CCM iende, Tanzania ibaki…Na Ilyas, O.S @ July 2008

Tangia serikali ya CCM kuamua kwa shingo upande kuanzisha mfumo wa siasa za vyama vingi hapa nchini kumekuwa na taharuki kubwa ndani ya chama hiki katika kuchagua kati ya maslahi ya nchi na maslahi ya chama. Hali hii imejengwa kutokana na sababu mbalimbali ndani na nje ya chama hicho. Moja ya sababu kuu ni kubadilika kwa falsafa na mantiki ya kisiasa ya chama hicho kutoka katika kumuendeleza mtanzania hadi
kulinda na kuendeleza maslahi na nafasi ya tabaka tawala.

Ni wazi kuwa CCM ililazimika kukubali mfumo wa vyama vingi sio kwa sababu waliamini ni njia muafaka ya kulinda amani na umoja wa kitaifa. Ni wazi kuwa waiamua kufanya hivyo baada ya kung’amua kuwa bila ya kufanya hivyo wakati wakati ule basi mbeleni wangelazimika kufanya hivyo kwa matakwa na shurutisho za umma. Hali ambayo ni wazi isingewapa nafasi waliyonayo sasa ambapo bado wameweza kuhodhi nguvu za kuzuia mabadiliko ya kweli ambayo hayahakikishi usalama wa nafasi ya tabaka tawala.

Hali hii ya kubadilika kwa mantiki ya kisiasa ya CCM kutoka kujenga na kuendeleza taifa hadi kulinda nafasi ya tabaka tawala naweza kusema ndio mzizi mkuu wa matatizo lukuki tunayokumbana nayo hivi sasa. CCM wamekuwa wakijali zaidi kulinda mfumo wa kisiasa na kiuchumi tulionao ili kuepusha uwezekano wa kutokea mabadiliko ambayo yatadhoofisha nafasi ya kiutawala hata kama uhalali wao utatetereka.

Matatizo hayo ni pamoja na yale mapya ya ufisadi, uongozi mbovu, ubaguzi wa kidini, kikabila, kimapato, kirangi na hata kimaeneo na mengine ya tangia zamani kama lile la la hali na hatma ya muungano wetu. Hivi sasa wapo wanaochukulia haya kama ndio matatizo haswa na kuamua kutumia muda mwingi kufikiria, kuongea na hata kulalama mfululizo kama vile kuna uwezekano wa kuyashinda majanga haya bila ya kuyafikiria kwa mapana yake. Wapo wafanyao kosa hili bila ya kujua lakini wapo ambao wanajua wazi kuwa hali ya kufikiri hivyo ni tatizo kwani kunawezesha kuendelea kwa mfumo tulionao sasa ambao wao ni wafaidika.

Suala la ufisadi ndilo limekuwa agenda kuu ya watanzania hivi sasa kiasi cha kufikia mahala ambapo ndio imekuwa kama taswira ya CCM miongoni mwa watanzania walio wengi, wana CCM na wasio wanaCCM. Bahati mbaya agenda hii ya UFISADI badala ya kutufanya watanzania tufikirie zaidi na zaidi inaelekea kuwa imeanza kutudumaza kifikira. Agenda ya UFISADI imekuwa kama kiongeza mwendo muhimu cha kufisadisha mustakabali wa Tanzania yetu badala ya kulitetea na kulilinda taifa letu.

Wapo wengi wanaoshangaa ni jinsi gani CCM imeshindwa kulishughulikia suala hili katika njia ambayo sio tu ingeweza kuliokoa taifa letu lakini pia kuokoa nafasi ya chama hicho katika utawala wa nchi. Wengi wanaamini kuwa CCM chini ya uongozi wa Jakaya Kikwete kwa kutumia nafasi yake kama mwenyekiti wake lakini zaidi rais wa dola la Tanzania, inaweza kabisa kuchukua hatua madhubuti kuondokana na janga hili.

Hata hivyo ni wazi kuwa wanaoamini hilo wanashindwa kutambua jambo moja muhimu. Kwamba Chama Cha Mapinduzi hakijabadili tu falsafa yake kutoka katika ujamaa na kujitegemea kuelekea kusikojulikana, lakini pia kimebadili hata mantiki ya kisiasa kutoka kujenga na kuendeleza taifa hadi sasa kuwa ni kulinda nafasi ya tabaka tawala. Tabaka linalojumuisha walio wanachama na wasio wanachama wa chama hiki. CCM ya sasa sio ile ya zamani inayoamini hakuna maisha yenye umuhimu kama Tanzania. CCM ya sasa inaamini kuwa maslahi ya tabaka tawala ambalo limehodhiwa na kuneemeshwa na UFISADI yana umuhimu zaidi ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Ni kwa mantiki hii ndio sasa tunaona sio tu tumekuwa na ongwa la uongozi linalosababisha kushindwa kwa kuchukuliwa hatua dhidi ya wale wanaosadikiwa kuwa ni MAFISADI lakini pia sasa kuhatarisha hata muungano wetu ambao wapo walio apa kiapo cha kuulinda kwa hali yoyote ile.

Hivi karibuni kumekuwa na watu wakisema waziwazi na wengine ndani ya vikao vikuu vya CCM kuwa na tuachane na muungano. Wengi wao ni wale ambao agenda ya ufisadi imewakaba kooni hivyo wangelipenda kutumia kila njia kuondoa fokasi ya watanzania kutoka huko. Kwao wao ni bora muungano uende lakini madhambi yao yasahaulike, kwao wa ni bora Tanzania iende na CCM ibaki. Kwao wao Tanzania si chochote si lolote na CCM ndio kila kitu.

Inasikitisha na inatisha kuona kuwa hata wale walioapa mbele ya mungu na watanzania kuwa wataulinda muungano kwa nguvu zote ndio wanafikia kusema maneno kama acha muungano uende. Kwa maana nyingine wanasema acha Tanzania iende kwani ukikubali kuvunjika kwa muungano hakuna Tanzania. Inawezekana kutokana na mfumo wa muungano tulionao wapo wanaodhani kuwa tukirudisha Tanganyika bado tutabaki na Tanzania.

Inasikitisha sana kuwa watanzania tumefikishwa mahala kama hapa ambapo tupo tayari kuvunja nchi yetu ili mradi maslahi ya wachache yaendelee kulindwa. Inatisha mno kuona kuwa wafanyao haya ni wale ambao walibahatika kulelewa kwa misingi madhubuti ya muungano wetu. Yaani wale wa kizazi ambacho Mwalimu Nyerere alijitahidi kwa nguvu zake zote kukijenga katika fikira za utanzania zaidi ya yote. Hawa ndio wamekuwa wa kwanza kuusaliti muungano wetu.

Cha ajabu ni kuwa haohao wanaodiriki kusema wacha muungano uvunjike ndio kwa miaka wamekuwa mstari wa mbele kuwaita wale wanaojaribu kushauri njia muafaka za kushughulikia changamoto za muungano kuwa ni maadui wa muungano.

Katika hali kama hii ni wazi watanzania tunapaswa kujiuliza masuala kadhaa magumu yatakayotapatia majibu muhimu.

Hivi kama hawa wanafanya hivi itakuwaje kizazi chetu cha vijana wa sasa ambacho kimenyimwa malezi ya kitanzania na kukuzwa katika fikira za ubinafsi na ufisadi kitafanyaje ?

Jee, kukubali usaliti huu unaoendelea sasa wa kuthamini maslahi ya CCM zaidi ya TANZANIA yetu ndio kutatuwezesha kutatua matatizo na changamoto tulizonazo sasa?

Hivi ni kipi muhimu kati ya CCM na maslahi ya tabaka tawala ama Tanzania na maslahi ya watanzania ?

Wakati umefika wa watanzania kuamka na kuwaeleza wazi na kwa nguvu zote ndugu zetu hawa kuwa ni bora CCM iende lakini Tanzania ibaki. Uoga wao wa kuthubutu kuchukua maamuzi magumu ambayo yaweza kuhatarisha usalama wa maslahi yao lakini ukalinda na kundeleza ujenzi wa taifa letu hauna uhalali wa kuifikisha Tanzania yetu tulipoifikisha.

Wakati umefika kwa viongozi wetu ambao wangependa tuendelee kuwatofautisha wao na mafisadi mashuhuri tunaowanyoshea vidole sasa, kuthubutu kusimama kidete na kusema, ni bora CCM iende lakini Tanzania ibaki.

No comments: