Mtizamo wangu kuhusiana na sarakasi za CHADEMA na Katiba Mpya!


CHADEMA wapongezwe kukwepa kitanzi cha kisiasa walichojiwekea!Kitendo cha CHADEMA kushindwa kutimiza ahadi yao ya kujitoa katika mchakato wa katiba mpya kama ilivyotangazwa hapo awali na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe alipotoa hotuba yake bungeni na kuwekewa msisitizo na Katibu Wilbroad Slaa kinatoa mafunzo mengi kisiasa.

Mosi, ni muhimu kuwapongeza wale waliothubutu kuona mbali na kukwepa mtego huo wa kisiasa waliojitegea hapo kabla ambao kama wangeuingia basi ungeliweza kuwamaliza kisiasa. Wahenga wanasema “never use toothless brinksmanship as it will only take you into oblivion”. CHADEMA walifanya makosa kuamua kutishia kujitoa lakini wanapaswa kupongezwa kwa kurudi nyuma kwa style ya aina yake.

Pili ni muhimu kuielewa CHADEMA katika suala zima la Katiba mpya. Kwa mtazamo wangu suala la katiba mpya ndani ya CHADEMA halikuwa na mvuto mkubwa kwa maana ya umuhimu wake katika kuendeleza na kusimika mfumo wa kidemokrasia kama ambavyo wengi tungelitegemea. Kwa CHADEMA Katiba mpya ilikuwa ni propaganda ya kisiasa iliyokuwa ikitumika pale inapotokea haja ya kutafuta mchawi wao kushindwa uchaguzi. Lakini pia kimkakati, katiba mpya ilipaswa kuwa ajenda endelevu ya kisiasa kuelekea katika uchaguzi wa 2015. 

Kitendo cha Rais Kikwete (sio CCM) kuikubali na kuitekeleza hoja hiyo ni kitendo ambacho hawakukitegemea na ukweli kimewaondolea ajenda muhimu kisiasa. Hivyo basi uungaji mkono wao wa hapo awali ulikuwa wa kulazimika lakini sio kwa kupenda hivyo ndio maana kila inapotokea mwanya wa kuchakachua uhalali wa mchakato huo, kina Tundu Lissu hawapotezi muda kuutumia.

Vilevile CHADEMA wanahofia uwezekano wa zoezi hili la katiba mpya kumalizika kwa mafanikio kwani ni wazi kitamkuza sana kisiasa, ndani na nje ya nchi, Rais Kikwete na hivyo yeye kuweza kuwa na ushawishi zaidi katika siasa za uchaguzi mkuu wa 2015. Hivyo kimkakati CHADEMA wanaonelea ni muhimu ama kuchakachua uhalali wa mchakato huo ama hata kuuvuruga kabisa usifanikiwe, hapo watakuwa wameweza kuikomboa ajenda hiyo na kuendelea kuitumia kuelekea 2015 lakini pia kumpunguzia nguvu za kisiasa Rais Kikwete kuelekea 2015.

Kwa nini tishio la CHADEMA kujitoa katika mchakato lilikuwa ni kitanzi cha wao wenyewe kujinyonga kisiasa?

Endapo CHADEMA wangejitoa leo na huko mbeleni, Tume ikaja na Rasimu ya Katiba Mpya ambayo itakuwa na mabadiliko makubwa yatakayokubalika na watanzania walio wengi wenye kuangalia mustakabali wa taifa zaidi ya ushabiki wa kisiasa, hilo lingekuwa kosa kubwa sana kwao kisiasa kwani wangeonekana wamekurupuka kuchukua msimamo wa kujitoa na pia ingelikuwa rahisi kwa wapinzani wao kisiasa kutumia hilo kudhihirisha kuwa CHADEMA ni chama pinga tu na hakina weledi wa kisiasa.

Vilevile mtego mwengine waliokuwa wamejiwekewa na ulikuwa ukiwasuburi kama hatua ya pili baada ya kujitoa ni jinsi gani wange-deal na uasu wa Prof Baregu ambaye amesema wazi kuwa akiambiwa kati ya kuchagua chama na Taifa basi atachagua chama. CHADEMA ambao wanatuhumu kuwa CCM inaingilia mchakato wamekuwa wakimlaumu Prof Baregu kwa kutuwapa ya ndani ya Tume ya Katiba kitu ambacho kwa wenye busara na maadili walipaswa kumpongeza Prof Baregu kwa kutii miiko ya kazi yake. Hapo ndipo wangelazimika kufanya makosa makubwa zaidi. Ukichukulia vita ya muda mrefu wanayompiga Naibu Katibu mkuu wao Zitto ambaye anaonekana kama sura ya siasa za kisomi na kimuono ndani ya CHADEMA na anayeonekena kushabihiana kifikra na Prof Baregu, CHADEMA wangefanya kosa kubwa sana kumuongeza na Prof Baregu katika listi yao ya wanaoawachimba kama maadui wa ndani. Ni dhahiri hili lingekuwa kosa jingine la kuwathibitishia wenye akili zao kuwa kile kirusi cha kupiga vita USOMI kimejikita pia CHADEMA. NA hapo wangeweza kupuputisha baadhi ya wasomi na watu wa tabaka la kati ambao wamekuwa waki-sympathies nao wakidhani kuwa kuna uwezekano wa CHADEMA kuwa mbadala makini wa CCM.

Kuhusu hoja ya kuwa CCM wanaingilia mchakato wa katiba, ukweli huu ni uthibitisho wa muendelezo wa siasa za hisia usio zisizojali kuchanganua ukweli ambazo wamekuwa wakizitegemea kufikia maamuzi yao mengi. Ni wazi kuwa vyama vyote vya siasa na hata makundi mengine ya kimaslahi vyote vimekuwa na mikakati ya kuhakikisha kuwa maon, mitizamo na maslahi yao yanakuwa na ushawishi katika mchakato huo. Cha ajabu ni kuwa CHADEMA hawakukemea wala kuhoji kitendo cha makundi ya kidini kuingilia mchakato huo kwa kuwaamuru wafuasi wao kwenda katika mikutano ya uchaguzi wa mabaraza ya katiba na kuchagua wawakilishi kwa vigezo vya Udini. Haya yamefanyika na makundi ya dini zetu zote mbili, Waislam na Wakristo na yamefanyika misikitini na makanisani. Kwanini CHADEMA hawajalichukulia kosa hilo kwa uzito unaostahili?

Kitendo cha viongozi wa CCM kujadiliana wao kwa wao bila ya kuwasiliana ama kushurutisha Tume ya Katiba hakuvunji sheria ya mchakato wa katiba kama Tundu Lissu alivyotaka kuaminisha umma. Walichofanya viongozi wa CCM ni kujipanga kisiasa kama ambavyo wenzao wengine wakiwemo CHADEMA wanavyofanya. Ni CHADEMA ambao wamefikia hata kukaa kama kamati kuu ya chama, kujadili kuhusu jinsi gani ya kuendeleza harakati zao ikiwemo jinsi gani ya kushutisha tume kufuata matakwa yao yatakayowezesha maslahi yao kisiasa, kumlaumu mwenzao kwa kukosa kuwapa ushirikiano na hata kufikia kupiga kura za kama chama kujitoa katika mchakato mzima na kumuondoa mwakilishi wao Prof Baregu katika tume ya katiba. CHADEMA wanapaswa kuchukulia matokeo ya kushindwa kupenyeza watu wao kwa wingi katika mabaraza ya katiba ni somo la wao kujijenga zaidi kimikakati na kuwa watanzania bado hawajawa mashabiki sana wa siasa za mipasho na kupiga kelele sana kama ambavyo makada wao wengi wamekuwa wakijipambanua hata huko mitaani kulipofanyika chaguzi za awali za mabaraza ya katiba.

Hivi kesho ikaja kujulikana kuwa hata Mwenyekiti wa CCM hakuwa tayari kutoa maoni yake mbele ya tume kwa kuepuka kuishinikiza ama labda maoni rasmi ya CCM yaliyowakilishwa katika tume hayana sehemu yoyote ambayo hawako tayari kutafuta muafaka wa pamoja, CHADEMA walionyesha wazi misimamo yao na kufikia hata kuweka vitisho endapo misimamo yao haitafuatwa, ni nani ataonekana hayuko makini?

Suala la kutumia ujanja wa kuikashifu, kuishusha na kuiadhiri Tume ya Katiba kwa kigezo cha posho wanazopangiwa na wizara sitaliingilia kwa undani wake, lakini mtizamo wangu ni kuwa siamini kama kuna Mbunge mwenye audacity ya kushutumu posho za wengine isipokuwa ndugu yangu Zitto Kabwe na wengine wachache ambao hadi leo wameendelea na msimamo wa kususia posho walizojiwekea wabunge wenzie. Tundu Lissu anapohoji walimu kulipwa shilingi 325,000 kwa mwezi anasahau kulinganisha na yeye anavyolipwa shilingi 330,000 za posho kwa siku. Mbunge anayelipwa milioni 11.2 kwa mwezi kwa kazi aliyogombania kutumikia anahoji malipo ya mil 7 kwa mwezi kwa kazi ya kuombwa kutumikia. Anasahau ama anajisahaulisha kuwa kila siku anakusanya posho ya kikao 200,000 na posho ya kujikimu 130,000 ambapo Jumla 330,000. Hapo bado mshahara na posho ya ubunge jumla tshs 11.2m kwa mwezi. Kwa ujumla kila siku Tundu Lissu anapokea wastani wa 370,000 awepo au asiwepo bungeni. ie mshahara na posho ya ubunge na 330,000 kwa siku katika siku 130 kama posho anapokuwepo bungeni na katika vikao vya kama. Sasa kwa kweli inahitaji ujasiri wa ajabu kwa mtu kama huyu kusimama na kuhoji posho za wenzie tena tofauti na yeye aliyegombea kutumikia, wenzake ambao wameombwa kutumikia Taifa na kuacha shughuli zao zingine.

Kwa kweli hadi kufikia sasa tumeona mengi na wenye upeo wa kujifunza naamini watakuwa wamefaidika sana kujifunza jinsi ya kutofanya makosa ya kisiasa kirahisirahisi kama wenzetu hawa, lakini zaidi kwa wanachama na wapenzi wa CHADEMA tambueni kuwa kwa maslahi ya nchi yetu, CHADEMA hakipaswi kurudia historia ya vyama vilivyokuja na kupita na hivyo kurudisha nyuma harakati za kujenga mfumo makini wa demokrasia ya vyama vingi nchini. Jitambueni, Jifunzeni na Jirekebisheni kwani mnaweza kama mlivyofanya leo kwa kuacha kutekeleza kitisho chenu cha kujitoa mlichokiweka wiki mbili zilizopita...No comments: