UFISADI KUSHIKA HATAMU?
Ilyas, O.S
Ni muda mrefu sasa nimekuwa na mtazamo kuwa baada ya
kuondokana na mfumo wa chama kushika hatamu, kuna mchakato umekuwa ukiandelezwa
na wajanja kadhaa katika nchi yetu wenye nia ya kujenga mfumo mpya ambao ninaita
MFUMO FISADI.
Matokeo na mchakato wa uchaguzi wa ndani unaolekea kkufika
tamati katika Chama cha Mapinduzi una kila dalili za kufikia hatua ya juu ya
mchakato huu wa ujenzi wa MFUMO FISADI kwa kufanikisha kusimika rasmi uhodhi wa
chama hicho mikononi mwa vinara na makuwadi ama mawakala wa mfumo huo na hivyo
kuwezesha kuhatamisha mfumo huo katika uongozi wa taifa letu.
MFUMO FISADI ni mfumo wenye nia ya kurasimisha na kuhalalisha
mambo ambayo ni kunyume kabisa na misingi ya utaifa wetu kama ambavyo ilijengwa
na kuachwa na Baba wa taifa letu Mwalimu Nyerere na wafuasi wake adhimu kuanzia
alipokuwa TANU na baadaye CCM.
Ni mfumo ambao umekuwa ukijengwa ama kujengeka katika sura mbalimbali
kama vile kujenga mfumo wa soko huria, kuendana na uhalisia na usasa wa kukubali
kuwa hatuna ujanja isipokuwa kukumbatia misingi ya kibepari, umuhimu wa kujenga
tabaka la kati, siasa za ushindani na kadhalika.
Wengi wetu kama si wote kwa namna moja ama nyingine
tumeshiriki katika harakati hizi za kujenga MFUMO FISADI. Ushiriki wetu upo katika ama katika kupanga
ama kutekeleza mikakati yake kwa kujua ama kutokujua, kuhalalisha mambo yake
kwa kutetea ama kuhalalisha chembechembe za ufisadi, kuwawezesha kiuchumi na
kisiasa wale vinara na mawakala wa ujenzi wa MFUMO FISADI na vinginevyo.
Naomba niweke wazi kabla sijaingia ndani katika kuchambua na
kuelezea mtazamo wangu kuhusu hili la ujenzi wa MFUMO FISADI na hatari
tunayokumbana nayo sasa ambapo yawezekana tukawa katika hatua za mwisho katika
kuusimika mfumo huu katika hatamu za nchi yetu.
MFUMO FISADI hauna chama wala wanachama. MFUMO FISADI hauna
dini hii ama ile. MFUMO FISADI hauna kabila hili ama lile. MFUMO FISADI hauna
rika hili ama lile. MFUMO FISADI hauna sekta moja ama nyingine. MFUMO FISADI
hauna tabaka hili wala lile. MFUMO FISADI unaratibiwa, kujengwa na kulindwa na
vyama vyote, sekta zote, dini zote, makabila yote, marika yote,matabaka yote na
makundi mengine.
Kwa leo nitaongelea mfumo huu haramu katika muktadha wa
kinachoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho hivi karibuni tumekuwa
tukisikia na kuona mengi yakitokea na kusemwa katika mchakato wa chaguzi za
ndani za chama hicho. Chama ambacho hadi sasa ndio chama tawala.
Moja ya kitu ambacho kimegeuka kama ndio kioo cha kupima
mafanikio ama athari za uchaguzi huu kimekuwa ni jinsi gani nguvu ya pesa
imeweza kuonyesha makucha yake katika uchaguzi huu.
Wengi tumekuwa tukiuangalia, kuupima na kuchanganua uchaguzi
huu kama ni kioo cha kupima nani atakuwa mgombea na wengine hata kuamini kuwa
ndiye atakayekuwa Rais ajaye.
Wengi tumekuwa tukiuangalia uchaguzi huu kama ishara ya ama
kukirudisha chama katika mstari ama kukiacha kiteketee kwa kukitunuku rasmi kwa
wale wanaonekana ama kujipambanua kama vinara na makuwadi wakuu wa ujenzi wa MFUMO
FISADI.
Kwa kiasi fulani kuna ukweli wake, kwani kuna wengi ama
wamegombea, wamechagua ama wamechaguliwa kutokana na kushawishiwa, kuwezeshwa
ama kuahidiwa neema na ama wapambe au vigogo wenye kuamini kuwa wakishashinda
ndani ya CCM basi Urais wa 2015 ni wao na kwamba ulaji utakaokuja nao utakuwa
wao wa kugawana.
Hali hii inasikitisha na kutisha sana kwa mustakabali wa
taifa letu. Inatia uchungu na kukatisha tamaa kwa mzalendo yeyote yule awe
mwanachama wa chama hiki na hata yule ambaye sio mwanachama wake lakini
anatambua umuhimu wa chama hiki kwa taifa letu haswa wakati huu wa
miparaganyiko lukuki.
Harakati za kujenga MFUMO FISADI zimelenga katika kuwaangusha
na kuwakatisha tamaa wale wote waliokiunga mkono chama cha CCM kutokana na
Misingi yake imara ya kuweka mbele UTU wetu na kukiaacha chama mikononi mwa
wale walioweka mbele IMANI YA NGUVU ZA FEDHA.
Wakati mwengine huwa najenga fikra kuwa yawezekana nguvu za
harakati hizi za vinara na makuwadi wa ujenzi wa MFUMO FISADI ndani ya CCM
zinatokana na nia ya dhati ya kukiondoa madarakani chama hiki. Kwao wao na
wakubwa zao wanakiona chama hiki chenye misingi na historia adhimu ya utu,
usawa na ukombozi wa ndani na nje ya mipaka yetu ni kama kizingiti dhidi ya nia
yao ya kuhatamisha mfumo fisadi kwa jina la Ubepari.
Yawezekana, na inajionyesha wazi kuwa vinara na mawakala wa MFUMO
FISADI huu ambao wengi tayari wana mahusiano maalum na vyama mbadala katika
kinyang’anyiro cha utawala wa nchi, nia yao hasa sio kuhodhi madaraka ya chama
hiki bali kukivunjilia mbali na baadaye kutumia vyama vyenye misingi ya
kibepari ambavyo sasa vimevaa ngozi za hisia za kijamaa katika mpango kabambe
wa kusimika rasmi MFUMO FISADI katika hatamu za utawala wa taifa letu.
Na hapa ndipo ninaona kuna tatizo kuu ya jinsi baadhi ya
wanaojitambulisha kama wapambanaji dhidi ya ujenzi wa MFUMO FISADI wanakosea
katika mapambano yao. Wengi wa wapambanji hawa, wa ndani na nje ya CCM,
wamekuwa wakijikita zaidi katika mkakati wa kupanga safu za uongozi wa chama
dhidi ya washindani wao ndani ya chama kama maandalizi ya mpambano mkuu ujao wa
kumpata mgombea wa Urais kupitia chama chao.
Kwa kuweka mbele ushindani huu unaotegemea sana wa nguvu za
fedha na sio imani ya wanachama kwa chama na viongozi wao kundi hili la wana
CCM limeweza kujenga mazingira ambayo maadui ama washindani wao katika sakata
la uhodhi wa chama wamepata urahisi wa kipropaganda na kimkakati.
Matokeo yake hata hao wenye kujipambanua kama CCM-Misingi
ambao wakati fulani walijulikana kama MTANDAO MATUMAINI wanalazimika katika
kuamini katika nguvu za fedha ili kupambana na washindani wao wa kundi la
MTANDAO MASLAHI ambao kwao wao nguvu za fedha ndio msingi mkuu wa mafanikio
yoyote.
Na hapa ndipo tunapokuja katika tatizo lingine katika hizi
juhudi za kupambana na harakati za MFUMO FISADI ambazo kama mambo
hayajabadilika sasa na sio baadaye basi ni wazi zitafanikiwa katika kushika
hatamu za taifa letu.
Kitendo cha wana CCM wengine na hasa wale ninaowaita CCM ASILIA,
yaani wana CCM wenye kuamini katika misingi ya chama na utaifa wetu, kuwaachia
“WANAMTANDAO” kupambana wenyewe kwa wenyewe ni kosa kubwa linaloendelea ambalo
nalo limewezesha ujenzi wa MFUMO FISADI na uwezekano wa mfumo huo kushika
hatamu.
Mapambano ya dhati ya kukikomboa chama hiki ambacho kwa
mtazamo wangu ni kuwa hadi sasa kimekosa mbadala makini wa kukibadili na
kutegemea ukombozi wa kweli hayatafanikiwa kwa kuwaacha wanamtandao wenyewe kwa
wenyewe kuhodhi uwanda wa mapambano.
Zaidi kuna uwezekano mkubwa wa hao tunaoamini kuwa
wanapambana dhidi ya wingu la vinara na mawakala wa MFUMO FISADI kutoka katika
kundi la MTANDAO MATUMAINI wakaishia kukubali kushindwa na kujiunga na timu ya
ushindi ya wenzao. Tukumbuke kuwa hawa kwa pamoja walishirikiana katika
kuendesha mapinduzi ya ndani ya chama hapo kabla na hivyo kuweka msingi wa
ujenzi wa mfumo fisadi. Wakati wao wameamua kujitenga na jitihada za kujenga
mfumo fisadi. Wenzao wa MTANDAO MASLAHI kwa nguvu zote wameamua kuubeba hadi
watakapofanikiwa kuuhatamisha katika siasa na uongozi wa nchi yetu.
Mapambano ya dhati na yanayoweza kuirudisha CCM katika mstari
na kukilinda dhidi ya nia mbaya za vinara na wapambe wa MFUMO FISADI ni yale
yatakayojikita katika ajenda za DIRA, MISINGI na ITIKADI ya chama na sio
vinginevyo.
Na hapa ndipo wana CCM, Wazee kwa Vijana wenye kuamini katika
umuhimu wa dira, misingi na itikadi za chama hicho na taifa letu wanakuwa na
umuhimu wake kwani ni wao tu na sio wengineo ndio watakaoweza kubadili mwenendo
wa mpambano huu na hatima ya chama chao na taifa letu.
Ndani ya kiwingu cha habari mbaya za ushindi wa nguvu za
fedha katika chaguzi hizi, pia kuna habari njema kiasi. Tofauti na chaguzi
zilizopita, katika chaguzi hizi wapo baadhi ya wagombea waliofanikiwa kushinda
hivi sasa ambao hapo nyuma walishindwa katika kila chaguzi walizokuwa
wakishiriki kutokana na “ushamba” wao wa kutokuamini katika nguvu za fedha na
kujikita katika kampeni za misingi na tamaduni za chama.
Ushindi wa hawa ambao wanaweza kuwa kidogo lakini wenye umuhimu
unaonyesha matumaini na uwezekano wa nguvu za MISINGI ndani ya chama hiki na kutoa
ujumbe kuwa hii kansa ya nguvu za fedha haijakikumba chama kizima. Hivyo endapo
wengi zaidi wa aina hiyo wakiamua kusimama na kupambana, bado kuna uwezekano wa
mpambano wa kuzuia uhodhi na hatimaye uwezekano wa Ufisadi kushika hatamu
kufanikiwa kwa manufaa ya chama chao na taifa letu.
Ni mapambano yaliyojikita katika nguvu za misingi tu na sio
nguvu za fedha ndio yatakayotuepusha na tishio la UFISADI KUSHIKA HATAMU na
madhara yake mengineo. Tishio ambalo kuna uwezekano mkubwa wa kurasimishwa
rasmi hivi karibuni tunapoelekea katika tamati ya chaguzi za ndani za CCM. Na
kama ikishindikana kuzuia tishio hilo sasa basi wote kwa pamoja tujiandae na
hasira za wapiga kura ambao wanaonyesha kila dalili za kukumbatia fikra ya
“bora mbadala na liwalo na liwe” kama fimbo yao kwa wasaliti wa imani yao
waliyoitunuku kwa miaka mingi ndani ya CCM.
Mwandishi ni Mkurugenzi
wa kampuni ya ushauri wa masuala ya siasa, uongozi na maendeleo inayoitwa
TANZANIANJEMA ADVISORY. Anapatikana omar.ilyas@tanzanianjema.com, www.omarilyas.com, twitter; @omarilyas
No comments:
Post a Comment