Tulimsaliti na tunaendelea kumsaliti Amina wetu….

I really thank u, from my heart, kuna vitu vingi ulinisaidia, kuna miongozo fulani, courage fulani na mambo mengine mengi, nimeona nikushukuru tu leo, asante na naappriciate as I said before, IT COMES FROM MY INSIDE, DEEPLY IN MY HEART, THANKS ONCE AGAIN, WISH U LUCKY, BE BLA$$ED. Amina chifupa mpakanjia.
Sender: +25577306944
Sent: 10:44:37
04/21/2007

Nimepigwa na butwaa, nimeishiwa na nguvu, sijui nifanyeje….najiuliza, hivi wapi ningelifanya zaidi na kwanini sikufanya mapema?

Hapo juu ni ujumbe alionitumia mtu ambaye karibia mwaka mmoja sasa nilimwita dada na yeye akaniita kaka. Ni Amina binti wa Chifupa. Huyu ni Amina niliye bahatika kumjua kwa kipindi cha karibia mwaka mmoja sasa. Katu sio Amina niliyekuwa nikijidai namjua miaka mitano kabla. Ni ujumbe ambao dada yangu amina alinitumia zaidi ya mara mbili katika usiku wa manane majira ya ughaibuni. Ni ujumbe ambao nilidharau kuujibu kwa siku mbili zaidi hadi Amina alipoamua kunipigia simu kunikumbusha kuhusu ujumbe huo. Sikujua kuwa ni ujumbe wa kwaheri ya milele.

Nakumbuka siku moja nikiwa mahala fulani naelekea nyumbani Tanzania nilimpigia simu rafiki yangu Zitto. Hii ilikuwa ni siku ambayo Rais Kikwete alihutubia Bunge letu kwa mara ya kwanza kama rais wa nne wa jamhuri yetu tukufu. Alitumia muda mwingi kunielezea ni jinsi gani alivyovutiwa na maudhui ya hotuba hiyo kitu ambacho kwa ninavyomjua rafiki yangu Zitto kilinishtua kiasi.

Katikati ya mazungumzo Zitto aliingiza suala la Amina. Akaniambia kuwa kwa muda mfupi aliofanya naye kazi anadhani kuwa Amina sio mtupu kama jamii inavyomtafsiri. Mimi nikamshauri kuwa jaribu kuwa naye karibu kumjua zaidi na kama kuna sehemu za kumsaidia basi asisite kufanya hilo kwa manufaa ya nchi yetu.

Mimi binafsi nilikuja kufunguliwa macho kutambua hazina iliyojificha ndani ya Amina siku alipopanda juu ya madhabahu ya kielemu katika ukumbi wa Nkurumah pale Chuo kikuu cha Dar Es Salaam. Hii ilikuwa ni miezi ya mwanzo ya mwaka 2006.

Mbele yangu nilishuhudia Amina tofauti kabisa na yule ambaye jamii ikiongozwa na wana udaku walivyokuwa wakimtafsiri. Mbele yangu nilimuona kijana mdogo aliyejawa na ushujaa, upendo wa dhati kwa nchi yake na zaidi mwenye kipaji cha hali ya juu cha siasa. Mbele yangu nilimwona kijana ambaye sio tu amejawa na uthubutu wa kujaribu lakini pia aliyekuwa na ndoto ya kufanikisha mambo makubwa katika maisha yake.
Mara baada ya Amina na wakina dada wengine mashujaa waliokuwepo pale kumaliza kutoa ushuhuda wao kuhusu nafasi ya mwanamke katika siasa za nchi yetu, nililazimika kusimama ili nami nitoe ushuhuda wangu.

Nilianza kwa kumuomba radhi dada Amina. Bila ya kusita nilimtaka radhi kutokana na mimi kuwa mmoja wa wale watanzania waliokubali kuamini kashfa, uzandiki, na zaidi unyanyapaa ambao baadhi wanajamii walikuwa wakimfanyia.Baada ya hilo nikamuahidi urafiki naye ili tuweze kubadilishana mawazo na ujuzi ambao niliamini kwa upande wake ungeweza kumwongezea pale alipopungukiwa na mimi kuongeza pale nilopopungukiwa na vilevile kutimiza lengo langu la kusaidia vijana wenzangu haswa kina dada kama Amina kufanikiwa ndoto zao katika ushiriki wa kujenga taifa letu kwa pamoja.

Baada ya muda mfupi wa kujuana na zaidi kufaidika na tabia ya ucheshi na upendo mkubwa aliokuwa nao Amina, nikajikuta naongeza rafiki mwingine wa karibu katika maisha yangu ambaye kwa kweli alifikia kuwa mdogo wangu mpendwa.

Mdogo wangu ambaye leo nasikitika kuwa sikufanya vya kutosha kwake yeye kunishukuru kama alivyofanya katika ujumbe huo hapo juu.

Mdogo wangu ambaye namshukuru mwenyezi mungu kwa kunipa nafasi ya kumtaka radhi kutokana na makosa niliyofanya hapo mwanzoni ya kumtafsiri vibaya.

Mdogo ambaye amenifundisha umuhimu wa kutowatafsiri na kuwahukumu watu ambao tunadhani tunawajua kumbe ukweli ni kuwa hatuwajui.

Mdogo ambaye alinifundisha kumpokea mtu kama alivyo na sio kama tunavyotaka sisi awe.
Mdogo ambaye kwa muda mfupi sana amenifunza mengi kuhusu dunia hii kuzidi hata niliyojifunza katika zaidi ya miaka ishirini niliyokaa darasani.

Muda uliruhusu machache kushauriana. Lakini katika muda huo kiduchu Amina alitokea kuwa mwalimu na mwanafunzi mzuri kwangu na mwenye kuthamini mawazo yangu kama ambavyo alivyokuwa akithamini na kutetea mawazo yake kwa uthabiti mkubwa. Amina hakuwa mtu wa kuburuzwa na wala kutishwa.

Ushahidi unaonyesha kuwa kadiri alivyokuwa akitishwa ndivyo alizidi kuwa na ushujaa wa kusimama na kuongea yale ambayo aliamini kuwa yanapaswa kusemwa bila ya kujali kama wale aliokuwa akiwasemea wanamshukuru ama kumdhihaki.

Siku moja nilikuwa nikipata nasaha za mzee mmoja ambaye alimjua mzazi wangu wakati akiwa hai. Mwishoni mwa mazungumzo aliniasa kitu kimoja. Mzee huyu aliniasa kuwa katika dunia yetu Mawalii huja kwa sura nyingi na mara nyingi huja katika sura ambayo wengi hawakutegemea na hivyo kushindwa kutambua bahati waliyoletewa na mwenyezi mungu hadi pale atakapotoweka. Waseme watakayosema lakini kwangu nathubutu kuamini kuwa Amina alikuwa ni walii aliyeletwa duniani kupima ubinadamu wetu na kutuelimisha mengi.Walii aliyekuja na ujumbe wa kuthubutu kupambana na moudhi yaliyoigubika jamii yetu bila ya woga.

Katika maisha yake tangia akiwa kigori hadi alipokabidhiwa majukumu makubwa ya kutetea maslahi ya vijana wenzake katika chama tawala, Amina amekumbwa na mengi. Kama ni mitihani basi ni wazi Amina alipata mitihani mikubwa sana. Mtihani mmojawapo ulikuwa ni ule wa wanajamii aliokuwa akiwapenda na kujitolea muhanga kuwatetea kujenga mazoea ya kumdharau, kumdhihaki, kumkejeli, kumbeza na zaidi kutomwamini katika katika uthabiti wake wa kutetea maslahi yao.

Wengi walikuwa wakimwona Amina kama mtu aliyekuwa amelewa na mafanikio. Wapo waliodhani kuwa Amina alikuwa akifurahia sana aina maisha aliyokuwa anakumbana nayo kila kukicha.

Masikini hawakujua kuwa ndani ya lile tabasamu murua lilojaa bashasha kulikuwa na mateso makubwa akilini na rohoni. Inasikitisha kuwa hata wale aliokuwa akiwaona kama kimbilio lake ndio kabisa hawakuweza kumpa nafasi ya kupunguza yaliyo rohoni.
Naamini kuwa kamwe sina haki ya kuwasema wanafamilia wake lakini nathubutu kuwasema wanajamii wengine wote. Hawa wakiwemo wanasiasa wenzake haswa wale wenziwe katika chama chake, waandishi wa habari, wanaharakati wa kijamii na hata wenzangu na mimi wasio na chao ambao Amina daima alikuwa akipenda kujinasabisha nao.

Kwa miaka mingi hawa wote nikiwemo na mimi tumekuwa tukimsaliti Amina kila kukicha. Wengi wetu tumekuwa tukimdharau, kumsimanga na hata kutengeneza na kushabikia maneno ya uzandiki ambayo yalikuwa yakitafuna furaha ya Amina kila uchao.

Wakati aliposimama kuwaongelea mamilioni ya watoto wa shule wanaotembea maili kadhaa bila ya viatu na wala uhakika wa kutia kitu tumboni siku nzima wawapo shuleni na hata wanaporudi nyumbani, tulimdhahaki na kumwambia anaongelea upuuzi. Eti amezidi umediocre. Aliposimama kuongelea maswahibu yanayowakuta watoto wa shule haswa katika wilaya za jiji la Dar es Salaam tulimwambia anataka kujijenga ili apate ubunge katika moja ya jimbo la jiji hilo. Waliodai kuwa ni jimbo lao hawakuacha kumtumia maonyo makalimakali.

Hata alipothubutu kusimama kuongelea manyang’au wanaojineemesha kwa kuwabebesha na kuwauzia maelfu wa vijana wenzetu sumu inayowamaliza kila siku, yaani madawa ya kulevya, tukamdhihaki kuwa ni mtoto mdogo hajui afanyalo. Wapo waliofikia kudai kuwa amefanya hivyo kumkomoa mumewe.

Ukweli ni kuwa hakuna aliyetaka kuamini kuwa ndani ya sura ile iliyojaa bashasha kuna uchungu wa dhati juu ya maslahi ya kijana mtanzania wa kawaida anayeathirika na hayo. Kijana wa kawaida ambaye tofauti na waheshimiwa wengine wengi katu Amina hakuacha kujinasabisha nao.

Mara dada yetu alipozimika kila mtu akaibuka kutafuta mchawi. Mara hili mara lile.
Kama kawaida ya wanadamu hakuna mwenye ubavu wa kuthubutu kujiangalia yeye binafsi ni vipi amechangia Dada yetu Amina kutuacha katika mazingira ambayo amefariki. Hakuna anayetka kung’amua ukweli kuwa wote kwa pamoja tulimsaliti Amina wetu. Wakati akituhitaji sisi tulikuwa tukimbeza na kumdharau. Wakati akihitaji mapendo yetu sisi tulimkejeli na kumzodoa.

Yote hayo aliyoyakusanya moyoni miaka nenda miaka rudi yakamalizwa kwa pigo la mwisho. Pigo ambalo lilimpelekea kuamini kuwa hata yule ambaye wazazi wake walitoa idhini ya kuwa mlinzi wa roho yake na mwili wake hapa duniani naye hakuweza kuwa naye pale alipokuwa akihitaji zaidi mapendao na uelewa zaidi. Na zaidi alipotaka kuyatoa yaliyokuwa yakimmaliza rohoni wapo waliothamini maslahi yao zaidi ya roho yake. Wote kwa pamoja tukaendela kumsaliti Amina wetu.

Inasikitisha zaidi kuona kuwa hata katika kifo chake tunaendelea kumsaliti Amina. Badala ya kujiuliza ni vipi tutaendeleza moto aliouwasha kuokoa vijana wenzetu na jamii yetu kwa ujumla, tunaendela kushabikia uzandiki, unafiki na udaku dhidi ya dada yetu Amina. Jamani tusitafute mchawi. Wengine walimalizia tu lakini sote tulimsaliti Amina wetu.

Kwa kweli natamani wote tungelimjua Amina wa kweli. Yule Amina niliyebahatika kumjua karibia mwaka mmoja tu kabla hajatuaga, Amina mwenye ucheshi wa haja. Amina mwenye nidhamu hata kwa wale aliokuwa akijua wanamdhihaki na kumdharau. Amina mwenye upendo wa kweli kwa watu wote, Amina asiyeogopa kusema na kufanya yale yote aliyoamini ni ya haki na yanapaswa kusemwa ama kutendwa. Amina mwenye uthubutu ambao wengi wetu tumeukosa. Amina nyota tuliyoizima hata kabla haijang'ara.

Mwenzenu natamani ningelifanya zaidi na zaidi kuonyesha urafiki wa kweli kwako dada yangu mpendwa Amina. Siamini kuwa eti nami sikuweza kuwa karibu nawe wakati ukihitaji zaidi urafiki wangu hata kwa uchanga wake. Amina dada yangu umetutoka lakini namshukuru mungu uliniaga kwa maneno ya upendo ingawa akati ule sikujua hilo.

Ni Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema tu ndiye ajuaye kuondoka kwako kuna funzo gani kwetu. Watasema yote lakini jua kuwa tupo tuliobahatika kukuamini na kukuthamini kwa dhati hata kama muumba hakutupa muda mrefu wa kufanya mengi. Nasema tumebahatika kwani ni nadra kwa dunia yetu hii kupata bahati ya kuitwa rafiki na walii kama wewe. Cheche ulizowasha kamwe hazitaenda bure. Bendera tutaipeperusha hadi mwisho sio kwa maneno bali kwa vitendo.

Msalimie kaka Chachage. Mwambie akusomee hadithi ya makuwadi wa soko huria. Mwambie ndoto yake ya ukombozi wa mlalahoi wa Tanzania yetu baada ya miaka kadhaa ya unyang’au wa soko huria inaelekea kutotimizika hivi karibuni. Mwambie kuwa yule mswahili mlalahai mwenzio Jakaya anahitaji makarama zaidi kutoka kwake huko alipo ili aweze kutimiza yale matumaini aliyokuwa nayo kwake kabla hajatuaga na kutuacha wapweke pale mlimani.

Namalizia kwa kunukuu ujumbe wa taarifa ya kifo chako kutoka kwa rafiki yetu kipenzi Zitto: AMINA AMETUTOKA….

No comments: