Ya Bungeni ni matunda ya soko la kura...
29 June 2011
Ni hatari, si salama na wala sio busara kuacha hatima ya taifa letu iamuliwe kwa mujibu wa maslahi ya soko la kura. Soko ambalo kwa muda mrefu tumekuwa tunalidumaza kifikira. Soko ambalo badala ya kuwa mkombozi wa mtanzania limegeuzwa kuwa janga la utaifa wetu. Soko lililogeuzwa kuwa mazalia uozo wa kisiasa. Soko ambalo kamwe halitaweza kutuondoa katika lindi la maadui umasikini, ujinga, maradhi, ufisadi na ubaguzi.
Bunge letu la sasa ni matunda ya mfumo na utamaduni wa kisiasa unaojengeka wenye kuweka mbele maslahi ya soko la kura na kusahau ama kudharau wajibu wa uongozi na kamwe sio kupanuka kwa demokrasia.
Wakati wanasiasa wetu wanaamini kuwa siasa za kukosa busara na staha dhidi ya "Watawala" zinashabikiwa na vijana wengi hivyo ni mtaji muafaka wa kura, wamesahau uongozi ni dhamana na una majukumu yake!
Kimsingi baadhi yao wanaamini kuwa hizo ndio siasa zinazovutia wapiga kura vijana. Hawajali wajibu wao kama viongozi. Wanasahau ni Tanzania wanayoijenga sasa ndiyo wayakayopaswa kuitawala wakishika dola.
Lakini zaidi ufinyu wa ustadi katika siasa za kujenga zenye kuambatana na uerevu wa masuala ya kitaifa na kidunia katika uga wa siasa unapelekea baadhi ya wanasiasa wetu kuamini katika siasa za ujanjaujanja ili kuficha mapungufu yao.
Naweza kusema hili ni zao historia ndefu ya nchi yetu kujikita katika utoaji wa bora elimu na pia tatizo la ukosefu wa watu wenye ujuzi, uwezo na umahiri wa masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika platform za siasa kama bunge letu.
Lakini pia ukosefu wa hulka ya uthubutu miongoni mwa watanzania wenye elimu bora, misingi thabiti na umahiri wa masuala ya uongozi na siasa kuingia katika taaluma ya siasa na kukimbilia maeneo salama kimaisha na kimaslahi.
Kwa upande mwengine soko hili la kura limefanikiwa kutupa viongozi tunaowaona na wakaendelea kupata ushabiki na hata ufuasi miongoni mwetu hasa sisi vijana kutokana na miaka mingi ya matumizi mabaya ya imani ya watanzania. Imani ambayo watanzania waliwapa viongozi wao pamoja na asasi za utawala.
Ni kutokana na tabia za baadhi ya viongozi wetu kutumia vibaya imani na ridhaa ya watanzania hata kufikia kuwadhihaki na kuwabeza huku wakishindwa kutatatua hata ya matatizo ya msingi ya wananchi hao nako kumewezesha wanasiasa wajanjawajanja kuchakachua soko la kura.
Uchakachuaji ambao badala ya kuwapa nafasi watanzania kuwa na upeo mkubwa wa kuchagua viongozi bora unawafanya wawe wahanga wa kuchagua viongozi wahuni zaidi, walafi zaidi, wazembe zaidi na wabinafsi zaidi.
Ili kuepukana na hatari hii ni wajibu wetu sote kuwa mstari wa mbele kujenga upya misingi ya siasa safi na uongozi bora. Na hili litafanikiwa endapo sote ambao tumebarikiwa kupata elimu na kujengeka kifikira kukataa kuwa wahanga wa siasa zenye kujali na kuamini katika kasumba za kisiasa badala Ukweli wa mambo.
Lakini pia kuwa tayari kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapaswa kujua ukweli wa mambo na kumuepusha kuwa mhanga wa siasa za kasumba, hovyohovyo na majitaka. Siasa ambazo huwezesha udumavu wa kifikira na pia kuwa mtaji wa wanasiasa wajanjawajanja, wahuni na hata madhalimu wanaojivika vilemba vya uwanamapinduzi, uzalendo na ukombozi. Wanasiasa ambao wako tayari kuweka rehani mustakbali wa taifa letu kwa maslahi yao ya kisiasa na binafsi.
No comments:
Post a Comment