TANZANIA BORA HAITAJENGWA KWA STAILI YA BANDIKABANDUA

Ilyas, O.S @ August 2008

Katika miaka ya hivi karibuni nchi yetu imekuwa ikipita katika mitihani migumu inayotishia hatima yake kama taifa na hatima ya watanzania kwa ujumla. Mitihani ambayo kwa hali moja inatusaidia kupevuka kama taifa na kwa hali nyingine inatishia mustakabali wetu kama taifa.

Hali hii imefuata baada ya miaka kadhaa ya mtindo wa bandika bandua katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikumba taifa letu. Mtindo ambao kwa mantiki ya hali ilivyo sasa na dalili zinazonyesha huko tuendako, inatubidi kuachana nao haraka kabla hatujachelewa zaidi.

Changamoto tulizonazo ni lukuki ambazo ni wazi uzito wake utatuelemea. Hizi ni pamoja na tatizo la ufisadi, kuporomoka kwa maadili ya uongozi, kukua kwa hisia na kuongezeka kwa matendo ya kibaguzi miongoni mwetu, kustawi kwa matumizi ya siasa chafu, kupanuka kwa tofauti za kipato na kuongozeka kwa dalili za kuvunjika kwa muungano wetu. Kwa ujumla Tanzania ya sasa ina kila dalili mbaya ambayo hutokea katika jamii na matifa mbalimbali duniani zikiashiria kuvunjika kwa jamii hiyo ama tifa hilo.

Hata hivyo ni bahati mbaya kuwa mabadiliko yanayoendelea yamekuwa ni yale ya mtindo wa bandikabandua ambao unalenga zaidi katika kuendeleza uhalali wa tabaka tawala ambalo limejihodhisha nguvu zote za mabadiliko ya kisasa na kiuchumi badala ya kushughulikia mizizi ya changamoto hizo. Tumegubikwa na ujanjaujanja wa kushughulikia matokeo ya matatizo badala kuwa na uthubutu wa kushughulikia sababu ama mizizi ya matatizo hayo.

Hali ya ufisadi unaokomaa, kuporomoka kwa maadili ya uongozi, kukua kwa hisia na kuongezeka kwa matendo ya kibaguzi miongoni mwetu, kustawi kwa matumizi ya siasa chafu, kupanuka kwa tofauti za kipato na kuongozeka kwa dalili za kuvunjika kwa muungano wetu hayo yote ni matokeo ya matatizo na sio tatizo lenyewe.

Viongozi wetu ni lazima wakubali kuwa wakati umefika kuacha kupendelea hatua za kufunika kombe mwanawazimu apite. Viongozi wetu wanapaswa kukubali kuwa suluhu la matatizo au changamoto tunazokumbana nazo ni kuzungumzia, kukubaliana na kutekeleza makubaliano ya jinsi gani ya kuikoa Tanzania yetu na jinsi gani ya kuijenga kwa pamoja Tanzania iliyo bora kwa wote.

Ni wazi kuwa wakati umefika kwa viongozi wetu kuonyesha njia kwa watanzania kukaa kwa pamoja kujadili na kukubaliana njia mwafaka na ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotukabili. Na viongozi wetu wakishindwa kupata uthubutu wa kuongoza katika hili basi wajue wazi kuwa si kitambo sana watanzania watajitwalia mikononi mwao jukumu hilo.

Yapo mengi ambayo watanzania tunapaswa kuwa tayari kuyaongea na kukubaliana kwa ukweli na uwazi bila ya kuogopa.

Watanzania tunahitaji kupata nafasi ya kuongelea masuala kama aina ya mfumo uchumi tupaswao kufuata, Mfumo wa kisiasa, mfumo wa muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar, Muungano wa Afrika Mashariki, sifa na maadili ya viongozi, utawala na sheria, haki na wajibu wa kijamii na jinsi gani tunaweza kuwa na mfumo wa uwezeshaji wa makundi maalumu ya kijamii bila ya kusababisha kutokuaminiana miongoni mwetu.

Tunapaswa kukaa pamoja na kuongelea kuhusu mfumo wa elimu, mahusiano kati ya vyama vya kisiasa na dola, mfumo wa uchaguzi na uwakilishi, nafasi ya vyama vya kiraia katika jamii yetu na suala zima la mila na tamaduni za kitaifa nayo ni muhimu yaka angaliwa upya kwa pamoja. Vilevile masuala ya uraia na siasa, suala heshima na maelewano ya kijamii na nafasi za viongozi wa kijamii katika uongozi wa nchi yetu.

Ni wazi kuwa hali ilivyo sasa ni ushahidi tosha kuwa wakati umefika sasa wa kuamua ni upi kati ya mfumo wa kibepari ama kijamaa tupaswao kuufuata na kwa faida ipi na njia zipi. Ni wazi kuwa bila ya uoga wowote tunapaswa kuliongelea suala la muungano ambalo kwa miaka sasa limekuwa kama donda liogopwalo kutibiwa ama hata kuguswa. Tunapaswa kulijadili sasa kuliko kuchelewa zaidi hadi kufika mahala chembe ya busara na uongozi thabiti iliyosalia, ikakosekana kabisa na kuacha chuki na dharau kuchukua mkondo kama dalili zinavyo onyesha.

Ni wazi kuwa tunapaswa kujadili suala la maadili katika jamii yetu kwa mapana yake na si hili la muono wa karibu wa siasa na biashara. Suala la maadili ni suala muhimu pia si tu kwa viongozi ambao wanapaswa kuwa kioo cha jamii lakini pia wananchi kwa ujumla. Hivi sasa jamii yetu inageuka jamii ya kichokoraa ambapo kila mtu akishindana na mwenzie kuvunja sheria za nchi na jamii kwa ujumla. Maadili sio suala la watoto na vijana wetu tu kama tulivyozoe. Ni suala la wazee, wazazi, viongozi wakuu na wadogo, matajiri na masikini, wenyeji na wageni, na watawala na watawaliwa.

Mfumo wa kisiasa nao unahitaji kufumwa upya ili kuwezesha demokrasia ya kweli kuweza kukomaa na kusaidia kujenga Tanzania yenye neema. Kamwe hili halitwezekana kama tutaendela na stili ya bandikabandua ambayo inalenga kulinda maslahi na nafsai za kundi fulani tu bila ya kujali mapungufu yanayotokana na staili hiyo ambayo yanamsabibishia mtanzania kuendelea kuishi katika maisha ya unyonge yasiyo na tija ya kimaendeleo.

Uamuzi wa kufanya mjadala huu wa kisiasa unapaswa kufikiwa sasa ili kuweza kutumia nafasi hii tuliyojikuta tunayo bila ya kuchelewa. Ni muhimu kufanikisha mjadala huo mapema ili kupelekea kutungwa kwa katiba mpya kabla ya mwaka 2010 itakayowezesha kuwa na uchaguzi ambao umefanyika chini ya mfumo mpya ulioshirikisha na kukubalika na watanzania wote. Tukawa na katiba ambayo itapata uhalali wa kila mtanzania aliye na haki ya kupiga kura.

Umuhimu wa kufanya hivyo unatokana na kuwa watanzania sasa zaidi ya wakati mwengine wowote wana shauku kubwa ya kuijenga nchi yao kwa uthabiti zaidi kama ari mpya inavyosomeka na wengi

Lakini vilevile ni muhimu kuamua sasa kwani siasa ni fani inayosifika kwa kubadili mwenendo wakati wowote ule. Kama uamuzi huo hautachukuliwa sasa na kutumia mazingira ya kisiasa na kijamii tuliyonayo sasa basi inaweza ikatokea hapo baadae hali ikawa mbaya zaidi na kulazimisha mabadiliko hayo yatokee baada ya kupitia njia mbadala ambayo itakuwa janga kubwa kwa taifa letu.

Tusingoje tufikie hali ya siasa za magomvi na chuki kama zilizowafikisha ndugu zetu wa Burundi, Sudan, Zaire (Kongo DRC), Siera Leone, Liberia walipofikia ndio tufikirie hilo. Na wala tusisubiri hali ya kutatanisha iliyojengwa katika upande mmoja wa muungano wetu yaani visiwa vya Unguja na Pemba ndipo tufikirie kufanya hilo.

Badala ya kuendelea kupoteza muda, fedha, na hata maisha ya watanzania, viongozi wetu wanaotaka kukumbukwa kwa mapendo na sio chuki dhidi yao na vizazi vyao hapo baadae, wanapaswa kuwa na uthubutu wa kushinikiza na kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhus hatima ya nchi yetu sasa bila ya kuechelewa zaidi.

Mjadala bora na wa kujenga, daima hufanyika pale wahusika wanapokuwa katika hali ya mapendo, maelewano na heshima miongoni mwao.

Wapo wanaodhani kuwa kuanzisha mjadala kama huu ni kufungulia matatizo ambayo yanaweza kushindikana kudhibitiwa.

Wapo wanaogopa kufungulia mabadiliko kwa kuwa wanaamini hali iliyopo sasa ni hali ya kupita tu na wataweza kubadili mwelekeo na ukawa unaoridhisha kwa upande wao.
Hawa wote kwa kweli wamesahau kusoma nyakati. Mwenendo uliopo sasa hautabadilika bila ya kuwa tayari kuchukua uamuzi thabiti wa kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu masuala yote muhimu yanayotusibu.

Badala ya leo kuwa na mjadala wa kuwa na KADHI, kesho mjadala wa kuhamia Dodoma, kesho kushokutwa mjadala wa URAIA, mtondogoo mjadala wa Uongozi na Biashara, ni muhimu tukawa makini zaidi na kuanzisha mjadala wa kitaifa wa pamoja ambako haya yote na mengineyo yatajadiliwa kwa mpangilio madhumubuti na utakaopunguza mzigo kwa walipa kodi wa nchi yetu.

Ni mjadala wa kitaifa tu na sio maamuzi ya bandikabandua yanayolenga kulinda mfumo fisadi tulionao ndio yataweza kujenga Tanzania iliyo na neema kwa wote kama kauli mbiu ya chama tawala CCM.

Ni mjadala wa pamoja na sio ule wa wakubwa wachache tu utawezesha kuongeza utashi wa watanzania kulitumikia taifa lao kwa nguvu na uminifu zaidi. Ni utashi binafsi wa watanzania ndio utakaorudisha nidhamu binafsi na uzalendo miongoni mwa watanzania. Na bila ya kurudisha haya tutaendelea longolongo hadi kukuche lakini Tanzania bora kamwe haitawezekana.

Tanzania bora kwa wote itajengwa kwa kushirikisha watanzania wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kamwe haitajengwa kwa mtindo wa mabadiliko ya bandikabandua kama tunaoendeleza sasa.

No comments: