CHADEMA Ishinde kwa Kushindwa!

22 Sept 2011

Matukio ya hivi karibuni ambayo yamefanikiwa kupata nafasi ya juu katika vyombo vya habari kuhusiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yamenijengea mtazamo kuwa ili CHADEMA kushinda katika safari ndefu iliyonayo kama mtawala mbadala kinapaswa kushindwa sasa.

Kitendo cha hivi karibu ambapo wafuasi na viongozi wa CHADEMA wakiwa pamoja na wabunge wawili wa chama hicho, Bwana Sylivester Kasulumbayi na Bi Susan Kiwanga kumtusi, kumkwida, kumteka na hata kumdhalilisha mkuu wa wilaya ya Igunga Bi Fatuma Kimario ni muendelezo wa dalili mbaya ya nini kinaendelea ndani ya chama hicho, ni wapi kinaelekea kama kundi la maslahi ya kisiasa na wapi kinaipeleka Tanzania yetu kama taifa.

Hata hivyo itakuwa kosa kuangalia kitendo hiki ambacho mimi nakiita kitendo cha kihuni ingawa wapo wanaothubutu kukiita kitendo cha kishujaa na ukombozi, kama tukio linalosimama pekee. Huu ni muendelezo wa mambo mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza ndani na nje ya chama hiki kwa muda mrefu sasa ambayo yamefanya baadhi ya watu ambao hapo kabla walithubutu kuamini kuwa chama hiki kinapaswa kuwa mbadala makini wa utawala wa nchi yetu kukitazama kwa jicho la tahadhari zaidi ya matumaini.

Nadhani sihitaji kuyataja matukio hayo ambayo mengi yamekuwa yakipata nafasi ya kipekee katika vyombo vya habari na mengine yakiwa yanafunikwa haramu ipite. Hapa ningependa kulipitia tukio hili la karibuni kuangalia linaelewekaje na nini athari yake kwa CHADEMA na taifa kwa ujumla endapo wapiga kura wa Igunga ama wataweza au hawataweza kumpa ushindi mgombea wake katika uchaguzi wa tarehe 2 Oktoba 2011.

Kwa miaka kadhaa sasa na tangia kuanzishwa kwa chama hiki, kimekuwa kikiandamwa na tuhuma za ukabila na udini. Yaani chama kinachoweka mbele maslahi ya kabila, eneo na dini fulani. Kabila likiwa wachaga, eneo likiwa la ukanda wa kaskazini wa Tanzania na udini ikiwa wakristo.

Kwa kiasi fulani CHADEMA wamekuwa wakijitahidi kushughulikia tatizo hili ama kwa kukanusha ama kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari kujivua tuhuma hizo. Hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi wa juu wa chama hicho ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti.

Hatua ambayo ilikuwa kwa kiasi fulani ikionyesha dalili za mafaniko hadi mwaka 2009 zilipolazimika kutuwama ambapo kwa mara ya kwanza kilipata mwenyekiti wa kwanza wa zaidi ya muhula mmoja tofauti na ilivyokuwa hapo awali kwa Mwanzilishi Mzee Mtei (Mkristo na mchaga) na baadaye Mzee Makani (Muislamu na Msukuma).

Katika uchaguzi wa mwaka 2009, Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe (Mkristo na Mchaga) kwa kutumia mbinu kadhaa alifanikiwa kuhalalishwa kuwa kiongozi wa chama hicho kwa kipindi cha pili mfululizo na hivyo kukiuka busara ya mabadiliko ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakihakikisha mwamko mpya(rejuvenation) wa kichama kila baada ya miaka michache.

Mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi wa juu yaliweza kutoa nafasi kwa chama kupanuka na kuondoa kiwingu kuwa chama hiki ni chama cha watanzania wa kabila la Uchaga na wengine ni wasindikizaji tu tofauti na wenzao wa CUF.

Uamuzi huu ulitibua nafasi ya chama hicho kuthibitishia kwa vitendo upotofu wa tuhuma za maadui zake na zaidi umma wa watanzania kuwa sio chama cha kikabila. CHADEMA ikashindwa kujiondoa katika tuhuma hizo na zaidi kujivika rasmi gamba la ukabila na udini mbele ya macho ya walio maadui na hata baadhi ya marafiki wakiwemo wanachama na wafuasi wake.

Kama vile hilo halitoshi, tukielekea katika uchaguzi wa rais na wabunge wa mwaka 2010 ambao CHADEMA ilionyesha muamko mkubwa katika medani za siasa nchini, CHADEMA ama kwa kudhamiria, kutokudhamiria au kwa kulazimika, wakafanya kosa jingine ambalo badala ya kuwanasua katika kiwingu cha ukabila na udini wakajikuta wanajisimika ndani ya wingu la Udini.

Ni ukweli ulio wazi kuwa kwa wa miaka kadhaa, wanamikakati wa CHADEMA wamekuwa wakitamani uungwaji mkono wa Kanisa la Katoliki ambao hadi miaka ya karibuni ulikuwa kama ngome muhimu ya kisiasa kwa CCM. Kwa CHADEMA kupata angalao chembe tu ya uungwaji mkono huo wa kanisa la katoliki katika chama chao ambacho wakati waislamu wamekuwa wakikiona kama chama cha waksrito zaidi, wakatoliki wamekuwa wakikiona kama chama cha Walutheri zaidi ilikuwa ni neema ya moto.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, kwa kiasi fulani CHADEMA ilifanikiwa kupata uungwaji mkono wa kanisa la katoliki kama mfumo imara wa kijamii na kisiasa katika nchi yetu. Hili lilikuja ama kutokana na kanisa hilo kama watanzania wengine kuchukizwa na maovu na usaliti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) au kutokana na dalili za uwezekano wa ushindi wa uhakika wa mgombea Urais wa CHADEMA ambaye ni kiongozi wa kiroho na aliyekuwa mtumishi wa ngazi za juu wa chombo nyeti cha kanisa hilo.

Kitendo cha viongozi wa kanisa la Katoliki kuanzisha na kuendeleza mpambano mkali wa majukwaani na katika alteri za kanisa kuwashutumu viongozi wa chama tawala cha CCM na serikali yake inayoongozwa na Rais na Mwenyekiti Muislamu, kabla na hata wakati wa uchaguzi huo kilijenga mtazamo wa kuwa kanisa hilo na hivyo wafuasi wake walipaswa kuiepuka CCM na wagombea wake na hivyo kuashiria kuwa CHADEMA ndio chaguo lao.

Hali hii ilileta mpasuko mkubwa wa kimitazamo katika kuelekea uchaguzi huo na hata baadhi ya wanasiasa, viongozi wa makanisa na misikiti na wapiga debe mbalimbali kuthubutu kuendeleza kampeni za udini. Kampeni zilizolenga ama katika kuhakikisha ushindi wa kutwaa nguvu za dola kwa upande wa CHADEMA na kulinda hatamu ya nguvu hizo kwa upande wa CCM.

Wakati hali hii kwa kiasi fulani iliwezesha kuongeza mafanikio ya CHADEMA katika uchaguzi wa ubunge na hata kura za urais, hali hii ilifanikiwa kusimika rasmi gamba la Udini dhidi ya CHADEMA. Kwa lunga nyingine uchaguzi wa mwaka 2010 kwa upande mmoja ulibariki CHADEMA kama chama cha ushindi kuelekea mwaka 2015 na wakati huohuo kukivika gamba la udini chama hicho ambalo ni kikwazo kwa kutimilika kwa baraka hiyo ya ushindi.

Ni katika muktadha huu wa nyota ya ubarikio wa ushindi kwa upande mmoja na gamba la dalili za laana kwa upande mwengine pamoja na matukio kadhaa tangia baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 ndio nalazimika kujenga mtazamo kuwa CHADEMA itashinda mbele kwa kushindwa hivi sasa.

Nasema hivyo kwa kuwa naamini kama ambavyo CCM walivyokumbwa na janga la kusarandiwa, kuvamiwa na baadaye kutekwa na mafisadi, CHADEMA ya sasa sio tu imekuwa kimbilio la wajanjawajanja wanaoamini kuwa katika mtaji wa chuki kuu inayokikumba CCM miongoni mwa watanzania wanaohisi kuwa wamesalitiwa lakini pia wanaoamini kuwa ushindi wao katika duru za siasa na uchumi unahakikishwa zaidi katika CHADEMA.

CHADEMA inageuka kutoka kuwa ngome ya mapambano ya demokrasia na upingaji wa maovu dhidi ya wananchi na taifa lao na kuelekea kuwa ngome ya mafanikio ya urahisi na uhakika kisiasa na kiuchumi.

Hali hii inakifanya CHADEMA kama chama kushindwa kupata nafasi ya kujichunguza na kujitambua na pia kuwa na wanaCHADEMA wakiwemo baadhi ya viongozi wake ambao wako tayari zaidi kujidanganya na kukimbilia kukumbatia siasa hovyohovyo na za hatari kwao binafsi na kwa taifa.Siasa ambazo wanaamini ndizo zinazowavutia zaidi watanzania waliochoka na CCM na kamwe haziwezi kuwageuka.

Kitendo cha viongozi wa chama kuthubutu kumteka na kumburuza kiongozi wa serikali kinafanya wengi wajiulize maswali kama kweli chama hiki ndicho kinapaswa kuwa chama tawala mbadala. Lakini zaidi kitendo cha viongozi wa chama ambacho kinakabiliwa na tuhuma ya udini kumdhalilisha Mwanamama wa Kiislamu kwa kumvua hijabu yake kinaonyesha jinsi gani chama hicho kilivyoingiliwa na watu ambao kwa idiadi yawezekana wakawa mtaji wa kisiasa lakini kwa kimantiki ni mzigo hatari.

Mbaya zaidi badala ya kuangalia ni jinsi gani wanaweza kulisawazisha kosa hilo kubwa kisiasa, wanatokea viongozi wakuu wa chama hicho na kutoa matamsha kama vile mwanamama yule alijitakia kukumbwa na udhalilishaji huo na hata wengine kujaribu kufananisha kitendo hicho cha kihuni na juhudi za viongozi adhimu kama Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Madiba Mandela. Kama ambavyo mbunge wa CHADEMA Bwana Tundu Lissu alivyoripotiwa katika magazeti akisema.

Ni wazi kuwa wakati CHADEMA kama chama kinaonyesha kukua kwa kupata wafuasi, washabiki na hata wanachama lukuki, ukuaji huu sio ukuaji wa kuaminika.
Ni ukuaji unaotokana na ubaya wa CCM zaidi ya uzuri wa CHADEMA.

Ni ukuaji ambao unaoetegemea kufaidika na makosa ya CCM na wengine zaidi ya ukuaji wa kufaidika na mikakati madhubuti yenye kujengwa katika misingi imara itakayohimili dharuba na tufani za kisiasa.

Ni ukuaji unaopalia makaa moto wa kujimaliza kuliko ule wa kupanda mbegu za matunda ya kudumu.

Ukweli ni kuwa wakati ushindi wa CHADEMA katika uchaguzi wa Igunga utapelekea viongozi wa aina hii wa CHADEMA na wafuasi wake wengi wenye mitazamo kama ya viongozi hao kuona kuwa siasa za aina hiyo zinalipa na hazina athari kwao, kushindwa katika uchaguzi huu kwaweza kuwa nafasi adimu kwa viongozi wa chama hiki kupata ushujaa wa kukaa chini kujiangalia na kuwa na uthubutu wa kujisahihisha kabla ya ama kukutana na tufani ya kisiasa huko mbeleni au kulifikisha taifa pabaya.

Wenzao wa CCM pamoja na makosa mengi wamekuwa wakiyafanya, kimbuka kidogo cha mwaka 2010 kimewaamsha, kujiangalia na kukubali kujisahihisha kwa njia ya kujivua gamba la ufisadi. CHADEMA kwa upande wake wanapaswa kutikiswa na kaupepo cha kisiasa huko Igunga ili kukubali kujiangalia na kuanza mikakati thabiti ya kujivua magamba ya ukabila na udini ambayo ni hatari zaidi kwake na kwa jamii na taifa letu kwa ujumla zaidi ya lile la ufisadi la CCM.

Lakini zaidi kushindwa kwa CHADEMA sasa kutawezesha uongozi wake na zaidi washabiki wao kuwashinikiza kujisahihisha na kuanza kufikiri na kutenda katika taathira ya hulka ya Serikali Mbadala (Government in waiting) inayosubiri kuongoza taifa hilihili ambalo matendo yao ya sasa yanaelekea kuliharibu.

Kushindwa kwa CHADEMA sasa ni kushinda kwa CHADEMA huko mbeleni.

1 comment:

Anonymous said...

It takes a wolf to fight a wolf. A sheep can never fight a wolf. CCM ndo vinara wa siasa chafu hivyo usitegemee CHADEMA wacheze siasa safi.