo yao ni rahisi kushinda jaribio la ugombea wa urais wakati huu.

Kwa bahati mbaya ama kwa kudhani kuwa ni uamuzi sahihi, mteule wa kundi hili linaloamini siasa za umaarufu zenye mlengo wa kile kinachoitwa utawala mpya na mawazo mapya, amewaachia manyang’au hawa nafasi kubwa katika mkakati wake za kuchukua madaraka ya nchi yetu.

Ndio maana imefika wakati watanzania kwa namba inayokuwa kila kukicha kuanza kuhoji kama kweli hata yeye binafsi ni suluhisho la madhila yanayowakumba na kama kweli anaweza kuundoa falsafa ya unyang’au wakati amekuwa akiwategemea manyang’au na kuachia mbinu za kinyanga’au kutawala mkakati wake kile wanachidai wa kujenga historia mpya hapa nchini.

Pamoja na mambo mengine, kutokana na hali hii ndipo likazuka kundi lingine ambalo ni dogo mno kwa hesabu lakini kubwa kwa kimkakati ambalo linadhani kuwa ni siasa za kanadhifu na kimaadili pekee ndizo zinaweza kutimiza ndoto za mwisho za baba wa Taifa za kuondokana na falsafa hii ya kinyang’au katika kundi kuu, yaani CCM na hivyo Tanzania kwa ujumla.

Kundi hli ambalo linajumuisha watu mashuhuri ambao baadhi yao walikuwa na nafasi katika tawala mbili za mwanzo za taifa letu pamoja na wanasiasa wapya wenye kukerwa na mambo na msuguano wa makundi mengine mawili limejikita chini ya mgombea wamuonaye makini zaidi yaani Dr Salim.

Kwao wao wanadhani uzoefu, ustaarabu, umakini na uaminifu wa kimaadili alio nao mgombea huyu ambaye kwa mara kadhaa marehemu baba wa taifa alipendelea awe mrithi wake wa uongozi wa siasa zake za Kinadhifu, kiupendo na kimaadili, ndio kweli unaweza kutuepusha na madhila ya unyang’au.

Madhila ambayo kama wao hawatafanikiwa yanaweza kuongezeka zaidi endapo waumini wa falsafa hiyo ya unyang’au ndani ya kundi lao la CCM wataweza kushika hatamu ama wao binafsi au kwa kutumia mgongo wa kiongozi mwingine.

Kundi hili linaamini siasa makini ndizo kama ndio silaha muhimu ya mwisho ya kunusuru ya kundi lao kuu (CCM) na Taifa letu na vilevile hatma ya watanzania kwa ujumla. Linaamini kuwa siasa za umakini zenye kuendeshwa na uaminifu wa uongozi wa kimaadili na wenye kung’amua hasara za siasa za kihafidhina na umaarufu sio tu unaweza kuondoa madhila ya unyang’au unao ota mizizi katika jamii yetu lakini vilevile kuepusha janga linalotujia mbeleni kutokana na msuguano wa hayo makundi mengine mawili.

Katika mtazamo wangu ninaamini kuwa angalao kundi hili ndilo linaloweza kutuokoa watanzania na kitimtimu kilichoko mbeleni cha wanamakundi mawili ya umaarufu na uhafidhina ambayo kwa kweli pamoja na mapungufu mengine yameonyesha chuki na uadui mkubwa ambao ni dhahiri ndio utakawo kuwa dira ya ama wateule wao wakuu au wateule wao vivuli watakaposhinda mpambano huu haramu.

Sio tu kwamba itawabidi kusafisafisha wale wanaodhani wanatofautiana na kifikira na kiutashi kuhusiana na vipi nchi yetu iendeshwe lakini vilevile ni dhahiri watalazimika kuwandoa au kuwanyamazisha wale wote waliokuwa wakiwaona ni maadui zao na pengine wakawa kikwazo kwao kufanikisha yale yaliyopelekea wao kuamua kupigania nafasi hiyo ya juu ya kimaamuzi ndani ya chama na jamii kwa ujumla endapo watashika hatamu zote zikiwemo za dola.

Mimi kama nilivyodokeza hapo juu sina mahusiano ya ki-uwanachama na kundi hilo kuu linalojiita la chama cha mapinduzi hivyo kwa kile tunachosema ni kawaida isingenipasa kuingilia mpambano wa ndugu zangu hawa wa CCM.

Lakini nikiwa kama mtanzania na muafrika ninayeamini amani na upendo kama nguzo kuu za uanadamu na mwenye uchungu na nchi yangu hii ninamuomba mungu asikie vilio vya wengi vya kuwaamsha baadhi ya wapiga kura ndani ya CCM.

Ndugu zetu ambao wamegubikwa na ushabiki na tama ya maslahi binafsi waweze kuzinduka na kuona umuhimu wa umakini katika kufikia uamuzi wao wa mwisho ili kuliepesha taifa letu na janga lunalotujia.

Janga la muendelezo wa falsafa ya unyang’au, ama kwa sura ya sasa ama sura, ambayo kwa muda wa sasa ndio imekuwa rutuba bora ya machafuko na ukosefu wa amani kwa taifa letu na hata majirani zetu.

Hatma ya watanzania ipo mikononi mwa ndugu hawa wachache ambao mpaka sasa wameweza kufanikiwa kutwaa utukufu wa kidunia wa kuwawezesha kutuamulia watanzania milioni 36 ni nani atakeyekuwa ameshika uhai wetu wa kifikira na kibailojia kwa miaka mitano ama kumi ijayo.

No comments: