Masikini Sumaye!

MASIKINI SUMAYE!!!!!
@Mtanzania Jumapili Newspaper. 2005.
Wakati kumebakia takribani wiki saba na siku chache kwa chama tawala cha CCM kuchagua mgombea wake wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao hapa nchini, vimbwanga vya kisiasa vinazidi kushamiri. Kwa sisi wachambuzi wa masuala ya kisiasa kazi inazidi kuwa kama kiswahili cha mtaani kinavyosema “kuchanganyia”.
Hivi karibuni baaada ya maneno mengi ya pembeni, mmoja wa wachangamkiaji wa nafasi hiyo ameamua kukata ngebe za wale aliowaita wapinzani wake “kisiasa” kwa kuudhihirishia umma kuwa baadhi ya mambo yanayosemwa kuhusu yeye ni kweli na wala sio umbea wa wadaku.
Hapa ninamaanisha kujitangaza rasmi kwa Waziriri Mkuu wa sasa Bwana Mheshimiwa Fredrick Sumaye, mbunge wa jimbo la Hanang kupitia chama cha CCM.
Ukiangalia kwa juu utakubaliana na mimi kuwa kitendo alichokifanya raisi mtarajiwa huyu kimeonyesha kile kitu ambacho wengi wamekuwa wakisema amekosekana nacho, yaani ushujaa wa hali ya juu.
Nasema ushujaa wa hali ya juu kwa sababu kufuatana na taratibu walizojiwekea waheshimiwa hawa katika chama cha CCM ni kuwa ni haramu kwa mtu mwenye nia ya kugombea uraisi kuanza kufanya kampeni za nafasi hiyo kabla ya tarehe maalum zilizopangwa na chama na kujitangaza rasmi ni moja ya njia za kampeni kama ilivyoelezewa na taratibu za kichama.
Vilevile kwa muangalio mwingine mheshimiwa huyu ameweza kuonyesha ujasiri wa kuwa mkweli na uwazi wa kuelezea dhahiri kwa umma wa watanzania kuwa ni kweli anajiandaa kwa nguvu zote kunyakua kiti hiko tofauti na hisia za walio wengi kuwa amekosa sifa hizo za kuwa mkweli na muwazi katika matendo yake.
Lakini ukiangalia kwa undani zaidi unaweza kugh’amua jinsi gani mheshimiwa huyu amejiingiza mtegoni kwa kuudhihirishia umma wa watanzania ambao wengi wanauona kama wa wadanganyika, mapungufu ambayo kwa lugha yake mheshimiwa huyu maadui zake wa kisiasa wanamzushia.
Mojawapo ya mapungufu hayo ni upeo wake wa kuona na kushungulikia mambo kama mwanasiasa mkomavu na aliye na uwezo wa kuendesha siasa kiufundi. Na hili sio tu ni mapungufu kwake yeye binafsi lakini na vilevile kwa wale waliomzunguka kutokana na kitendo chao kumwachia akiingia mtegoni kirahisi kama alivyofanya.
Nasema ni upungufu kwa kuzingatia maswala afuatayo. Moja ni muda wa kutoa tangazo hilo, pili njia alizotumia kutoa tangazo hilo na tatu sababu alizosema kuwa zinampelekea kugombea nafasi hiyo.
Kuhusiana na muda wa kutoa tangazo hili muhimu, hili nimgependa kiliainisha katika viwango viwili vifuatavyo.
Kwa wale ambao wanatambua umuhimu wa kufuatitilia hatima ya nchi yetu tukufu hasa kwa kuzingatia utamaduni wa kinyang’au unaojitandaza katika jamii yetu hasa kenye medani ya siasa, ni wazi wamekuwa wakifuatilia mawazo ya wachambuzi wenzangu wa kisiasa ambao wamekuwa kama anavyodai mheshimiwa huyu wakimfuatafuata na kumzushia majungu kila kukichwa.
Lakini katika gazeti la RAI la tarehe…..mwandishi mmoja wa siku nyingi aliandika makala ambayo kwa mara ya kwanza imekuwa imemchambua kwa wazi kabisa mheshimiwa huyu. Mwandishi huyu bila ya woga ameeleza kwa wazi kabisa baadhi ya mapungufu aliyonayo mheshimiwa huyu kiasi cha kuwa hafai kabisa kugombea nafasi ya urais. Mimi nisingependa kuyarudia hayo kwa sasa lakini kitendo cha mheshimiwa huyu kuripuka kujibu mapigo katika wakati kama huu ambao aliyoyasema mwandishi Salva bado yapo kichwani na kwa kawaida yasemwayo mwanzo ndio yenye uwezekano wa kuganda vichwani mwa watu, mheshimiwa Sumaye amejikuta akimsidia kazi ya kummaliza aliyoianza mwandishi huyo.
Hili linaonyesha jinsi gani mheshimiwa ambaye mwandishi Salva amemwita MNYAPARA ALIYECHOKA asivyo makini. Badala ya kusubiri a ditect mazingira yeye ameruhusu mazingira kumditact yeye, kwa kiingereza ni kuwa ameonyesha kuwa REACTIONARY na siyo PROACTIVE kama wanasayansi wa siasa tunavyoamini mwanasiasa bora awe.
Vilevile muda unamtupa mkono mheshimiwa huyu kwa upande wa taratibu za kichama. Kujitangaza wazi kwa mheshimiwa huyu ni wazi kumemuweka katika mazingira mabaya kwa wapinzani wake ndani ya vyombo husika vya chama kama vile Sekretarieti kuu yenye jukumu la kutoa maksi kwa kila mgombea kumnyima points muhimu kwa kosa hilo la kiutaratibu. Hili vilevile linaonyesha upeo mdogo wa kufikiria.
Nikija pungufu la pili ambalo ni njia aliyotumia mheshimiwa huyu kujitangaza rasmi kuwa atagombea urais wa nchi hii nasema ni upungufu kutokana na mambo mawili. Ningelikuwa ni mimi ninayegombea katika hali mbaya ya kisiasa kama mtanzania mwenzangu huyu kamwe nisingelichagua mwandishi mjanja kama Manyerere ambaye sio tu hawakuwa na mahusiano mazuri hapo kabla kutokana na habari alizokuwa akiripoti hapo zamani. lakini vilevile hata kama anaona kuwa karibu magezeti yote isipokuwa gazeti lake la WAZO LA WIKI na la vijana wake la HOJA, hayamwandiki vizuri lakini sio gazeti alilotokea mwandishi huyu.
Hivi mtu kama waziri mkuu anashindwa kujua washika dau wa magazeti yetu na kujua ni yapi mawazo yao kuhusiana na yeye. Hata kama gazeti hili katika siku zake za hizi za mwanzo linajitahidi kuwa mstari wa mbele kwa kutoa habari bila ya kuegemea upande wowote lakini kamwe si vigumu kung’amua chachu ya waandishi na wamiliki wa maagazeti yetu katika suala zima la kutengeneza mawazo ya jamii. Mheshimiwa Sumaye alitakiwa kuonyesha umakini kidogo katika hili na sio kuingia mtegoni kirahisi hivyo.
Upungufu wa tatu kwa upande wa mheshimiwa huyu unaonekana katika sababu alizosema kuwa zinampelekea kugombea nafasi hiyo. Kwa mujibu wa muandishi Manyerere, mheshiwa huyu ametoa sababu kuu tatu zinazomfanya yeye agombee Urais, nazo ni kuendeleza siasa za uwekezaji, kudumisha aliyoyaita mafanikio ya rais mkapa na nafasi yake katika serikali ya sasa.
Ni wazi kuwa hizo ndizo sababu zake za dhati kabisa kugombea nafasi hiyo na hapo lazima apongezwe kwa kuwa mkweli na muwazi wa hali ya juu. Lakini kama mwanasiasa ni umakini gani alioutumia kujiuza kwa wapiga kura wake ndani na nje ya chama chake kwa kudiriki kusema hadharani kuwa hizo ndizo sababu zinazompelekea kugombea nafasi ya urais wa nchi hii.
Nasema ni upungufu kwa sababu hata kama ndio ukweli hizi ndio sababu kuu zinazompelekea yeye kugombea nafasi za urais, mwanasiasa makini kamwe asingeropoka kama alivyofanya yeye. Hivi ina maana hajui jinsi gani wananchi wa chini walio wengi walivyo na hasira dhidi ya hawa jamaa tunaowaita wawekezaji. Hata kama wamewezesha baadhi ya vijana wa kitanzania wachache tena wengi kati yao wenye majina “mazuri” na waliopelekwa kusoma elimu bora ughaibuni kupata ajira “nzuri” na kuweza kuendesha vigari vya mikopo na kujifaragua Sheraton, aaah ni Royal Palm, opss nini tena???. Ukiangalia kwa undani vijana hawa wengi wao wamefika huko ama kwa kodi ya walalahoi wetu au kile kinachoitwa “scholarship” zinazotolewa na hao waitwao wawekezaji.
Hivi hizo ndio siasa za kuwaingia watanzania walio wengi wanaolala bila ya uhakika wa mlo wa kesho kwa sababu mzungu amepewa kijiardhi chake alichokuwa anajipatia shibe ya kutosha yeye na familia yake? Hivi mheshimiwa Sumaye anafikiri akitoa wale “vijana wake” wachache pale Mererani ambao wengi wao ni watoto wa “nyumbani”, ni nani kati ya wengine watakompigia kura au hata kutaka kusikia jina lake linaelekea ikulu? Hivi huyu jamaa ni makini kweli au anataka kuuza majimbo ya chama chake kwa CHADEMA au CUF kwa bei ya che. Au labda mheshimiwa huyu ana mpango wa kutoitisha uchaguzi wa wabunge na madiwani kule Bulyanhulu na kwengineko kama anavyofanya jimboni kwake Hanang hadi hivi sasa.
Kwa kweli kama ni ajenda za kuwaomba Urais watanzania, na hata wanachama wa CCM pekee, sera ya wawekezaji iliyojawa utapeli kama hii ya kwetu si mojawapo kwa mtu makini kuingilia nayo uwanjani. Kwani hii ni moja ya sera iliyo wazi au ashakum si matusi, iliyo uchi zaidi kushutumiwa na wapinzani wake kisiasa kiasi ya wananchi wakamuona mheshimiwa huyu hana jipya zaidi ya kuendeleza “kuiuza” nchi yetu kwa makaburu na wazungu.
Kuhusiana na ajenda ya kuendeleza mazuri yaliyofanywa na rais mMkapa hapa nako kuna utata. Ingawa ni kweli kama atatokea mtu kubadilisha kila kilichopo hata kama kweli ni vingi ni vibaya, kuna hatari kubwa ya nchi hii kukumbwa na janga kubwa la umasikini mara mia kuliko hivi sasa, lakini ni wazi kuwa mheshimiwa huyu kama waziri mkuu anayesifika kwa kutoa maamuzi mengi ya kupingana na sera za uchumi za CCM, kamwe hawezi kuwa chaguo la wananchi. Hivi akitokea mtu akaelezea jinsi Rais Mkapa alivyomfanya mheshimiwa huyu kuwa ni waziri mkuu wa pekee Tanzania ambaye alinyang’anywa madaraka mengi kuliko yeyote katika historia ya Tanzania baada ya uhuru, ajenda hii kweli itafanya kazi?
Au wakitokea wapinzani wake wa ndani ya CCM wakatoa mahesabu ya maamuzi mangapi makubwa ya maana yaliyotolewa na Rais wetu na mheshimiwa huyu akahusika atasemaje?
Hili na lile la kuwa yeye ndiye msaidizi wa karibu wa Rais Mkapa kwa miaka tisa na miezi kadhaa sasa ni ajenda dhaifu mno na rahisi kuwapa watu umaarufu wa kisiasa bure bure. Kwani rekodi inaonyesha wazi kuwa mheshimiwa huyu amekuwa akivurunda tu na ndio maana wapo baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanaona udhaifu wake kama waziri mkuu ndicho kilichomhakikishia kiti chake kwa muda mrefu kwani Rais Mkapa kama anavyonekana hakupenda kuwa na mtu atakeyemfunika ki umaarufu. Anaposema hivi anataka kutuambia rais Mkapa amechoka kuiona CCM madarakani hadi kufikiria kumrithisha mheshimiwa huyu Urais wa nchi hii. Ina maana viongozi wenzie waandamizi katika serikali hii ya tatu ni wabovu na hawawezi kuaminiwa kuendeleza yale yanayoitwa mafanikio ya serikali ya Rais Mkapa.
Vile vile hoja hizi mbili kwa kweli zinawahakikishia watanzania kuwa yanayosemwa na wale anaowaita maadui zake kisiasa kuwa mheshimiwa huyu anataka nafasi hii ya Urais si kuwa ana dira bora kwa nchi yetu bali kulinda mafanikio yake binafsi aliyoweza kujikusanyia kwa miaka hii michache aliyokuwa madarakani kama waziri wetu mkuu. Haya ni pamoja na nafasi ya uheshimiwa ndani na nje ya jamii yetu na bila kusahau mashamba kule mvomero, majumba na viwanja kila pande ya nchi na miradi mingine inayochipuka bila ya uoga ama kwa jina lake binafsi, mama watoto wake, watoto au wafanyibiahsara walio karibu naye.
Kwa kweli pamoja na kuwaonea huruma viongozi wenzie wa CCM wanaoshiba kwa chama chao kuwa madarakani bila ya upinzani wa maana, namuonea huruma sana Mheshimiwa huyu. Ni wazi mheshimiwa huyu hata kama mapungufu yake yamekuwa sio ya kuficha, inaonekana timu yake inayomsaidia kwenda ikulu, ukitowa mapesa bwerere waliyonayo hakuna watu makini wa kupanga mchezo wa kisiasa ambao wangemshauri asikurupukie mtego aliowekewa kirahisi kama alivyofanya.
Kama nilivyoelezea hapo juu, kazi yangu mimi sio kumchambua sana mheshimiwa huyu na nafasi yake kama mgombea urais wa nchi yetu katika uchaguzi ujao bali kuchambua udhaifu alio uonyesha katika kile alichokisema kukata ngebe za wapinzani wake kisiasa. Si vibaya nikawanong’oneza wasomaji kuwa kazi ya kumchambua yeye na wenzanke wengineo ambao wao ama kwa kuheshimu taratibu walizojiwekea ndani ya chama chao au kwa mahesabu yao ya kisiasa wameamua kuendelea kutamba gizani, itakuja kwenu hivi karibuni.
Napenda kuwakilisha uchambuzi wangu kwa wakubwa zangu katika fani hii. Karibuni.

No comments: