Huyu ndio Lwaitama... Sijashangaa!

25th Nov 2013

Nimesoma andiko la Dr Lwaitama. Mzee wetu na mwalimu wetu lakini pia mpambanaji wa kudumu katika mapambano ya kifikra. 

Nimeangalia andiko lake katika angle mbalimbali na kugh'amua sababu ya alichokiandika, sina uhakika kama ndio msimamo wake lakini nia ya andiko lake linalolenga kuhalalisha hatua ya CHADEMA kuwasimamisha uongozi Zitto na Kitila.

Naamini andiko lake linalenga katika kitu kimoja kikubwa. Hofu ya kuwa na upinzani legevu ama kudumaa kwa nguvu za upinzani zilizokuwa zikionyesha kukuwa. Hofu ambayo hata mimi ninayo na inapaswa kuwepo miongoni mwa wote wapenda maendeleo ya demokrasia nchini kama mimi na ndugu yangu Zitto na pia wale waumini wa ajenda ya kuing'atua CCM madarakani hata kwa mbadala wowote.

Katika andiko la Mzee Lwaitama ameangalia kitu kimoja pekee, nacho ni ule mkakati wa mabadiliko ndani ya chama uliondaliwa na Samson Mwigamba na kuhaririwa na Dr Kitila Mkumbo.

Mzee Lwaitama amejaribu kufumbia macho sababu zingine zote zilizofikisha hitimisho la kuwavua nafasi zoteuongozi Zitto na Kitila. Uamuzi ambao sasa unaonyesha wazi kuwa ni batili kutokana na ukiukaji mkubwa wa katiba ya chama hicho na uchakachuaji wa taratibu zao, ingawa wahusika wameamua kukubaliana nao. 

Ningeliweza kusema kuwa hiyo yawezekana ni kwa sababu yeye kama walivyo wengi wanategemea habari za siasa zetu zaidi kutoka na kile kinachoripotiwa ama kuwekwa wazi katika vyombo va habari. Yaani ametengeneza angalizo lake katika muktadha wa taarifa rasmi ya uongozi wa CHADEMA pekee. Ningeliweza kusema labda hakusikia utetezi wa kina Zitto ambao ulikuwa na ufafanuzi wa kile kilichojiri katika kikao kilichofikia maamuzi hayo magumu aliyoyasifia. Lakini hapana. Katika andiko lake pia amewatuhumu kina Zitto kutokana na utetezi wao hivyo ni wazi amesikia ama kusoma taarifa ya kina Zitto kwa umma kupitia vyombo vya habari.

Mzee Lwaitama kama ilivyo kwa uongozi wa CHADEMA na pia muasisi wa chama hicho Mzee Mtei wamekwepa kabisa kukubali ukweli kwamba, moja; uamuzi uliofikiwa ni kilele cha safari ndefu iliyoanzia mwaka 2009 mara baada ya Zitto kutaka kugombea Uenyekiti wa chama hicho na kuambulia kuambiwa na mwenye chama kuwa kama anataka uenyekiti aende akaanzishe chama chake. Pili; uamuzi uliofikiwa ulifuatia mjadala mrefu wa zaidi ya nusu ya muda wote wa kikao uliohusiana na kinachoitwa usaliti wa Zitto wa kukiumbua chama chake kwa unafiki wa suala la uwazi na umakini wa matumizi ya kodi ya wananchi wanayopata kama ruzuku. Tatu; kuwa mbali na tuhuma ya kuandaa mkakati wa kugombea uongozi kinyume na mipango rasmi ya viongozi na wenye chama, kilichotokea ni hitimisho la tuhuma na juhudi lukuki za kumtuhumu Zitto kwa usaliti wa maslahi ya chama chake na hata kumbambikia fitna ya kuhongwa na CCM na vyombo vya usalama ili kufanikisha hilo.

Mzee Lwaitama hakufanya hilo kwa kupitiwa bali kwa makusudi ya kuweza kujenga hoja yake ambao imelenga katika kuilinda CHADEMA na athari za uamuzi wao ambao umekiuka hata misingi ya katiba yao. Na hapa ndipo namuona Mzee Lwaitama amepitiliza hata ile hulka yake niliyoizoea. Kwa andiko hilo ni wazi anapambanua kuwa kwake yeye ni sawa kabisa kuvunja katiba ama kutumia vibaya misngi ya katiba ili kufanikisha mchakato wa kuonyesha kuwa CHADEMA ni mahiri zaidi ya CCM. 

Lakini pia hata tukiangalia suala hili kwa msingi wa huo mkakati pekee. Hapa Mzee Lwaitama hajaitendea haki sifa yake ya uanamapinduzi. Labda ndio masuala ya ustaafu haya, spirit ya uanamapinduzi inapungua kiasi. 

Unapoahalalisha matumizi mabaya ya sheria ama uchakachuaji wa misingi ya katiba yako ili kufanikisha maamuzi unayo amini ni muhimu kwa usalama wa kundi lako na maslahi yake, ni dalili ya ama kutokuwa muaminifu wa siasa za misingi ama kuwa tayari na kuenzi hulka ya uvunjaji misingi ndani ya kundi hilo na kwa kuwa kundi hilo ni kundi la kisiasa ina maana kuwa unarasimisha utamaduni hatari ambao utaathiri zaidi taifa letu kuliko kuliokoa kama ambavyo Mzee Lwaitama anaamini kuhusiana na utume wa CHADEMA.

Vilevile inaelekea Mzee Lwaitama ama hajasikia ama hataki kuamini kuwa ingawa Zitto ni mlengwa nambari moja wa mkakati huo lakini yeye hakuhusika kuandaa wala hata kuona hadi ulipowekwa wazi katika kikao cha kamati kuu ya chama chake. Ukiondoa ushuhuda wa kitila kuwa Zitto hakuona mkakati huo hapo kabla lakini hilo linajionyesha wazi hata ndani ya waraka huo ambao unaema wazi kabisa kuwa endapo Zitto ambaye ndio mlengwa mkuu akikataa kukubaliana na mkakati huo yaani kukubali kugombea uenyekiti wa chama chake katika uchaguzi unaokuja basi wengine akiwemo Kitila na Mwigamba na wengineo ndio waangaliwe kuchukua nafasi ya Zitto kufanikisha mkakati ho.

Vilevile nashindwa kukubali kuwa Mzee Lwaitama ameshindwa kung'amua kuwa kama ni suala la makundi basi hata hao waliowashughulikia Zitto na Kitila ni sehemu ya siasa za makundi ndani ya chama hicho na pia tuhuma hizo pamoja na uamuzi wa tuhuma uamuzi wa kuwasimamisha uongozi na kutaka kuwanyang'anya uanachama ni sehemu ya mkakati wa upande mwengine kuhusiana na mchakato wa madaraka ya ndani ya chama hicho. Yawezekana kundi lingine ama pia wakawa na waraka wao ama wakawa wamekosa weledi wa kuweza kujenga mikakati yao kisomi kama inayojioyesha katika mkakati wa Mwigamba, lakini mkakati upo na unatekelezwa kwa rasilimali na vikao halali na haramu vya chama chao.

Lakini zaidi, Mzee Lwaitama anapohalalisha siasa za makundi za upande wa watawala wa chama na kuwataka kina Zitto kuendelea kukandamizwa na wao kujizui kutojitetea ama kupanga mipango itakayokikomboa chama chao kutoka katika hatima inayojongea kwa vhama chao na taifa lao kutokana na fikra potofu na matendo maovu ya walio madarakani  ati kwa kuwa taratibu za chama chao haziruhusu hilo, hapo ni sawa na kuwaambia ndugu zetu wa Palestina kuwa wana makosa ya kupanga na kutekeleza mipango yao ya kulikomboa taifa lao kutokana na ukoloni, ukandamizaji na ubaguzi wa Waisraeli kwa kuwa wanakiuka sheria za watawala wao na waliopaswa kutokujiona wanaweza bali wafuate taratibu zilizopo.

Lakini pia katika hili ndipo ninaposema kuwa Mzee Lwaitama ameandika andiko lake kama vile ni mmoja wa wale wachambuzi wetu mahiri ambao hufanya uchambuzi wao katika masuala mbalimbali kwa kutegemea hisia zao, maslahi yao na taarifa aka propaganda zinazopatika katika vyombo vya habari pekee. Kitu ambacho sitaki kukiamini kwani hakujuana na Zitto na Kitila barabarani kama alivyojuana na Mbowe, Dr Slaa na Tundu Lissu hivyo ni wazi anajua maswahiba yaliyowakumba ndugu zake hawa kwa miaka zaidi ya mitano sasa hadi kufikia kilele chake sasa.

Anajua wazi ni jinsi gani Zitto amejitahidi kunyamazia mengi na hata wakati mwengine kudanganya umma kuwa hakuna mgawanyiko ndani ya chama chake au hata kuwa hakuna mipango ya kummaliza kisiasa na kimaisha pale yanapotokea mambo kama hayo mradi tu kulinda usalama na ustawi wa chama chake.

Mzee Lwaitama anapowakemea ndugu na wadogo zake Zitto na Kitila kwa kuthubutu kujitetea hadharani kutokana na ujahili wa kisiasa wa baadhi ya viongozi wa chama chao kitu ambacho anakiona kama kinatishia uimara usiokuwepo wa CHADEMA, Ni tukio ambalo kulielewa unapaswa kujua kwa undani jinsi anavyongalia siasa za nchi yetu na ni jinsi gani anaamini ndio inaweza kututoa hapa tulipo. 

Nakubaliana na hisia za baadhi ya watu akiwemo Mzee Lwaitama ambao wanaamini kuwa CHADEMA na mapungufu yake yote ilifikia lile lengo la kuwa na upinzani utakaoweza kuipa changamoto CCM na serikali yake na hali hii inaathari katika hilo. Lakini pia kinachoendelea sasa ni zaidi ya kuendeleza nguvu hizo za uoinzania mahiri. Ni mpambano wa kujenga upinzani madhubuti wenye kulenga kuandaa mbadala makini badala ya bora mbadala. 

Mzee Lwaitama anaungana na wanaojaribu kujidanganya kuwa mapungufu makubwa yaliyopo CHADEMA yanapaswa kuendelea kuachwa hadi pale ushindi wa kuiondoa CCM madarakani utakapopatikana. Lakini ukiwauliza baada ya ushindi kupatikana, yaani waheshimiwa hawa wanaofanya haya sasa watakapokuwa na dola mikononi mwao, inawezekana kweli wakajirudi na kuondokana na mapungufu yao ya sasa kwa manufaa ya kuepusha athari zake kwa Watanzania na Tanzania yetu? Mimi naamini hapana. Kama ilivyo vigumu kwa CCM kujisafisha hivi sasa ndivyo itakavyokuwa vigumu CHADEMA kusafishika ikiwa madarakani. Cha ajabu yeye kama mmoja wa wanaoamini kuwa njia pekee ya CCM kujisafisha na uozo uliokigubika chama hicho ni wao kutolewa madarakani ndio pia mmoja wa wanaojidanganya kuwa CHADEMA ya sasa itaweza kubadilika itakapokuwa madarakani.


Kwa kifupi andiko la Mzee Lwaitama halijalenga kujipendekeza kwa watawala watarajiwa wa CHADEMA bali kujaribu kupunguza athari za mafanikio ya kimtizamo maslahi lakini makosa ya kisiasa ya kundi la viongozi hao katika kulidhibiti kundi la wanamadiliko ndani ya chama katika muktadha mzima wa hatma ya chama hicho na nafasi yake katika kuwabana CCM.

Salamu kutoka Jeriho na Dead Sea

14th Nov 2013


Jana siku ya Jumanne mimi na wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kutembelea mji wa Jericho. Huu ni mji ulio chini kabisa kwa kiasi cha mita 250 chini ya kina cha bahari. Ni mji wa kale zaidi duniani ambapo utafiti wa kihistoria unaonyesha ulikuwepo tangia miaka 10,000 iliyopita. Ni mji wenye umuhimu mkubwa kwa waumini wa dini ya kikristo kwani ndio mji ambao Nabii Issa bin Mariam ama Yesu alitumia sehemu kubwa ya maisha yake ya unabii akiwa hapo. 

Mji wa Jericho upo kiasi cha kilometa.... kutoka Ramallah. Safari ya kwenda Jericho ikanikutanisha tena na uhalisia wa ukoloni wa kiisraeli. Njiani unapotoka Ramallah unapita pembezoni mwa ukuta wa utenganisho na vizuizi mbalimbali vya kutoka na kuingia upande wa maeneo rasmi ya Waisraeli vikiwa na ulinzi mkali wa wanajeshi na ngome za Waisraeli. Karibia barabara zote za kutoka mji wa Ramallah kuelekea Jericho ambako pia ndio mwelekeo wa Bethlehem na Hebron, kuna misururu mirefu inayotokana na magari yanayotumia masaa kadhaa kuvuka vizuizi hivyo kikiwemo kile cha khalandiya kinachounganisha Ramallah na Jerusalem.

Njiani kuanzia hapo Ramallah tunaweza kuona makazi mbalimbali haramu ya waisraeli katika ardhi ya wapalestina pamoja na kuta zinazozungukua makazi hayo. Mara tu tunapotoka katika viunga vya mji wa Ramallah tunaanza kukitana na magari ya wanajeshi wa Israeli na matangazo mbalimbali ya lugha ya kiisraeli na machache yenye tafsiri ya kiarabu. Lakini kila tunapozidi kuelekea Jericho ama Jeriho kiyahudi na Ariha kwa kiaarabu, ndipo sura ya ukoloni wa waisraeli inazidi kujionyesha.
Njiani tunapita barabara ya kuelekea Nabil Mussa ambako inasemekana ndipo alipozikwa Nabii Musa. Pia tunapita katika sehemu maarufu ya Good Samaritan ambapo katika masimulizi ya dini kuna hadithi ya watu waliokuwa na sifa ya kutoa msaada kwa wageni na wapota njia. Hapa ndio asili ya jina la Good Samaritans. 

Tunapoingia tunakutana na ngome ndogo ya wanajeshi wa Israel ikililinda mashamba na viwanda vya waisraeli katika eneo hilo. Tunapowasili Jericho, tunakwenda moja kwa moja katika mti wa kihistoria ujilakanao kama Sacyamore ambao mtoza ushuru fisadi aliyeitwa Zakeo aliyekuwa akichukiwa sana na wenyeji kwa kuwafanyia kazi wakoloni wa kirumi alipanda kutokana na ufupi wake ili kuweza kumuona Nabii Issa bin Mariam kabla ya nabii kumuuliza maswali na kumtaka amkaribishe nyumbani kwake. Tukio hilo liliwashangaza sana wenyeji na kuhoji kwanini Nabii Issa alitaka kwenda kwake mtu mbaya kwao.

Baada ya hapo tukaelekea katika kisima ambacho kipo katika mji wa kale wa Jericho. Hapa kuna kisima chenye historia ambapo inasemekana kuwa Nabii Elisha alifika pale na kukutana na watumiaji wa maji hayo wakilalamika kuwa maji hayo yanasababisha magonjwa mengi na kinamama kuharibu mimba. Naye akayabariki na kutamka kuwa kuanzia wakati huo maji hayo yatakuwa salama kwa wanayoyatumia. Juu ya kisima hicho kuna machimbo mbalimbali ambayo yamechimbwa kuibua mabaki ya majengo ya zamani ya mji wa kale.

Baada ya hapo tukaanza safari ya kuona mlima wa majaribu aka Mountain of Temptation ambao Nabii Issa kabla ya kuanza maisha ya Utume wake alikwenda huko kwenye mfungo wa siku arobaini kwa utakaso. Baada ya hapo tukaenda katika Hekalu la Mfalme Harrod ambalo lilikuwa ni makazi yake ya wakati wa baridi.

Kutoka hapo tukaanza safari ya kuona Bahari Mfu aka Dead Sea. Huko nako tukakumbana na jeuri ya ukoloni wa Waisraeli. Njiani tunakutana na magari ya kijeshi ya Waisraeli huku mabango yote ya barabarani yakiwa yameandikwa kwa lugha ya kiyahudi pekee. Huko tunaingia katika hoteli ya kitalii iliyo kando na bahari hiyo. Hapo tunakaribishwa na bendera za Israel zikithibitisha kuwa eneo hilo ni mali ya Waisraeli. Hapo tunakutana na kundi kubwa la Waafrika wakiwa na mabasi makubwa ya kitalii yenye namba za kiisraeli. Hili ni kundi la Wanigeria walio katika safari ya Hijja. Mbele ya basi lao kuna bango linalosema Vuguvugu la Wakristo wa Nigeria Marafiki wa Ardhi Takatifu na kwamba ziara ya yao ni sehemu ya ziara ya Rais wao Goodluck Jonathan atakayoifanya nchini Israel. 

Baada ya kuulizia tunambiwa kuwa hapo wanaingia watu walio katika makundi maalum (walioingia kupitia Israel na kutumia makampuni ya utalii ya kiisraeli). Wageni hatari sisi inatubidi kwenda kutafuta sehemu nyingine ya kuingia katika bahari hiyo ya kihistoria. 

Baada ya mwendo mfupi tunaingia katika eneo lingine nalo likiwa na bendera ya Israeli. Hapo tunakutana na mama wa Kiyahudi mlangoni na baada ya kujitambulisha anatueleza kuwa alikuwa Tanzania miezi michache iliyopita na kwamba ameipenda sana nchi yetu. Hapo tunatakiwa kulipa hela za kiyahudi 50 zenye thamani ya dola 15 ili kuingia katika eneo la bahari hiyo. Hapo tunakuta mamia ya watalii wakikoga maji hayo yenye chumvi kali na wengine wakijipaka udongo kwa imani kuwa maji pamoja na udongo huo ni dawa ya magonjwa mbalimbali ya ngozi. Wapo walikuwa na chupa za maji wakijaza maji hayo na wengine wakijaza udongo wa hapo. Zote hizo zawadi kwa ndugu waumini wenye kuamini katika baraka ya maji na udongo huo.

Ukitaka kudumaza mapinduzi waonjeshe utamu wa maisha


12th Nov 2013




Kutembelea Palestina ni somo la kisiasa. Kila unapokwenda unazungukwa na uhalisia wa siasa za kikoloni na kibaguzi lakini pia hulka ya watu wake katika mapambano ya kupigania uhuru wao na kuboresha maisha yao. 

Siku ya jumatatu jioni mimi na wenzangu tulipata nafasi ya kushiriki maandamano ya kupinga mauji ya Comrade Arafat hapa mjini Ramallah! Maandamano hayo yaliongozwa na bendi ya Scouts na vikunfi vya chipukizi na vijana wa chama cha Fatah wakiwa kayika mavazi ua mapambano! Maandamano hayo yalipita katika barabara mbalimbali za Ramallah.

Mji wa Ramallah ni mji unaofanana sana na miji mingi ya nchi zikizoendelea kiasi cha kuweza kujisahau kuwa upo katika utawala na ukandamizi wa kikoloni wa Waisraeli. Mji wa Ramallah ndio makao makuu ya Mamlaka ya Wapalestina. Ni mji uliojengwa katika vilima mithili ya ile milima ya mji wa wanza lakini hapa ni mji mzima ni vilima vikali. Ni mji unaopendeza saa na unaojengeka na kupangika barabara mithali ya mji mpya kabisa. Ni mji ambao una kila mandhari ya miji ya ulaya hasa ile iliyopo katika ukanda wa bahari ya mediteranian. Kitu kimoja kilicho wazi ni jinsi gani ujenzi wa mji huo unavyofuata sheria za mipango miji. Karibia majumba yote yamejengwa kwa kutumia matofali ama mawe yaliyokatwa kwa mfano wa matofali ya aina moja. Nyumba zote zimenakshiwa kwa nakshi za mithili ya majengo ya kizamani. Majengo yote yana rangi moja ya maziwa. Shughuli za ujenzi zinaendelea kila mahala.

Mji wa Ramalla ni mji wa kisasa uliojaa majengo ya kuvutia na ujenzi kila upande. Ni mji wa wasomi kukiwa na asilimi tatu ya wasiosoma. Wakazi wengi wa Ramallah wana elimu ya chuo kikuu. Kwa mujibu wa Nabil Shath, elimu ni sehemu ya mapambano ya wapalestina.

Najaribu kutafuta alama zozote za majumba yaliyoshambuliwa nakubomolewa na waisraeli katika mojaya kampeni zao dhidi ya mji huu bila ya mafanikio. Uzuri wa mji huu umenishtua sana na kujaribu kujiuliza kama ndugu zangu hawa baada ya kuonjeshwa utamu wa maisha haya wanweza kweki kusimam kidete kupambana na ukoloni wa Waisrael ambao ni wazi hawana mpango wa kuondoka katika maeneo waliyoyakwapua na kuyakalia kimabavu kuanzia Mashariki ya Jerusalem hadi ukingo wa mto jordan. 

Moja ya picha nilizobahatika kuzipiga ni picha ya kikundi cha maskauti kikiwa katika gwaride mbele ya KFC, moja ya alama za nguvu ya tamaa za kibepari duniani. Ni vigumu kuamini kuwa pale siku ya kuanzisha mapambano mengine ambayo yanaweza kupelekea Waisraeli kubomoa kila kilichojengwa kama wafanyavyo, vijana hawa watakuwa tayari ku-risk kupoteza ulabu huu wa masiha ya kiulaya. Hata hivyo nakumbuka hali ya kambi ya wakimbizi iliyo karibu na mji wa Ramallah ambayo tuliona wakati tukiwa tunakuja Ramallah kutokea mpakani. Ni wazi hali mbaya wanayoishi wakimbizi hawa bado ni chachu ya utayari wa mapambano ya ukombozi kamili kwa wapalestina wote.



Maandamano yalifikia mwisho katika eneo la mashujaa ambako kuna kaburi la muda la Comrade Arafat. Ni kaburi la muda kwa sababu mpango ni kumzika Jerusalem mara baada ya harakati za ukombozi kamili kufanikiwa. Hapo tunakutana na jengo zuri la aina yake likiwa limezungukwa na ukuta mkubwa wenye ulinzi mkali wa askari wa kipalestina. Ndani ya eneo hilo tunakuta askari wa kipalestina wakijipanga kwa gwaride maalum huku vigogo mbalimbali wa historia ya mapambano ya wapalestina, wengi wao ni wazee wa miaka sitini hadi themanini, wakijipanga pembeni. Lakini pia kuna kundi kubwa la watoto wadogo wakiwa katika mavazi maalum wakiwa na bendera na mapicha ya Comrade Arafat. 

Baadaye kidogo aliwasili Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina ambaye baada ya kusalimiana na vigogo wenzie anapita katikati ya garide la askari kwenda kuweka shada la maua katika kaburi la Comrade Arafat. Kaburi hilo lipo ndani ya jumba kubwa likiwa limezungukwa na walinzi maalum wawili wakiwa mbele ya mlango wa kuingilia na wengineo wakiwa wamesambaa kulizunguka jengo hilo. Baada ya hapo ndipo makundi ya watu mbalimbali kutoka kila pande ya dunia walipoanza kwenda kuwe mashada ya maua katika kaburi la Comrade Arafat.

Baada ya shughuli hiyo mimi na mwenzangu tunaamua kutembea kwa miguu kuzunguka mji huo. Tofauti na nyumbani huku maduka yanabaki wazi hadi saa nne usiku. Tunajaribu kuulizia bei za vitu tukilinganisha na nyumbani, ukweli vitu hapa ni ghali kiasi na hii inasababishwa na kodi kubwa inayotozwa na mamlaka ya kodi ya Israeli. Hata kama kodi hiyo inapaswa kukabidhiwa kwa mamalaka ya wapalestina ambapo mara nyingi wamekuwa wakikataa kukabidhi kama sehemu mojawapo ya vikwazo dhidi ya wapalestina, kodi hiyo ni kubwa sana ukilinganisha na kipato chao na kile cha waisraeli. Wakati Waisraeli kiwango cha chini cha mshahara ni pesa za kiisraeli 4,500 kwa mwezi, kwa upande wa wapalestina ni 1500. Mmoja wa wauza duka alitueleza kuwa endapo wapalestina wasingekuwa na umuhimu kwa uchumi wa Israel basi wangekuwa wameshatoswa baharini.

Hii inanifungua macho kuwa utawala wa kimabavu wa Waisraeli katika maeneo ya Wapalestina sio kwa minajili ya imani za kidini na uasili pekee bali pia u a umuhimu wa kipekee kwa uchumi wa Israeli. Kwa kifupi wapalestina wanachangia kama sio kulipia kila matumizi ya waisraeli katika kuwakandamiza wapalestina naia kulinda na kupanua ukoloni wao. Israeli inafaidika sana kiuchumi kutokana na kodi, cheap labour, maliasili, utalii na hata soko la wapalestina.


USO KWA USO NA UKOLONI WA ISRAEL


Nov 11, 2013

"Unaenda kufanya nini Israel?" Hilo ndilo swali ambalo linalonikaribisha uso kwa uso na madhila ya ukoloni wa Waisrael katika ardhi ya wapalestina. Huu ndio uhalisia ninaokaribishwa nao nikianza msafara wangu wa kihistoria katika ardhi ya Wapalestina. Ni swali ambalo naulizwa na afisa uhamiaji wa Kiisrael katika mpaka wa kuingia Palestina kutokea nchi ya Jordan. Ni uhalisia ambao nimekuja kuona kwa macho yangu zaidi ya ule niujuwao kwa miaka mingi kutoka katika vitabu, magazeti, hadithi na mitandaoni.

Ni siku ya Jumapili ya tarehe 10 mwezi novemba 2013. Mimi na watanzania wenzangu watatu tulianza msafara wetu wa kuingia katika ardhi ya wapalestina tukitokea mjini Amaan Jordan ambako tuliwasili huko siku ya Jumamosi. Kutokana na kuwa siku hiyo ni siku ya mapumziko kwa Wayahudi, ilitubidi tulale mjini Amman kabla ya kuanza msafara wetu kuelekea mpakani. Safari ya kuelekea mpakani ilituchukua muda wa saa moja kabla ya kufika katika mji mdogo wa South Ashooh ambapo ndipo kuna ofisi za uhamiaji za kwa upande wa Jordan. Tulipofika hapo tukaagana na gari lililotuleta kutoka mjini Amman. Hapo mambo yalikwenda haraka na baadae tukapanda basi maalum la kuvusha wasafiri kataka pande mbili za mpaka. Kati ya geti la Jordan na ardhi ya Wapalestina tunakita katika vizuizi viwili ambapo tulitakiwa kuonyesha kipande cha ruhusa ya kuvuka mpaka. Katikati tunavuka daraja la Mfalme Feisal katika mto Jordan. Hali yake ni sawa na mipaka mingine duniani ukiondoa magari machache ya kijeshi yakiwa na silaha nzito na askari wawili watatu. 

Hali haikuwa hivyo katika mpaka wa kuingilia katika ardhi ya Wapalestina. Baada ya safari ya dakika tano hivi tunaingia katika mpaka wa ardhi ya Wapalestina. Hapo tunakutana na uzio wa waya za umeme pamoja na maaskari wa Kiisraeli. Ndio, mpaka wa kuingilia katika ardhi ya Wapalestina unasimamiwa na Waisraeli kama ilivyo katika maeneo mengine ya wapalestina. Tukiwa ndani ya basi tunaangalia majabali ya udongo wa jangwani yaliyozunguka eneo hilo. Mahandaki kila mahala pamoja na mitambo maalum ya uchunguzi. Tunafika geti la kwanza ambapo raia wote wa Palestina wanashuka na kuingia katika eneo maalum. Wengine wageni tunasubiri kwa zaidi ya dakika 20 kabla ya kuruhusiwa kuvuka kizuizi hicho cha kwanza. Eneo hilo hakuna mabasi mengine isipokuwa mabasi maalum ya kuvusha wageni na magari ya binafsi na ya mizigo. Baada ya hapo tunaenda kwa mwendo wa dakika moja na kufika katika kituo kikuu cha mpakani kinachoitwa King Feisal bridge kwa upande wa Jordan na .... Jina la kiisraeli kwa upande wa Ardhi ya Wapalestina.

Tulipofika katika kituo kikuu cha mpakani tulianza na kusubiri ndani ya basi kwa karibia nusu saa tukisubiri amri kutoka kwa vijana wa kiisraeli wenye silaha kali. Tukiwa ndani ya gari tunaangalia kwanza jinsi eneo hilo lilivyopangwa kiusalama likizungukwa na uzio wa waya pamoja na vijilima na viabanda vya juu vya walinzi wenye silaha. Nje tunaona vijana wa kiarabu wakiwa ndio wabeba mizigo na wasimamizi wao. Wengine wote ni Waisraeli na wengi wao ni askari wakiwa na mavazi yenye nembo ya Idara ya usalama wa ndani ya Israel. 

Tunaanza kwa kusimama katika foleni huku kila mtu akiwa na mzigo wake kuelekea katika sehemu maalum ya kuingiza mizigo kwenye mashine za ukaguzi. Kila msafiri anatakiwa kukabidhi passport yake ili kuandikishwa katika nembo maalum inayobandikwa katika mizigo yake kwa utambulisho. Baada ya hapo unajipanga katika foleni nyingine ya ukaguzi wa passport. Hapo unakutana na mabinti wa kiisraeli ambao wanakuuliza kila kilichoandikwa katika passport yako kutuibitisha kama ni yako. Hapo nikakutana na kizingiti cha kwanza. Passport yangu inatiliwa mashtaka. Inaelekea kwao wao Tanzania ni nchi ngeni na zaidi sio nchi ya waislam hivyo inakuwaje ninakuwa majina ya kiarabu. Baada ya kupitiwa na wenzake watatu binti huyo anaweka alama tatu kuonyesha kuwa nahitaji kuangaliwa zaidi. Tayari nimeshakuwa mshukiwa hatari. Baada ya dakika kadhaa naruhusiwa kuingia katika sehemu ya tatu ya ukaguzi ambayo natakiwa kuingiza kila kitu changu katika mshine maalum. 

Tofauti na wenzangu wengine wanaokwenda moja kwa moja katika sehemu ya viza, mimi nakutana na kijana mwengine ambaye ananichukua katika chumba maalum na kunihoji maswali kadhaa ikiwemo kama nimebeba silaha ya aina yoyote. Baada ya kunihoji anachukua passport yangu na kumkabidhi binti mwengine ambaye anaichukua na kuipaka mafuta maalum kabla ya kuingiza katika mashine maalum ya ukaguzi. Nadhani ilikuwa kukagua kama ina alama yoyote ya material za silaha. Baada ya hapo anamuonyesha mtu mwengine na kujadiliana naye kwa dakika moja kabla ya kunipa passort yangu na kuniambia lile neno la uchungu "Welcome to Israel"

Nachukua passport yangu na kuelekea katika sehemu ya nne ambayo sasa nawasalisha karatasi yangu ya viza niliyotumia kwa njia ya mtandao baada ya kuomba mwezi mmoja kabla. Hapo nakutana na shock nyingine. Napewa kibalia maalum cha kuingia Israel kwa upande wa ukingo wa magharibi wa mtu Jordan pekee. Kutoka hapo hadi kwenye kuchukua mizigo yangu nakutana na vizuizi vitatu ambavyo natakiwa kuonyesha passport yangu na kibali cha kuingia kwa uhakiki. Baada ya hapo tunakwenda kuchukua mizigo yetu kabla ya kupita katika kizuizi kingine kwa ukaguzi. Hapo wapo waliokuwa wakipita bila ya ukaguzi mwengine lakini kila Mpalestina analazika kukaguliwa upya. 

Nje ya mlango wa kutokea tunakuatana na duka la kubadilishia fedha na duka la bidhaa nyingine. Naulizia kubadili fedha naambiwa hapo ni fedha za Kiisraeli pekee na ndio fedha rasmi ya matumizi katika ardhi ya wapalestina. Naulizia vocha za simu ya kampuni inayotumika Palestina naambiwa hapo ni naweza kupata za makampuni ya Israel pekee na eneo la katibu kwa vocha za makampuni ya Wapalestina ni Jericho kwa Kiisraeli na Ailah kwa kipalestina. 

Natoka hapo kichwani nikijiuliza... Kama mimi nasikia uchungu wa kukumbana uso kwa uso na uhalisia huu wa ukoloni kwa Wapalestina, hali ikoje kwa Wapalestina wenyewe?

Salaam kutoka Ardhi ya Wapalestina


Salaam kutoka Ardhi ya Wapalestina: 



Jana jioni nimewasili katika mji wa Ramallah baada ya kukaa katika mpaka wa Palestina na Jordan unaosimamiwa na Waisrael kwa muda wa masaa matatu. Tofauti na picha niliyokuwa nayo hapo kabla kuhusu mji huu ulio chini ya ukoloni wa Waisraeli na uliowahi kukumbwa mashambulizi kadhaa ya majeshi ya Waisrael likiwemo lile lilomuweka kizuizini Comrade Arafat kwa miaka kadhaa kabla ya kuawa na sumu, mji huu ni mji mzuri kupita kiasi. Ni mji mzuri mara kadhaa zaidi ya miji yetu mingi ya kiafrika kama Dar es Salaam. Nategemea kuwa huku kwa wiki nzima kama mgeni wa Wapalestina nikiwa na wenzangu wanne kutika Tanzania na marafiki wengine wa Wapalestina kutoka nchi kadhaa duniani. Kitu kimoja nilichokutana nacho jana mara nilipofika hotelini ni kukutana na mzee mmoja katika lifti ambaye baada ya kujua natoka tanzania akaniambia "Karibu sana Palestina" kwa kiswahili fasaha. Then akanieleza kuwa ametembelea sehemu mbalimbali za Tanzania kwa mara kadhaa na ni rafiki mkubwa wa Mwalimu, Mkapa na Salim Ahmed Salim. Baadae akanichukua kwa meneja wa Hoteli na kumuambia kuwa mimi ni rafiki yake... "Ndugu yangu huyu. Take good care of him" Baada ya kumuuliza sana ananiambia alikuwa mshauri wa Arafat kwa miaka mingi na kunipa kadi yake ili niwasiliane naye kwa chochote kile nitakachotaka. Tukio hili limeniongezea majivuno yangu ya kuwa MTANZANIA! Proudly Tanzaniana forever! 

Leo ni shughuli maalum ya kumbukumbu ya mauaji ya Comrade Arafat na kutembela kaburi lake! Safari yangu nategemea kunifikisha Bathlehem, Nazareth, Jerusalem, Neblus, Jericho na sehemu nyingine mbalimbali ikiwemo kambi za wakimbizi wa kipalestina waliondolewa katika maeneo yao na utawala wa kimabavu wa Waisraeli na pia ukuta wa ubaguzi!

Kuhusu Hekaya ya wahafidhina wa CHADEMA dhidi ya ZItto

Kuna watu wengi wamekuwa wakiniuliza ... Eti kaka hii ripoti ina ukweli wowote... Kwa ni ninaowaheshimu nimewajibu kuwa hiyo ni riwaya ya kawaida ya chadema maslahi ambayo ilianza kuatengenezwa wakati uke Zitto alipojaribu kugombea uenyekiti. Nahata base ya kiasi cha fedha kinachotajwa ni kilekile ambacho wakati ule Mbowe alijaribu kuwarubuni waandishi akidai kuwa ndio alichonacho katika benki ya .... Kitu ambacho waandishi makini kama Msaki na Kibanda walikataa ujinga huo lakini ukachukuliwa na kutumiwa na Said Kubenea ambaye kuanzia wakati huo akawa mshirika wa Mbowe hadi hivi karibuni alipohamia kwa Mr Robot. Kwa wengine ambao siwathamini sana nawaambia, namshukuru Mungu kwa kuniepusha ukaribu na mtu mwenye akili fupi kama wewe ambaye unashindwa kung'amua kwa urahisi kuwa hiyo ni riwaya ya wajinga wakiwa na malengo ya kuteka akiki za wajinga kama wewe! Siwezi kuwa na rafiki anayeweza kuhadaika na riwaya ya kina Slaa na mwenza wake, nasikia siku hizi anajita bulisha kama mkewe, na vijana wao wehu kama kina Yericko, Ben Saanane na wengineo wenye chuki zao kama mtuhumiwa ugaidi Kilewo na jamaa zake wengine wanaodhani kuwa chama hicho ni chama cha nyumbani na wengine wote wanaothubutu kutishia nafasi yao huko ni maadui wa kuangamizwa. Lakini pia nafurahishwa kuwa hii vita ya akili fupi dhidi ya fikra pana imefikia kuwaibua maadui wote Zitto na sasa wanaonekana mchana kweupe kwa kujianika na siasa zao za fitna, uzandiki na chuki. Kwa wanaosema kuwa uongozi wa chama uongee, acheni kujidanganya kwani uongozi wa chama huo unahusika moja kwa moja na riwaya hii na hata kuipigania kutolewa mitandaoni....

Zitto na suala la uwazi katika ruzuku za vyama

Kama kuna suala ambalo Zitto amewahi kulisimamia na kulisema wazi na likawaumiza sana wale wanaojiona ndio wenye chama cha CHADEMA ni hili la kukosa uadilifu katika masuala ya fedha za umma. Tangia kamati ya Zitto kuibua tena hoja ya matumizi ya fedha za umma katika vyama na Zitto kuongelea tena suala la posho na maslahi manono ya viongozi, wenye chama wamejitokeza waziwazi kumpiga vita pamoja na kusambaza propaganda chafu dhidi yake wakiamini hilo litawafanya watanzania wasihoji uchafu wa nyumbani wakati wakijidai kuhoji uchafu wa jirani. Tofauti na hapo nyuma ambako walijitahidi sana kutojionyeha waziwazi kuwa ni wao ndio walionyuma ya fitna na hata jitihada za kummaliza Zitto kama walivyomfanyia Chacha Wangwe na wengineo, sasa wamejitoa waziwazi. Alianza Munisi, akaja Mbasa, akaja Mrema kupitia Makene na sasa kajitokeza Lema ambaye hivi karibuni alithubutu kumpora laptop na simu na kumpiga kiongozi wake wa chama wa mkoa wa Arusha kwa kumtuhumu kuwa anapeleka matatizo yao kwenye mitandao ya jamii. Leo Lema huyu mwenye sifa ya ujambazi, ulaghai na uhuni wa kila aina anajivika sifa ya kupigania uadilifu... Hali ni kama hii hapa chini;



ILIANZA NA SHUTUMA ZA LEMA: 

UNAFIKI WA ZITTO KABWE NA SUALA LA POSHO Kama nilivyosema jana kuwa leo kabla ya saa nane mchana nitaweka wazi unafiki wa Zitto katika suala la posho , suala ambalo halihitaji vikao vya Chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususani mitandao ya kijamii kama yeye anavyofanya na kujaribu kupotosha ukweli na kutafuta sifa ambazo kimsingi hana. CHADEMA wakati inaamua kulijadili suala hili la posho , msingi wake mkuu ulikuwa kama ifuatavyo : 1) CHADEMA iliona na kutambua ubadhirifu unaofanyika kupitia kivuli cha posho katika Taasisi za Umma na Serikali na sio Bunge pekee , hivyo CHADEMA ikapendekeza mishahara ipandishwe na posho zisizo za lazima ziondolewe ili kuondoa mwanya wa ubadhirifu wa fedha za Umma .Huu ndio uliokuwa msimamo wetu . Kulikuwa na msingi mkuu ambao ungekuwa na faida kubwa kwa Nchi na Watu wake lakini kabla msimamo huu haujawekwa hadharani na kutafsiriwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe tayari alishatoka katika vyombo vya habari ni kujipambanua kuwa yeye hataki posho na wala hatachukua posho , na hapa vyombo vya habari vilichukua jambo hili kama hoja yake binafsi na huku mantiki ya hoja kamili ikipotea . (Mantiki ilikuwa ni kuondoa posho zisizo za msingi kwa Watumishi wote wa Umma na kuboresha masilahi yao kwa maana ya mishahara ) Lengo kubwa la Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA ni kupigania masilahi bora ya Watumishi wa Umma na Sekta binafsi katika Nchi hii . Msingi wa CHADEMA ulikuwa na maana pevu kwani tulijua kama mishahara ikiongezwa itampa fursa Mtumishi kuwa na Maisha bora leo na hata baadaye kwa mafao bora baada ya utumishi wake kazini . Lakini ingekuwa rahisi pia kwa Mtumishi kuwa na uwezo mkubwa wa kutafuta mikopo kwa ajili ya maendeleo kwani Mabenki yanatoa mikopo kupitia mishahara ya Watumishi . Ikumbukwe kwamba , mtumishi mwenye mshahara mzuri anakuwa na fursa ya kupata mkopo mkubwa ambao utatatua matatizo yake mengi . Kwa hiyo msingi wa kutaka posho zisizo na msingi ziondolewe ilikuwa ni mkakati wa CHADEMA kuboresha masilahi ya Umma kupitia mishahara . Niliposema Mh Zitto ni mnafiki kuhusu suala hili , nilikuwa na maana ifuatavyo : Kwamba , sio kweli kuwa kukataa posho ni uzalendo na hata ingekuwa ni uzalendo Zitto sio mzalendo katika suala hili la fedha na maisha yake . Aliposema hatachukua posho Wananchi wengi walimuona ni shujaa , ushujaa ambao hana katika jambo hili . Nasema hivi kwa sababu , Wakati Zitto anakataa posho ya kikao ya shilingi sabini elfu ( 70,000/=) kwa siku ambayo ni sawa na shilingi takribani milioni kumi na mbili kwa vikao vyote vya Bunge kwa Mwaka , Zitto huyo huyo , anapokea posho ya kikao kati ya shilingi laki saba hadi milioni moja kwa kikao kimoja katika vikao vinvyofanywa na mashirika mbali mbali hususani Mashirika ya hifadhi za Jamii . Maana yake ni kwamba kama anapokea laki saba kwa siku na mashirika haya kwa ujumla wake yakafanya vikao ishirini tu kwa mwaka na mara nyingi Zitto kama Mwenyekiti wa PAC huwa anapata mwaliko wa kuhudhuria vikao hivi , basi atakuwa akipata posho ya kikao takribani ya shilingi milioni kumi na nne mpaka milioni ishirini kwa vikao visivyozidi ishirini , wakati kule juu amekataa posho ya shilingi milioni takribani kumi na mbili kwa vikao vya siku takribani mia moja na themanini ambayo ni miezi sita . Ikiwa vikao hivyo vya mashirika anayohudhuria Zitto kama Mwenyekiti wa PAC ni vya siku mia moja themanini kama ilivyo kwa vikao vya Bunge basi Zitto atakuwa anapokea posho kati ya ya shilingi milioni mia moja na ishirini na sita elfu na laki sita ( 126,600,000) na milioni mia moja na themanini ( 180,000,000) . Na hapa naomba kutaja masilahi yangu katika hili kwani Wabunge wa kawaida ikiwa wakialikwa katika vikao hivyo huwa wanalipwa shilingi laki tano kwa kikao kwa siku . Mimi nimewahi kuhudhuria vikao hivyo mara mbili na nikalipwa hivyo pamoja na chai na chakula cha mchana . Tofauti na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC yeye pamoja na posho anayochukua ( 700,000 - 1,000,000) hupewa mafuta ya gari au tiketi ya ndege yamkutoa alipo na kumrudisha na kukodiwa Hoteli yenye hadhi ya nyota nne mpaka tano ambayo kwa siku . Hotel hiyo hulipiwa kati ya dola za Marekani mia moja mpaka dola mia sita kwa siku . Ø JE MTU HUYU ANAYEPINGA POSHO YA ELFU SABINI YA KIKAO CHA BUNGE AMBACHO MSINGI WAKE NI UWAKILISHI WA WANANCHI NA KUKUMBATIA POSHO YA YA SHILINGI LAKI SABA HADI MILIONI MOJA YA MASHIRIKA AMBAYO MSINGI WAKE PENGINE NI KUWAZIBA MIDOMO WENYEVITI WA KAMATI ZA BUNGE KATIKA MASHIRIKA HAYO NDIYO UZALENDO ? HUU NI UNAFIKI WAKUTAKA SIFA AMBAZO HAZINA MSINGI. Lakini huyu Zitto anatoka Jimbo lenye Umasikini mkubwa ambapo naamini kuwa kuna wahitaji wengi kama yatima , wajane , wazee , na wasiojiweza kwa namna mbali mbali , kama yeye ni mzalendo kwa nini asingetumia malipo yake hayo halali kuwasaidia hao ndugu na Jamaa na Wapiga kura wake ? Ø NI NA WASI WASI NA UZALENDO ANAOUHUBIRI ZITTO , NA AMEPOTEZA MWELEKEO WA HOJA YA MSINGI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI INAYOONGOZWA NA CHADEMA JUU YA FIKRA SAHIHI YA KUBADILISHA MFUMO WA KIBADHIRIFU ULIOJIFICHA KWENYE POSHO ZISIZO ZA MSINGI NA KUBORESHA MASILAHI YA WATUMISHI WA UMMA KUPITIA MISHAHARA YAO. MSIMAO WANGU Kwanza najua na ninamini kuwa “ UMASIKINI SIO UZALENDO “ sipendi umasikini , nachukia umasikini lakini pia sipendi kuona mafanikio yangu yanabaki kwangu tu huku wengine wakiteseka , lakini siwezi pia kukumbatia umasikini kwa lengo lakuthibitisha uzalendo wangu . Najua watu wa Jimbo langu wanataka maji , umeme na huduma bora za Afya na mambo mengi yenye sura hii lakini sitang’oa bomba la maji nyumbani kwangu kwa sababu jirani yangu hana maji ila nimtasaidia kwa kadri nitakavyoweza na yeye aepukane na adha hiyo ya ukosefu wa maji . Najua shule za Kata hazina ufaulu mzuri na mazingira yake ni magumu , lakini sitampleka mtoto wangu kwenye shule zisizo na waalimu ili kuonyesha uzalendo bali nitapigania ubora wa shule hizo kuongezeka ili Wananchi wote wapate Elimu bora . Zitto Julai 2012 stahili za Mbunge ziliongezwa kwa takribani shilingi milioni tatu ambazo ni sawa na milioni thelasini na sita kwa mwaka , je kwani Zitto hakugoma kupokea pesa hizo ili kuonyesha uzalendo wake ? Zitto kuna wakati uliumwa ukapelekwa India kutibiwa , sasa kwani hukuwa mzalendo na kufanya mgomo ili utibiwe hapa Nchini ili kuonyesha Uzalendo wako ? na kuokoa pesa ya serikali kama ambavyo unaionea huruma kwenye posho ? Zitto ningekuelewa , kama maisha unayoishi yangeendana na kauli zako za Kikomunisti lakini maisha yako na matendo yako na mienendo yako yanashindwa kutafsiri kauli zako . MWISHO – MIMI SIAMINI KAMA MSINGI WA UZALENDO NI UMASIKINI . LAITI INGEKUWA HIVYO MAKUSUDI YA KUANZISHA MFUMO WA VYAMA VINGI ILI KUWAKOMBOA WATANZANI NA LINDI LA UMASIKINI ULIOSABABISHWA NA CCM YASINGEKUWA NA HAJA , NAJUA ASILIMIA 80 YA WATANZANIA NI MASIKINI SANA , JE WATANZANIA NI WAZALENDO KWA TAIFA LAO KULIKO WAMAREKANI ? Namalizia kwa maneno ya Charles Darwin “ If the misery of the poor be caused not by the laws of nature, but by our institutions, great is our sin.” Godbless J Lema 2/11/2013


MAJIBU YA Zitto:
Mwaka 2009 nikiwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya POAC nilikuta utamaduni wa Mashirika ya Umma/Taasisi za Serikali kuwalipa wabunge wanapoitwa kwenye kamati. Niliwashitaki Wabunge PCCB kwa matumizi mabaya ya madaraka na kujilipa posho ambazo hawastahili maana Bunge linakuwa limelipa. PCCB wakazuiwa uchunguzi wao na Spika Sitta, hata hivyo utamaduni huo ulikufa na siku hizi hakuna kitu kinachoitwa 'Parliamentary Expenses' kwenye mahesabu ya mashirika yote ya Umma. 

PAC ilipiga marufuku Taasisi za Serikali au Mashirika ya Umma kulipa wabunge kwa kazi za kibunge. Hivyo hakuna hata mjumbe mmoja wa PAC anayelipwa posho na Taasisi yeyote ya Serikali kwa kazi za kibunge. Wajumbe wa PAC wanalipwa posho kama kamati nyingine, na posho za vikao mimi sichukui maana nimezikataa bungeni, nimezikataa Halmashauri ya Wilaya Kigoma, nimezikataa Baraza la Ushauri la Mkoa wa Kigoma. Hata nikialikwa na NGOs kwa kazi zangu za ubunge sichukui posho yeyote. It is a matter of principle! 

Sipendi hata kidogo kulumbana na wabunge wenzangu kuhusu suala hili. Ni jambo la hiari ya mtu kuchukua au kutochukua posho. Hebu tujielekeze kutatua kero za wananchi badala ya kulumbana kunakosababisha tutunge uongo ili tu kulilia posho. Mbunge anayelilia posho hastahili kuwa mbunge. Akatafute kazi nyingine....



NA HII PIA KUTOKA KWA ZITTO:"Kuchukua au kutochukua posho za vikao kama mbunge ni suala la misingi (principles) na sio suala la uwezo kifedha. Kuna wabunge matajiri sana lakini wakachukua posho na wengine wa kawaida kabisa hatuchukui posho. Sio posho tu, hata msamaha wa kodi wa kuingia magari nimeukataa sababu ya misingi tu, kwamba siwezi kuwa Waziri kivuli ninayepinga misamaha ya kodi wakati huo huo nikachukua misamaha ya kodi. Ninaamini katika siasa za kutenda ninachosema. Mjadala wa posho kwangu mimi nimeufunga toka Juni 8, 2011 nilipoacha kupokea posho za vikao. Mwaka huo pia nilikataa msamaha wa kodi ya kuingia gari. Ni msimamo tu, hapa mtu hupendi msimamo wangu isiwe uadui, wewe endelea kuchukua posho, omba ziwe nyingi zaidi na wala sitatia neno kwenye msimamo huo japo nitaudharau maana posho za vikao ni kuwaibia wananchi ambao hawana maji safi na salama, watoto wao hawana walimu sababu Serikali haiwalipi walimu vizuri, kina mama waja wazito wanakufa kutokana na huduma mbovu za afya huko vijijini nk. Haya ndio masuala ya wananchi wetu na sio kudai kuongezewa posho."



NA HII PIA KUTOKA KWA ZITTO:"Kuchukua au kutochukua posho za vikao kama mbunge ni suala la misingi (principles) na sio suala la uwezo kifedha. Kuna wabunge matajiri sana lakini wakachukua posho na wengine wa kawaida kabisa hatuchukui posho. Sio posho tu, hata msamaha wa kodi wa kuingia magari nimeukataa sababu ya misingi tu, kwamba siwezi kuwa Waziri kivuli ninayepinga misamaha ya kodi wakati huo huo nikachukua misamaha ya kodi. Ninaamini katika siasa za kutenda ninachosema. Mjadala wa posho kwangu mimi nimeufunga toka Juni 8, 2011 nilipoacha kupokea posho za vikao. Mwaka huo pia nilikataa msamaha wa kodi ya kuingia gari. Ni msimamo tu, hapa mtu hupendi msimamo wangu isiwe uadui, wewe endelea kuchukua posho, omba ziwe nyingi zaidi na wala sitatia neno kwenye msimamo huo japo nitaudharau maana posho za vikao ni kuwaibia wananchi ambao hawana maji safi na salama, watoto wao hawana walimu sababu Serikali haiwalipi walimu vizuri, kina mama waja wazito wanakufa kutokana na huduma mbovu za afya huko vijijini nk. Haya ndio masuala ya wananchi wetu na sio kudai kuongezewa posho."