Kama kuna mhimili pekee wa utaifa wetu ambao hadi sasa umeweza kuhimili mikiki mikiki lukuki yenye nia ya kuubomoa na kuufutilia mbali katika historia ya nchi yetu basi ni jina la Mwalimu Nyerere.
Miaka kumi baada ya Mwalimu kuondoka duniani bado jina la Mwalimu limekuwa kama nguzo kuu ambayo watanzania kwa pamoja wamekuwa wakiendelea kutegemea kama turufu pekee ya kulinda, kutetea na zaidi kuhalalisha maoni, matakwa, mitizamo na hata matumaini yao. Jina la Mwalimu Nyerere limeendelea kuwa turufu pekee ya watu mbalimbali katika ulingo wa kisiasa, kiuchumi na hata kijamii kuhalalisha maoni, mitizamo na hata maslahi yao. Jina la Mwalimu Nyerere limeendelea kuwa lulu ya wengi hata kufikia wengine kudai kuwa na hati miliki ya matumizi yake na kuwanyima wengine haki hiyo.
Wakati nchi yetu ilipokuwa ikilazimika kufuata mkumbo wa kuanzisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, Mwalimu Nyerere aliweza kujitokeza kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko hayo. Mengi yemesemwa kuhusu nini alisema na alikuwa na maana gani. Mojawapo ni lile la kuwa upinzani imara utatoka ndani ya CCM.
Imekuwa ni kawaida siku hizi kusikia watanzania wengi wakilalama, kusema na hata kupayuka kuwa ili nchi yetu iwe na demokrasia imara basi ni sharti CCM imeguke na kutimiza kile wanachodai utabiri wa Mwalimu Nyerere.
Mwanzoni haya yalikuwa yakizungumzwa sana miongoni mwa wachache waliopo katika vyama vya upinzani. Baadae hali hii ikaanza kujitokeza zaidi miongoni mwa watanzania waliochoshwa na “maovu” ya CCM lakini hawako tayari kujiunga ama kuunga mkono na vyama vya upinzani vilivyopo wakiamini kuwa huo sio upinzani wa kuaminika na utakaoweza kutoa mbadala makini wautakao wao.
Katika miaka ya hivi karibuni kinachoitwa utabiri wa Mwalimu Nyerere umekuwa zaidi ukizungumziwa sana na wana CCM wakiwemo viongozi waandamizi, viongozi wastaafu na hata wanachama wa kawaida.
Kufuatia mparaganyiko mkubwa uliojitokeza kuanzia mkutano wa halmashauri kuu ya CCM wa mwaka 2002 na kuhalalishwa rasmi wakati wa uchaguzi wa wagombea wa CCM katika uchaguzi wa mwaka 2005 ambao matunda yake yakaanza kujitokeza rasmi na kwa uwazi zaidi ndani ya bunge hili la sasa na kusambaa pande zote za nchi. Kile kinachoitwa “Utabiri wa Mwalimu” kimegeuzwa kuwa mtaji mkubwa wa kisiasa miongoni mwa wanaCCM na hata katika vyama vingine.
Kutokana na kugubikwa na utamaduni wa siasa chafu zenye kuendekeza rushwa na ufisadi, ubinafsi, migongano ya kimaslahi, chuki, uadui, majungu, kutokuaminiana na kukosa dira ndani ya chama hicho, watanzania wengi wamejikuta wakilazimika kukaa mkao wa kula kusubiri kutimia kwa utabiri wa Mwalimu wa kuwa upinzani imara utatokana na kumeguka kwa CCM.
Kwao wao ni kuwa matatizo yanayolikumba taifa letu yanatokana na sababu mbili. Moja ni migogoro ya ndani ya chama ambayo kwa maoni yao inasababishwa na baadhi ya wanachama wenye hulka ya kuthamini rushwa na ufisadi zaidi ya “maslahi ya chama na taifa” na Pili ni kukosekana kwa upinzani imara utakaoweza kukishurutisha chama cha CCM kurudi katika mstari ulionyooka na kukifanya kuwa imara kama inavyotakiwa.
Ni wazi kuwa wakati Mwalimu akitoa hicho tunachokiita utabiri wa kumeguka kwa CCM na kupatikana kwa upinzani imara nchini, alikuwa akifikiria ni jinsi gani chama chake alichokipenda na kukitumikia kwa uaminifu mkubwa kinaweza kurudi katika mstaari mnyoofu.
Hata hivyo wengi wetu tunashindwa kuangalia mazingira na mantiki halisi yaliyompelekea Mwalimu kuamini kuwa upinzani imara utatoka ndani ya CCM.
Mwalimu aliamini kuwa kutokana na misingi imara aliyoiwekeza katika CCM ni wazi kuwa kitaendelea kuwa chama imara kama kitapata upinzani imara utakaowalazimu wanaCCM kujiangalia na kujisafisha ili kuendelea kutawala. Kwa hali iliyokuwepo wakati ule Mwalimu alipotoa matamshi yale ni wazi aliona mkanganyiko wa kimisingi na kiitikadi ambao ulikuwa ukichipua ndani ya chama hicho. Ni wazi kuwa Mwalimu aliposema upinzani imara alimananisha kuwa upinzani ambao utakuwa unatofautiana na CCM kimisingi, kisera na kiitikadi na sio magomvi na ushindani wa nani anafaidika zaidi na ufisadi na nani anazuiliwa kufaidika zaidi na ufisadi huo kama hali ilivyo sasa.
Mimi naamini kuwa Mwalimu hakuwa mzembe wa kimawazo wa kuamini kuwa upinzani imara utatoka CCM bila ya kutambua sehemu ya tofauti za kimisingi na kiitikadi ambazo zingelipelekea baadhi ya wanaCCM kujitoa na kuanzisha chama chao.
Mwalimu aliongelea mgawanyiko wa CCM kwa mantiki ya kuwa kwa kuwa kulikuwa na baadhi ya wanaCCM wakiwemo viongozi wakuu wakiamini kuwa misingi, sera na itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea imepitwa na wakati na wangependa kuona CCM na Tanzania zinafuata misingi ya ubepari. Ni wazi hali hiyo ingepelekea chama hicho kugawanyika katika misingi hiyo na hivyo kuleta upinzani imara wenye kufuata tofauti za kimisingi, kisera na kiitikadi.
Tukumbuke kuwa ni wakati huohuo ndipo Mwalimu aliwahi kutamka kuwa kati ya vyama vilivyokuwepo aliamini kuwa CHADEMA ambacho kilikuwa kikijinasabisha na sera na itikadi za KIBEPARI kwa waziwazi bila ya kificho kama ilivyo kwa CCM ndicho kitaweza kuwa imara hapo mbeleni.
Ni vizuri tukajiuliza, Mwalimu akiwa kama mjamaa aliyekubuhu ni kwa nini hakusema kuwa NCCR ingeliweza kuwa chama makini wakati wao walikuwa wakijinasabisha na ujamaa wa mrengo wa kati lakini akasema ni CHADEMA. Iweje Mwalimu adhani kuwa CHADEMA kilichoanzishwa na mtu ambaye alimtaka ajiuzulu uwaziri wa fedha kutokana na kuonyesha nia ya kukumbatia ubepari kiwe cha kutolea mfano wa upinzani makini na sio NCCR iliyokuwa bado ikithamini chembechembe za ujamaa?
Vilevile tusisahau ukweli kuwa wakati hadi siku zake za mwisho Mwalimu aliendelea kuamini katika ujamaa lakini pia alishangaa rafiki yake mwaminifu Mzee Kawawa aliposema atakuwa na CCM hadi mwisho wa maisha yake. Ni wazi Mwalimu alishangaa ujasiri wa Mzee Kawawa kusema kuwa atakuwa mwanachama muaminifu wa CCM hata kama kitaamua kukumbatia ubepari kama dalili zilivyokuwa zikianza kujionyesha wakati ule.
Kwa Mwalimu suala la misingi na itikadi ndilo lilikuwa suala la yeye kuendelea kuwepo CCM ama kuachana nacho. Hivyohivyo alikuwa akiamini katika suala la kumeguka kwa CCM kutokana na tofauti za kimisingi na kiitikadi na kutokea kwa upinzani imara hapa nchini na si vinginevyo.
Hapa ndipo ninakuja kuona kuna upotoshaji mkubwa sana wa kile kinachoitwa utabiri wa Mwalimu kuhusu upinzani imara nchini. Ninaamini kuwa upotoshaji huu unafanyika ama kwa kutokujua ama kwa makusudi kabisa ili kuendelea kumtumia Mwalimu Nyerere kuhalalisha maslahi na mikakati ya kuendeleza mfumo fisadi unaoendelea kushamiri nchini mwetu.Hawa wapo tayari kuwaaminisha Watanzania kuwa endapo wao watatoka CCM na kuanzisha ama kujiunga na chama kingine basi chama hicho ndicho kitakuwa upinzani makini. Hawa wasingependa watanzania kuwauliza na hata wao wenyewe kujiuliza maswali magumu ya kama kweli kumeguka kwa CCM kutokana na hali na sababu za hivi sasa ndio kunatosheleza kuleta upinzani imara katika mntiki ya ule alioutabiri Mwalimu Nyerere.
Inatia wasiwasi zaidi kuona kuwa hivi sasa wakati tunaelekea katika uchaguzi mkuu wapo baadhi ya wanaCCM na hata wasio wana CCM wamekuwa mstari wa mbele kuendeleza upotoshaji huu kuwa mpasuko utakaotokea hapo ndio utakaoleta upinzani imara nchini.
Mbaya zaidi inasikitisha kuona kuwa miongoni mwa vyama vya upinzania wapo ambao badala ya kutilia mkazo suala la kujenga upinzani imara wameamua kuendelea kukaa mkao wa kula kusubiri kile wakiitacho mmeguko wa CCM ili nao wafaidike na makapi ya chama tawala kufanikisha ndoto zao za kurithi mfumo fisadi.
Inatisha kuona ni jinsi gani kwa muda wa miezi michache sana tayari kuna zaidi ya watanzania elfu kumi ambao wanadhani tayari wamepokea mwito wa utabiri wa mwalimu wa kujenga upinzani imara kutokana na mmeguko wa CCM.
Siamini kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa ameshindwa kufikiri kiasi cha kudhani kuwa bila ya kujali sababu na mitizamo ya hao Kimisingi, Kiitikadi na Kisera basi hao watakaotoka CCM wataweza kujenga upinzani imara aliokuwa akiufikiria yeye.
Sidhani kama Mwalimu alikuwa amechoka kuifikiria Tanzania yake hadi kuamini kuwa tofauti zinazoonekana sasa zinazohusishwa na suala la rushwa na ufisadi ama ushindani wa kimakundi wenye taswira ya uhodhi wa madaraka ndani ya CCM, zinatosheleza kupelekea kupatikana kwa upinzani imara nchini.
Naamini kuwa wapo wengi wanaotambua kuwa utabiri wa Mwalimu Nyerere kuhusu upinzani imara ulikuwa na maana ya kuwa utatokana na kumeguka kwa CCM kwa tofauti za misingi, itikadi na sera na sio tofauti hizi tunazoziona sasa.
Naamini kuwa Mwalimu Nyerere aliona upinzani imara utakaotokana kuvunjika kwa CCM kutokana na kukua tofauti za kimisingi, kiitikadi na kisera ambazo zitasimamiwa kidete na kupelekea ama wahafidhina waumini wa Ujamaa kuondoka katika chama hicho na kuwaachia wajanjawajanja waumini wa Ubepari au waumini wa ukombozi wa Kibepari kuondoka katika chama hicho na kuwaacha waumini wa Imani za Kijamaa kuendeleza kile ambacho yeye alikianzisha.
Ni wazi kuwa kutokana na hali inavyokwenda sasa uwezekano ni mkubwa wa CCM kumeguka katika misingi ya wale walio mstari wa mbele katika vita ya ufisadi. Yaani wale ambao wanaona kuwa ufisadi sio tatizo kubwa ndani ya chama chao na wale ambao wanaodhani kuwa ufisadi ni mzigo mkubwa ambao chama kinapaswa kujivua ili kuweza kuendelea kulinda uhalali wa kuwa chama tawala.
Yawezekana kuwa hili litaweza kupunguza ukiritimba wa CCM katika utawala. Lakini sidhani na wala siamini kuwa Mwalimu aliufikiria mgawanyiko wa aina hiyo ndio upinzani imara kama ambavyo wengi wanavyopotosha.
Upinzani ambao utatokana na kumeguka kwa CCM kutokana na ushindani wa kimakundi ambao umeegemea zaidi katika masuala (kama vile ufisadi na ushindani wa uhodhi wa nguvu za kiushawishi ndani ya chama) na sio kuegemea katika misingi, itikadi na sera, ni upinzani unaojengwa kwa nguzo legelege.
Ni wazi kuwa upinzani wa aina hiyo hautaweza kuwa imara kwani ni rahisi kujikuta yale ambayo wameyaacha huko walikotoka ili kuanzisha ama kuhamia chama kingine yataibuka tena huko walikoenda lakini zaidi hauwezi kuwa wenye kuweza kuleta suluhu la matatizo ya kitaifa yanayotukuma hivi sasa na hata huko mbeleni.
Upinzani imara ambao utakuwa na manufaa ya kwa watanzania ni ule utakaotokana na tofauti za kimisingi, kiitikadi na kisera na sio tofauti hizi za kiujanjaujanja tunazoziona sasa.
No comments:
Post a Comment