WAANDISHI WETU NA UKUWADI WA UNYANG'AU

@14th July 2006, Published by Tanzania Daima Newspaper.

Comrade Chachage aliwaita makuwadi wa soko huria, mimi nawaita makuwadi wa unyang’au. Makala hii niliandika miezi mingi iliyopita lakini mengi yalinisababisha kutoiwakilisha kwa wapendwa watanzania. Kutangulia kwa kaka yangu na mwalimu wangu wa fikra changanuzi, kumenipa nguvu za kuwasilisha hoja yangu kwa watanzania, wanyonyaji kwa wanyoge.

Neno manyang’au lina tafsiri mbalimbali katika macho ya watanzania. Kwangu mimi unyang’au ni ile hali ya kufikiri na kutenda mambo ambayo yanaathiri mustakabali mzima wa mwananchi wa kawaida. Manyang’au ni wale wote wanaotenda mambo mbalimbali kwa maslahi ya uchu wao pekee bila ya kujali madhara makubwa ya matendo hayo kwa jamii.

Hawa ni wale walio katika nafasi zote na haswa za juu za kutoa maamuzi serikalini, kwenye vyama vya kisiasa na katika makundi mengine ya kijamii. Hapa nchini mwetu utawakuta katika kila pembe ya maisha yetu. Wapo wenye nguvu kisheria kuwemo katika kundi hilo na wapo walioweza kujipenyeza humo kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile uwezo wa kiuchumi na nafasi zao katika makundi ya kijamii.

Manyang’au wapo wakubwa na wadogo. Wapo wa kutoka nje na wapo wengi tunaotoka nao katika nchi yetu hii hii iliyojaa harufu na ladha ya umasikini wa kutupwa.
Unyang’au ni mfumo rasmi katika jamii yetu ukiwa na baraka za kisheria kama zile za takrima na nyinginezo nyingi.

Makuwadi wa unyang’au ni wengi na wapo katika sekta zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Wapo wanaojiita wafanyabiashara, wapo wanaojiita makada, wapo wanaojiita wasomi, wapo wanaojiita watumishi wa serikali na wengine wengi.
Wapo ambao wanafaidika kweli na unyang’au huo na wapo wale wanaodhani kuwa wanafaidika lakini kumbe wakipatacho ni makombo tu.

Wapo wanaojiona kuwa wanakundi halali katika mfumo wa kinyang’au na wapo waliomo humo kwa kujipendekeza na kuifaragua. Wapo waliomo humo kwa kupenda na wapo waliojikuta humo bila ya wao kujijua. Wakiulizwa wanadai ni kulazimika kutokana na mazingira yaliyopo.

Hawa wote wamekuwa tayari kuuza uwezo na ujuzi wao kifikira na kikazi kutetea, kusadifu na kulinda mfumo unaohalalisha unyang’au katika jamii yetu. Wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa kudhani kuwa wanaenda na wakati ambao unashurutisha kila mmoja wao kuwa na “mahusiano mazuri” na manyang’au wa nchi yetu na wale kutoka nje ya mipaka yetu.

Kwao wao, ili kuwa na kile wakionacho ni mafanikio kimaisha, ni lazima wajitumikishe kwa manyng’au wa nchi hii ambao wengi wao wana nguvu za ushawishi katika dola la nchi yetu.

Moja ya sifa ya pamoja ya ndugu zangu hao walio amua kukuwadia unyang’au ni kutoacha kulalamika kuhusu masahibu ya unyang’au katika jamii lakini kwa upande mwingine wanageuka kuwa ndio wasadifu na walinzi mahiri wa mfumo sababishi.Hapo mbeleni tutawachambua wote kwa makundi yao, katika makala hii ningependa kuongelea makuwadi waliomo katika sekta ya uandishi wa habari.

Fani ya uandishi ya habari ni moja ya nguzo muhimu za kiutawala ambazo jamii yoyote inayothamini umuhimu wa mfumo wa demokrasia inapaswa kuipa kipaumbela na umuhimu wa hali ya juu. Bahati mbaya katika Tanzania yetu fani hii imegeuka kuwa adui mkubwa wa demokrasia ya kweli na hata kutishia hatima ya mchakato mzima wa kuanzisha na kuboresha misingi ya kidemokrasia katika jamii yetu.

Kwa miaka mingi sasa, wachunguzi wa mambo ya siasa na jamii wamekuwa wakijadili nafasi ya fani ya uandishi wa habari katika nchi yetu. Wengi wamekuwa wakihoji uwezo wa wahusika wa fani hii. Wengi wamekuwa wakijaribu kuchambua uwezo wa kitaaluma wa wengi wa waandishi wetu ambao wameonekana kana kwamba huwa wakifanya kazi hiyo bila ya kuwa na sifa za kitaalamu zinazohitajika katika fani hiyo.

Kwa kweli ukiangalia historia ya nchi yetu na zaidi sera za serikali yetu kuhusiana na suala zima la elimu na sio katika fani ya uandishi wa habari tu, utang’amua kuwa mfumo mbovu wakutojali elimu bora ni moja ya sababu kuu ya tatizo hilo. Hata hivyo ukosefu wa nia thabiti, utashi wa kutetea haki zao na hata uzalendo wa kweli, ndugu zangu waandishi wa habari ambao mimi huwaita wahandisi wa habari, wamegeuka kuwa makuwadi wa unyang’au unaoendelea kuligubika taifa letu.

Ndugu zangu hawa ama kwa kupenda au kulazimika kimazingira wamegeuka kuwa watetezi na waficha maovu ya manyang’au wa nje na wa ndani.

Ndugu zangu hawa wameamua kuwa wasadifu wa manyang’au wa nchi yetu na mfumo wao. Kazi yao kubwa imekuwa ni kuhalalisha na kuusimika mfumo wa kinyang’au uliojengeka katika nchi yetu katika fikira za watanzania.

Waandishi wetu wamekuwa tayari kuwapaka rangi za kuvutia baadhi ya manyang’au wa nchi hii, wakubwa wao kwa wadogo, na kuwavika sura ya utakatifu mbele ya watanzania walio wengi.

Wakati vyama vya upinzani vikiwa vimenyang’anywa nguvu za kutekeleza ipasavyo jukumu kukosoa na kuwaeleza wananchi ubaya ama uwongo wakubwa wa mfumo wetu wa kinyang’au, ndugu zangu waandishi wameamua kuwaacha watanzania katika msitu wa giza.

Wanahabari wetu wanapaswa kujua kuwa ushabiki wa ajabu wanao uonyesha kwa watawala wetu ambao miongoni mwao wamelewa utamaduni wa kuwadhulumu watanzania haki zao za msingi, unalipeleka taifa letu katika mustakabali wa kutisha.

Ni wazi kuwa kama ndugu zetu wanahabari hawatazinduka na kuanza kutekeleza kwa dhati wajibu wao kwa wananchi, kuna hatari ya wajanjawajanja miongoni mwetu kutulazimisha kurudi rasmi katika enzi za siasa za chama kimoja.

Wakati wa uchaguzi na mchakato mzima ndani ya vyama kuelekea katika uchaguzi huo, tulishuhudia jinsi kujitokeza wazi kwa hali hii ya ukuwadi miongoni mwa ndugu zangu.
Mwanzoni wengi wetu tulidhani kuwa hilo lilikuwa ni zoezi muda mfupi la wachache kujipenyeza katika timu ya ushindi na wengine kutimiza wajibu wao kutoka kwa wafadhili wao waliogeuka kuwa waajiri mbadala wao.

Lakini kwa hali inavyoendelea hivi sasa, inaelekea uozo uliopo ambao tayari umeshatanda katika nyanja zote za fani hii ya uandishi. Hii ni kuanzia wamililiki, waajiri, wahariri, waandishi wa kawaida na hata wasomaji umesababisha donda ndugu ambalo linaweza likashindwa kutibika.

Wapo waliofikia hata kubeza na kudhihaki juhudi za wachache waliokubali kuchukua jukumu la kuendeleza mapambano ya kutukomboa katika mfumo butu wa utawala wa chama kimoja. Tabia hii ya kuwakuwadia manyang’au kwa kutumia wino ni kuwageuza watanzania kuwa kama bendera inayofuata upepo ambayo haina uwezo wa kuhoji maamuzi yanayobariki unyang’au katika jamii yetu.

Kukuwadia unyang’au wa aina yoyote na mahala popote ni kujidanganya nafsi zetu. Sumu ya unyang’au kamwe haiachi kumdhuru kila mtu katika jamii husika na hata ile ya mbali. Hata kama madhara yake hayataonekana kwa mhusika binafsi wakati wa uhai wake, ni lazima itamsibu huko aendako kupitia kwa vizazi vyake.

Hivyo, ni wajibu wa ndugu zangu waandishi wa habari kuwa wa mwanzo kujinasua katika laana ya unyang’au kwa kuacha kuwakuwadia makuwadi wetu, wa ndani na nje na kuwaonya wengine wa aina yao katika sekta zengine.

No comments: