Mkataa asili hubaki kuwa mtumwa wa asili!
Vyama vya siasa kama yalivyo makundi mengine huwa vinakuwa
na asili yake hata kabla ya kuwa vyama rasmi. Kuna wanaoamini kuwa hakuna
dhambi ya asili ingawa usipokuwa makini asili inaweza kuwa jinamizi na hata
msingi mkuu wa maendeleo yako. Mimi nakubaliana nao kwa kiasi fulani na ndio
maana naamini kuwa badala ya kushindana kukana asili ya chama fulani ni vizuri
na muhimu kwa maendeleo ya muda mrefu kisiasa kujitambua na kukubali asili ili
kuweza kuiwekea mazingira ya kuhakisha kuwa asili hiyo inakuwa mtaji bora na
sio mzigo wa miba.
Mfano ni asili ya CCM ambayo ni kikundi cha kupigania
maslahi cha watu wa waliojinasibu kama waungwana wa Mzizima. Wao walikuwa
wepesi kung’amua hasara ya kukataa asili yao. Hata katika enzi hizi daima
inapoelezewa historia ya CCM, asili yake kama kikundi cha wachache cha maslahi
ya kijamii kama ilivyokuwa katika enzi za TAA hutambuliwa na hata kuenziwa. Na
asili ya CCM ina pande mbili. Pia kuna ya upande wa Zanzibar ambako nako asili ya
ASP ilikuwa makundi mawili ya maslahi ya kijamii ambayo yalikuwa kundi la
Wazanzibari wenye asili ya Bara yaani waafrika na wengine wenye asili ya
Ushirazi.
Kwa upande mwengine wa kisiasa huko Zanzibar kulikuwa na
vyama vya ZPPP ambacho hadi mwisho wake kilibaki kuwa kundi la maslahi ya
kijamii katika siasa na ZNP ambacho ingawa asili yake ilikuwa ni kundi la
maslahi ya kijamii kiliweza kujijenga kuwa chama cha makundi mbalimbali kabla
ya kurudi nyuma kilipokaribia kuchukua madaraka kwa maslahi ya kundi la kijamii
kuibuka na kuhodhi chama hicho tena na kulazimu Mapinduzi ya 1964 ambayo
yalikisambaratisha hadi baadaye mabaki ya kundi hili yalipoweza kuungana na
kundi maslahi la jamii nyingine na kuibuka kama CUF.
Upeo na uthubutu wa viongozi wa Tanganyika African
Association kwa upande wa Tanganyika na African Association na Shirazi
Association kwa upande wa Zanzibar na baadae TANU na ASP kutambua zaidi umuhimu
wa kuunganisha makundi maslahi ya kijamii na kitaifa na kuunda CCM ndio moja ya
misingi ya uthabiti wa CCM hadi sasa. Uthubutu wa kutambua madhara ya jinamizi
la uasili hapo kabla umeweza kuwajngea msingi imara CCM na kuweza kupambana na
jitihada zozote za washindani wao sasa kujaribu kutumia siasa za maslahi ya
kijamii dhidi yao.
Huku bara nako kulikuwa na makundi mengine ya maslahi ya
kijamii ambayo yaligeuka kuwa maslahi ya kisiasa lakini nayo yalisambaratishwa
na nguvu za Mwalimu Nyerere na TANU. Kusambaratishwa kwa makundi maslahi yenye
mlengo wa maslahi ya kundi fulani la kijamii zaidi ya utaifa hakukuwa na maana
kuwa fikra ama mitandao ya siasa zenye mlengo wa maslahi ya makundi ya kijamii
zilikwisha. Harakati za chinichini kwa chini ziliandelea na utamaduni wa
maslahi siasa za maslahi ya makundi jamii kama dini, kabila ama eneo
yaliendelea katika mifumo isiyo rasmi kama ilivyo mifumo ya biashara zisizo
rasmi ambayo yawezekana ikawa haramu kifikra, kiitikadi ama hata kisheria
lakini mifumo hiyo ikaendelea kuwepo na hata kustawi kutokana na uhalali wa
kijamii.
Na hapa ndipo inapokuja asili ya CHADEMA ambayo
inasemekana ilikuwa ni vuguvugu la kupigania, kulinda na kuendeleza maslahi ya
kabila fulani. Yasemekana, na hili nimelifanyia uchunguzi kiasi kabla ya
kulitilia maanani na natambua kuwa bado sijapata undani zaidi, asili ya CHADEMA
ilikuwa ni kundi la vizito flani wanaotoka katika kabila moja ambao walianzisha
kundi liloitwa ambalo lililenga kutetea maslahi ya kijamii, kiuchumi na hata
kisiasa ya waanzilishi kwa kupitia kabila lao. Kundinhili lilijulikana kama
Chaga Development Association. Ni wazi kama yalivyo makundi mengine ya maslahi
ya kijamii kundi hili halikuwa na uhalali wa watu wote wa kabila hilo na ukweli
ni kuwa lilikuwa kundi la wateule kadhaa ambao kwa mtazamo wao ilikuwa ni sawa
na muhimu kwao wao kuwapigania wenzao kwa mfumo huo.
Lilipokuja vuguvugu la vyama vingi baadhi ya wateule wa
kundi hili walikuwemo katika mstari wa mbele wa vuguvugu hilo ambapo baadae
iliporuhusiwa kuanzishwa vyama vingi vya kisiasa, katika mijadala ya mwanzoni,
mtandao wa mageuzi ya kisiasa ambao ulikuwa na watanzania wa kila aina uliafiki
kuwa jina la CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO litumike kuanzisha chama cha
pamoja. Kilichofuata ni sarakasi ambazo kwa mtazamo wangu ilikuwa ni makosa
makubwa ambayo hadi sasa yanakisumbua chama cha CHADEMA. Wateule kadhaa ambao
waliamini kuwa jina hilo halipaswi kutumiwa na kundi ambalo hawana uhakika wa
kuendeleza malengo asili ya kundi lao na kudhani kuwa asili hiyo inapaswa
kuenziwa katika mkakati mpya kutokana na mazingira mapya, waliwahi kwa msajili
wa vyama na kusajili chama chao pekee huku wakiwatenga wenzao ambao walikuwa
pamoja katika harakati za mageuzi kitu ambacho kilipekea kutumika kwa jina la
NCCR badala ya CDM kama ilivyokubaliwa kwa pamoja hapo kabla.
Jinamizi la ujanja huu ndio linalokisumbua CHADEMA hadi
sasa wakati kikionekana kinapata mafanikio kadhaa. Wakati vyama vingine
viliweza kujitambua na kuona mbali kuhusiana na asili ya vyama vyao na
kuhakikisha kuwa badala ya kuukwepa ukweli huo wanautambua na kuutumia kama
somo la kisiasa, CHADEMA wao hadi sasa wameng'ana vinginevyo. Wameamua kuukana
na kuukandamiza ukweli huo. Kwa mtazamo wangu hili limewapelekea kujikosesha
nafasi ya kuzika jinamizi hilo kwa uwazi na udhati. Asili haipaswi kuwa kioo
cha maendeleo lakini yaweza kuwa msingi mkubwa wa maendeleo. Yawe maendeleo
chanya ama maendeleo hasi. Jinsi gani unaipambanua asili hiyo ndiyo inapelekea
aina ya maendeleo yanayoathiriwa na asili.
Ni wazi kuwa kutokuweza kuruhusu uwazi kuhusiana na asili
ya CHADEMA, iwe jina ama ajenda asilia, kunakifanya chama hicho kuwa vulnerable
katika mashambulizi ya nje lakini pia mashindano ya siasa za ndani za chama
pia. Kukataa asili hiyo hakuna maana hakutakuwa na wachache ambao wanaendelea
kutumia asili hiyo kwa faida yao wawe maadui nje ama wa ndani au asili hiyo
kutumika na wateule kadhaa kufanikisha jitihada zao za kuhodhi ushawishi wa
kisiasa na kimaslahi katika maendeleo ya chama hicho na siasa za nchi. Haya
hayawezi kuepukika hadi pale kutakapokuwa na utayari ya kutambua asili hiyo kwa
uwazi, bila ya kujiona ni wakosa na kukubaliana kwa pamoja juu ya mikakati
rasmi ya kuhakikisha asili hiyo haikwazi maendeleo ya chama hicho hasa
kuhusiana na haiba yake mbele ya jamii zingine.
Hisia na wala harakati za wale wenye kuamini
katika ajenda asilia hazitaisha kwa kuendeleza utaratibu wa kubadili uongozi
kila baada ya kipindi cha uongozi mmoja kwisha ambao hapo kabla ulisaidia
CHADEMA kuibuka kisiasa kitu ambacho hivi sasa wamekuwa wanaonekana kukidharau
ama kukiogopa. Lakini ni wazi utamaduni huo kama ungeendelezwa ungeweza
kupunguza mazingira ya kulistawisha suala la hisia za ukabila ama maslahi
asilia. Naamini kuwa kwa faida ya CHADEMA lakini zaidi kwa faida ya nchi yetu na
kutuepusha kubaya zaidi tunakoelekea, muungano wa CHADEMA na CUF ni muhimu sana
ingawa wengi wanaona hilo kama ni ndoto tu kutokana na kutambua nguvu za
maslahi ya makundi ya kijamii katika vyama vyote hivyo ingawa wasengependa
suala hilo kuongelewa kwa uwazi.
Ieleweke kuwa siamini kuwa hadi sasa CHADEMA ni chama cha
ukabila. Ni wazi agenda rasmi ya CHADEMA kama chama cha siasa chenye uhitaji wa
kukubalika kitaifa haiwezi kuwa maslahi ya ukabila. Lakini hiyo haiondoi ukweli
kuwa nguvu za maslahi ya kijamii ambayo ndio yalikuwa ajenda asilia zinaweza
kuendelea kuathiri maendeleo ya chama hicho. Hiyo inaweza kutokana na kuendelea
kwa fikra asili miongoni mwa baadhi ya wateulena ambazo zikaendelea kuwa na
nguvu kiasi fulani ama mtazamo wa watu dhidi ya chama hicho kutokana na asili
yake hiyo ambayo imeweza kuathiri haiba ya chama hicho hasa kutokana na
kushindwa kulikabili zimwi la uasili kwa uwazi na upana wake.
Chukulia mfano wa suala la uongozi wa chama hicho. Angalia
zile harakati za kumrithi Mzee Mtei ambapo kulikuwa na jitihada nyingi za
kumrithisha Mzee Ndesamburo ambaye naye ni mmoja wa wa wa kabila hilo na
alikuwemo katika mkakati asili. Kilichotokea ni mgawanyiko mkubwa wa chama
baada ya kushinda Mzee Makani ambaye kwa wenye kuendeleza fikra za agenda
asilia walimuona kama wakuja na kufikia kukizira chama hadi pale kiliporudi
mikononi mwa mwenzao ambaye anaweza kuaminika, kuhalisia ama kihisia, kulinda
nafasi na maslahi ya agenda asilia.
Hili pia limethibitishwa na yaliyowatokea kina Mzee
Mchata, Mzee Ngululupi, Kaburu, Wangwe, Zitto na wengineo wengi walionekana
kutishia nafasi ya ajenda asili. Na haya yanaendelea hadi sasa katika harakati
za M4C ambazo ingawa zimewezesha kukitanua chama kwa maana ya idadi ya
wanaojiunga lakini kinaendelea kukigawanya chama hicho katika siasa za ndani.
Ni wazi kuwa kushindwa kulikabili janga la uasili kwa uwazi, udhati na uthabiti
kunaendelea kuwa kikwazo cha kuondokana na haiba ya maslahi jamii hata kama kuna
kutambua kuwa suala hilo linaathari yake kwa mipango ya kisiasa ya chama hicho.
Bila ya kulikabili jinamizi hili kwa uwazi na ushiriki mpana litaendea kuathiri
chama na siasa za nchi hata pale ambapo chama hiki kitakapoweza kufanikia
kukwapua madaraka kutoka kwa washindani wao.
Kuhusiana na kukubalika kwa CHADEMA katika
pande mbalimbali za nchi ama makundi mbalimbali ya kijamii hilo halina maana
kuwa athari za uasili hazipo ama hakuna wanaondeleza siasa za agenda asilia
kichinichini. Lakini pia unaposema kukubalika kwa maana ya kuwa chama hicho
kimeweza kupata viti vya kisiasa bila ya kuangalia factor zingine za kisiasa
katika maeneo hayo au idadi ya kukubalika kwa muktadha wa ujumla wa kura zote
za eneo tajwa, nadhani kaka unakosea. Ni wazi kuwa kupigiwa kura hakuna maana a
kukubalika pekee bali kunajengwa na sababu nyingi na hivyo kutoa maana nyingi.
Kwa mfano, ni wazi kuwa jimbo la Ausha na yale ya Mwanza yalienda CHADEMA sio
kwa sababu ya kukubalika kwa chama ama mgombea bali ni ushindani wa kisiasa na
kimaslahi ndani ya CCM. Tukumbuke, hisia za kisiasa zinaweza kuwa na mahusiano
ya hisia mbalimbali za kijamii, kisiasa na hata kiuchumi hivyo haziwezi
kutafsiriwa kwa muktadha mmoja tu.
Ukweli ni kuwa hizi siasa za maslahi ya makundi
jamii zipo hata CCM. Hivi sasa makundi ya kikabila, kimikoa, kidini, kimaeneo,
kikanda yanaendelea kushamiri ndani ya CCM. Tofauti ya CCM na vyama vingine ni
kuwa kwa CCM jinamizi hili lilitambuliwa na kushughulikiwa mapema hivyo kujenga
mfumo na utamaduni wa kisiasa ambao hakuna kundi lolote linaloweza kuhodhi
nafasi ama kwa kiasi kikubwa au kwa muda mrefu na hivyo kuweza kuhakikisha kuwa
hakuna kundi linalojiona wakuja ama wateule na ushindani wao unakuwa maintained
katika muktadha huo.
Kukimbilia kupiga kelele za ukabila kila
wanapotokea wenye uthubutu wa kuliweka suala hilo wazi, ama kwa faida ya
makundi mengine ama kwa faida ya siasa makini hakusaidii hatma ya chama na wala
hatma ya siasa zetu. Bila ya kutambua umuhimu wa mjadala wa wazi wa mambo
mbalimbali ya kweli ama ya hisia hakuna kikundi cha siasa ambacho kinaweza
kufanikiwa katika mazinira ya jamii, utaifa na siasa za Tanzania. CHADEMA na
vyama vingine kama CUF wanapaswa kuondokana na utumwa wa kukataa asili na ndipo
mwatakapoweza kuthubutu kuchukua hatua za dhati na madhubuti ya kuondokana na
jinamizi la asili! Jinamizi hili litaendelea kusinya na hata kudumaza maendeleo
ya kisiasa hadi pale watakapokuwa tayari kulizika rasmi kwa uwazi na
ushirikishi wa dhati wa makundi mengine kijamii.
Kuendelea kukandamiza mijadala ya suala hili kunaendeleza
hisia za kutokuamini haiba na malengo hasa ya chama hicho na pia kunatoa mwanya
kwa baadhi ya wanaojiona ni masalia ya wateule wa agenda asilia kuendelea
kuamini katika matumizi ya uasili huo kwa faida yao na wakati mwengine hata
chama chao lakini kwa upande mwengine kuendelea kukigharimu chama katika
muktadha wa maslahi ya muda mrefu. Hili nalo lipo kwa upande wa CUF ambayo
historia imeshawaonyesha jinsi gani jinamizi hilo linavyweza kuwa na faida ya
muda mfupi lakini hasara ya muda mrefu na bila ya kusahau MTIKILA na kundi lake
la siasa za wazawa dhidi ya wakuja zilipomfikisha.
No comments:
Post a Comment