Salamu kutoka Jeriho na Dead Sea

14th Nov 2013


Jana siku ya Jumanne mimi na wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kutembelea mji wa Jericho. Huu ni mji ulio chini kabisa kwa kiasi cha mita 250 chini ya kina cha bahari. Ni mji wa kale zaidi duniani ambapo utafiti wa kihistoria unaonyesha ulikuwepo tangia miaka 10,000 iliyopita. Ni mji wenye umuhimu mkubwa kwa waumini wa dini ya kikristo kwani ndio mji ambao Nabii Issa bin Mariam ama Yesu alitumia sehemu kubwa ya maisha yake ya unabii akiwa hapo. 

Mji wa Jericho upo kiasi cha kilometa.... kutoka Ramallah. Safari ya kwenda Jericho ikanikutanisha tena na uhalisia wa ukoloni wa kiisraeli. Njiani unapotoka Ramallah unapita pembezoni mwa ukuta wa utenganisho na vizuizi mbalimbali vya kutoka na kuingia upande wa maeneo rasmi ya Waisraeli vikiwa na ulinzi mkali wa wanajeshi na ngome za Waisraeli. Karibia barabara zote za kutoka mji wa Ramallah kuelekea Jericho ambako pia ndio mwelekeo wa Bethlehem na Hebron, kuna misururu mirefu inayotokana na magari yanayotumia masaa kadhaa kuvuka vizuizi hivyo kikiwemo kile cha khalandiya kinachounganisha Ramallah na Jerusalem.

Njiani kuanzia hapo Ramallah tunaweza kuona makazi mbalimbali haramu ya waisraeli katika ardhi ya wapalestina pamoja na kuta zinazozungukua makazi hayo. Mara tu tunapotoka katika viunga vya mji wa Ramallah tunaanza kukitana na magari ya wanajeshi wa Israeli na matangazo mbalimbali ya lugha ya kiisraeli na machache yenye tafsiri ya kiarabu. Lakini kila tunapozidi kuelekea Jericho ama Jeriho kiyahudi na Ariha kwa kiaarabu, ndipo sura ya ukoloni wa waisraeli inazidi kujionyesha.
Njiani tunapita barabara ya kuelekea Nabil Mussa ambako inasemekana ndipo alipozikwa Nabii Musa. Pia tunapita katika sehemu maarufu ya Good Samaritan ambapo katika masimulizi ya dini kuna hadithi ya watu waliokuwa na sifa ya kutoa msaada kwa wageni na wapota njia. Hapa ndio asili ya jina la Good Samaritans. 

Tunapoingia tunakutana na ngome ndogo ya wanajeshi wa Israel ikililinda mashamba na viwanda vya waisraeli katika eneo hilo. Tunapowasili Jericho, tunakwenda moja kwa moja katika mti wa kihistoria ujilakanao kama Sacyamore ambao mtoza ushuru fisadi aliyeitwa Zakeo aliyekuwa akichukiwa sana na wenyeji kwa kuwafanyia kazi wakoloni wa kirumi alipanda kutokana na ufupi wake ili kuweza kumuona Nabii Issa bin Mariam kabla ya nabii kumuuliza maswali na kumtaka amkaribishe nyumbani kwake. Tukio hilo liliwashangaza sana wenyeji na kuhoji kwanini Nabii Issa alitaka kwenda kwake mtu mbaya kwao.

Baada ya hapo tukaelekea katika kisima ambacho kipo katika mji wa kale wa Jericho. Hapa kuna kisima chenye historia ambapo inasemekana kuwa Nabii Elisha alifika pale na kukutana na watumiaji wa maji hayo wakilalamika kuwa maji hayo yanasababisha magonjwa mengi na kinamama kuharibu mimba. Naye akayabariki na kutamka kuwa kuanzia wakati huo maji hayo yatakuwa salama kwa wanayoyatumia. Juu ya kisima hicho kuna machimbo mbalimbali ambayo yamechimbwa kuibua mabaki ya majengo ya zamani ya mji wa kale.

Baada ya hapo tukaanza safari ya kuona mlima wa majaribu aka Mountain of Temptation ambao Nabii Issa kabla ya kuanza maisha ya Utume wake alikwenda huko kwenye mfungo wa siku arobaini kwa utakaso. Baada ya hapo tukaenda katika Hekalu la Mfalme Harrod ambalo lilikuwa ni makazi yake ya wakati wa baridi.

Kutoka hapo tukaanza safari ya kuona Bahari Mfu aka Dead Sea. Huko nako tukakumbana na jeuri ya ukoloni wa Waisraeli. Njiani tunakutana na magari ya kijeshi ya Waisraeli huku mabango yote ya barabarani yakiwa yameandikwa kwa lugha ya kiyahudi pekee. Huko tunaingia katika hoteli ya kitalii iliyo kando na bahari hiyo. Hapo tunakaribishwa na bendera za Israel zikithibitisha kuwa eneo hilo ni mali ya Waisraeli. Hapo tunakutana na kundi kubwa la Waafrika wakiwa na mabasi makubwa ya kitalii yenye namba za kiisraeli. Hili ni kundi la Wanigeria walio katika safari ya Hijja. Mbele ya basi lao kuna bango linalosema Vuguvugu la Wakristo wa Nigeria Marafiki wa Ardhi Takatifu na kwamba ziara ya yao ni sehemu ya ziara ya Rais wao Goodluck Jonathan atakayoifanya nchini Israel. 

Baada ya kuulizia tunambiwa kuwa hapo wanaingia watu walio katika makundi maalum (walioingia kupitia Israel na kutumia makampuni ya utalii ya kiisraeli). Wageni hatari sisi inatubidi kwenda kutafuta sehemu nyingine ya kuingia katika bahari hiyo ya kihistoria. 

Baada ya mwendo mfupi tunaingia katika eneo lingine nalo likiwa na bendera ya Israeli. Hapo tunakutana na mama wa Kiyahudi mlangoni na baada ya kujitambulisha anatueleza kuwa alikuwa Tanzania miezi michache iliyopita na kwamba ameipenda sana nchi yetu. Hapo tunatakiwa kulipa hela za kiyahudi 50 zenye thamani ya dola 15 ili kuingia katika eneo la bahari hiyo. Hapo tunakuta mamia ya watalii wakikoga maji hayo yenye chumvi kali na wengine wakijipaka udongo kwa imani kuwa maji pamoja na udongo huo ni dawa ya magonjwa mbalimbali ya ngozi. Wapo walikuwa na chupa za maji wakijaza maji hayo na wengine wakijaza udongo wa hapo. Zote hizo zawadi kwa ndugu waumini wenye kuamini katika baraka ya maji na udongo huo.

No comments: