UFISADI KUSHIKA HATAMU?


UFISADI KUSHIKA HATAMU?
Ilyas, O.S

Ni muda mrefu sasa nimekuwa na mtazamo kuwa baada ya kuondokana na mfumo wa chama kushika hatamu, kuna mchakato umekuwa ukiandelezwa na wajanja kadhaa katika nchi yetu wenye nia ya kujenga mfumo mpya ambao ninaita MFUMO FISADI.

Matokeo na mchakato wa uchaguzi wa ndani unaolekea kkufika tamati katika Chama cha Mapinduzi una kila dalili za kufikia hatua ya juu ya mchakato huu wa ujenzi wa MFUMO FISADI kwa kufanikisha kusimika rasmi uhodhi wa chama hicho mikononi mwa vinara na makuwadi ama mawakala wa mfumo huo na hivyo kuwezesha kuhatamisha mfumo huo katika uongozi wa taifa letu.

MFUMO FISADI ni mfumo wenye nia ya kurasimisha na kuhalalisha mambo ambayo ni kunyume kabisa na misingi ya utaifa wetu kama ambavyo ilijengwa na kuachwa na Baba wa taifa letu Mwalimu Nyerere na wafuasi wake adhimu kuanzia alipokuwa TANU na baadaye CCM.

Ni mfumo ambao umekuwa ukijengwa ama kujengeka katika sura mbalimbali kama vile kujenga mfumo wa soko huria, kuendana na uhalisia na usasa wa kukubali kuwa hatuna ujanja isipokuwa kukumbatia misingi ya kibepari, umuhimu wa kujenga tabaka la kati, siasa za ushindani na kadhalika.

Wengi wetu kama si wote kwa namna moja ama nyingine tumeshiriki katika harakati hizi za kujenga MFUMO FISADI.  Ushiriki wetu upo katika ama katika kupanga ama kutekeleza mikakati yake kwa kujua ama kutokujua, kuhalalisha mambo yake kwa kutetea ama kuhalalisha chembechembe za ufisadi, kuwawezesha kiuchumi na kisiasa wale vinara na mawakala wa ujenzi wa MFUMO FISADI na vinginevyo.

Naomba niweke wazi kabla sijaingia ndani katika kuchambua na kuelezea mtazamo wangu kuhusu hili la ujenzi wa MFUMO FISADI na hatari tunayokumbana nayo sasa ambapo yawezekana tukawa katika hatua za mwisho katika kuusimika mfumo huu katika hatamu za nchi yetu.

MFUMO FISADI hauna chama wala wanachama. MFUMO FISADI hauna dini hii ama ile. MFUMO FISADI hauna kabila hili ama lile. MFUMO FISADI hauna rika hili ama lile. MFUMO FISADI hauna sekta moja ama nyingine. MFUMO FISADI hauna tabaka hili wala lile. MFUMO FISADI unaratibiwa, kujengwa na kulindwa na vyama vyote, sekta zote, dini zote, makabila yote, marika yote,matabaka yote na makundi mengine.

Kwa leo nitaongelea mfumo huu haramu katika muktadha wa kinachoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho hivi karibuni tumekuwa tukisikia na kuona mengi yakitokea na kusemwa katika mchakato wa chaguzi za ndani za chama hicho. Chama ambacho hadi sasa ndio chama tawala.

Moja ya kitu ambacho kimegeuka kama ndio kioo cha kupima mafanikio ama athari za uchaguzi huu kimekuwa ni jinsi gani nguvu ya pesa imeweza kuonyesha makucha yake katika uchaguzi huu.

Wengi tumekuwa tukiuangalia, kuupima na kuchanganua uchaguzi huu kama ni kioo cha kupima nani atakuwa mgombea na wengine hata kuamini kuwa ndiye atakayekuwa Rais ajaye.

Wengi tumekuwa tukiuangalia uchaguzi huu kama ishara ya ama kukirudisha chama katika mstari ama kukiacha kiteketee kwa kukitunuku rasmi kwa wale wanaonekana ama kujipambanua kama vinara na makuwadi wakuu wa ujenzi wa MFUMO FISADI.

Kwa kiasi fulani kuna ukweli wake, kwani kuna wengi ama wamegombea, wamechagua ama wamechaguliwa kutokana na kushawishiwa, kuwezeshwa ama kuahidiwa neema na ama wapambe au vigogo wenye kuamini kuwa wakishashinda ndani ya CCM basi Urais wa 2015 ni wao na kwamba ulaji utakaokuja nao utakuwa wao wa kugawana.

Hali hii inasikitisha na kutisha sana kwa mustakabali wa taifa letu. Inatia uchungu na kukatisha tamaa kwa mzalendo yeyote yule awe mwanachama wa chama hiki na hata yule ambaye sio mwanachama wake lakini anatambua umuhimu wa chama hiki kwa taifa letu haswa wakati huu wa miparaganyiko lukuki.

Harakati za kujenga MFUMO FISADI zimelenga katika kuwaangusha na kuwakatisha tamaa wale wote waliokiunga mkono chama cha CCM kutokana na Misingi yake imara ya kuweka mbele UTU wetu na kukiaacha chama mikononi mwa wale walioweka mbele IMANI YA NGUVU ZA FEDHA.

Wakati mwengine huwa najenga fikra kuwa yawezekana nguvu za harakati hizi za vinara na makuwadi wa ujenzi wa MFUMO FISADI ndani ya CCM zinatokana na nia ya dhati ya kukiondoa madarakani chama hiki. Kwao wao na wakubwa zao wanakiona chama hiki chenye misingi na historia adhimu ya utu, usawa na ukombozi wa ndani na nje ya mipaka yetu ni kama kizingiti dhidi ya nia yao ya kuhatamisha mfumo fisadi kwa jina la Ubepari.

Yawezekana, na inajionyesha wazi kuwa vinara na mawakala wa MFUMO FISADI huu ambao wengi tayari wana mahusiano maalum na vyama mbadala katika kinyang’anyiro cha utawala wa nchi, nia yao hasa sio kuhodhi madaraka ya chama hiki bali kukivunjilia mbali na baadaye kutumia vyama vyenye misingi ya kibepari ambavyo sasa vimevaa ngozi za hisia za kijamaa katika mpango kabambe wa kusimika rasmi MFUMO FISADI katika hatamu za utawala wa taifa letu.

Na hapa ndipo ninaona kuna tatizo kuu ya jinsi baadhi ya wanaojitambulisha kama wapambanaji dhidi ya ujenzi wa MFUMO FISADI wanakosea katika mapambano yao. Wengi wa wapambanji hawa, wa ndani na nje ya CCM, wamekuwa wakijikita zaidi katika mkakati wa kupanga safu za uongozi wa chama dhidi ya washindani wao ndani ya chama kama maandalizi ya mpambano mkuu ujao wa kumpata mgombea wa Urais kupitia chama chao.

Kwa kuweka mbele ushindani huu unaotegemea sana wa nguvu za fedha na sio imani ya wanachama kwa chama na viongozi wao kundi hili la wana CCM limeweza kujenga mazingira ambayo maadui ama washindani wao katika sakata la uhodhi wa chama wamepata urahisi wa kipropaganda na kimkakati.
Matokeo yake hata hao wenye kujipambanua kama CCM-Misingi ambao wakati fulani walijulikana kama MTANDAO MATUMAINI wanalazimika katika kuamini katika nguvu za fedha ili kupambana na washindani wao wa kundi la MTANDAO MASLAHI ambao kwao wao nguvu za fedha ndio msingi mkuu wa mafanikio yoyote.

Na hapa ndipo tunapokuja katika tatizo lingine katika hizi juhudi za kupambana na harakati za MFUMO FISADI ambazo kama mambo hayajabadilika sasa na sio baadaye basi ni wazi zitafanikiwa katika kushika hatamu za taifa letu.

Kitendo cha wana CCM wengine na hasa wale ninaowaita CCM ASILIA, yaani wana CCM wenye kuamini katika misingi ya chama na utaifa wetu, kuwaachia “WANAMTANDAO” kupambana wenyewe kwa wenyewe ni kosa kubwa linaloendelea ambalo nalo limewezesha ujenzi wa MFUMO FISADI na uwezekano wa mfumo huo kushika hatamu.

Mapambano ya dhati ya kukikomboa chama hiki ambacho kwa mtazamo wangu ni kuwa hadi sasa kimekosa mbadala makini wa kukibadili na kutegemea ukombozi wa kweli hayatafanikiwa kwa kuwaacha wanamtandao wenyewe kwa wenyewe kuhodhi uwanda wa mapambano.

Zaidi kuna uwezekano mkubwa wa hao tunaoamini kuwa wanapambana dhidi ya wingu la vinara na mawakala wa MFUMO FISADI kutoka katika kundi la MTANDAO MATUMAINI wakaishia kukubali kushindwa na kujiunga na timu ya ushindi ya wenzao. Tukumbuke kuwa hawa kwa pamoja walishirikiana katika kuendesha mapinduzi ya ndani ya chama hapo kabla na hivyo kuweka msingi wa ujenzi wa mfumo fisadi. Wakati wao wameamua kujitenga na jitihada za kujenga mfumo fisadi. Wenzao wa MTANDAO MASLAHI kwa nguvu zote wameamua kuubeba hadi watakapofanikiwa kuuhatamisha katika siasa na uongozi wa nchi yetu.

Mapambano ya dhati na yanayoweza kuirudisha CCM katika mstari na kukilinda dhidi ya nia mbaya za vinara na wapambe wa MFUMO FISADI ni yale yatakayojikita katika ajenda za DIRA, MISINGI na ITIKADI ya chama na sio vinginevyo.

Na hapa ndipo wana CCM, Wazee kwa Vijana wenye kuamini katika umuhimu wa dira, misingi na itikadi za chama hicho na taifa letu wanakuwa na umuhimu wake kwani ni wao tu na sio wengineo ndio watakaoweza kubadili mwenendo wa mpambano huu na hatima ya chama chao na taifa letu.

Ndani ya kiwingu cha habari mbaya za ushindi wa nguvu za fedha katika chaguzi hizi, pia kuna habari njema kiasi. Tofauti na chaguzi zilizopita, katika chaguzi hizi wapo baadhi ya wagombea waliofanikiwa kushinda hivi sasa ambao hapo nyuma walishindwa katika kila chaguzi walizokuwa wakishiriki kutokana na “ushamba” wao wa kutokuamini katika nguvu za fedha na kujikita katika kampeni za misingi na tamaduni za chama.

Ushindi wa hawa ambao wanaweza kuwa kidogo lakini wenye umuhimu unaonyesha matumaini na uwezekano wa nguvu za MISINGI ndani ya chama hiki na kutoa ujumbe kuwa hii kansa ya nguvu za fedha haijakikumba chama kizima. Hivyo endapo wengi zaidi wa aina hiyo wakiamua kusimama na kupambana, bado kuna uwezekano wa mpambano wa kuzuia uhodhi na hatimaye uwezekano wa Ufisadi kushika hatamu kufanikiwa kwa manufaa ya chama chao na taifa letu.

Ni mapambano yaliyojikita katika nguvu za misingi tu na sio nguvu za fedha ndio yatakayotuepusha na tishio la UFISADI KUSHIKA HATAMU na madhara yake mengineo. Tishio ambalo kuna uwezekano mkubwa wa kurasimishwa rasmi hivi karibuni tunapoelekea katika tamati ya chaguzi za ndani za CCM. Na kama ikishindikana kuzuia tishio hilo sasa basi wote kwa pamoja tujiandae na hasira za wapiga kura ambao wanaonyesha kila dalili za kukumbatia fikra ya “bora mbadala na liwalo na liwe” kama fimbo yao kwa wasaliti wa imani yao waliyoitunuku kwa miaka mingi ndani ya CCM.

Mwandishi ni Mkurugenzi wa kampuni ya ushauri wa masuala ya siasa, uongozi na maendeleo inayoitwa TANZANIANJEMA ADVISORY. Anapatikana omar.ilyas@tanzanianjema.com, www.omarilyas.com, twitter; @omarilyas