DHANA YA ARI MPYA NA SIASA ZA MATUMBO

@2005...kuelekea uchaguzi mkuu. Published by Mtanzania Jumapili..


Baada ya mbio za ugombea nafasi ya Urais katika Chama Cha Mapinduzi kutulia na anayedhaniwa kuwa mkombozi kupatikana sasa mapambano yamehamia katika nafasi za ubunge na udiwani.

Katika siku za hivi karibuni sura nyingi mpya zimeibuka zikijitangaza kuwa na nia ya kuomba ama kupigania uwakilishi wa watanzania katika nafasi mbalimbali za uwakilishi zilizobadilishwa jina na wajanjawajanja wa sasa na kuitwa nafasi za uongozi na uheshimiwa.

Tofauti na miaka iliyopita ambapo tulizoe sura Fulani fulani tu, mwaka huu mambo ni nguvu mpya tu.

Ni dhahiri kuwa hivi sasa zaidi ya wakati mwengine wowote vijana wanawake kwa waume wamekuwa tayari zaidi kuwania nafasi za uongozi (uwakilishi) katika jamii zao kitu ambacho kwa upande mmoja ni kizuri na muhimu kwa taifa letu kwa ujumla.

Ni wazi kuwa ushindi wa mgombea wa CCM aliyetumia jukwaa la ujana katika kujihakikishia nafasi hiyo umekuwa na athari kubwa katika mfumo mzima wa siasa ndani na nje ya CCM.

Kwa kiasi Fulani ushindi huo umekuwa ni chachu kwa wanasiasa wachanga ambao hapo awali kamwe hawakuthubutu kusimama na kuhoji uhalali wa wazee wao pekee kuendelea kushika nafasi za kiutawala milele amina.

Ushindi huu dhidi ya wale walioitwa wazee umeweza kuwatia moyo vijana kwa malaki kuwa hata wao wanaweza kupata uheshimiwa kama wataamua kama alivyoamua “kijana” mwenzao.
Ushindi huo umeweza kuwaamsha vijana wote kwa pamoja, makini na wajanjawajanja, ambao kwa miaka kadhaa walikuwa katika ndoto ya kuweza ama kuwa wawakilishi makini au kuukwa uheshimiwa kama walivyo wengine.

Kwa ujumla vijana wa kitanzania wameonyesha nia ya dhati ya kuacha kutumiwa kama ngazi za madaraka na wale wanaowaita wazee waliochoka na sasa wameamua kuingia uwanjani wao wenyewe.

Leo ningependa kuchambua suala zima la ari mpya na nguvu mpya katika taswira inayojengeka ya maelfu ya vijana kuonyesha nia na kuanza kampeni kubwa ili kuaminiwa na kupewa nafasi ya uwakilishi katika utawala ujao.

Kati ya vijana waliojitokeza wapo vijana wa makundi mawili ama matatu.
Wapo vijana wazee ambao ni zaidi ya miaka 35-40. Hawa wanatumia dhana ujana kama propaganda ya kukubalika katika jamii iliyogubikwa na ndoto ya “ujana ukombozi”. Hawa wengi wao ni vijana wa zamani kiumri lakini wanaweza kuwa vijana wa sasa kimatendo.

Wao wamekuwa wakitumia nafasi walizonazo kisiasa, kiserikali ama kibinafsi kujikusanyia nguvu za kifedha (kiuchumi) ili wakati ukifika waweze kujichomeka ndani ya mioyo ya watanzania na ili ama wawatumikie watanzania au waweze kujiongozea walichonacho.

Wengi wao ni wanajiita wasomi kwa kuwa wana digrii kadhaa hata kama zengine ni za kudesa na hazina uhusiano wowote na uongozi, mimi siwezi kuwaita wasomi.

Kwa mahesabu yao ni kuwa kijana mwenzao akishapewa madaraka basi ni wazi atataka kushirikiana nao kutekeleza kauli mbiu ya “ARI MPYA, NGUVU MPYA NA KIZAZI KIPYA”
Hivyo basi wao wanadhani ama wanadai wanamtayarishia mazingira kijana mwenzao ili atakapokuwa anatengeneza jeshi lake la makomando wa kichina aweze kuwaona na kuwasimika utukufu.

Kundi la pili ni lile la vijana wenzangu wenye miaka kati ya 25-40 ambao kwa kweli wengi wao ni vijana kweli kiumri, kifikira na kimatendo.

Wengi wao hawana elimu ya kutosha ya kujiita wasomi lakini wapo walio na digrii moja nao lakini wana ujasiri wa kujitanabahisha na kina Prof Shivji, Baregu na wengineo.

Katika kundi hili wapo wengi ambao hadi hivi karibuni uongozi kwao ulikuwa ni kupoteza muda na kuhatarisha maslahi yao binafsi. Hii iwe maofisini wanapofanya kazi, mashuleni wanaposoma na vilevile katika biashara zao binafsi haramu na halali.

Katika kundi hili ambalo ni kubwa si haba, kuna wengine ambao uwezo wao wa kifedha ambao hata kama umetokana na kuibia serikali, kulisha watanzania vyakula vyenye sumu, kuuza siri za nchi, kutetea majambazi na wezi wa mali za umma, kusainisha nchi mikataba ya kihuni na machafu mengineyo, umewapa jeuri kuwa hakuna cha kuwazuia na wao kuwa waheshimiwa.

Kwao wao kujiingiza kwenye siasa ilikuwa ni mwiko eti watahatarisha maslahi yao. Wengi wa hawa katika siku za nyuma kamwe hawajawahi kujitokeza kipigania hai ya yeyote yule hata kama ni motto ananyanyaswa katika daladala. Kwao wao ilikuwa ni bora wao wamekaa kwenye viti ya wengine shauri yao.

Wengi wa hawa siku hizi ndio wamekuwa wakombozi kila sehemu mradi kuna wapiga kura wanawaona.

Kundi la tatu ambalo ni dogo mno lakini ndilo muhimu kwa taifa letu ni la wale vijana wa kati ya umri wa miaka 20-35 ambao katika maisha yao yote ya nyuma wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania maisha mema kwa watanzania wote.

Katika kundi hili wapo wenye elimu ya kutosha na elimu ndogo kama tukipima kwa vigezo vya madarasa.

Lakini zaidi wana elimu ya matitizo ya kijamii na kisiasa yaliyomzunguka mtanzania na kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa mstari wa mbele kuyaongelea kila pale inapowapasa kufaya hilo.

Kwa vitendo wameweza kuonyesha umma jinsi gani walivyoweza kujitoa mhanga katika nyakati mbalimbali kwa ajili ya kutaka kuona watanzania wenzao wakiacha kuteseka na kuonewa kwa kunyimwa haki zao mbalimbali.

Tatizo ni kuwa kundi hili halina fedha za kufanya kile tunachokiita kampeni hivyo kuna hatari kubwa ya kushindwa ama kununuliwa na wenye fedha hivyo kushindwa kutekeleza kile wanachofikiria kukifanikisha.

Watashindwa kwa kuwa tayari na kuna wajanja wajanja ambao kwa ufanisi wa hali ya juu wameweza kubadilisha kabisa maana nzima ya uongozi na kiongazi.

Hawa wamefanikiwa kutumia mwanya wa demokrasia kufanya mchakato mzima wa kuchagua wawakilishi wetu kutoka kuwa wa kutafuta yule mwenye sifa za kuongoza wenzie kwa umakini hadi kuwa kama vile kazi ya kuchagua bidhaa katika mfumo huu tunaouita wa soko huria.

Mfumo ambao hivi sasa ndio unatopatia viongozi wa kila aina kwa kuwa unaruhusu yeyote yule kuweza kushinda kuwa kiongozi mradi ana uwezo wa kujiuza na kuulaghai umma kwa nguvu kuwa yeye ndio anameremeta hata kama kwa kutumia mkorogo tunaouita takrima.

Bahati mbaya zaidi wapiga kura wa sasa tumeondokana na umakini wa kuhoji ubora wa bidhaa kama hizo na kukubali kuvutiwa na mwonekano wake tu eti kuwa Fulani anakubalika.

