12th Nov 2013
Kutembelea Palestina ni somo la kisiasa. Kila unapokwenda unazungukwa na uhalisia wa siasa za kikoloni na kibaguzi lakini pia hulka ya watu wake katika mapambano ya kupigania uhuru wao na kuboresha maisha yao.
Siku ya jumatatu jioni mimi na wenzangu tulipata nafasi ya kushiriki maandamano ya kupinga mauji ya Comrade Arafat hapa mjini Ramallah! Maandamano hayo yaliongozwa na bendi ya Scouts na vikunfi vya chipukizi na vijana wa chama cha Fatah wakiwa kayika mavazi ua mapambano! Maandamano hayo yalipita katika barabara mbalimbali za Ramallah.
Mji wa Ramallah ni mji unaofanana sana na miji mingi ya nchi zikizoendelea kiasi cha kuweza kujisahau kuwa upo katika utawala na ukandamizi wa kikoloni wa Waisraeli. Mji wa Ramallah ndio makao makuu ya Mamlaka ya Wapalestina. Ni mji uliojengwa katika vilima mithili ya ile milima ya mji wa wanza lakini hapa ni mji mzima ni vilima vikali. Ni mji unaopendeza saa na unaojengeka na kupangika barabara mithali ya mji mpya kabisa. Ni mji ambao una kila mandhari ya miji ya ulaya hasa ile iliyopo katika ukanda wa bahari ya mediteranian. Kitu kimoja kilicho wazi ni jinsi gani ujenzi wa mji huo unavyofuata sheria za mipango miji. Karibia majumba yote yamejengwa kwa kutumia matofali ama mawe yaliyokatwa kwa mfano wa matofali ya aina moja. Nyumba zote zimenakshiwa kwa nakshi za mithili ya majengo ya kizamani. Majengo yote yana rangi moja ya maziwa. Shughuli za ujenzi zinaendelea kila mahala.
Mji wa Ramalla ni mji wa kisasa uliojaa majengo ya kuvutia na ujenzi kila upande. Ni mji wa wasomi kukiwa na asilimi tatu ya wasiosoma. Wakazi wengi wa Ramallah wana elimu ya chuo kikuu. Kwa mujibu wa Nabil Shath, elimu ni sehemu ya mapambano ya wapalestina.
Najaribu kutafuta alama zozote za majumba yaliyoshambuliwa nakubomolewa na waisraeli katika mojaya kampeni zao dhidi ya mji huu bila ya mafanikio. Uzuri wa mji huu umenishtua sana na kujaribu kujiuliza kama ndugu zangu hawa baada ya kuonjeshwa utamu wa maisha haya wanweza kweki kusimam kidete kupambana na ukoloni wa Waisrael ambao ni wazi hawana mpango wa kuondoka katika maeneo waliyoyakwapua na kuyakalia kimabavu kuanzia Mashariki ya Jerusalem hadi ukingo wa mto jordan.
Moja ya picha nilizobahatika kuzipiga ni picha ya kikundi cha maskauti kikiwa katika gwaride mbele ya KFC, moja ya alama za nguvu ya tamaa za kibepari duniani. Ni vigumu kuamini kuwa pale siku ya kuanzisha mapambano mengine ambayo yanaweza kupelekea Waisraeli kubomoa kila kilichojengwa kama wafanyavyo, vijana hawa watakuwa tayari ku-risk kupoteza ulabu huu wa masiha ya kiulaya. Hata hivyo nakumbuka hali ya kambi ya wakimbizi iliyo karibu na mji wa Ramallah ambayo tuliona wakati tukiwa tunakuja Ramallah kutokea mpakani. Ni wazi hali mbaya wanayoishi wakimbizi hawa bado ni chachu ya utayari wa mapambano ya ukombozi kamili kwa wapalestina wote.
Maandamano yalifikia mwisho katika eneo la mashujaa ambako kuna kaburi la muda la Comrade Arafat. Ni kaburi la muda kwa sababu mpango ni kumzika Jerusalem mara baada ya harakati za ukombozi kamili kufanikiwa. Hapo tunakutana na jengo zuri la aina yake likiwa limezungukwa na ukuta mkubwa wenye ulinzi mkali wa askari wa kipalestina. Ndani ya eneo hilo tunakuta askari wa kipalestina wakijipanga kwa gwaride maalum huku vigogo mbalimbali wa historia ya mapambano ya wapalestina, wengi wao ni wazee wa miaka sitini hadi themanini, wakijipanga pembeni. Lakini pia kuna kundi kubwa la watoto wadogo wakiwa katika mavazi maalum wakiwa na bendera na mapicha ya Comrade Arafat.
Baadaye kidogo aliwasili Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina ambaye baada ya kusalimiana na vigogo wenzie anapita katikati ya garide la askari kwenda kuweka shada la maua katika kaburi la Comrade Arafat. Kaburi hilo lipo ndani ya jumba kubwa likiwa limezungukwa na walinzi maalum wawili wakiwa mbele ya mlango wa kuingilia na wengineo wakiwa wamesambaa kulizunguka jengo hilo. Baada ya hapo ndipo makundi ya watu mbalimbali kutoka kila pande ya dunia walipoanza kwenda kuwe mashada ya maua katika kaburi la Comrade Arafat.
Baada ya shughuli hiyo mimi na mwenzangu tunaamua kutembea kwa miguu kuzunguka mji huo. Tofauti na nyumbani huku maduka yanabaki wazi hadi saa nne usiku. Tunajaribu kuulizia bei za vitu tukilinganisha na nyumbani, ukweli vitu hapa ni ghali kiasi na hii inasababishwa na kodi kubwa inayotozwa na mamlaka ya kodi ya Israeli. Hata kama kodi hiyo inapaswa kukabidhiwa kwa mamalaka ya wapalestina ambapo mara nyingi wamekuwa wakikataa kukabidhi kama sehemu mojawapo ya vikwazo dhidi ya wapalestina, kodi hiyo ni kubwa sana ukilinganisha na kipato chao na kile cha waisraeli. Wakati Waisraeli kiwango cha chini cha mshahara ni pesa za kiisraeli 4,500 kwa mwezi, kwa upande wa wapalestina ni 1500. Mmoja wa wauza duka alitueleza kuwa endapo wapalestina wasingekuwa na umuhimu kwa uchumi wa Israel basi wangekuwa wameshatoswa baharini.
Hii inanifungua macho kuwa utawala wa kimabavu wa Waisraeli katika maeneo ya Wapalestina sio kwa minajili ya imani za kidini na uasili pekee bali pia u a umuhimu wa kipekee kwa uchumi wa Israeli. Kwa kifupi wapalestina wanachangia kama sio kulipia kila matumizi ya waisraeli katika kuwakandamiza wapalestina naia kulinda na kupanua ukoloni wao. Israeli inafaidika sana kiuchumi kutokana na kodi, cheap labour, maliasili, utalii na hata soko la wapalestina.
No comments:
Post a Comment