BARUA WAZI KWA WAPIGA KURA WA CCM..

@2005..published by RAI

Ndugu watanzania wenzangu,
Kwanza hongereni kwa kuweza kuwa miongoni mwa watanzania wachache ambao mungu amewajalia kuwa na nafasi ya juu kabisa nchini mwetu ya kuamua ni nani anakuwa kiongozi wa nchi yetu kwa miaka mitano au kumi ijayo.

Vilevile nawapongezeni kwa kuwa wavumilivu wa madhila ya usumbufu wa hali ya juu kutoka kwa wale wanaowakilisha maslahi ya wakubwa wenzenu wanaotaka kuingia ikulu kwa makeke ya karne.

Ndugu zangu mimi si mwanachama wa chama chenu kitukufu lakini kama mtanzania ninayejua wajibu wangu najua umuhimu mlio nao wakati huu katika kuamua maslahi yangu, ya ndugu zangu na watanzania wenzangu wote kwa ujumla.

Ninajua kuwa chaguo lenu ndilo litakalofanikisha au kuvuruga ndoto zangu nyingi kuhusiana na nchi yangu na bara langu nilipendalo la Afrika.

Ninajua kuwa ufunguo wa chembe ya uhuru ninayo jivunia hivi sasa na nikaweza kukaa hapa nilipo na kuandika barua hii kwenu mnao ninyi na ni ninyi ndio mtakaoamua kama nitaendelea kuwa nao hata baada ya usiku wa tarehe nne mwezi ujao.

Ninajua kuwa ni ninyi wenye kushika mstakabali wa maisha yangu ya upendo na uvumilivu kwa watanzania wenzangu ambao daima nimekuwa nikiwapenda bila ya kujali dini zao, makabila yao, rangi zao ama hali zao za kimaisha.

Ninajua kuwa kura zenu mtakazopiga wiki ijayo ndizo zitakazoamua kama na mimi nitabahatika kuoana na nimpendaye na kuzaa naye watoto wazuri watakaojivunia na Tanzania nitakayowachia.

Ninajua kuwa wengi wenu tayari mmeshamua ni nani mngependa awe rais wa nchi yetu ama kutokana na mvuto wake, ukaribu wake nanyi, umaarufu wake, ucheshi wake, unyenyekevu wake na hata uchapakazi wake mnaodhani kuwa ni muhimu kwa uongozi wa nchi yetu kuondokana na hali tuliyonayo sasa.

Ninajua kuwa wengi wenu mnadhani kuwa ni lazima kulipa fadhila kwa wale waliofanikisha ninyi kupata nafasi hii hata kama kwa masharti ya kudhalilisha kama kulazimika kumpigia kura mgombea wa yule aliyekusaidia kufanikisha mambo na wewe ukapata nafasi uliyona nayo.

Ninajua kuwa wengi wenu mna deni la kulipa kutokana na misaada mbalimbali kama vile kumlipia mwanao ada ya shule, kulipia matibabu yako au ya mpendwa wako wakati akiumwa, au kukupa nafasi ya kwenda kusoma elimu ya juu ama pale mlimani ama kwengineko duniani. Haya yote mliyopata kutoka ama kwa wafadhili mbalimbali waliokaribu na mgombea Fulani ama hata mgombea mwenyewe.

Najua kuwa wengine tayari mmeshaahidiwa nafasi kubwa kubwa za uongozi katika nchi yetu ili mradi mhakikishe kura yako inaandikwa jina la mgombea Fulani.

Najua wengine mna amini kabisa kuwa kutokana na ukweli kuwa wagombea wengine wote ni ‘wachafu’ na wengine sio watanzania basi huna la kufanya ispokuwa kumpigia kura mgombea ambaye mnadhani kuwa ni msafi na hana hata tone la uchafu isipokuwa harufu ya neema tu.

Ndugu watanzania wenzangu naomba uchukue muda huu hata vidakika vichache kwanza kufikiria kama hayo unayoamini kuhusu mgombea huyo ni kweli na hakuna uwezekano kuwa kuna upande mwingine wa mgombea huyo ambaye wewe hujapata nafasi ya kuujua kwa sababu wenye majukumu ya kukujulisha wamelazimika kutokujulisha.

Halafu ndugu mtanzania mwenzangu naomba ufikirie kama kweli vigezo unavyotumia kuamua mtu wa kumpigia kura yako tukufu ni vigezo tosha vya kumpa mtu jukumu zito la kuwa rais wako mwenye nguvu za juu za kimaamuzi katika kila kona ya maisha yako kwa mika mitano ama kumi ijayo?

Hivi vigezo hivyo vimeweza kukusaidia kutambua mtu ambaye kweli na sio anayejidai, ambaye atahakikisha chama chako kinaendelea kuwa na umoja na nidhamu ya kweli iliyowezesha kushinda mitihani mbalimbali ambayo kimekumbana nayo kwa miaka yote hii tangu kianzishwe na wazee wetu waliotutangulia?

Hivi vigezo hivyo vilijitosheleza kukuongoza wewee kufikia uamuzi wako kwa umakini wenye kuhitajika kuamua mtu bora wa kumkabidhi hazina yetu, utamaduni wetu, uvumilivu wetu, upendo wetu, unoja wetu na zaidi maisha yetu na wote tuwapendao na watupendao.
Hivi uamuzi wako umetilia maanani kama huyo utakayemchagua atakuwa ndiye anayetakiwa kukuongoza wewe na familia yako katika mapambano dhidi ya gonjwa la ukimwi kwa yeye mwenyewe kuwa mfano bora wa kubadili tabia.

Hivi huyo mgombea umpendaye au unayelazimika kumchagua ndio kweli yeye atayeweza kuiongoza Tanzania katika dunia hii ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa umakini wa hali ya juu wenye kutambua nini haswa kinatakiwa kifanyike ili nchi yetu iheshimike duniani na hivyo kusikilizwa matakwa yake.

Hivi huyo mgombea anaweza kumlinda mdogo wako, dada yako, kaka yako, mpendwa wako, mwanao au rafiki yako mpendwa na masahiba ya utandawazi yaliyojaa ulaghai na utapeli wa kila aina.

Ndugu yangu umejaribu kufikiri ikiwa ni mgombea wako anayeweza kutuokoa katika janga la kuvunjika kwa amani ya nchi yetu kutokana na tamaa ya madaraka ya baadhi ya wagombea ambao wameamua kutumia mbinu za chuki na visasi ili kufanikisha matamanio yao ya kidunia.

Hivi ni kweli mgombea unayetka kumpigia kura yako anaweza kusema hapana kwa wababe wa dunia pale wanapotka kufanya nchi yetu ni tambara lao bovu la kufutia vinyesi vyao vya kibeberu vinavyopita vikidondoka kila kukicha.

Hivi kweli ndugu yangu hudhani kuwa hata kama una deni la kulipa fadhila za mgombea uliyeambiwa umpigie kutokana na mamilioni uliyopewa, maslahi ya ndugu zako pale nyumbani na watanzania kwa ujumla yana umuhimu zaidi kuliko ya hao.

Hivi kweli ndugu yangu unadhani kuwa mgombea uliyeambiwa umpigie kura ulipokuwa unapewa msaada ule wa kifedha ndiye atakeyeweza kukupunguzia kero la rushwa linalowasibu kila siku wewe na familia yako.

Hivi ni kweli kuwa mgombea huyo uliyevutiwa naye anaweza kujenga nyufa za nguzo za dola letu zinazobomolewa na wapambe wake kila kukicha ili nao wapate kuingia ikulu bila ya appointment kuanzia mwezi wa kumi na moja mwaka huu.

Hivi umefikiria jinsi kura yako inavyoweza kuwaingiza ikulu mabaradhuli, wezi, wauza nchi, waruka kodi, mafuska na walaghai ambao wanakuja kwako na sura ya ucheshi lakini ndani imejaa ushetani wa hali ya juu kabisa.

Ndugu yangu kwa kweli sipendi kukuchosha maana najua hapo ulipo una majukumu makubwa mbele yako, lakini naomba ufikirie kidogo kama kura yako haiendi kwa mtu ambaye ameonyesha dhahiri kuwa hakubaliani kabisa na nyendo na maadili ya utanzania ambayo mwalimu wetu baba wa Taifa alituwekea kama vipimo vya mapenzi yetu ya kweli kwa nchi yetu.

Mwisho ndugu yangu mpendwa naomba ufikiri hivi ni kweli kura yako haiwezi ikatoa chaguo bora zaidi litakalotuwezesha kuokoa taifa letu kutoka katika janga la kuangamia, litakalotuwezesha watanzania kwa mara nyingine kutembea vichwa juu kwa kujiamini, litakalotuwezesha kutuepusha kuwa na baraza la mawaziri lilojaa matapeli na walaghai watakaokuwa wakitudanganya kila kukicha, chaguo litakalotuletea viongozi waadilifu kwa mungu na kwetu sisi bila ya kujali hali zetu za kimaisha, chaguo litakalolinda thamani ya kila mtanzania, chaguo litakalotusaidia kuinua hali ya elimu ya nchi yetu kwa kujua thamani yake na zaidi chaguo litakalo simama kidete kuchukua maamuzi kwa utulivu na umakini wa hali ya juu ilojawa na busara za kiuongozi bila ya kuhatarisha maisha yetu na wala kurubuniwa na wapambe uchwara.

Ndugu yangu mwana CCM, ni wewe ndiye utakeyeamua ni Tanzania ya aina gani tutakayokua nayo wiki mbili zijazo.

No comments: