@1st Sept 2011
Nashindwa kuelewa kama serikali ya CCM hapo mwanzoni ilikuwa na nia ya kuanzisha mahakama ya Kadhi hadi pale viongozi na asasi za "kanisa" walipokuja juu dhidi yake na kupelekea kutikiswa kwa mtaji wake katika soko la kura, iweje leo tujidanganye kuwa uamuzi wa serikali haukushawishiwa ama kushuritishwa na kanisa!
Lakini pia wakati naamini katika busara za kukubali hoja hii kwa maslahi ya utanzania wetu, nashindwa kuelewa hii hoja ya kuwa kodi ya mtanzania haiwezi kutumika kuendesha mahakama ya Kadhi.
Iweje isiwe sawa kutoa kodi hizo kwa asasi za dini wakati tayari tumekuwa na tunaendelea kufanya hilo kwa kusaidia mabilioni ya kodi hizo kwa asasi na mashirika ya kidini?
Nimewahi kusikia kuwa mara baada ya Rais kushinda uchaguzi ambao inaaminika kuwa uliathiriwa na msimamo hasi wa "kanisa" dhidi ya serikali na CCM, serikali imeahidi ama kutoa zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa mashirika na asasi kadhaa za "kanisa".
Nashindwa pia kuelewa ni vipi kodi ya mtanzania haipo kwa ajili ya maslahi ya watanzania wakati waislamu ni sehemu ya watanzania?
Na pia ni utanzania gani tunaoujenga kwa kudai kuwa ni haramu kwa kodi ya David kutumika kwa maslahi ya Omar?
Naamini kuwa msimamo huu unaweza kuwa hafueni ama ushindi kwa mtizamo wa watanzania wa upande mmoja lakini kuongeza malalamiko na hisia hasi upande mwengine. Lakini pia ni muhimu kutambua kuwa wakati wale wa upande mmoja wanadhani kuwa hotuba hii ya Rais imeonyesha uthabiti ambao wengi tunapenda kuuona unaongoza asasi hii nyeti ya Uongozi, wapo wa upande mwengine ambao watachukulia hotuba hii kama ulegelege wa kukubali kushindwa na nguvu za upande mwengine na sio kwa busara za kulinda utaifa wetu.
Ukweli ni kuwa mzizi wa tatizo hili ni ujanjaujanja uliotumika kuliingiza suala hili la mahakama ya Kadhi katika ilani ya CCM ambayo ililenga kuidhibiti CUF katika soko la kura.
Na sasa nahofia msimamo wa sasa wa serikali ya CCM ni kujaribu kuidhibiti CHADEMA katika soko la kura la 2015.
Ni wazi pia kuwa ubinafsi na ujanjaujanja wa baadhi ya wanasiasa, wasomi na zaidi viongozi wa dini ulifanikiwa katika kubomoa hoja hii ya mahakama ya kadhi na kuijengea mazingira ya uadui kati yetu badala ya kuijenga kama chachu ya upendo kati yetu.
Hii imetokana na hulka ya ushindani na propaganda hasi iliyogubika mjadala mzima wa mahakama ya Kadhi kama ilivyokuwa ukiendelea bungeni, katika vyombo vya habari, katika kampeni, misikitini na makanisani, vijiweni na hata majumbani mwetu.
Wakati waislamu waliongea kwa mtazamo wa haki yao na hisia za kubaguliwa na mfumo, wakristo walijikita zaidi "ubaya" na nia mbaya ya Mahakama ya Kadhi.
Wengi wao walikwepa kuongelea yaliyomo katika mchakato mswada wa sheria ya kuendesha mhakama hiyo na sehemu ya katiba katika suala hilo.
Kwa mtazamo wangu hutuba hii ni kipenga cha kuanzisha rasmu mjadala huu na sio kuhitimishwa.
Mwisho naamini kuwa hii ni sehemu ya changamoto ambazo kama taifa linaloendela tumekuwa na tunapaswa kupitia ili kukomaa kidemokrasia.
Muhimu ni kuendeleza utamaduni wa shauku ya kutaka kujua mambo kwa undani wake zaidi ya propaganda za viongozi wawe wa kisiasa ama kijamii na wajenga maoni wetu, kuvumiliana na pengine kuaminiana kwamba wote tuna nianjema katika kujenga tanzanianjema.
No comments:
Post a Comment