Kwa kweli wanaotoka katika kundi hili ni wachache mno lakini wapo wakijaribu nafasi yao hata wakijua kuwa wanacheza katika uwanja huu wa kisiasa uliojaa visiki na mbigili.

Wao ndio pekee wanaoweza kuwambia watanzania ni kipi wamekifanya kwa faida ya jamii wakati wakiwa bado wachanga kiumri na kisiasa hata kama hawakuwa na uwezo wa kutosha.

Hawa ndio wanaweza kuwaambia wananchi ni maslahi mangapi binafsi wameyapoteza kwa kujaribu kusimamia ukweli pale inapobidi.

Mfano wa hawa ni kijana mwenzangu mmoja mwenye umri wa miaka ushirini na nne ambaye siku alipojitokeza kutangaza kugombea ubunge jimbo fulani jijini Dar es Salaam, vyombo vya habari vilimkejeli kuwa ni motto na kumchora akiwa na nyonyo mdomoni akidai haki yake ya kupigiwa kura.

Pamoja na umri wake mdogo kwa kipimo cha uwana siasa wa Tanzania, kijana huyu niliyotokea kumjuwa wakati bado akiwa mwanafunzi wa kidato cha tano lakini tayari mpambanaji shupavu wa haki za binadamu na vijana kwa ujumla ndio mfano wa wale haswa wanaoweza kutekeleza kwa dhati ari mpya hii tunayoahidiwa endapo ni ari ya kumkomboa mtanzania kama wengi tunavyodhania.

Nasema hivyo kwa kuwa tofauti na hao wengine wanaotaka kutumia dhana ya Ujana ama ari mpya , nguvu mpya na kizazi kipya, kwa bahati mbaya au nzuri ndio waliojazana katika uwanja wa CCM, vijana wa namna hii ni nadra sana katika jamii yetu iliyogubikwa na siasa za ndio mzee kwa miaka mingi sasa.

Ni nadra kuwaona kwa sababu nyingi tu lakini moja ya wazi ni ile hali ya kutopenda kuingia katika mpambano wa kisiasa kama unaoendelea hivi sasa kwa kuwa umejaa uchafu ambao wengi wao wasingependa kujitambulisha ama kujihusisha nao.

Bahati mbaya ni kuwa kwa kufanya hivyo ndipo wanaacha mwanya kwa “vijana” wa aina ya kundi la kwanza na la pili ambao ni wachache mno ndio wenye uchungu wa kweli na taifa letu ukiachilia mbala na swala zima la sifa za kiuongozi waliaonazo, kuweza kutawala ulingo wa kisiasa nchini.

Ingawa nakubali kuwa wapo wachache walio tofauti, wengi wa vijana wenzangu hawa wa kundi la kwanza na la pili kwa kweli ukiwauliza ni kwa nini wanataka kupewa nafasi kwa kweli hawana jipya zaidi ya yaleyale tuliyoyazoea na hadithi nyingine za kizazi kipya

Kwa kweli hawana ajenda mpya kabisa zaidi ya kuukwaa uheshimiwa ili waweze kuyafanya kwa ufanisi zaidi yale mambo hovyo waliyokuwa wakiyafanya wakati huu wasipokuwa na nguvu za kisiasa.

Kwao wao nguvu za kisiasa ni muhimu sasa ili kujihakikishia nafasi yao katika mfumo wa kinyanga’u uliojaa rushwa, ufuska, uonevu, ufujaji wa mali za umma na uozo wa kila aina tunaojitahidi kuusimika katika jamii yetu.

Yupo msomi mmoja ambaye alikuwa akijaribu kuangalia aina ya siasa katika upande wetu huu wa dunia. Yeye aliita aina za siasa za dunia ya tatu kama nchi yetu ilivyo ni siasa za matumbo.

Siasa ambazo kwanza zinajali matumbo ya wachache walio na nguvu na suala la kusaidia jamii linakuja pale tu kura zao zinapohitajika ili kuendeleza nafasi ya utawala kwa wale waliomo na kutoa mwanya ya kuingia kwa wale wajanjwajanja wengine waliochoka kula mabaki.

Kwa kweli kwa kutumia dhana hii ndipo ikanijia washawasha ya kujaribu kufuatilia mchakamchaka huu wa vijana wenzangu katika kugombea nafasi za uwakilishi ambao wao kwao ni nafasi za uheshimiwa.

Hapo ndipo nilipochukua juhudi zaidi za kujua nani na nani anayetaka uheshimiwa hapo mwezi Oktoba na kwa nini yeye na nini sifa zake.

Kitu kimoja ambacho uchambuzi wangu unaniambia ni kuwa kuna hatari ya kuwa badala ya kutengeneza safu ya wachezaji wa kweli wenye kuweza kuweza kutimiza ndoto ya taifa jipya kama tunaloambiwa na kuishia kubadili sura za manyag’au tu.

Na ubaya ni kuwa manyang’au wa damu mpya huwa daima wanakuwa hatari zaidi kwa jamii kutokana na ukweli kuwa wametumia muda wa mwingi kusoma siasa chafu ambazo daima ndizo watakazotumia kufanikisha malengo yao binafsi na kuwanyamazisha wale watakaukuwa na kuburi cha kuhoji machafu yao hapo mbeleni.

Tofauti na tuliowazoea, hawa manyang’au watarajiwa ni wazi kima chao cha kuridhika ni kigumu kufikika na hivyo ari na nguvu watakazotumia kushibisha matumbo yao na ya wapambe wao zitakuwa ni za kutisha mno kuliko tunazoziona hivi sasa.
Si ajabu kuona kuwa aina hii ya vijana kwa wingi wapo katika chama tawala. Jibu ni rahisi mno.

Kwao wao kugombea kwa chama tawala kunawahakikishia usalama wao wa kutuanikwa machafu yao, kunawahakikishia ushindi kama wataweza kuteuliwa, kunawapa nafasi kubwa zaidi ya kukumbukwa na Rais ajaye ambaye kwa mahesabu yao ni lazima atoke huko na vilevile hata wakishindwa bado maslahi yao yatendelea kulindwa kwa kuwa wameonyesha kuwa wenzi wa watawala.

Kwa kifupi hawana jeuri ya kujaribu kubadili mfumo kwani siku nyingi wameshakubali yaishe, dhana yao ni kuwa huu ni wakati wa kucheza na timu ya ushindi ili kufanikisha mambo.

Kwa kweli ukiangalia mwenendo huu kwa ujumla ni wazi hatima ya Tanzania yetu ipo katika hatihati kwani kwa jinsi hali inavyokwenda ni dhahiri vijana wa kundi la kwanza na la pili ndio watakaoibuka washindi.

Hii ni kwa kuwa wazee wetu walishabadili mfumo wa siasa ndani na nje ya chama cha mapinduzi kuweza kufanya iwe rahisi kwa aina hiyo ya wanasiasa kupenya katika nafasi za uongozi katika jamii yetu.

Ni watanzania wenye ujasiri wa hali ya juu tu ndio wanaoweza kuwazuia hawa jamaa wanapita wakitufitinisha na kila aliye na umri mkubwa ili wao waoenekane ndio watakatifu.

Kama vijana wachache wenye uchungu wa kweli na taifa lao wataamua kusimama kidete na kuwapinga hawa walaghai wanaotumia madhila yetu kwa faida ya matamanio yao binafsi ni wazi makali yake yanaweza kupunguzwa kabla hawajafika mbali.

Ni wazi tukiamua hilo litafanikiwa kwani hawa tuko nao mitaani, viwanjani, mashuleni, majumbani na hata kwenye taasisi mbalimbali za umma na binafsi walipojaza historia ya machafu ya kila aina.

Kusimama na kuwaelezea machafu yao kwa wapiga kura ni wajibu wetu sote kwani ushindi wao ni balaa kwetu na salama yetu inategemea ujasiri wetu.

Tukiwaacha hawa malaghai wa kizazi chetu ni wazi tutakuwa tunajipotezea nafasi hii tuliyoipata baada ya muda mrefu wa kulalama kuwa vijana tunanyimwa haki yetu ya kujiongoza na kuongoza taifa letu.

No comments: