Ujumbe mfupi kwa Godless Lema, M.B





Dear Lema


Unapojiandaa na ushahidi wako wa udini dhidi ya CCM kumbuka wapo wanaojiandaa na uhsahidi dhidi ya CHADEMA. Unapojiandaa na ushahidi wako dhidi ya Udini wa Viongozi waislam, kumbuka kuwa wapo wanaojiandaa na ushahidi dhidi ya Viongozi wakristo. Katika kujiandaa huko kuna wenye dhana na wenye uhalisia na kuna wenye vyote hivyo viwili. Dubwana hili la Udini halitaondoka kwa wewe kuwatuhumu wao na wao kukutuhumu wewe. Dubwana hili litaondoka kwa wao kujiangalia na kujitambua makosa yao na wewe kujiangalia na kutambua makosa yako/yenu. Kudhani kuwa CHADEMA itajisafisha na tuhuma za udini wa kikristo kwa kutuhumu CCM kwa udini wa kiislam, ni ama ujinga ama nia halisi sio kuupiga vita udini bali ni kuuendeleza na kuukuza udini huo ukiamini ndio njia ya kulinda na kupigania maslahi ya upande wako.


Kama nilivyowahi kusema hapo kabla anayedhani kuwa Kikwete ni mdini na ndiye mwanzilishi wa vuguvugu hili la udini hana tofauti na wanaodhani ama kuamini kuwa Nyerere alikuwa mdini na ndiye aliyepanda mbegu za udini huu. Kwangu mimi wote hawa ni wajinga. Simuoni Lema kama mdini lakini naamini ni mjinga na pia anasukumwa na dhambi zake katika kujaribu kujikosha kwa kuwashutumu wengine na kujaribu kuwanasabisha na ubaya wake. Hizi ni aina ya suluhu za mambo makubwa zinazoletwa na wale wenye upeo mdogo wa kisiasa, kihistoria na kiuongozi. Ni suluhu za aina ya siasa nyepesinyepesi zenye kulenga zaidi utashi wa siasa za matumbo zaidi ya siasa za maendeleo.


Udini kama ulivyo ukabila ni sehemu ya fikra za kijamii yetu. Tunachotofautiana sisi na mataifa mengine ni kuwa sisi kama Taifa tunaona udini na ukabila kama tatizo kubwa kuliko tatizo lingine lolote na katika historia ya ujenzi wa UTAIFA wetu hilo limewekewa kipaumbele. Ukweli kuwa hili limesaidia kutulinda na maafa mengi kama yaliyowafikia wenzetu wengine waliojaribu kuukubali na kuurasimisha udini na ukabila kama ni kitu cha kawaida. Naamini hadi sasa tuna mjadala huu kwa sababu tumeaminishwa katika utaifa wetu kuwa hili ni tatizo ambalo tunapaswa wakati wote kulikwepa na kulipiga vita.

Mpaka sasa watanzania tume-epushwa na janga la kupata kiongozi mdini ingawa tunapoelekea siasa hizi zitatufikisha mikononi mwa viongozi wenye hulka na kuendeshwa na fikra hizo. Hizi shutuma dhidi ya Mwalimu Nyerere na Rais Kikwete zinaendeshwa kwa hisia zaidi ya uhalisia. Ndio maana naamini kuwa kama kiongozi haupaswi kufanya siasa hizo bali unapaswa kufanya siasa makini, zenye kuonyesha weledi wa tatizo na zitakazoleta suluhu ya muda mrefu na sio ushindi wa muda mfupi wa upande mmoja utakaoleta maafa ya muda mrefu kwa pande zote.

Kinachoendelea sasa ni kukua na kuelekea kuota mizizi kwa fikra hizi na kupata uungwaji mkono wa baadhi ya viongozi wa kisiasa na kijamii ambao wako tayari kuzitumia fikra hizi kama mtaji wa siasa za kulinda maslahi ya kundi na ubinafsi wao au kuwa silaha dhidi ya maslahi ya kundi ama ubinafsi wa wengine. Kinachoendelea sasa ni kustawi kwa mazingira ya kukuwa kwa tatizo na kulegalega kwa uwezo wa kupambana nalo na hili ni zaidi ya mapungufu ya uongozi kama tuliozoea majibu mepesi tungelipenda kuamini, hii sehemu ya evolution ya siasa zetu za ndani na za kimataifa. Kujaribu kutuhumu kuwa mbegu za udini huu zimepandwa na kundi fulani ama mtu fulani ni propaganda za kisiasa, ufinyu wa kifikra na ujinga wa kimtazamo ambao unaweza kumsaidia mtu ama kundi moja kwa muda mfupi lakini kuwa hasara kwa wote kwa muda mrefu.

Kuhusu ya CUF na pia UAMSHO, CHADEMA na CCM, yote hayo yapo katika hali ya hisia na uhalisia. Kuna yanayosemwa na kuaminiwa kutokana na hisia tu na kuna ambayo yanatokana na uhalisia wa matendo ama muonekano wa baadhi ya wanachama ama kama chama. Matendo na muonekano ambao hushawishiwa na kujidanganya na kuamini kuwa kutumia siasa za udini ama ukabila katika harakati zao ama katika mapambano dhidi ya wengine kunawasaidia kuwahakikishia strong and viable political base ama wengine kuamini kuwa ni sehemu ya siasa. Na kama ambavyo nilivyowahi kusema hapo nyuma, baadhi ya hizi hisia zinajengwa kutokana na kuangalia sana nguvu za chama ama kundi fulani katika dini ama kabila fulani bila ya kupima hayo katika muktadha wa sababu halisi zilizopelekea hivyo kama vile historia ya chama ama kundi hilo.

Lakini kwa upande wangu, sikusita kushutumu tatizo hilo ndani ya CUF (UDINI NA UKABILA) enzi zile na sasa katika sura ya UAMSHO, au katika CHADEMA (UDINI NA UKABILA) na CCM (UDINI NA KUCHIPUKA KWA UKABILA PIA) kuanzia katika uchaguzi wa mwaka 2005 na zaidi 2010. Naamini ni muhimu kukemea pande zote kuliko kukekemea upande mwengine pekee kwani kufanya hilo ni ujinga, unafiki, uzandiki na kama nilivyosema, ni siasa nyepesi nyepesi.

Kujidai kupambana na UDINI kwa kushutumu wenzio tu na kukimbilia kuhalalisha yako kwa msingi kuwa eti wewe una-react tu kutokana na udini wa wengine, kama ilivyo upande wa Uislam na makabila madogo yanayoamini kuwa yana haki ya kuendesha udini na ukabila wao kama njia ya kupambana na udini na ukabila wa wengine, ni kuuendeleza na kuukuza Udini na sio njia muafaka ya kutatua tatizo hili.

Lakini vilevile naamini kuwa katika game hili la kutumia siasa hizi dhidi ya mwenzako, kati ya CUF na CHADEMA kwa upande mmoja na CCM kwa upande mwengine, ni CUF na CHADEMA ndio wenye urahisi wa kuathirika zaidi ya kufaidika na siasa hizi. Historia, ukomavu na utamaduni wa kisiasa ndani ya CCM unawasaidia sana katika kupunguza madhara ya siasa hizi kuliko hali ilivyo katika vyama vingine. Huo ni ukweli mchungu ambao washindani wa CCM mnapaswa kuutambua. Athari za siasa hizi ni kubwa na zenye uwekano mpana zaidi kuumiza CHADEMA na CUF kuliko CCM. Kwa CCm itawachubua tu, kwa CHADEMA na CUF itawadumaza na kuwaangamiza kisiasa.

Ndugu yangu Edward Kinabo anadai hili suala la ushahidi dhidi ya udini wa Rais Kikwete ni zigo la Lema. Naamini hapa na yeye anajidanganya. Hadi sasa wanasiasa waliowahi kutuhumu Udini wa CCM na Kikwete on the record ni Lema, Mchungaji Msigwa na Selasini. Hawa wote ni viongozi wa CHADEMA na wote hawa wamewahi kusikika wakitamka maneno ya chuki ama kuchochea udini. Lema ameyasema yake katika Uchaguzi, Selasini amesema yake wakati wa sakata la kutaka kumuondoa Zitto katika uongozi wa wabunge wa CHADEMA kule Kunduchi wakati Zitto yuko hospitalini akipambana na tatizo la sumu mwilini, Mchungaji Msigwa ukitoa mengi anayoropoka amethubutu kununua filamu ya kumtukana na Mtume Muhammad na kwenda kuionyesha kwa wapiga kura nyumbani kwake na huu ni ushuhuda wa Mbunge mwezake wa CHADEMA. 

Ukichukulia kuwa Lema amesikika akisema kuwa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe ambaye mimi naamini kuwa yeye si mjinga wala si mdini amemzuia kutoa huo ushahidi wake bungeni kwani sio wakati muafaka pamoja na hayo mengine niliyoyagusia hapo juu, ni wazi kuwa endapo Lema na hawa vinara wengine wa CHADEMA wataendelea na siasa hizi (najua kuwa wapo vinara wa CCM pia wanaozishabikia siasa hizi chini kwa chini), CHADEMA haitaweza kupambana na hisia zitakazojenga mtazamo kuwa zigo hili ni la CHADEMA na sio la Lema pekee.


Ndio maana nasema kuwa UDINI huu hautaondoka kwa kutuhumiana bali kujitambua, kubadilika na kutafuta muafaka na kamwe hautaweza kupigwa vita kwa kuruhusu waliokosa uhalali wa kimsingi ndio kuwa sura ya mapambano dhidi ya udini, hasa udini wa wengine na sio udini wao.


Katika hali iliyofikia sasa, mimi naamini kuwa moja ya njia madhubuti ya kupambana na udini ni sisi wenyewe kuangalia udini wa pande zetu, Kuuepuka, kuukemea na kuupinga wakati tukijaribu kuuelewa undani wa udini wa upande mwengine na kutafuta muafaka wa kukabiliana nao kama kwa kuutambua chembe ya ukweli wa hisia zao ama kuupiga vita kwa ujumla wake. 

Zaidi mimi naamini njia moja kubwa ya kuhakikisha tunadhibiti uhodhi wa siasa nyepesi zinazoshamiri katika kushape mjadala huu wa udini kama inavyoelekea kuwa, na kama njia ya kuondoa mazingira ya siasa hizo kustawi, kuna haja ya kuunda Tume ya Ukweli, Uwazi na Maridhiano ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa jukwaa la kuweka wazi ukweli ili kudhibiti hisia na kutambuana misingi ya madai ya msingi ya pande zote na kukubaliana kwa pamoja jinsi ya kuondokana na janga hili. Na haya tutaweza kuyafanya kwa kukubali kuwa Udini haujaanza na Kikwete wala Nyerere.


Muafaka haupatikani kwa ushindani wa nani mbaya nani mzuri, Muafaka unapatikana kwa kushirikiana wabaya na wazuri. Tujitambue, tubadilike na tuafikiane ndio njia salama.

No comments: