Katika kuendeleza maoni yangu kuhusu umuhimu wa CHADEMA kushinda kwa kushindwa sasa ni vizuri kurudia makala hii hapa chini ambayo niliandika miaka sita iliyopita mara baada ya mchakato wa kupata mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri na Muungano kupitia tiketi ya CCM......
TULIKOTOKA: MWANZO WA SAFARI YA MWISHO YA CCM
Na Ilyas, O.S
20/05/2005
Ni ukweli usiopingika kuwa matokeo ya uchaguzi wa mgombea wa nafasi ya urais katika Chama Cha Mapinduzi yameweza kuliepusha kundi hili kisiasa katika hatari ya kugawanyika kwa kasi kama ilivyokuwa ikionekana awali.
Naongelea dhana ya kugawanyika kwa kasi tu, kwa kuwa nina uhakika kuwa mwenendo mzima wa siasa za uchaguzi huo na mambo kadhaa yaliyojitokeza katika siku za mwisho za shughuli hizo ndani ya chama hicho, zimeleta mgawanyiko mkubwa na wa hatari zaidi utakaodumu daima.
Hata kama kwa njia za ajabu mno ndugu hawa wameweza kumchagua mtu ambaye kwa maoni yao wana uhakika wa kuendelea kutawala watazania kwa miongo kadhaa ijayo.
Ni wazi kuwa CCM ya sasa si ile tena iliyokuwa ikiwavutia watu kwa utulivu wake, uongozi wa kufuata maadili ya utanzania, falsafa zake zenye kujali utu, kupinga ubaguzi na mengineyo mengi mazuri yaliyokuwa yakitofautisha chama hiki na makundi mengine ya kisiasa.
Chama cha mapinduzi kama ilivyo kwa vyama vingine vikubwa tawala barani afrika, kimepitia mabadiliko mbalimbali hadi kufikia sasa.
Mabadiliko hayo yameanzia kutoka kuwa chama cha ukombozi, kikaja kuwa chama cha kujenga utaifa na baadaye kuwa chama cha kuimarisha uchumi na kuboresha maisha ya watanzania kabla ya sasa kugeuka kuwa chama cha kuhakikisha kuendelea kubaki madarakani kwa tabaka tawala.
Mbadiliko huu umekuja kutokana na nguvu mbalimbali za kimfumo na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani ambayo yamepelekea washika dau wa chama hiki ambao mwanzo walijitahidi kukabiliana vilivyo, kuamua kufuata mkondo wa mabadiliko ili kuweza kuendelea kuongoza taifa hili.
Mfano mkubwa wa mabadiliko haya nje ya mipaka yetu ni chama cha Labour cha Uingereza kinachoongozwa na mwanasiasa “kijana” machachari Tony Blair. Chama ambacho wiki iliyopita kilipata pigo kubwa la kisiasa kwa kupoteza viti vingi katika baraza la wanaojiita wawakilishi wa makabwela.
Kama ilivyokuwa CCM, chama hiki kilianzishwa kama kundi la kutetea wafanyakazi na makabwela wa Taifa hilo la kibwanyenye.
Kama ilivyo kwa vyama vingi vya aina hii duniani, chama cha Labour kama kilivyokuwa CCM hapo awali, kilikuwa ni chama kinachoendeshwa na misingi na falsafa madhubuti za kutetea wanyonge.
Falsafa na misingi ambayo walijiwekea ili kila anayetaka kuchaguliwa kukiongoza chama hicho na hivyo kugombea nafasi ya kuongoza serikali ya Uingereza alipaswa kuonyesha wazi kuwa ni mfuasi makini na mwaminifu wa misingi hiyo kwa kauli thabiti na vitendo.
Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani yalikipelekea chama hicho kukosa mvuto wa kuaminiwa na wapiga kura wengi na hivyo kuwekwa kando katika kuingoza Uingereza kwa miaka kadhaa.
Hali hiyo iliwapelekea kundi dogo la wanasiasa vijana machachari wa chama hicho akiwemo bwana Mandelson ambaye aliwahi kuishi Musoma, Tanzania kwa miaka kadhaa akitafiti siasa ya ujama na kujitegemea na utaalamu wa kiuongozi wa baba wa Taifa, kuja na mbinu mpya walioita LABOUR MPYA.
Tofauti na Labour ya kihistoria, New Labour kama ilivyo CCM hivi sasa, ililenga matumizi ya siasa za kubabaisha zilizo tofauti na misingi na falsafa asilia ya chama hicho ili kuweza kuwalaghai wapiga kura waliokitupa, kukichagua na kukirudisha madarakani.
Kwao wao ni kuwa mara baada ya kurudi madarakani wangeweza kuzirejesha siasa makini za kihistoria za chama hicho na hivyo kuendeleza misingi na falsafa zake asilia kwa mtindo unaoendana na wakati uliopo.
Kama hapo baadae ilivyokuwa kwa upande wa wahafidhina wa chama cha Republican cha Marekani walipomchagua George W Bush kuwauzia fikira zao za kulinda nafasi ya ubabe wa marekani duniani, Mandelson na wenzake waliamua kumchagua mwanasiasa machachari aliyekuwa akikubalika wakati huo yaani Tony Blair kuongoza mpango huo.
Matokeo yake ni hali inayonekana hivi sasa huko Uingereza. Sio tu chama hicho kimegeuka kuwa cha kinyang’au zaidi kuliko chama cha mahafidhina wa kijadi cha Conservative, hivi sasa kinaelekea kaburini kwa mwendo wa kasi mno.
Kitu pekee kinachowezesha wao kuwa madarakani hadi hivi leo sio uhalali wa kidhati kutoka kwa wananchi isipokuwa propaganda za kuwapumbaza wapiga kura.
Propaganda zinazolenga kuwaweka mateka Waingereza walio wengi kwa kutumia dhana ya kuwa hakuna mwengine mwenye mvuto kama yeye anayeweza kuwalinda waingereza kwa madhila makubwa zidi kutoka kwa chama cha wahafidhina.
Ukiangalia mlolongo mzima wa historia ya chama cha Labour ni wazi kuwa kuna mambo yanayoshabihiana na hali inayojikita ndani ya chama cha mapinduzi.
Hapo zamani hata baada ya kuruhusu siasa za vyama vingi chama cha mapinduzi kilikuwa ni chama kilichokuwa kinapata wafuasi wengi kutokana na hali ya kuwa wengi wa wananchi hawa walikuwa wakijinasabisha na misingi na falsafa za chama hicho.
Hata kama wengi walikuwa wakikatishwa tamaa na matendo ya viongozi walio wengi wa chama hicho ambayo ni tofauti na sura yake asili, kuwepo kwa umakini wa kimaamuzi haswa yale makubwa kama vile mtiririko mzima wa kubadilishana madaraka kuliwapa faraja wanachi wengi waliokuwa wanaendelea kukata tamaa.
Hili na lile la kuwepo kwa baadhi ya viongozi wachache ambao tofauti na walio wengi, kauli zao na matendo yao yenye kuonyesha kuendelea kwao kuamini misingi na falsafa asilia za chama hicho, kuliwapa moyo wa matumaini watanzania walio wengi, wanachama na wasio wanachama.
Hali hii iliweza kuwazuia wanachama waaminifu wa chama hicho vijana kwa wazee, wenye sifa za umakini wa hali ya juu kutokisusa ama kutohama chama hicho kwa muda mrefu sasa.
Wengi hawa walikuwa bado wakiamini kuwa ipo siku chama hiki kitapata uongozi imara na makini utakaowezesha kurudisha chama na nchi yetu katika mstari ulionyooka na kuachana na siasa za sera za kukurupuka kwa minajili ya kuwalaghai wapiga kura tu.
Ndio maana hata hivi karibuni tulipokuwa tukishuhudia siasa chafu za kupindukia mipaka ya utanzania na ubinadamu kwa ujumla, bado walikuwepo waliukuwa wakiamini kuwa mwishoni busara za uongozi wa chama hicho zingesimama na kurekebisha mambo.
Hata hivyo hilo halikutuokea na waliukuwa wakiaminiwa kwa kazi hiyo ama walinyamaza kimya, walinyamazishwa au waliamua kukubali yaishe na kubariki siasa chafu zenye kukiuka misingi madhubuti ya chama hicho kutawala maamuzi ya vikao vyake vikuu.
Yote yanaweza kufumbiwa macho lakini kitendo cha Mwenyekiti wa chama hicho kuamua kuzuia taarifa ya siri ya sekretarieti ya maadili ya chama hicho iliyokuwa ikielezea vigezo vya kimaadili vya wagombea wote kuzungumziwa na wanakamati kuu ni kosa kubwa la kihistoria.
Maelezo kuwa wote wametoa rushwa hivyo wote sawa, kwa kweli ni upuuzi wa hali ya juu ambao kamwe hakuna aliyefikiri kuna siku Mwenyekiti wa chama hicho anaweza akaufanya.
Hata kama historia na tafiti mbalimbali zinaonyesha wazi kuwa chama hiki kimekuwa kikumbatia rushwa na kiongozi wake kuishia kutoa vitisho vya mdomo tu, lakini inapofika mkuu huyo anahalalisha uchafu huo ambao ni tofauti na nguzo kuu asili za chama hicho ati kwa kuepusha kubomoka kwa chama, ni wazi safari ya mwisho imewadia.
Lingine ni lile la kuruhusu wanakamati kuu ambao wengine ni viongozi waandamizi bila ya aibu kutumia siasa ya ubaguzi ndani ya vikao vikuu kama hivyo.
Pale machizi mbalimbali walioshindwa maisha walipokuwa wakitumia siasa haramu na chafu kama hizo kwenye vyombo mbalimbali vya habari, halali na haramu, baadhi ya watanzania makini ambao ndio walikuwa ngome ya mwisho wa chama hiki waliweza kuelewa na kuvumilia.
Lakini pale anapokuja mtu mkubwa kama waziri mwandamizi akasimama akipinga kuchaguliwa kwa fulani kwa kuwa amezaliwa akiwa na mchanganyo wa kabila au rangi fulani, na wakubwa hao wakapigia makofi, kunyamaza au Mwenyekiti akahalalisha jambo hilo kama ni demokrasia, kwa kweli hiyo ni ishara mbaya mno.
Vilevile ni dalili mbaya pale wakuu wa chama hicho na haswa wazee wenye busara waliokuwa katika makuzi ya siasa asilia za chama hicho na wengine kushiriki katika ujenzi wake wanapokuwa tayari kuweka kando maslahi ya watanzania kwa ujumla na kujali ushindi wa chama tu kama dira yao kuu ya kufanya maamuzi.
Ushindi ambao kwao wao ni muhimu tu kutokana na uhakikisho wa kuwa wao na vizazi vyao vitaendelea kuwa madarakani daima milele hata kama ishara zinaonyesha kupotea kabisa kwa utaifa wetu ambao ndio umekuwa nguzo yetu muhimu kama nchi na jamii staarabu.
Kwa ujumla ingawa wengi wanaamini kuwa chama cha mapinduzi kimeweza kuvuka mtihani mkubwa kwa ushindi, ni wazi kuwa ushindi huo unaendana na kujisimika rasmi kwa siasa mpya zisizojali misingi na falsafa asilia za chama hicho ambazo kwa kweli ndizo zimekuwa nguzo kuu za kuendelea kwa uimara wake wakati wote huu.
Siasa hizi mpya ambazo zinalenga wingi wa kura tu na sio mipango madhubuti ya muda mrefu yenye kulenga kustawisha jamii kwa mapana na marefu daima haziwezi kuifanya CCM kuendelea kuwa chama cheney mvuto asili ambo hata kama mambo hayaenda sawa wananchi wataendelea kukiamini na kikihamini.
Siasa hizi zinazofuata mbinu za soko huria ambazo zinalenga kumnadi mtu kama bidhaa nyingine sokoni zinafanya chama hicho kutegemea uhalali wa umaarufu wa mwanasiasa huyo tu na sio mapenzi na imani juu ya chama hicho.
Bahati mbaya umaarufu huu unajengwa na matarajio hewa ndani ya mioyo ya wananchi, ambayo ama kwa mapungufu ya kiutendaji ya mwanasiasa huyo au ya kimfumo ni vigumu kuyafanikisha.
Hivyo basi kukifanya chama hicho kuwa mateka wa mwanasiasa huyo na wajanja wachache waliomzunguka wanye uwezo wa kucheza na akili za wapiga kura kwa muda Fulani tu.
Hawa huwezesha hilo kwa kutumia mbinu mbalimbali za kihadaa ambazo daima huishia ama kuvuruga jamii au kuchokwa na wapiga kura.
Wapo wanaofikiri kuwa kupatikana kwa mgombea na baadaye kiongozi mwenye mvuto kama aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa ni silaha muhimu ya kuhakikisha uimara wa chama hiki.
Mimi nasema ndio lakini ni kwa muda mfupi tu na hiyo hiyo ndiyo silaha ya kujiangamiza kwa muda mrefu.
Ni wazi ushindi uliopatikana Dodoma hivi karibuni ni mwanzo wa safari isiyo rasmi ya mwisho ya chama cha mapinduzi.
No comments:
Post a Comment