USO KWA USO NA UKOLONI WA ISRAEL


Nov 11, 2013

"Unaenda kufanya nini Israel?" Hilo ndilo swali ambalo linalonikaribisha uso kwa uso na madhila ya ukoloni wa Waisrael katika ardhi ya wapalestina. Huu ndio uhalisia ninaokaribishwa nao nikianza msafara wangu wa kihistoria katika ardhi ya Wapalestina. Ni swali ambalo naulizwa na afisa uhamiaji wa Kiisrael katika mpaka wa kuingia Palestina kutokea nchi ya Jordan. Ni uhalisia ambao nimekuja kuona kwa macho yangu zaidi ya ule niujuwao kwa miaka mingi kutoka katika vitabu, magazeti, hadithi na mitandaoni.

Ni siku ya Jumapili ya tarehe 10 mwezi novemba 2013. Mimi na watanzania wenzangu watatu tulianza msafara wetu wa kuingia katika ardhi ya wapalestina tukitokea mjini Amaan Jordan ambako tuliwasili huko siku ya Jumamosi. Kutokana na kuwa siku hiyo ni siku ya mapumziko kwa Wayahudi, ilitubidi tulale mjini Amman kabla ya kuanza msafara wetu kuelekea mpakani. Safari ya kuelekea mpakani ilituchukua muda wa saa moja kabla ya kufika katika mji mdogo wa South Ashooh ambapo ndipo kuna ofisi za uhamiaji za kwa upande wa Jordan. Tulipofika hapo tukaagana na gari lililotuleta kutoka mjini Amman. Hapo mambo yalikwenda haraka na baadae tukapanda basi maalum la kuvusha wasafiri kataka pande mbili za mpaka. Kati ya geti la Jordan na ardhi ya Wapalestina tunakita katika vizuizi viwili ambapo tulitakiwa kuonyesha kipande cha ruhusa ya kuvuka mpaka. Katikati tunavuka daraja la Mfalme Feisal katika mto Jordan. Hali yake ni sawa na mipaka mingine duniani ukiondoa magari machache ya kijeshi yakiwa na silaha nzito na askari wawili watatu. 

Hali haikuwa hivyo katika mpaka wa kuingilia katika ardhi ya Wapalestina. Baada ya safari ya dakika tano hivi tunaingia katika mpaka wa ardhi ya Wapalestina. Hapo tunakutana na uzio wa waya za umeme pamoja na maaskari wa Kiisraeli. Ndio, mpaka wa kuingilia katika ardhi ya Wapalestina unasimamiwa na Waisraeli kama ilivyo katika maeneo mengine ya wapalestina. Tukiwa ndani ya basi tunaangalia majabali ya udongo wa jangwani yaliyozunguka eneo hilo. Mahandaki kila mahala pamoja na mitambo maalum ya uchunguzi. Tunafika geti la kwanza ambapo raia wote wa Palestina wanashuka na kuingia katika eneo maalum. Wengine wageni tunasubiri kwa zaidi ya dakika 20 kabla ya kuruhusiwa kuvuka kizuizi hicho cha kwanza. Eneo hilo hakuna mabasi mengine isipokuwa mabasi maalum ya kuvusha wageni na magari ya binafsi na ya mizigo. Baada ya hapo tunaenda kwa mwendo wa dakika moja na kufika katika kituo kikuu cha mpakani kinachoitwa King Feisal bridge kwa upande wa Jordan na .... Jina la kiisraeli kwa upande wa Ardhi ya Wapalestina.

Tulipofika katika kituo kikuu cha mpakani tulianza na kusubiri ndani ya basi kwa karibia nusu saa tukisubiri amri kutoka kwa vijana wa kiisraeli wenye silaha kali. Tukiwa ndani ya gari tunaangalia kwanza jinsi eneo hilo lilivyopangwa kiusalama likizungukwa na uzio wa waya pamoja na vijilima na viabanda vya juu vya walinzi wenye silaha. Nje tunaona vijana wa kiarabu wakiwa ndio wabeba mizigo na wasimamizi wao. Wengine wote ni Waisraeli na wengi wao ni askari wakiwa na mavazi yenye nembo ya Idara ya usalama wa ndani ya Israel. 

Tunaanza kwa kusimama katika foleni huku kila mtu akiwa na mzigo wake kuelekea katika sehemu maalum ya kuingiza mizigo kwenye mashine za ukaguzi. Kila msafiri anatakiwa kukabidhi passport yake ili kuandikishwa katika nembo maalum inayobandikwa katika mizigo yake kwa utambulisho. Baada ya hapo unajipanga katika foleni nyingine ya ukaguzi wa passport. Hapo unakutana na mabinti wa kiisraeli ambao wanakuuliza kila kilichoandikwa katika passport yako kutuibitisha kama ni yako. Hapo nikakutana na kizingiti cha kwanza. Passport yangu inatiliwa mashtaka. Inaelekea kwao wao Tanzania ni nchi ngeni na zaidi sio nchi ya waislam hivyo inakuwaje ninakuwa majina ya kiarabu. Baada ya kupitiwa na wenzake watatu binti huyo anaweka alama tatu kuonyesha kuwa nahitaji kuangaliwa zaidi. Tayari nimeshakuwa mshukiwa hatari. Baada ya dakika kadhaa naruhusiwa kuingia katika sehemu ya tatu ya ukaguzi ambayo natakiwa kuingiza kila kitu changu katika mshine maalum. 

Tofauti na wenzangu wengine wanaokwenda moja kwa moja katika sehemu ya viza, mimi nakutana na kijana mwengine ambaye ananichukua katika chumba maalum na kunihoji maswali kadhaa ikiwemo kama nimebeba silaha ya aina yoyote. Baada ya kunihoji anachukua passport yangu na kumkabidhi binti mwengine ambaye anaichukua na kuipaka mafuta maalum kabla ya kuingiza katika mashine maalum ya ukaguzi. Nadhani ilikuwa kukagua kama ina alama yoyote ya material za silaha. Baada ya hapo anamuonyesha mtu mwengine na kujadiliana naye kwa dakika moja kabla ya kunipa passort yangu na kuniambia lile neno la uchungu "Welcome to Israel"

Nachukua passport yangu na kuelekea katika sehemu ya nne ambayo sasa nawasalisha karatasi yangu ya viza niliyotumia kwa njia ya mtandao baada ya kuomba mwezi mmoja kabla. Hapo nakutana na shock nyingine. Napewa kibalia maalum cha kuingia Israel kwa upande wa ukingo wa magharibi wa mtu Jordan pekee. Kutoka hapo hadi kwenye kuchukua mizigo yangu nakutana na vizuizi vitatu ambavyo natakiwa kuonyesha passport yangu na kibali cha kuingia kwa uhakiki. Baada ya hapo tunakwenda kuchukua mizigo yetu kabla ya kupita katika kizuizi kingine kwa ukaguzi. Hapo wapo waliokuwa wakipita bila ya ukaguzi mwengine lakini kila Mpalestina analazika kukaguliwa upya. 

Nje ya mlango wa kutokea tunakuatana na duka la kubadilishia fedha na duka la bidhaa nyingine. Naulizia kubadili fedha naambiwa hapo ni fedha za Kiisraeli pekee na ndio fedha rasmi ya matumizi katika ardhi ya wapalestina. Naulizia vocha za simu ya kampuni inayotumika Palestina naambiwa hapo ni naweza kupata za makampuni ya Israel pekee na eneo la katibu kwa vocha za makampuni ya Wapalestina ni Jericho kwa Kiisraeli na Ailah kwa kipalestina. 

Natoka hapo kichwani nikijiuliza... Kama mimi nasikia uchungu wa kukumbana uso kwa uso na uhalisia huu wa ukoloni kwa Wapalestina, hali ikoje kwa Wapalestina wenyewe?

No comments: