Asili za vyama vyetu na siasa za nchi yetu;



Mkataa asili hubaki kuwa mtumwa wa asili!

Vyama vya siasa kama yalivyo makundi mengine huwa vinakuwa na asili yake hata kabla ya kuwa vyama rasmi. Kuna wanaoamini kuwa hakuna dhambi ya asili ingawa usipokuwa makini asili inaweza kuwa jinamizi na hata msingi mkuu wa maendeleo yako. Mimi nakubaliana nao kwa kiasi fulani na ndio maana naamini kuwa badala ya kushindana kukana asili ya chama fulani ni vizuri na muhimu kwa maendeleo ya muda mrefu kisiasa kujitambua na kukubali asili ili kuweza kuiwekea mazingira ya kuhakisha kuwa asili hiyo inakuwa mtaji bora na sio mzigo wa miba.

Mfano ni asili ya CCM ambayo ni kikundi cha kupigania maslahi cha watu wa waliojinasibu kama waungwana wa Mzizima. Wao walikuwa wepesi kung’amua hasara ya kukataa asili yao. Hata katika enzi hizi daima inapoelezewa historia ya CCM, asili yake kama kikundi cha wachache cha maslahi ya kijamii kama ilivyokuwa katika enzi za TAA hutambuliwa na hata kuenziwa. Na asili ya CCM ina pande mbili. Pia kuna ya upande wa Zanzibar ambako nako asili ya ASP ilikuwa makundi mawili ya maslahi ya kijamii ambayo yalikuwa kundi la Wazanzibari wenye asili ya Bara yaani waafrika na wengine wenye asili ya Ushirazi.

Kwa upande mwengine wa kisiasa huko Zanzibar kulikuwa na vyama vya ZPPP ambacho hadi mwisho wake kilibaki kuwa kundi la maslahi ya kijamii katika siasa na ZNP ambacho ingawa asili yake ilikuwa ni kundi la maslahi ya kijamii kiliweza kujijenga kuwa chama cha makundi mbalimbali kabla ya kurudi nyuma kilipokaribia kuchukua madaraka kwa maslahi ya kundi la kijamii kuibuka na kuhodhi chama hicho tena na kulazimu Mapinduzi ya 1964 ambayo yalikisambaratisha hadi baadaye mabaki ya kundi hili yalipoweza kuungana na kundi maslahi la jamii nyingine na kuibuka kama CUF.

Upeo na uthubutu wa viongozi wa Tanganyika African Association kwa upande wa Tanganyika na African Association na Shirazi Association kwa upande wa Zanzibar na baadae TANU na ASP kutambua zaidi umuhimu wa kuunganisha makundi maslahi ya kijamii na kitaifa na kuunda CCM ndio moja ya misingi ya uthabiti wa CCM hadi sasa. Uthubutu wa kutambua madhara ya jinamizi la uasili hapo kabla umeweza kuwajngea msingi imara CCM na kuweza kupambana na jitihada zozote za washindani wao sasa kujaribu kutumia siasa za maslahi ya kijamii dhidi yao.

Huku bara nako kulikuwa na makundi mengine ya maslahi ya kijamii ambayo yaligeuka kuwa maslahi ya kisiasa lakini nayo yalisambaratishwa na nguvu za Mwalimu Nyerere na TANU. Kusambaratishwa kwa makundi maslahi yenye mlengo wa maslahi ya kundi fulani la kijamii zaidi ya utaifa hakukuwa na maana kuwa fikra ama mitandao ya siasa zenye mlengo wa maslahi ya makundi ya kijamii zilikwisha. Harakati za chinichini kwa chini ziliandelea na utamaduni wa maslahi siasa za maslahi ya makundi jamii kama dini, kabila ama eneo yaliendelea katika mifumo isiyo rasmi kama ilivyo mifumo ya biashara zisizo rasmi ambayo yawezekana ikawa haramu kifikra, kiitikadi ama hata kisheria lakini mifumo hiyo ikaendelea kuwepo na hata kustawi kutokana na uhalali wa kijamii.

Na hapa ndipo inapokuja asili ya CHADEMA ambayo inasemekana ilikuwa ni vuguvugu la kupigania, kulinda na kuendeleza maslahi ya kabila fulani. Yasemekana, na hili nimelifanyia uchunguzi kiasi kabla ya kulitilia maanani na natambua kuwa bado sijapata undani zaidi, asili ya CHADEMA ilikuwa ni kundi la vizito flani wanaotoka katika kabila moja ambao walianzisha kundi liloitwa ambalo lililenga kutetea maslahi ya kijamii, kiuchumi na hata kisiasa ya waanzilishi kwa kupitia kabila lao. Kundinhili lilijulikana kama Chaga Development Association. Ni wazi kama yalivyo makundi mengine ya maslahi ya kijamii kundi hili halikuwa na uhalali wa watu wote wa kabila hilo na ukweli ni kuwa lilikuwa kundi la wateule kadhaa ambao kwa mtazamo wao ilikuwa ni sawa na muhimu kwao wao kuwapigania wenzao kwa mfumo huo.

Lilipokuja vuguvugu la vyama vingi baadhi ya wateule wa kundi hili walikuwemo katika mstari wa mbele wa vuguvugu hilo ambapo baadae iliporuhusiwa kuanzishwa vyama vingi vya kisiasa, katika mijadala ya mwanzoni, mtandao wa mageuzi ya kisiasa ambao ulikuwa na watanzania wa kila aina uliafiki kuwa jina la CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO litumike kuanzisha chama cha pamoja. Kilichofuata ni sarakasi ambazo kwa mtazamo wangu ilikuwa ni makosa makubwa ambayo hadi sasa yanakisumbua chama cha CHADEMA. Wateule kadhaa ambao waliamini kuwa jina hilo halipaswi kutumiwa na kundi ambalo hawana uhakika wa kuendeleza malengo asili ya kundi lao na kudhani kuwa asili hiyo inapaswa kuenziwa katika mkakati mpya kutokana na mazingira mapya, waliwahi kwa msajili wa vyama na kusajili chama chao pekee huku wakiwatenga wenzao ambao walikuwa pamoja katika harakati za mageuzi kitu ambacho kilipekea kutumika kwa jina la NCCR badala ya CDM kama ilivyokubaliwa kwa pamoja hapo kabla.

Jinamizi la ujanja huu ndio linalokisumbua CHADEMA hadi sasa wakati kikionekana kinapata mafanikio kadhaa. Wakati vyama vingine viliweza kujitambua na kuona mbali kuhusiana na asili ya vyama vyao na kuhakikisha kuwa badala ya kuukwepa ukweli huo wanautambua na kuutumia kama somo la kisiasa, CHADEMA wao hadi sasa wameng'ana vinginevyo. Wameamua kuukana na kuukandamiza ukweli huo. Kwa mtazamo wangu hili limewapelekea kujikosesha nafasi ya kuzika jinamizi hilo kwa uwazi na udhati. Asili haipaswi kuwa kioo cha maendeleo lakini yaweza kuwa msingi mkubwa wa maendeleo. Yawe maendeleo chanya ama maendeleo hasi. Jinsi gani unaipambanua asili hiyo ndiyo inapelekea aina ya maendeleo yanayoathiriwa na asili.

Ni wazi kuwa kutokuweza kuruhusu uwazi kuhusiana na asili ya CHADEMA, iwe jina ama ajenda asilia, kunakifanya chama hicho kuwa vulnerable katika mashambulizi ya nje lakini pia mashindano ya siasa za ndani za chama pia. Kukataa asili hiyo hakuna maana hakutakuwa na wachache ambao wanaendelea kutumia asili hiyo kwa faida yao wawe maadui nje ama wa ndani au asili hiyo kutumika na wateule kadhaa kufanikisha jitihada zao za kuhodhi ushawishi wa kisiasa na kimaslahi katika maendeleo ya chama hicho na siasa za nchi. Haya hayawezi kuepukika hadi pale kutakapokuwa na utayari ya kutambua asili hiyo kwa uwazi, bila ya kujiona ni wakosa na kukubaliana kwa pamoja juu ya mikakati rasmi ya kuhakikisha asili hiyo haikwazi maendeleo ya chama hicho hasa kuhusiana na haiba yake mbele ya jamii zingine.

Hisia na wala harakati za wale wenye kuamini katika ajenda asilia hazitaisha kwa kuendeleza utaratibu wa kubadili uongozi kila baada ya kipindi cha uongozi mmoja kwisha ambao hapo kabla ulisaidia CHADEMA kuibuka kisiasa kitu ambacho hivi sasa wamekuwa wanaonekana kukidharau ama kukiogopa. Lakini ni wazi utamaduni huo kama ungeendelezwa ungeweza kupunguza mazingira ya kulistawisha suala la hisia za ukabila ama maslahi asilia. Naamini kuwa kwa faida ya CHADEMA lakini zaidi kwa faida ya nchi yetu na kutuepusha kubaya zaidi tunakoelekea, muungano wa CHADEMA na CUF ni muhimu sana ingawa wengi wanaona hilo kama ni ndoto tu kutokana na kutambua nguvu za maslahi ya makundi ya kijamii katika vyama vyote hivyo ingawa wasengependa suala hilo kuongelewa kwa uwazi.

Ieleweke kuwa siamini kuwa hadi sasa CHADEMA ni chama cha ukabila. Ni wazi agenda rasmi ya CHADEMA kama chama cha siasa chenye uhitaji wa kukubalika kitaifa haiwezi kuwa maslahi ya ukabila. Lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa nguvu za maslahi ya kijamii ambayo ndio yalikuwa ajenda asilia zinaweza kuendelea kuathiri maendeleo ya chama hicho. Hiyo inaweza kutokana na kuendelea kwa fikra asili miongoni mwa baadhi ya wateulena ambazo zikaendelea kuwa na nguvu kiasi fulani ama mtazamo wa watu dhidi ya chama hicho kutokana na asili yake hiyo ambayo imeweza kuathiri haiba ya chama hicho hasa kutokana na kushindwa kulikabili zimwi la uasili kwa uwazi na upana wake.

Chukulia mfano wa suala la uongozi wa chama hicho. Angalia zile harakati za kumrithi Mzee Mtei ambapo kulikuwa na jitihada nyingi za kumrithisha Mzee Ndesamburo ambaye naye ni mmoja wa wa wa kabila hilo na alikuwemo katika mkakati asili. Kilichotokea ni mgawanyiko mkubwa wa chama baada ya kushinda Mzee Makani ambaye kwa wenye kuendeleza fikra za agenda asilia walimuona kama wakuja na kufikia kukizira chama hadi pale kiliporudi mikononi mwa mwenzao ambaye anaweza kuaminika, kuhalisia ama kihisia, kulinda nafasi na maslahi ya agenda asilia.

Hili pia limethibitishwa na yaliyowatokea kina Mzee Mchata, Mzee Ngululupi, Kaburu, Wangwe, Zitto na wengineo wengi walionekana kutishia nafasi ya ajenda asili. Na haya yanaendelea hadi sasa katika harakati za M4C ambazo ingawa zimewezesha kukitanua chama kwa maana ya idadi ya wanaojiunga lakini kinaendelea kukigawanya chama hicho katika siasa za ndani. Ni wazi kuwa kushindwa kulikabili janga la uasili kwa uwazi, udhati na uthabiti kunaendelea kuwa kikwazo cha kuondokana na haiba ya maslahi jamii hata kama kuna kutambua kuwa suala hilo linaathari yake kwa mipango ya kisiasa ya chama hicho. Bila ya kulikabili jinamizi hili kwa uwazi na ushiriki mpana litaendea kuathiri chama na siasa za nchi hata pale ambapo chama hiki kitakapoweza kufanikia kukwapua madaraka kutoka kwa washindani wao.

Kuhusiana na kukubalika kwa CHADEMA katika pande mbalimbali za nchi ama makundi mbalimbali ya kijamii hilo halina maana kuwa athari za uasili hazipo ama hakuna wanaondeleza siasa za agenda asilia kichinichini. Lakini pia unaposema kukubalika kwa maana ya kuwa chama hicho kimeweza kupata viti vya kisiasa bila ya kuangalia factor zingine za kisiasa katika maeneo hayo au idadi ya kukubalika kwa muktadha wa ujumla wa kura zote za eneo tajwa, nadhani kaka unakosea. Ni wazi kuwa kupigiwa kura hakuna maana a kukubalika pekee bali kunajengwa na sababu nyingi na hivyo kutoa maana nyingi. Kwa mfano, ni wazi kuwa jimbo la Ausha na yale ya Mwanza yalienda CHADEMA sio kwa sababu ya kukubalika kwa chama ama mgombea bali ni ushindani wa kisiasa na kimaslahi ndani ya CCM. Tukumbuke, hisia za kisiasa zinaweza kuwa na mahusiano ya hisia mbalimbali za kijamii, kisiasa na hata kiuchumi hivyo haziwezi kutafsiriwa kwa muktadha mmoja tu.

Ukweli ni kuwa hizi siasa za maslahi ya makundi jamii zipo hata CCM. Hivi sasa makundi ya kikabila, kimikoa, kidini, kimaeneo, kikanda yanaendelea kushamiri ndani ya CCM. Tofauti ya CCM na vyama vingine ni kuwa kwa CCM jinamizi hili lilitambuliwa na kushughulikiwa mapema hivyo kujenga mfumo na utamaduni wa kisiasa ambao hakuna kundi lolote linaloweza kuhodhi nafasi ama kwa kiasi kikubwa au kwa muda mrefu na hivyo kuweza kuhakikisha kuwa hakuna kundi linalojiona wakuja ama wateule na ushindani wao unakuwa maintained katika muktadha huo.

Kukimbilia kupiga kelele za ukabila kila wanapotokea wenye uthubutu wa kuliweka suala hilo wazi, ama kwa faida ya makundi mengine ama kwa faida ya siasa makini hakusaidii hatma ya chama na wala hatma ya siasa zetu. Bila ya kutambua umuhimu wa mjadala wa wazi wa mambo mbalimbali ya kweli ama ya hisia hakuna kikundi cha siasa ambacho kinaweza kufanikiwa katika mazinira ya jamii, utaifa na siasa za Tanzania. CHADEMA na vyama vingine kama CUF wanapaswa kuondokana na utumwa wa kukataa asili na ndipo mwatakapoweza kuthubutu kuchukua hatua za dhati na madhubuti ya kuondokana na jinamizi la asili! Jinamizi hili litaendelea kusinya na hata kudumaza maendeleo ya kisiasa hadi pale watakapokuwa tayari kulizika rasmi kwa uwazi na ushirikishi wa dhati wa makundi mengine kijamii.

Kuendelea kukandamiza mijadala ya suala hili kunaendeleza hisia za kutokuamini haiba na malengo hasa ya chama hicho na pia kunatoa mwanya kwa baadhi ya wanaojiona ni masalia ya wateule wa agenda asilia kuendelea kuamini katika matumizi ya uasili huo kwa faida yao na wakati mwengine hata chama chao lakini kwa upande mwengine kuendelea kukigharimu chama katika muktadha wa maslahi ya muda mrefu. Hili nalo lipo kwa upande wa CUF ambayo historia imeshawaonyesha jinsi gani jinamizi hilo linavyweza kuwa na faida ya muda mfupi lakini hasara ya muda mrefu na bila ya kusahau MTIKILA na kundi lake la siasa za wazawa dhidi ya wakuja zilipomfikisha.

Ujumbe mfupi kwa Godless Lema, M.B





Dear Lema


Unapojiandaa na ushahidi wako wa udini dhidi ya CCM kumbuka wapo wanaojiandaa na uhsahidi dhidi ya CHADEMA. Unapojiandaa na ushahidi wako dhidi ya Udini wa Viongozi waislam, kumbuka kuwa wapo wanaojiandaa na ushahidi dhidi ya Viongozi wakristo. Katika kujiandaa huko kuna wenye dhana na wenye uhalisia na kuna wenye vyote hivyo viwili. Dubwana hili la Udini halitaondoka kwa wewe kuwatuhumu wao na wao kukutuhumu wewe. Dubwana hili litaondoka kwa wao kujiangalia na kujitambua makosa yao na wewe kujiangalia na kutambua makosa yako/yenu. Kudhani kuwa CHADEMA itajisafisha na tuhuma za udini wa kikristo kwa kutuhumu CCM kwa udini wa kiislam, ni ama ujinga ama nia halisi sio kuupiga vita udini bali ni kuuendeleza na kuukuza udini huo ukiamini ndio njia ya kulinda na kupigania maslahi ya upande wako.


Kama nilivyowahi kusema hapo kabla anayedhani kuwa Kikwete ni mdini na ndiye mwanzilishi wa vuguvugu hili la udini hana tofauti na wanaodhani ama kuamini kuwa Nyerere alikuwa mdini na ndiye aliyepanda mbegu za udini huu. Kwangu mimi wote hawa ni wajinga. Simuoni Lema kama mdini lakini naamini ni mjinga na pia anasukumwa na dhambi zake katika kujaribu kujikosha kwa kuwashutumu wengine na kujaribu kuwanasabisha na ubaya wake. Hizi ni aina ya suluhu za mambo makubwa zinazoletwa na wale wenye upeo mdogo wa kisiasa, kihistoria na kiuongozi. Ni suluhu za aina ya siasa nyepesinyepesi zenye kulenga zaidi utashi wa siasa za matumbo zaidi ya siasa za maendeleo.


Udini kama ulivyo ukabila ni sehemu ya fikra za kijamii yetu. Tunachotofautiana sisi na mataifa mengine ni kuwa sisi kama Taifa tunaona udini na ukabila kama tatizo kubwa kuliko tatizo lingine lolote na katika historia ya ujenzi wa UTAIFA wetu hilo limewekewa kipaumbele. Ukweli kuwa hili limesaidia kutulinda na maafa mengi kama yaliyowafikia wenzetu wengine waliojaribu kuukubali na kuurasimisha udini na ukabila kama ni kitu cha kawaida. Naamini hadi sasa tuna mjadala huu kwa sababu tumeaminishwa katika utaifa wetu kuwa hili ni tatizo ambalo tunapaswa wakati wote kulikwepa na kulipiga vita.

Mpaka sasa watanzania tume-epushwa na janga la kupata kiongozi mdini ingawa tunapoelekea siasa hizi zitatufikisha mikononi mwa viongozi wenye hulka na kuendeshwa na fikra hizo. Hizi shutuma dhidi ya Mwalimu Nyerere na Rais Kikwete zinaendeshwa kwa hisia zaidi ya uhalisia. Ndio maana naamini kuwa kama kiongozi haupaswi kufanya siasa hizo bali unapaswa kufanya siasa makini, zenye kuonyesha weledi wa tatizo na zitakazoleta suluhu ya muda mrefu na sio ushindi wa muda mfupi wa upande mmoja utakaoleta maafa ya muda mrefu kwa pande zote.

Kinachoendelea sasa ni kukua na kuelekea kuota mizizi kwa fikra hizi na kupata uungwaji mkono wa baadhi ya viongozi wa kisiasa na kijamii ambao wako tayari kuzitumia fikra hizi kama mtaji wa siasa za kulinda maslahi ya kundi na ubinafsi wao au kuwa silaha dhidi ya maslahi ya kundi ama ubinafsi wa wengine. Kinachoendelea sasa ni kustawi kwa mazingira ya kukuwa kwa tatizo na kulegalega kwa uwezo wa kupambana nalo na hili ni zaidi ya mapungufu ya uongozi kama tuliozoea majibu mepesi tungelipenda kuamini, hii sehemu ya evolution ya siasa zetu za ndani na za kimataifa. Kujaribu kutuhumu kuwa mbegu za udini huu zimepandwa na kundi fulani ama mtu fulani ni propaganda za kisiasa, ufinyu wa kifikra na ujinga wa kimtazamo ambao unaweza kumsaidia mtu ama kundi moja kwa muda mfupi lakini kuwa hasara kwa wote kwa muda mrefu.

Kuhusu ya CUF na pia UAMSHO, CHADEMA na CCM, yote hayo yapo katika hali ya hisia na uhalisia. Kuna yanayosemwa na kuaminiwa kutokana na hisia tu na kuna ambayo yanatokana na uhalisia wa matendo ama muonekano wa baadhi ya wanachama ama kama chama. Matendo na muonekano ambao hushawishiwa na kujidanganya na kuamini kuwa kutumia siasa za udini ama ukabila katika harakati zao ama katika mapambano dhidi ya wengine kunawasaidia kuwahakikishia strong and viable political base ama wengine kuamini kuwa ni sehemu ya siasa. Na kama ambavyo nilivyowahi kusema hapo nyuma, baadhi ya hizi hisia zinajengwa kutokana na kuangalia sana nguvu za chama ama kundi fulani katika dini ama kabila fulani bila ya kupima hayo katika muktadha wa sababu halisi zilizopelekea hivyo kama vile historia ya chama ama kundi hilo.

Lakini kwa upande wangu, sikusita kushutumu tatizo hilo ndani ya CUF (UDINI NA UKABILA) enzi zile na sasa katika sura ya UAMSHO, au katika CHADEMA (UDINI NA UKABILA) na CCM (UDINI NA KUCHIPUKA KWA UKABILA PIA) kuanzia katika uchaguzi wa mwaka 2005 na zaidi 2010. Naamini ni muhimu kukemea pande zote kuliko kukekemea upande mwengine pekee kwani kufanya hilo ni ujinga, unafiki, uzandiki na kama nilivyosema, ni siasa nyepesi nyepesi.

Kujidai kupambana na UDINI kwa kushutumu wenzio tu na kukimbilia kuhalalisha yako kwa msingi kuwa eti wewe una-react tu kutokana na udini wa wengine, kama ilivyo upande wa Uislam na makabila madogo yanayoamini kuwa yana haki ya kuendesha udini na ukabila wao kama njia ya kupambana na udini na ukabila wa wengine, ni kuuendeleza na kuukuza Udini na sio njia muafaka ya kutatua tatizo hili.

Lakini vilevile naamini kuwa katika game hili la kutumia siasa hizi dhidi ya mwenzako, kati ya CUF na CHADEMA kwa upande mmoja na CCM kwa upande mwengine, ni CUF na CHADEMA ndio wenye urahisi wa kuathirika zaidi ya kufaidika na siasa hizi. Historia, ukomavu na utamaduni wa kisiasa ndani ya CCM unawasaidia sana katika kupunguza madhara ya siasa hizi kuliko hali ilivyo katika vyama vingine. Huo ni ukweli mchungu ambao washindani wa CCM mnapaswa kuutambua. Athari za siasa hizi ni kubwa na zenye uwekano mpana zaidi kuumiza CHADEMA na CUF kuliko CCM. Kwa CCm itawachubua tu, kwa CHADEMA na CUF itawadumaza na kuwaangamiza kisiasa.

Ndugu yangu Edward Kinabo anadai hili suala la ushahidi dhidi ya udini wa Rais Kikwete ni zigo la Lema. Naamini hapa na yeye anajidanganya. Hadi sasa wanasiasa waliowahi kutuhumu Udini wa CCM na Kikwete on the record ni Lema, Mchungaji Msigwa na Selasini. Hawa wote ni viongozi wa CHADEMA na wote hawa wamewahi kusikika wakitamka maneno ya chuki ama kuchochea udini. Lema ameyasema yake katika Uchaguzi, Selasini amesema yake wakati wa sakata la kutaka kumuondoa Zitto katika uongozi wa wabunge wa CHADEMA kule Kunduchi wakati Zitto yuko hospitalini akipambana na tatizo la sumu mwilini, Mchungaji Msigwa ukitoa mengi anayoropoka amethubutu kununua filamu ya kumtukana na Mtume Muhammad na kwenda kuionyesha kwa wapiga kura nyumbani kwake na huu ni ushuhuda wa Mbunge mwezake wa CHADEMA. 

Ukichukulia kuwa Lema amesikika akisema kuwa Mwenyekiti wake Freeman Mbowe ambaye mimi naamini kuwa yeye si mjinga wala si mdini amemzuia kutoa huo ushahidi wake bungeni kwani sio wakati muafaka pamoja na hayo mengine niliyoyagusia hapo juu, ni wazi kuwa endapo Lema na hawa vinara wengine wa CHADEMA wataendelea na siasa hizi (najua kuwa wapo vinara wa CCM pia wanaozishabikia siasa hizi chini kwa chini), CHADEMA haitaweza kupambana na hisia zitakazojenga mtazamo kuwa zigo hili ni la CHADEMA na sio la Lema pekee.


Ndio maana nasema kuwa UDINI huu hautaondoka kwa kutuhumiana bali kujitambua, kubadilika na kutafuta muafaka na kamwe hautaweza kupigwa vita kwa kuruhusu waliokosa uhalali wa kimsingi ndio kuwa sura ya mapambano dhidi ya udini, hasa udini wa wengine na sio udini wao.


Katika hali iliyofikia sasa, mimi naamini kuwa moja ya njia madhubuti ya kupambana na udini ni sisi wenyewe kuangalia udini wa pande zetu, Kuuepuka, kuukemea na kuupinga wakati tukijaribu kuuelewa undani wa udini wa upande mwengine na kutafuta muafaka wa kukabiliana nao kama kwa kuutambua chembe ya ukweli wa hisia zao ama kuupiga vita kwa ujumla wake. 

Zaidi mimi naamini njia moja kubwa ya kuhakikisha tunadhibiti uhodhi wa siasa nyepesi zinazoshamiri katika kushape mjadala huu wa udini kama inavyoelekea kuwa, na kama njia ya kuondoa mazingira ya siasa hizo kustawi, kuna haja ya kuunda Tume ya Ukweli, Uwazi na Maridhiano ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa jukwaa la kuweka wazi ukweli ili kudhibiti hisia na kutambuana misingi ya madai ya msingi ya pande zote na kukubaliana kwa pamoja jinsi ya kuondokana na janga hili. Na haya tutaweza kuyafanya kwa kukubali kuwa Udini haujaanza na Kikwete wala Nyerere.


Muafaka haupatikani kwa ushindani wa nani mbaya nani mzuri, Muafaka unapatikana kwa kushirikiana wabaya na wazuri. Tujitambue, tubadilike na tuafikiane ndio njia salama.

Mtizamo wangu kuhusiana na sarakasi za CHADEMA na Katiba Mpya!


CHADEMA wapongezwe kukwepa kitanzi cha kisiasa walichojiwekea!



Kitendo cha CHADEMA kushindwa kutimiza ahadi yao ya kujitoa katika mchakato wa katiba mpya kama ilivyotangazwa hapo awali na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe alipotoa hotuba yake bungeni na kuwekewa msisitizo na Katibu Wilbroad Slaa kinatoa mafunzo mengi kisiasa.

Mosi, ni muhimu kuwapongeza wale waliothubutu kuona mbali na kukwepa mtego huo wa kisiasa waliojitegea hapo kabla ambao kama wangeuingia basi ungeliweza kuwamaliza kisiasa. Wahenga wanasema “never use toothless brinksmanship as it will only take you into oblivion”. CHADEMA walifanya makosa kuamua kutishia kujitoa lakini wanapaswa kupongezwa kwa kurudi nyuma kwa style ya aina yake.

Pili ni muhimu kuielewa CHADEMA katika suala zima la Katiba mpya. Kwa mtazamo wangu suala la katiba mpya ndani ya CHADEMA halikuwa na mvuto mkubwa kwa maana ya umuhimu wake katika kuendeleza na kusimika mfumo wa kidemokrasia kama ambavyo wengi tungelitegemea. Kwa CHADEMA Katiba mpya ilikuwa ni propaganda ya kisiasa iliyokuwa ikitumika pale inapotokea haja ya kutafuta mchawi wao kushindwa uchaguzi. Lakini pia kimkakati, katiba mpya ilipaswa kuwa ajenda endelevu ya kisiasa kuelekea katika uchaguzi wa 2015. 

Kitendo cha Rais Kikwete (sio CCM) kuikubali na kuitekeleza hoja hiyo ni kitendo ambacho hawakukitegemea na ukweli kimewaondolea ajenda muhimu kisiasa. Hivyo basi uungaji mkono wao wa hapo awali ulikuwa wa kulazimika lakini sio kwa kupenda hivyo ndio maana kila inapotokea mwanya wa kuchakachua uhalali wa mchakato huo, kina Tundu Lissu hawapotezi muda kuutumia.

Vilevile CHADEMA wanahofia uwezekano wa zoezi hili la katiba mpya kumalizika kwa mafanikio kwani ni wazi kitamkuza sana kisiasa, ndani na nje ya nchi, Rais Kikwete na hivyo yeye kuweza kuwa na ushawishi zaidi katika siasa za uchaguzi mkuu wa 2015. Hivyo kimkakati CHADEMA wanaonelea ni muhimu ama kuchakachua uhalali wa mchakato huo ama hata kuuvuruga kabisa usifanikiwe, hapo watakuwa wameweza kuikomboa ajenda hiyo na kuendelea kuitumia kuelekea 2015 lakini pia kumpunguzia nguvu za kisiasa Rais Kikwete kuelekea 2015.

Kwa nini tishio la CHADEMA kujitoa katika mchakato lilikuwa ni kitanzi cha wao wenyewe kujinyonga kisiasa?

Endapo CHADEMA wangejitoa leo na huko mbeleni, Tume ikaja na Rasimu ya Katiba Mpya ambayo itakuwa na mabadiliko makubwa yatakayokubalika na watanzania walio wengi wenye kuangalia mustakabali wa taifa zaidi ya ushabiki wa kisiasa, hilo lingekuwa kosa kubwa sana kwao kisiasa kwani wangeonekana wamekurupuka kuchukua msimamo wa kujitoa na pia ingelikuwa rahisi kwa wapinzani wao kisiasa kutumia hilo kudhihirisha kuwa CHADEMA ni chama pinga tu na hakina weledi wa kisiasa.

Vilevile mtego mwengine waliokuwa wamejiwekewa na ulikuwa ukiwasuburi kama hatua ya pili baada ya kujitoa ni jinsi gani wange-deal na uasu wa Prof Baregu ambaye amesema wazi kuwa akiambiwa kati ya kuchagua chama na Taifa basi atachagua chama. CHADEMA ambao wanatuhumu kuwa CCM inaingilia mchakato wamekuwa wakimlaumu Prof Baregu kwa kutuwapa ya ndani ya Tume ya Katiba kitu ambacho kwa wenye busara na maadili walipaswa kumpongeza Prof Baregu kwa kutii miiko ya kazi yake. Hapo ndipo wangelazimika kufanya makosa makubwa zaidi. Ukichukulia vita ya muda mrefu wanayompiga Naibu Katibu mkuu wao Zitto ambaye anaonekana kama sura ya siasa za kisomi na kimuono ndani ya CHADEMA na anayeonekena kushabihiana kifikra na Prof Baregu, CHADEMA wangefanya kosa kubwa sana kumuongeza na Prof Baregu katika listi yao ya wanaoawachimba kama maadui wa ndani. Ni dhahiri hili lingekuwa kosa jingine la kuwathibitishia wenye akili zao kuwa kile kirusi cha kupiga vita USOMI kimejikita pia CHADEMA. NA hapo wangeweza kupuputisha baadhi ya wasomi na watu wa tabaka la kati ambao wamekuwa waki-sympathies nao wakidhani kuwa kuna uwezekano wa CHADEMA kuwa mbadala makini wa CCM.

Kuhusu hoja ya kuwa CCM wanaingilia mchakato wa katiba, ukweli huu ni uthibitisho wa muendelezo wa siasa za hisia usio zisizojali kuchanganua ukweli ambazo wamekuwa wakizitegemea kufikia maamuzi yao mengi. Ni wazi kuwa vyama vyote vya siasa na hata makundi mengine ya kimaslahi vyote vimekuwa na mikakati ya kuhakikisha kuwa maon, mitizamo na maslahi yao yanakuwa na ushawishi katika mchakato huo. Cha ajabu ni kuwa CHADEMA hawakukemea wala kuhoji kitendo cha makundi ya kidini kuingilia mchakato huo kwa kuwaamuru wafuasi wao kwenda katika mikutano ya uchaguzi wa mabaraza ya katiba na kuchagua wawakilishi kwa vigezo vya Udini. Haya yamefanyika na makundi ya dini zetu zote mbili, Waislam na Wakristo na yamefanyika misikitini na makanisani. Kwanini CHADEMA hawajalichukulia kosa hilo kwa uzito unaostahili?

Kitendo cha viongozi wa CCM kujadiliana wao kwa wao bila ya kuwasiliana ama kushurutisha Tume ya Katiba hakuvunji sheria ya mchakato wa katiba kama Tundu Lissu alivyotaka kuaminisha umma. Walichofanya viongozi wa CCM ni kujipanga kisiasa kama ambavyo wenzao wengine wakiwemo CHADEMA wanavyofanya. Ni CHADEMA ambao wamefikia hata kukaa kama kamati kuu ya chama, kujadili kuhusu jinsi gani ya kuendeleza harakati zao ikiwemo jinsi gani ya kushutisha tume kufuata matakwa yao yatakayowezesha maslahi yao kisiasa, kumlaumu mwenzao kwa kukosa kuwapa ushirikiano na hata kufikia kupiga kura za kama chama kujitoa katika mchakato mzima na kumuondoa mwakilishi wao Prof Baregu katika tume ya katiba. CHADEMA wanapaswa kuchukulia matokeo ya kushindwa kupenyeza watu wao kwa wingi katika mabaraza ya katiba ni somo la wao kujijenga zaidi kimikakati na kuwa watanzania bado hawajawa mashabiki sana wa siasa za mipasho na kupiga kelele sana kama ambavyo makada wao wengi wamekuwa wakijipambanua hata huko mitaani kulipofanyika chaguzi za awali za mabaraza ya katiba.

Hivi kesho ikaja kujulikana kuwa hata Mwenyekiti wa CCM hakuwa tayari kutoa maoni yake mbele ya tume kwa kuepuka kuishinikiza ama labda maoni rasmi ya CCM yaliyowakilishwa katika tume hayana sehemu yoyote ambayo hawako tayari kutafuta muafaka wa pamoja, CHADEMA walionyesha wazi misimamo yao na kufikia hata kuweka vitisho endapo misimamo yao haitafuatwa, ni nani ataonekana hayuko makini?

Suala la kutumia ujanja wa kuikashifu, kuishusha na kuiadhiri Tume ya Katiba kwa kigezo cha posho wanazopangiwa na wizara sitaliingilia kwa undani wake, lakini mtizamo wangu ni kuwa siamini kama kuna Mbunge mwenye audacity ya kushutumu posho za wengine isipokuwa ndugu yangu Zitto Kabwe na wengine wachache ambao hadi leo wameendelea na msimamo wa kususia posho walizojiwekea wabunge wenzie. Tundu Lissu anapohoji walimu kulipwa shilingi 325,000 kwa mwezi anasahau kulinganisha na yeye anavyolipwa shilingi 330,000 za posho kwa siku. Mbunge anayelipwa milioni 11.2 kwa mwezi kwa kazi aliyogombania kutumikia anahoji malipo ya mil 7 kwa mwezi kwa kazi ya kuombwa kutumikia. Anasahau ama anajisahaulisha kuwa kila siku anakusanya posho ya kikao 200,000 na posho ya kujikimu 130,000 ambapo Jumla 330,000. Hapo bado mshahara na posho ya ubunge jumla tshs 11.2m kwa mwezi. Kwa ujumla kila siku Tundu Lissu anapokea wastani wa 370,000 awepo au asiwepo bungeni. ie mshahara na posho ya ubunge na 330,000 kwa siku katika siku 130 kama posho anapokuwepo bungeni na katika vikao vya kama. Sasa kwa kweli inahitaji ujasiri wa ajabu kwa mtu kama huyu kusimama na kuhoji posho za wenzie tena tofauti na yeye aliyegombea kutumikia, wenzake ambao wameombwa kutumikia Taifa na kuacha shughuli zao zingine.

Kwa kweli hadi kufikia sasa tumeona mengi na wenye upeo wa kujifunza naamini watakuwa wamefaidika sana kujifunza jinsi ya kutofanya makosa ya kisiasa kirahisirahisi kama wenzetu hawa, lakini zaidi kwa wanachama na wapenzi wa CHADEMA tambueni kuwa kwa maslahi ya nchi yetu, CHADEMA hakipaswi kurudia historia ya vyama vilivyokuja na kupita na hivyo kurudisha nyuma harakati za kujenga mfumo makini wa demokrasia ya vyama vingi nchini. Jitambueni, Jifunzeni na Jirekebisheni kwani mnaweza kama mlivyofanya leo kwa kuacha kutekeleza kitisho chenu cha kujitoa mlichokiweka wiki mbili zilizopita...